Irene Mark
HIVI karibuni, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alikaririwa na vyombo vya habari akiueleza umma kwamba kwa sasa ofisi yake haina fedha za kuhakiki majina ya wanachama wa Chama Cha Jamii (CCJ).
Kauli hiyo ya Tendwa, ilikuja siku moja baada ya viongozi wa muda wa CCJ, kuwasilisha mafaili yenye majina ya wanachama 2,000 kila mkoa kwa mikoa 10 Tanzania Bara na Visiwani.
Hiyo ilikuwa hatua ya mwisho ya CCJ katika kuomba usajili wa kudumu ili nayo iingie kwenye mchakato wa kupata wawakilishi (madiwani, wabunge ama rais), wa wananchi kupitia sanduku la kura zitakazopigwa nchi nzima Oktoba 31, mwaka huu.
Ni hatua nzuri yenye kustahili pongezi. Ndiyo, wanafaa kupongezwa maana ni kawaida ya waungwana kukosoa na kupongeza panapobidi. Nami nafanya hivyo.
Kama ilivyo ada kwa waungwana, na ndivyo ilivyo kwamba kila kizuri kina ubaya wake. Leo nitajadili pia mabaya ya viongozi wa CCJ na safu nzima ya chama hicho kilichojipambanua mwanzoni mwa mwaka huu na kufanikiwa kukitikisa chama kikongwe nchini yaani, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati wa mchakato wa kuomba usajili wa muda, waandishi wa habari, nikiwemo, walikuwa watu muhimu kwa viongozi hao. Ilifika wakati hata kabla ya kufanya jambo ilibidi wawafuate waliowaamini na kuomba ushauri.
Kwangu hilo ni jambo jema sana. Hali iliendelea hivyo mpaka siku walipoitwa rasmi kwenda kupokea cheti cha usajili wa muda pale kwenye ofisi za msajili katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Waandishi tulitimiza wajibu wetu. Umma ukahabarika, wapenda mageuzi wakajitokeza kwa wingi kiasi chao kwenda kushuhudia ujio wa chama kilichonadiwa kufanya mapinduzi ya fikra kwa Watanzania.
Wachache walioisikia CCJ walitamani kujua historia za waasisi wake (kisiasa zaidi) ambao walitajwa sana kwa nafasi ya uenyekiti na ukatibu. Kwa bahati mbaya, ni sura ngeni mno kwenye medani ya siasa.
Viongozi hao wakatokea kukubalika (kwa kipindi kile), wakapokelewa kwenye jamii kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari. Misukosuko waliyoipata ilikemewa na waandishi wa habari, ukawa urafiki mwema kati ya viongozi wa muda wa CCJ na wahabarishaji wa umma.
Wapo waliokitilia hofu chama hicho kipya kwa madai ya kuwepo kwa kazi maalum ya kuuvuruga upinzani nchini, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Nilitafakari kwa kina na kuandika kwenye safu hii nikiwauliza; ‘CCJ mmetumwa kutuvuruga?'
Hii ni baada ya wao kuanza kupanga ratiba za kesho… kesho pindi walipotaka kuzungumza na waandishi wa habari ili kueleza mkakati wao wa kuyapata majina 2,000 kila mkoa kwa mikoa 10 na mipango yao ya baadaye katika kufikia vigezo vya kupata usajili wa kudumu. Hapo ni baada ya kujiridhisha kwamba watapata usajili wa muda.
Kilichonisukuma kuandika mtazamo wangu ni hali ilivyobadilika punde baada ya kupata usajili wa muda ambapo viongozi hawa na wengine ndani ya CCJ walianza kususurika. Ushirikiano mwema kati yao na wanahabari ukaota ‘mbawa'.
Kumbukumbu zangu zinanilazimisha kunukuu baadhi ya maneno ya waandishi ‘marafiki' wa CCJ kwamba uongozi mzima wa chama hicho ni wa ‘kisanii', viongozi wote ni wasemaji wa chama hicho, matokeo yake wanaupotosha umma. Ndiyo, kwa takribani juma zima lililopita vyombo mbalimbali vya habari hususan magazeti, viliripoti kwamba chama hicho kingetoa tamko lao kuhusu kauli ya msajili kukosa pesa za kuhakiki majina yao ili kuharakisha mchakato wa kukipatia usajili wa kudumu. Sasa jamii imechoka kusikia simulizi za CCJ. Swali na mshangao vinabaki ni kwanini wasemaji wake wanatofautiana? Ni kweli kimepoteza mwelekeo? Kwanini mnatoa taarifa zisizo rasmi? Nawashauri, msipojipanga vema jamiii itawatenga na imani yao kwenu itapotea.