Wito: Pamoja na kusainiwa kwa mikataba mitatu ya wawekezaji wa Dubai Serikali ibainishe maudhui yake na mabadiliko yaliyofanywa kwenye mkataba wa IGA

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478


Sote tunafahamu kwamba, kwa nchi changa duniani, fursa za uwekezaji wa kigeni sio tu kwamba ni chache, lakini pia zinakuja na mashari ya kikatili, kinyonyaji na kikoloni. Na wakati mwingine zinakuja kwa ghrama kubwa sana.

Kuna wakati mazingira asilia ndiyo yanaharibiwa na wawekezaji wa kigeni. Wakati mwingine ni wafanyakazi wanaonyonywa. Wakati mwingine wafanyakazi wa kigeni wanaletwa na kupora fursa za wafanyakazi wa ndani. Na wakati mwingine ukuu wa mamlaka za kitaifa, kama vile ukuu wa serikali, ukuu wa bunge na ukuu wa mahakama unawekwa kwenye kwapa la wawekezaji wa kigeni.

Lakini, hakuna nchi inayopaswa kukubali wawekezaji wa kigeni unaomabatana na sharti kwamba nchi mwenyeji lazima ikubali kuuza ukuu wa serikali, ukuu wa mahakama, ukuu wa bunge, na urithi asilia wa wazawa kwa wageni hao.

Lakini, jambo hili limetokea nchini Tanzania kati ya tarehe 25 Oktoba 2022 na tarehe 22 Oktoba 2023, ambapo baadhi ya viongozi wa serikali ya awamu ya sita na baadhi ya viongozi wa chama tawala cha CCM wameuza ukuu wa serikali, ukuu wa mahakama, ukuu wa bunge, na urithi asilia wa Watanzania kwa wageni wa Dubai na washirika wao.

Kitendi hiki ni sawa na ku
nzisha vita ya kiuchumi dhidi ya bandari 88 za Tanzania Bara, yaani uhaini wa kiuchumi.


Uthibitisho ni taarifa ya Ikulu ya Dodoma iliyotolewa tarehe 22 Oktoba 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Zuhura Yunus, kwenda kwa umma. Nakala imeambatanishwa mwishoni mwa uchambuzi huu.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, mpaka tarehe 22 Oktoba 2023 idadi ya “mikataba iliyosainiwa" kati ya Tanzania na Dubai ni minne, ambayo ni:

  • (1) "Mapatano ya awali" (Inter-Governmental Agreement, IGA);
  • (2) "Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement, HOGA);
  • (3) "Mkataba wa Upangishaji wa Ardhi (Land Lease Agreement, LALA)" na
  • (4) "Mkataba wa Uendeshaji wa bandari (Port Concession Agreement, POCA).”
1698328225991.png

Mchoro: Mfumo wa mikataba ya kimataifa unaotumiwa na wawekezaji wa Kampuni ya DP World PLC nchini Tanzania. Kilicho wazi katika mchoro huu ni kwamba Emirati ya Dubai ni dalali wa Amerika.

Taarifa hiyo inamnukuu Rais Samia akisema kwamba, "mikataba [mitatu] iliyosainiwa 22 Oktoba 2023 imetokana na makubaliano ya awali [ya IGA yaliyofanyika] kati ya serikali [ya Tanzania] na Mamlaka ya Dubai," mapatano yaliyoidhinishwa na Bunge la Tanzania tarehe 10 Juni 2023.

Aidha taarifa hiyo imemnukuu Rais Samia akisema kuwa "mikataba iliyosainiwa" ni zao la "mahitaji na matakwa ya nchi kama yalivyoainishwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa" la Tanzania.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alitaja mambo kumi na tano yaliyomo katika mikataba hii mitatu. Mambo hayo ni:

(1) Mikataba kuhusisha magati namba 0-7 ya Bandari ya Dar es Salaam badala ya magati yote 14 ya Bandari ya Dar es Salaam na mikataba; (2) TPA na DPW kuendesha kwa pamoja magati namba 0-3 kuhusu masuala ya kibiashara na kiserikali; (3) DPW kuendesha peke yake magati namba 4-7; (4) Mikataba kutohusisha bandari nyingine za mwambao wa Pwani wala maziwa yaliyoko Bara; (5) Mikataba kuwa na ukomo wa miaka 30; (6) Utekelezaji wa mikataba kuwa unarejewa kila baada ya miaka mtano; (7) TPA kumiliki hisa katika kampuni ya uendeshaji itakayosajiliwa na DPW; (8) Kuwekwa kwa viwango vya utendaji (KPI's) katika mikataba; (9) Uhuru wa watumishi wa sasa wa TPA kuchagua kubaki TPA au kuhamia DPW; (10) Jukumu la ulinzi na usalama katika bandari yote kubaki mikononi mwa Serikalini; (11) Mwekezaji kulipa kodi na tozo zote za Serikali kwa mujibu wa Sheria za Tanzania; (12) Sheria za Tanzania kutumika katika utekelezaji wa Mikataba hii mitatu; (13) Uwepo wa fursa za watanzania kushiriki katika uwekezaji huu kupitia vifungu vya Sheria vinavyolinda maudhui ya ndani ya nchi (local contents); (14) Haki ya serikali ya Tanzania kujiondoa katika Mikataba hiyo kama ikiona inafaa kufanya hivyo; na (15) serikali kupata 60% ya faida itakayopatikana.

Hata hivyo, baadhi ya matamko ya Rais Samia na Mbossa, yanapingana na maudhui ya mapatano ya awali ya IGA yaliyoidhinishwa na Bunge tarehe 10 Juni 2023, na hadi sasa bunge halijabatilisha uamuzi wake huo.

Kwa mfano, matamko namba 2 na 14 hapo juu, hayawezekani kuwa kweli kamwe mpaka kwanza mapatano ya awali ya IGA yarekebishwe na Bunge la Tanzania. Hivyo, matamko haya yanakanushika na hayaaminiki.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Feleshi, amesikika akisema kwamba, kwa kuwa "kazi za serikali zinasimamiwa na Bunge na zinafanyika kwa mujibu wa sheria" basi "Wakati ukifika Kamati ya Bunge husika au Bunge kwa ujumla litafahamu kilichomo."

Lakini, Bunge lilipaswa kurekebisha mapatano ya IGA kabla ya kuandikwa na kusainiwa kwa HOGA, maana HOGA inapaswa kutokana na IGA, na sio kinyume chake.

Utata wa taarifa ya serikali

Tatizo liko hivi: Rais Samia na wenzake wanasema kwamba serikali imesikia maoni ya Wananchi na kuchukua hatua stahiki za kurekebisha Mkataba wa Bandari.

Lakini, serikali wanasema uwongo kwa sababu wananchi walilalamikia mkataba wa IGA kuhusu vipengele kama vile uwezo wa Dubai kusaini mkataba, kukiukwa kwa sheria za ndani ya Tanzania, kuweka maliasili za Tanzania kwenye mikono ya wageni bila ukomo wa muda, na mambo kama hayo.

Kwa hiyo serikali wanapozungumza kwamba Host Government Agreement (HOGA) iliyosainiwa imezingatia maoni ya wananchi wakati wananchi wanachotaka ni marekebisho ya IGA, huo ni ulaghai, maana IGA na HGA ni vitu viwili tofauti, ambapo HGA haiwezi kubatilisha kifungu chochote cha IGA kwa sababu IGA ni kama kichwa wakati HOGA ni kama sikio. Na sikio haliwezi kuzidi kichwa.

Hivyo, kusema kwamba HGA iliyosainiwa ni ya miaka 30 haimanishi kwamba umilele wa mkataba wa awali wa IGA umeondoka, maana, kwa mujibu wa IGA, kuna HGA zaidi ya moja zitakuja kusainiwa.

Hivyo, ni wazi kwamba hapa serikali imetanguliza mkokoteni mbele ya punda. Hii tabia ya kutumia njia haramu kwa ajili ya kutafuta matokeo halali inaitwa tabia ya "umachiaveli."

Aidha, tofauti na ilivyotarajiwa na wakosoaji makini wa "mapatano ya awali" ya IGA kati ya Tanzania na Dubai, taarifa ya Ikulu haikuambatanisha ushahidi halisi wa kuyathibitisha matamko tuliyoyasikia wakati wa hafla ya kusaini mikatabai.

Wito kwa serikali ya Tanzania

Hivyo, chini ya ibara za 8(1)a, 8(1)(c) na 132(5)(f) za Katiba ya Tanzania (1977), kama zikisomwa kwa pamoja, tunatoa wito kwa serikali kutoa taarifa za aina mbili kwa umma haraka iwezekanavyo.

Kwanza ni taarifa kwa umma kuhusu maudhui ya mikataba ya HOGA, LALA, na POCA iliyosainiwa tarahe 22 Oktoba 2023, mjini Dodoma. Hatutaki kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa kuaminishwa kwamba ni mwanakondoo.

Na pili ni taarifa kwa umma kuhusu marekebisho yote ambayo Rais Samia anasikika hapo juu kwenye video akidai kwamba yamefanyika kwenye mkataba wa awali wa IGA, uliosainiwa kisiri tarehe 25 Oktoba 2022.

Taarifa hizi zitatuwezesha sisi umma kutathmini na kujiridhisha kuhusu mambo kadhaa tuliyoyalalamikia tangu mkataba tata wa IGA ulipoanguka mikononi mwa umma kinasibu mwezi Juni mwaka 2023. Kosa la usiri ulioghubika kusainiwa kwa mkataba wa awali wa IGA lisirudiwe tena.

Taarifa ya Ikulu ilifafanua kwamba, “mikataba ya uwekezaji wa bandari iliyosainiwa imezingatia maoni yaliyotolewa kupitia makundi mbalimbali ya kijamii,” kwani “serikali ilisikiliza maoni mbalimbali yaliyotolea na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati, vyombo vya habari, mitando ya kijamii, viongozi wa dini na baadhi ya viongozi wastaafu.”

Aidha, taarifa hiyo inafafanua kwamba, “mikataba iliyosainiwa imetokana na makubaliano ya awali kati ya serikali na mamlaka ya Dubai,” na kwamba, Wakuu wa mamlaka ya Dubai “wameridhia mahitaji na matakwa ya nchi kama yalivyoainishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.”

Hata hivyo, tukio la kusainiwa kwa HOGA, LALA, na POCA halikuambatana na ushahidi wowote wenye kuonyesha kama kuna kipengele chochote cha mkataba wa awali wa IGA kinachomomonyoa ukuu wa serikali, ukuu wa Bunge na ukuu wa mahakama, na mipaka ya nchi kimebadilishwa na serikali.

Vifungu vya mkataba wa awali wa IGA vilivyokoselewa na umma

Kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawa, hapa chini tunabainisha vifungu vya mkataba wa awali wa IGA vilivyokataliwa na/au kuhojiwa na umma wa Watanzania:

(a) Kifungu cha 2(1), kuhusu "lengo la mkataba," kinachosema kwamba, "Madhumuni ya Mkataba huu ni kuweka mfumo wakisheria wa maeneo ya ushirikiano kwa ajili ya ujenzi, uboreshaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari za bahari na maziwa, kanda maalum za kiuchumi, hifadhi za usafirishaji, korido za kibiashara na miundombinu mingine ya kimkakati ya bandari nchini Tanzania."

(b) Kifungu cha 4(1) kinachosema kwamba, "Upeo wa Mkataba huu ni kuwezesha utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa katika Kiambatisho cha 01 cha Mkataba huu," ambapo, Kiambatisho cha 01 kinataja maeneo yafuatayo:

Awamu ya 1 ya Miradi: "(1) Ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa Gati 0, Gati 1-4 na Gati 5-7 ya Bandari ya Dar es Salaam. (2) Ujenzi wa Dhow Wharf Terminal na Kituo cha Abiria cha Bandari ya Dar es Salaam kuendeshwa na TPA. (3) Ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa Eneo la Bandari Kavu la Kwala na Kurasni bandari kabla ya lango. (4) Ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa gati 0, Gati 1-4, kwa kuihamishia Gati 0 kwenye eneo jipya la EPZA ambako kutajengwa Orofa Kubwa la Kuhifadhi ya Magari."

Awamu ya 2 ya Miradi: "(1) Ujenzi wa majukwaa ya vifaa, maeneo maalum ya kiuchumi, mbuga za viwanda na miundombinu mingine ya vifaa ili kusaidia ukuaji na maendeleo ya biashara na njia za usafirishaji zinazohudumia nchi zisizo na mlango bahari katika Mashariki na Kusini mwa Afrika. (2) Ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa bandari za ziada za bahari na/au maziwa kwa kuboresha na kuendeleza bandari nchini Tanzania pamoja na kuunganishwa na biashara kati ya Tanzania na Nchi nchi zisizo na mlango bahari kama inavyopendekezwa na TPA na kukubaliana na DPW."

(c) Kifungu cha 5(1), kuhusu “haki za kujenga, kusimamia au kuendesha”, kinachosema kwamba, "Nchi Wanachama zinakubali kwamba DPW itakuwa na haki ya kipekee ya kujenga, kusimamia na/au kuendesha Miradi kama ilivyoainishwa katika Kiambatisho cha 01 Awamu ya 01, moja kwa moja au kupitia Washirika wake chini ya Mkataba huu kama itakavyoainishwa zaidi katika Mikataba ya Mradi husika na HOGAs husika."

(d) Kifungu cha 6(1), kuhusu "ridhaa na vibali vya serikali," kinachosema kwamba, "Serikali ya Tanzania itahakikisha kwamba Kampuni ya Mradi husika inapewa vibali vyote muhimu vya kiserikali, ridhaa, haki za ardhi, vivutio vya uwekezaji na misamaha inayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Mikataba ya Mradi na mikataba yoyote ya ziada kwa mujibu wa sheria husika."

(e) Kifungu cha 7(3), kuhusu "vibali vya miradi," kinachosema kwamba, "Iwapo vibali vikisha tolewa kwa mradi wowote havitoweza, kubatilishwa, kubadilishwa, kurekebishwa, au kushindwa kuhuishwa au kuongezwa na Serikali ya Tanzania au mamlaka husika ya serikali au wakala bila ya mashauriano ya awali na PCFC inayowakilisha Serikali ya Dubai ikiwa ubatilishaji kama huo, mabadiliko, urekebishaji au kushindwa kuhuisha au kuongezwa kunaweza kuwa na athari mbaya kwa Miradi (au yoyote kati ya hizo)."

(f) Kifungu cha 8(1), kuhusu "haki juu ya umiliki wa matumizi na faida kutokana na ardhi," kinachosema kwamba, "Serikali ya Tanzania itachukua hatua zote zinazohitajika ili kuhakikisha upatikanaji na utoaji wa haki za ardhi kwa DPW au kampuni ya mradi husika ili: (a) kupata, kumiliki na kutumia ardhi inayohusiana na kila Mradi (“Haki juu ya umiliki wa matumizi na faida zitokanazo na Ardhi”); (b) Kutunza na kumiliki Haki hizo za Ardhi; na (c) kulinda haki hizo za ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu husika za utoaji na utumizi wa haki za ardhi kwa DPW," ambapo, maneno "haki juu ya umiliki wa matumizi na faida kutokana na ardhi" yamefasiliwa kumaanisha: "haki zote (bila kujumuisha haki za umiliki msingi wa ardhi nchini Tanzania) juu ya ardhi zinazohusiana na uchunguzi, upimaji na tathmini, uchambuzi, ukaguzi, ujenzi, matumizi, umiliki, ugawaji wa udhibiti na starehe (ikiwa ni pamoja na kukodisha, haki za njia, urahisi na haki za kumiliki matumizi ya ardhi) kama inavyohitajika kwa ajili ya kutekeleza Shughuli za Mradi."

(g) Kifungu cha 11(1), kuhusu "utendaji wa haki sawa kwa wote bila ubaguzi," kinachosema kwamba, "Nchi zilizosaini mapatano haya zinakubaliana kwamba mamlaka zinazohusika nchini Tanzania zitafanya kazi ya: (a) kutoza kodi, ushuru, na tozo nyinginezo kwa kampuni ya mradi ya mradi husika, Shughuli za Mradi au watu (ikiwa ni pamoja na wasambazaji au watoa huduma) kwa mujibu wa Mwongozo wa Kifedha uliokubaliwa [katika ibara ya 18]"

(h) Kifungu cha 14(2), kuhusu "hofu ya utaifishwaji wa mali ya mwekezaji," kinachosema kwamba, "Tanzania inakubali kwamba, endapo Serikali ya Tanzania itaamua kufanya utaifishaji, utaifishaji huo utakidhi masharti yafuatayo: (i) hatua za utaifishaji huo zitachukuliwa kwa maslahi ya umma na kwa mujibu wa taratibu za kisheria; (ii) hatua hizo si za kibaguzi; na (iii) hatua za ulipaji wa fidia kwa watu walioathirika zitachukuliwa mara moja, kwa kutumia sarafu madhubuti na ykwa kiwango kinachotosheleza hasara ya mtaji na faida ambayo ingepatikana kama utaifishaji usingefanyika , ambazo fidia hii itatolewa kwa mujibu wa kanuni ambazo zitawekwa katika HOGA husika na Mikataba ya Miradi husika."

(i) Kifungu cha 18(2), kuhusu "kodi, ushuru na malipo mengine," kinachosema kwamba, "(1) Nchi Wanachama zinakubaliana kwamba kodi, ushuru na tozo zingine zitatozwa kwa mujibu wa sheria zilizopo za kodi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na masharti mengine na motisha kama itakavyokubaliwa katika HOGA husika na Mikataba ya Miradi kwa kuzingatia sheria za Tanzania. (2) Motisha wa uwekezaji na misamaha ya kodi, ushuru na tozo zingine (inapohitajika) vitatolewa kwa kuzingatia sheria za kodi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na masharti yatakayokubaliwa katika HOGA husika na Mikataba ya Miradi kwa kufuata sheria za Tanzania."

(j) Kifungu cha 23, kuhusu "urefu na usitishwaji wa mkataba ," kinachosema kwamba, (1) Kwa mujibu wa aya ya 2 ya ibara hii ya 23, Mkataba huu utaendelea kutumika hadi pale itakapotokea mojawapo ya yafuatayo: (i) kusitishwa kabisa kwa shughuli zote za mradi; au (ii) kumalizika muda kwa mikataba yoye ya HOGA na Mikataba yote ya Mradi (pamoja na ya nyongeza yoyote ya muda itakayo fanyika) na utatuzi wa migogoro, ikiwa ipo, kama inavyoelezwa hapochini. (2) ........ (3) Kusitishwa kwa Mkataba huu kutategemea idhini ya awali ya Nchi Wanachama, idhini hiyo haipaswi kuzuiliwa bila sababu. (4) Nchi Wanachama hazitakuwa na haki ya kushutumu, kujiondoa, kusimamisha au kusitisha Mkataba huu katika hali yoyote, hata ikitokea ukiukwaji wa mkataba (material breach), mabadiliko ya kimsingi ya hali, kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia au kibalozi, au sababu zingine zozote zinazotambuliwa chini ya sheria ya kimataifa. Bila kujali yaliyotajwa hapo juu, mgogoro wowote kati ya Nchi Wanachama kuhusiana na hali kama hizo utashughulikiwa kulingana na mahitaji ya Ibara ya 20 ya Mkataba huu.

(k) Kifungu cha 26, kuhusu "kumahalisha mkataba wa IGA," kinachosema kwamba, "Serikali ya kila Nchi Mwanachama itachukua hatua zote zinazohitajika kwa haraka ili kufanya Mkataba huu na mikataba ya HOGA husika kumahalishwa na kutumika chini ya sheria yake ya ndani kama mfumo wa kisheria uliopo kuhusiana na Miradi inayopendekezwa, ikijumuisha, pale inapobidi, kuwasilisha rasimu ya sheria zote wezeshi zinazohitajika, na itatumia juhudi zake zote kupata, haraka iwezekanavyo, kupitishwa kwa sheria wezeshi. Serikali za kila Nchi Wanachama zitafahamishana kwa wakati kuhusu hatma ya sheria hiyo wezeshi."

(l) Kifungu cha 30, kuhusu "kutengamaza mkataba kwa kuyumbisha ukuu wa vyombo vya dola katika nchi mwenyeji (stabilisation clause)," kinachosema kwamba, (1) Nchi Wanachama zinakubali kwamba utulivu wa mazingira ya kisheria na ya kimkataba yanayohusiana na Miradi utadhibitiwa kwa namna ambayo ni yenye kuridhisha kwa Nchi Wanachama na Kampuni ya Mradi. Maelezo ya uimarishaji huo yatakubaliwa kati ya DPW au Kampuni husika ya Mradi na TPA na kuonyeshwa katika mkataba wa HOGA husika. Utulivu huo utatumia tarehe ya kutia saini IGA kama tarehe ya marejeleo ya uimarishaji, ili kushughulikia mabadiliko yoyote katika Sheria au mabadiliko ya kodi yanayoathiri Miradi husika. (2) Tanzania itachukua hatua zote zinazohitajika au zinazofaa kufanya, kutoa au kutekeleza ndani ya eneo lake sheria zote wezeshi na hatua nyingine za kisheria zinazohitajika ili kuwezesha na kutekeleza ahadi zilizoainishwa katika Mikataba ya Mradi na HOGA.

Angalizo muhimu kuhusu maslahi ya Taifa

Maeneo yaliyokolezwa hapo juu na kupigiliwa mistari, yanaashiria dhamira ya serikali ya kuuza mustakabali wa watoto, wajukuu, na vitukuu wa Tanzania kwa wageni.

Hivyo, kulihitajika na bado kunahitajika ufafanuzi wenye kuonyesha serikali imechukua hatua gani hadi sasa, maana hayo ndiyo maeneo yalipingwa na umma mpana, wakiwemo Maaskofu wa TEC. Taarifa hizo hazikutolewa na serikali.

Kwa hiyo, bado ni mapema kutathmini kama vipengele vya mkataba wa awali wa IGA vinavyohalalisha ukoloni mamboleo vimebadilishwa. Hakuna taarifa za kutosha zilizotolewa a serikali kwa ajili ya kuruhusu kazi hii kufanyika.


Hizi ndizo sababu zinazotufanya kutoa wito kwa serikali kuweka bayana maudhui ya mikataba ya IGA iliyorekebishwa, HOGA, LALA, na POCA ili umma uweze kujiridhisha kuhusu mambo haya.

Na hizi ndizo sababu zilizowafanya Maaskofu wa TEC, mnamo tarehe 22 Oktoba 2023, kutoa tamko wakisema kwamba bado hawaungi mkono Mikataba kati ya Tanzania na Dubai.

Tamko hilo lilitolewa na Mwadhama Protase Kardinalu Rugambwa, akiwa huko Vatican, siku mikataba mitatu ikiwa inasainiwa mjini Dodoma, Tanzania.
Msingi wa kikatiba na kisheria wa kupewa taarifa za mikataba ya bandari

Ni muhimu tukumbushane kwamba, madai yetu ya kupewa taarifu kamilifu kuhusu kilichomo kwenye mikataba mitatu iliyosainiwa yanao msingi wa Kikatiba na kisheria.

Tunapenda serikali ielewe kwamba, ibara ya 8(1)(a) inatamka kwamba, kwa kuwa "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii," basi, "wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii";

Kwamba, ibara ya 8(1)(c) inatamka kwamba, kwa kuwa "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii," basi, "Serikali itawajibika kwa wananchi."

Na kwamba, ibara ya 132(5)(f), ya Katiba ya Tanzania (1977) inafafanua “Misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma” kwa kusisitiza umuhimu na ulazima wa “kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali nyinginezo za umma.”

Kwa hiyo, fikra kwamba, sheria za mikataba zinazuia kuwekwa wazi kilichomo ndani ya mkataba, kama alivyotamka Mbossa, hazina uhalali wa kikatiba.

Mbossa alisema kwamba, "mikataba ya kibiashara kati ya DPW na TPA haitolewi hadharani kwa sababu kila mtu ana washindani wake," na kwamba "ukikiuka unaweza kusababisha kuvunja mkabata au kulipa pesa."

Lakini sisi tunachoongelea hapa sio kutoa "hadharani" hiyo "mikataba ya kibiashara kati ya DPW na TPA." Tunaongelea mikataba hiyo kutolewa kwa "concerbed third parties," ambao ni raia wenye nchi chini ya ibara za 8(1)(a), 8(1)(c) na 132(5)(f) za Katiba ya Tanzania (1977), au kwa wawakilishi wao halali.

Kanuni za usiri wa kimataba yote duniani zinatambua uwepo wa "concerbed third parties." Mfano mzuri ni pale mtu anapokwenda hospitalini na kutoa siri za ugonjwa wako kwa daktari.

Watu wa maabara watakaochukua vipimo ni "concerbed third parties" wenye haki ya kujua siri hizo "automatically."

Hicho ndicho tunataka serikali ifanye kwa mujibu wa Data Protection Act, Sheria ya Ukuu wa Nchi Juu ya Maliasili zake, na Katiba ya nchi (1977) na sio vinginevyo.

Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DP World


Kwa mujibu wa tovuti ya Kampuni ya DP Wolrd, ndoto ya Kampuni hii ni "kuongoza biashara zote duniani katika siku za usoni."

Na dhima ya DP World ni kufanikisha ndoto hii kwa "kuwatangulia wengine wakiwa na fikra kuhusu mabadiliko kwa kutumia ubunifu wa kuibua majawabu ya matatizo ya kibiashara huku wakihakikisha mchango endelevu katika uchumi na jamii duniani kote."

Katika muktadha huu, akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba mitatu kati ya Tanzania na Dubai, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wawekezaji na Mkurugenzi Mtendaji wa DP World, Sultan Ahmed Bin Sulayem alisema:

“Tuna heshima kubwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufufua bandari ya Dar es Salaam. Hii inaendana na mipango mkakati ya maendeleo ya Tanzania na ni uthibitisho wa maono ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan."

Sulayem alifafanua kwamba, "Maendeleo hayo yatatoa fursa za kibiashara kwa kanda hii, kuunganisha Afrika Mashariki na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na masoko ya kimataifa, kusukuma ukuaji wa uchumi, kubuni nafasi za kazi, kuimarishwa kwa upatikanaji wa bidhaa na huduma, na kuleta thamani kwa wadau wetu wote.

Pia Sulayem aliongeza kwamba, "Sambamba na bandari zingine tunakofanya kazi, makubaliano haya ya uendeshaji wa bandari yanaashiria hatua nyingine muhimu katika juhudi zetu za pamoja za kuimarisha utaalamu wa kimataifa na wa ndani wa DP World ili kuimarisha shughuli za ugavi katika kanda ya Afrika ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa bara zima".


Baadhi ya wageni katka hafla ya kusaini mikataba ya Dubai

Lakini, pamoja na haya yote, sisi tunaona kwamba, bado safari ya “kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma" ni ndefu sana, na watu wafuatao, waliohudhuria kwenye hafla ya kusaini mikataba mitatu ya Dubai ni mashuhuda kuhusu changamoto hii.

1698152054661.png


1698043769958.png


1698035756523.png


1698035779977.png


1698035805579.png


1698035841638.png


1698035864353.png


1698035887987.png


1698035911106.png


1698043063686.png


1698405420394.png


1698577254238.png


1698042661420.png

Mama Amon,
MKurugenzi Mtendaji Mkuu,
Dawati la Utafiti la Mama Amon (DUMA)
S.L.P P/Bag
"Sumbawanga Town"
Sumbawanga.
 

Attachments

  • 1698074378414.png
    1698074378414.png
    13.8 KB · Views: 4
Back
Top Bottom