Aina ya uongozi tulio nao; anayechelewesha msafara ng'ombe wa mbele, anatandikwa wa nyuma

Burkinabe

JF-Expert Member
Feb 12, 2023
1,896
3,206
Bara la Afrika pamoja na kuwa na raslimali za kila namna lakini bado ndo bara linaloongoza kwa umaskini kati ya mabara yote 7.

Hii inachagizwa na ukosefu wa viongozi bora.

Viongozi wengi wa nchi za Kiafrika wanafanana karibia kwa kila kitu (ukitoa wachache tu wanaojitambua). Wengi wao hawana uzalendo kabisa kwa nchi zao na hugeuka vibaraka wa mabeberu mara tu waingiapo madarakani.

Sasa jambo la kusikitisha, mara nyingi katika hizi nchi zetu mkubwa akifanya kosa, anaadhibiwa mtu wa chini yake ili ionekane hatua zilichukuliwa!

Hii ni sawa sawa na wachungaji wa ng'ombe kuwatandika ng'ombe wa nyuma ilhali ng'ombe wa mbele ndo wanachelewesha msafara!

Na kwa uzoefu wangu wa kufuga kwa takribani miaka 12, nilichogundua ni kwamba wale ng'ombe wavivu na wenye kiburi, mara nyingi ndo huwa wanajitanguliza mbele ili kukwepa kichapo toka kwa Mchungaji wao kutokana na kujua kwamba ni wavivu na wana kiburi! Hivyo, utawakuta wanatembea kwa mwendo wa madaha huku wenzao nyuma wakiadhibiwa kwa makosa yao walioko mbele!

Nihitimishe kwa kusema kwamba, siku kama nchi za Kiafrika tukichoka kuishi kwenye lindi la umaskini uliotopea, tunaosababishiwa na viongozi wetu wakubwa (ng'ombe wa mbele wanaochelewesha msafara), basi tutawatoa kwa nguvu warudi nyuma ili tuwatangulize wenye kasi mbele. Tumechoka kuadhibiwa (ng'ombe wa nyuma) kwa makosa yasiyotuhusu. Maana tunaadhibiwa kwa namna nyingi ikiwemo tozo zisizo na kichwa wala miguu, mfumko wa bei kwa bidhaa mbalimbali, ukali wa maisha, ukosefu wa ajira n.k.

Ee Mungu, tunakuomba uibariki nchi yetu na bara letu la Afrika.

Amin.
 
Back
Top Bottom