Wadau wa Kiswahili wahimizwa kuitangaza lugha hiyo nje ya nchi na kuwa na matumizi fasaha na sanifu

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
VCG41N94261979.jpg

Wikiendi iliyopita yaani tarehe 18 na 19 Machi, lilifanyika Kongamano kubwa visiwani Zanzibar nchini Tanzania ambalo limeshirikisha vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili.

Kongamano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Kikwajuni, Zanzibar lilionekana kufana sana mwaka huu, na kusindikizwa na shamrashamra mbalimbali ambazo zilimalizia kwa usiku wa Waswahili.

Lengo kubwa la kuwakutanisha pamoja wanahabari na watangazaji wa idhaa za Kiswahili ni kujadili fursa na changamoto za mawasiliano ya habari katika maendeleo ya Kiswahili pamoja na kuangalia changamoto za matumuzi ya Kiswahili katika utangazaji ndani ya vituo vya kazi.

Wakati anafungua Kongamano hilo Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alitoa wito kwa washiriki wote kutumia vyema taaluma wanayoipata na kuamini kwamba watajifunza mambo mengi yanayohusu Kiswahili, Utangazaji na uandishi wa habari.

Wahenga wanasema “Mcheza Kwao Hutuzwa”. Ili kukipa Kiswahili thamani inayostahili zaidi duniani, sasa tunaelekea mwaka wa pili tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) litangaze katika Mkutano wake Mkuu wa 41 kwamba ifikapo tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani.

Kiswahili sasa kinaendelea kukuwa na kupanua mawanda yake kila kona duniani. Ni wajibu wa kila Mswahili kuhakikisha kuwa anaitumia vyema lugha hii, tena si kwa waandishi wa habari ama watangazaji pekee bali hata kwa jamii nzima ya Waswahili.

Sasa hivi Kiswahili kimekuwa na fursa kubwa duniani, kwani nikiangalia China pekee bila kutaja nchi nyingine, sasa kuna vyuo vikuu sita ambavyo vinatoa kozi ya Kiswahili, na hii yote ni kwasababu lugha hii ambayo hapo awali Wachina hata walikuwa hawaijui, inaonekana kuwa na fursa nyingi za ajira na kuongeza idadi ya wazungumzaji wake.

Hata hivyo tunasema hakuna kizuri kisicho na kasoro, kwenye Kongamano hilo changamoto zilizojadiliwa hasa na watangazaji wanaotangaza kwenye idhaa za Kiswahili za nje ya Tanzania ni matumizi mabaya na yenye utata ya lugha.

Hivi sasa kumekuwa na wimbi la matumizi mabaya ya Kiswahili, ambalo linapelekea hata wale wageni wanaojifunza kuchanganyikiwa. Kwa watangazaji na waandishi, wao wanaona kuna mapungufu makubwa ya misamiati hasa maneno ya vitu ambavyo havipatikani katika jamii ya Waswahili.

Misamiati inayosumbua zaidi ni ile ya majina ya wanyama, mimea, samaki n.k, lakini hata tofauti ya utamaduni na mifumo ya siasa ya nchi walizopo na zile wanazotoka watangazaji na waandishi pia zinaibua changamoto kubwa.

Mathalan hapa nchini China tunafahamu kuwa sarufi ya Kichina ni ngumu hivyo baadhi ya maneno inakuwa vigumu sana kutafsiri na kupata maana halisi ambayo itaridhisha pande zote mbili yaani Kichina na Kiswahili, hivyo uwepo wa mabaraza kama BAKIZA na BAKITA utasaidia kutoa maelekezo na kuweza kupata maneno mapya ambayo yatakubalika katika pande zote mbili.

Hizo ni baadhi tu ya changamoto ambazo wanakumbana nazo waandishi na watangazaji wa idhaa za za Kiswahili za kimataifa.

Akifunga Kongamano hilo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari na wadau wote wa Kiswahili waweke mkakati wa pamoja wa kuitangaza lugha hiyo nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, kuweka mkakati wa kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa na kuhakikisha kuwa maelezo ya matumizi ya bidhaa yanawekwa kwa Kiswahili.

Mabaraza ya Kiswahili Tanzania BAKIZA na BAKITA yanapaswa kuwa mstari wa mbele na kushirikiana kwa karibu na wadau wa habari wakiwemo wahariri, maana hawa ndio wanaonekana kukipotosha zaidi Kiswahili.

Pia kujitahidi kufanya utafiti hasa kwa misamiati ya maneno au majina ya vitu ambavyo havipatikani kwenye jamii ya Waswahili na kujaribu kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi ikiwemo kuongeza misamiati hiyo kwenye makamusi ya Kiswahili ili wadau wa Kiswahili wasisumbuke sana wanapofanya shughuli zao.
 
Back
Top Bottom