elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
WATU na taasisi wameguswa na uamuzi wa serikali kujenga daraja la aina yake la Kigongo-Busisi wilaya Misungwi kwa kumhakikishia Rais John Magufuli kuwa naye bega kwa bega wakimsihi aendelee kuchapa kazi bila kujali kelele.
Aidha, daraja hilo refu kuliko yote katika Afrika Mashariki na la sita katika Afrika, limeelezewa kwamba litakapokamilika, wanaovuka watatumia dakika nne badala ya saa mbili na nusu zinazotumika sasa kuvuka kati ya Kigongo na Busisi kutokana na wingi wa magari.
Hayo yalielezwa jana Rais Magufuli alipoweka jiwe la msingi la mradi huo ambao Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale alieleza serikali ilivyoanza muda mrefu na namna wafadhili walivyogoma kuanza ujenzi. Miongoni mwa waliopewa nafasi na Rais Magufuli kuzungumza ni Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliyemwambia, “Mungu akujalie afya njema na sisi tulio pembeni tuko pamoja na wewe tutakufia.
” Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo alimuomba Rais Magufuli kuendelea kuchapa kazi akisema, “sisi tupo nyuma yako tutakutetea mahala ambapo kutakuwa na matatizo.” Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema mradi huo ni historia kubwa na unathibitisha uthubutu wa hali ya juu.
Akielezea daraja hilo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mfugale alisema daraja litafupisha urefu wa eneo hilo la Busisi na Kigongo linalotenganishwa na Ziwa Victoria hivyo badala ya saa mbili na nusu, watu na magari yatatumia dakika nne. Daraja litakuwa na urefu wa kilometa 2.3, upana wa meta 28.45 na litakuwa la njia nne. Litakuwa na nguzo 67 na likikamilika litakuwa na ubora kwa zaidi ya miaka 100 ijayo.
Daraja hilo litajengwa na kampuni ya CCECC na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) zote za China kwa gharama ya Sh bilioni 699.2 likitarajiwa kukamilika baada ya miaka minne. Litakamilika baada ya miezi 48; ni pamoja na muda wa kujiandaa wa miezi mitatu.