Sijui kuwa mada hii tayari imeshawekwa hapa au la. Kama ishawekwa mnisamehe.
Napenda kuuliza kuwa, hivi maana ya kuwa na matawi ya vyama vya siasa ughaibuni ni nini? Ni harakati gani za kisiasa zinazoendelea katika nchi za watu ambazo zinahitaji kuwa na chama cha siasa humo? Wakati ule wakati nchi nyingi zilikuwa bado zinagombea uhuru, tulishuhudia kuwepo kwa vyama vya siasa nchini mwetu. Vyama hivyo vilikuwa, kwa mfano, FRELIMO, ANC, MPLA, ZANU,ZAPU, SWAPO, PAC, PLO na kadhalika. Vyama hivyo vilikuwepo Tanzania kwa sababu haikuwezekana kuwa na harakati za kisiasa nchini mwao. Walipewa kibali na serikali ya Tanzania kuwepo kwa vyama humo nchini.
Je haya matawi yanayofunguliwa ughaibuni yana malengo gani? Ni jinsi gani wanachama wake wanaweza kushiriki katika siasa nyumbani? Watanzania tuishio ughaibuni kwa kiasi kikubwa hatuwezi kushiriki katika mambo ya kisiasa yanayoendelea nyumbani, hii ni pamoja na kupiga kura. Hivyo binafsi, sioni maana ya kuwa na matawi haya. Kama kungekuwa na uwezekano wa waishio ughaibuni kupiga kura, maana ya matawi anagalau ingekuwepo.
Watanzania wengi, tukiwa nje ya mipaka yetu, kitu kinachotujumuisha wote ni Utanzania wetu. Kitendo hiki cha umoja na undugu wa Watanzania unawashangaza wengi, hasa Waafrika wa nchi zingine ambao hawana umoja kama sisi. Mara nyingi tunaulizwa, 'je yule ni ndugu yako, mlikuwa mnafahamiana zamani'? Wakijua ndio kwanza mmekutana huwa wanashangaa, na jibu wanalopata ni, 'Sisi ni Watanzania.' Hapo ndipo wakati ambapo najivunia kuwa Mtanzania.
Kwa maoni yangu naona kwamba kuanza kuwepo kwa matawi ya vyama vya kisiasa ughaibuni kutaanza kuleta mgawanyiko kwa Watanzania waishio huku. Hata siku moja sijawahi kusikia au kuona kama kuna matawi ya Republicams, Democrats, Labour, Conservatives, CDU au Forza Italia katika nchi zingine! Au huu ni mtindo mpya wa siasa za kimataifa ambao unahamishia siasa za ndani ya nchi, kwenda nchi zingine? Ikumbukwe kuwa, nauliza tu.