Nyani Ngabu, mimi namuomba Raisi John Pombe Magufuli apate ujasiri, kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya CCM, awaombe radhi Watanzania halafu ndio sote tukae pamoja tushirikiane kulijenga upya taifa hili. Akifanya hivyo nitaamini kwamba kweli sasa tunafungua ukurasa mpya kwa sababu pamoja na jitihada anazofanya kujiweka mbali na tawala zote zilizopita kabla yake, hawezi kukwepa ushiriki wake katika kutufikisha hapa tulipo kama taifa. Lazima kwanza akiri ushiriki wake, atuombe radhi na ndipo hapo ataweza kutushawishi kwamba kazaliwa upya na hivyo kutuondolea shaka katika kumuunga mkono ili tufanye kazi pamoja.
Hatujawahi kuwa na Mkuu wa nchi, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wizara, Mkuu wa Chombo chochote cha dola (Jeshi, Polisi, Usalama wa Taifa), Mkuu wa Shirika lolote la serikali, Mkuu wa Mahakama (Jaji Mkuu), Mkuu wa Bunge (Spika), Mkuu wa taasisi yoyote ya serikali n.k.
ambaye kigezo kilichotumika kumteua si U-CCM wake. Machafu yote ndani ya nchi hii yalipandwa, yakachanua, yakalelewa, yakakomaa chini ya uongozi wa wote niliowataja hapo juu na ndio wahusika wakuu. Magufuli, kwa niaba ya CCM, pia aliombe radhi taifa kwa kukosa katiba iliyotokana na maoni ya wananchi wake kwa shinikizo la CCM.
Si rahisi kwa mtu mchafu kuongoza mapambano dhidi ya uchafu mpaka kwanza ameoga na kuwa msafi na asipofanya hivyo lazima wasafi watasita kumuunga mkono. Na ndivyo ilivyo kwa Magufuli, aanze kwa kutubu na ingawa inawezekana ana nia ya dhati ya kimageuzi lakini shati lake la njano, linalohitaji maji na sabuni, linamuumbua.