Dhamana ya akina Yona yabaki fumbo
Shadrack Sagati
Daily News; Monday,December 01, 2008 @21:15
Mambo yameendelea kuwa magumu kwa mawaziri wawili wa zamani Basil Mramba na Daniel Yona baada ya juhudi za kuwatoa rumande kukwama tena jana. Washitakiwa hao wawili ambao wanadaiwa kuitia hasara ya Sh bilioni 11. 7 serikali, walishindwa kupata dhamana baada ya Mahakama ya Kisutu kugoma kusikiliza shauri lao kwa maelezo kuwa taratibu za mahakama zilikiukwa.
Hakimu Hezron Mwankenja ambaye anasikiliza kesi hiyo, hakuthubutu kuwapandisha kizimbani washitakiwa hao, baada ya kung'amua kuwa hakukuwa na hati ya kuwapeleka mahakamani hapo (Remove Order). Hakimu huyo pia alisema hata jalada ambalo lilitoka Mahakama Kuu, halikuwa na amri ya Msajili au ya Jaji inayomtaka yeye kusikiliza shauri hilo kwa siku ya jana, kitendo ambacho kilimfanya kugoma kusikiliza shauri hilo.
Jana haikuwa siku ambayo washitakiwa hao walipangiwa kwenda mahakamani, ila kwa washitakiwa ambao dhamana zao ziko wazi huwa wanafikishwa mahakamani kutoka rumande kwa hati maalumu ya hakimu. Lakini kwa Mramba na Yona mahakama hiyo haikuwa na habari za wao kufikishwa kuendelea na mchakato wa dhamana.
Badala yake kesi hiyo ilishapangwa leo kwa ajili ya kutajwa tena; fursa ambayo washitakiwa wanaweza kuitumia kuendelea na mchakato wa dhamana zao. Hata agizo la msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Lameck Mlacha, alilolitoa siku ya Ijumaa kuwa mchakato wa kupata dhamana kwa washitakiwa hao ungeendelea jana Kisutu, halikuwekwa kwa maandishi.
Ni kwa sababu hiyo, Hakimu Mwankenja hakuwa na njia nyingine; bali kuwaeleza kwa kina mawakili wa pande zote kuwa hawezi kuendelea na shauri hilo kwa vile taratibu za mahakama hazikufuatwa hasa za kuwapeleka washitakiwa hao mahakamani hapo jana. Aliwaeleza kuwa yeye hakutoa hati ya kuwapeleka mahakamani washitakiwa kuendelea na mchakato wa kupata dhamana, hivyo hawezi kusikiliza shauri hilo.
Kutokana na msimamo huo wa hakimu, mawakili wa upande wa utetezi na wale wa upande wa mashitaka walilazimika kurudi katika ukumbi namba moja wa mahakama na kuchukua nyaraka zao na kuondoka ukumbini. Kitendo hicho kiliwaduwaza ndugu wa washitakiwa ambao tayari walishajazana katika ukumbi huo, kwa matumaini kuwa taratibu za dhamana zingekamilika na kujumuika nao uraiani.
Ndugu hao baada ya kuona mawakili wanaondoka, nao walitoka nje ya ukumbi wakiwa na shauku ya kilichotokea. Hata mawakili wa washitakiwa hawakuwapa maelezo ya sababu ya kesi hiyo kutoendelea jana. Badala yake ndugu hao sasa wakataka kujua habari hizo kutoka kwa wanahabari "Jamani twambieni ni nini kinaendelea, maana tumeona mawakili wanatoka nje ya ukumbi wa mahakama bila kutuambia kilichotokea."
Mmoja wa mawakili wa utetezi alipoulizwa na wanahabari kuhusiana na hali hiyo alijibu "hata mimi sijui ninachosubiri hapa ni kuitwa mahakamani kuendelea na kesi, hayo unayoniuliza siyajui." Mwendesha Mashitaka wa Serikali Boniface Stanslaus alipoulizwa sababu ya kesi hiyo kutoendelea jana naye alijibu. "Mimi sio msemaji wa suala hilo, ila niko hapa nasubiri tuitwe mahakamani."
Mmoja wa ndugu wa Yona alipoulizwa kama mahakama iliwataarifu kinachoendelea naye alijibu "kwa kweli ndugu yangu na sisi tumebaki tunashangaa, hatujui kinachoendelea hapa mahakamani." Baadaye waandishi wa habari walimfuata Hakimu Mwankenja kupata ufafanuzi wa suala hilo, ndipo alipotoa ufafanuzi wa namna taratibu zilivyokiukwa.
Kutokana na msimamo huo wa Hakimu Mwankenja, washitakiwa waliondolewa eneo la Mahakama ya Kisutu saa 7.10 na basi la Magereza lenye namba za usajili STK 4373 huku wakisindikizwa na magari mengine manne. Walionekana watu wasio na furaha, tofauti na siku zingine wakati wanaondolewa katika eneo hilo la mahakama. Katika basi hilo walipanda pamoja na washitakiwa wengine.
Kabla ya tukio hilo la kesi yao kutosikilizwa jana, washitakiwa hao mara tu baada ya kufikishwa mahakamani hapo saa mbili asubuhi, waliondolewa katika eneo hilo la mahakama na kupelekwa Mahakama Kuu. Baadaye tena saa tatu walirudishwa Kisutu na kufikishiwa rumande kusubiri taratibu zao za kupata dhamana.
Asubuhi Hakimu Mwankenja alipoulizwa kama alikuwa na taarifa za washitakiwa hao kupelekwa mahakamani hapo alijibu "Hapa nilipo sijapata jalada kutoka Mahakama Kuu, tusubiri tuone kitakachokuja kimeandikwa kwenye jalada hilo." Ila alisisitiza kuwa yeye hakuwa ametoa hati ya kuwapeleka Kisutu, ila yuko tayari kuendelea na shauri hilo kama jalada litakuwa na amri ya Mahakama Kuu ya kumtaka aendelee kulisikiliza shauri hilo kwa siku ya jana.
Mramba na Yona wanashitakiwa kwa makosa 13 ambayo ni kuipendelea kampuni ya Alex Stewart kwa kuipa mkataba bila kufuata sheria za ununuzi na kuisamehe kodi hivyo kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. Mramba katika kesi hiyo anaguswa na mashitaka yote 13 wakati Yona anagushwa na mashitaka sita. Mashitaka yanayomgusa Yona ni yale ya kushiriki kuipendelea kampuni ya Alex Stewart kwa kuipa nyongeza ya mkataba.
Lakini pia Waziri huyo wa zamani wa nishati na madini anatuhumiwa kuipendelea kampuni hiyo na kuiachia suala la ukaguzi wa hesabu za kampuni zinazochimba madini nchini kufanywa kiholela na kampuni hiyo bila kuishirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kutokana na kutokuwa makini Yona anahusishwa kuchangia kuisababishia hasara ya Sh bilioni 11.7 Serikali ya Tanzania. Mramba licha ya kuguswa na mashitaka hayo; lakini pia anatuhumiwa kutoa misamaha mbalimbali ya kodi kwa kampuni ya Alex Stewart na kusababisha hasara hiyo ya Sh bilioni 11.7.