Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

SEHEMU YA 19

Hakukuwa na majibu yoyote yale, simu ilikuwa ikiita tu lakini haikuwa ikipokelewa. Alishindwa kujua kulikuwa na tatizo gani lakini kila alipofikiria kwamba alikwenda kumpokea Mchungaji Mark, alihisi kwamba mwanaume huyo huyo alikuwa bize katika kufanya mazungumzo na mchungaji.

Muda ulizidi kusogea, mpaka inaingia saa tisa usiku wa manane bado majibu yalikuwa yaleyale. Hilo kidogo likaanza kumtia hofu na kitu kimoja na cha kwanza kilichomjia kichwani mwake ni kwamba Cassian alikuwa amepata ajali mbaya.

Akahisi mwili wake ukipigwa ganzi, hakutaka kuona hilo likitokea, kitu alichokuwa akikihitaji ni kuona akifunga ndoa naye na hata kama angepata ajali na kufa, basi kitu hicho kitokee wakati wakiwa ndani ya ndoa.

“Mpenzi nina wasiwasi,” alisema Evelyne, alikuwa amempigia simu Mwajuma.
“Wasiwasi wa nini tena?”
“Cassian. Aliondoka kwenda kuonana na Mzungu ambaye ndiye atakuwa mchungaji wa kesho. Hajarudi mpaka sasa hivi,” alisema Evelyne.

“Aliondoka saa ngapi?”
“Tangu saa tatu usiku!”
“Mmh! Lakini usijali! Inawezekana kaenda sehemu kunywa. Si unajua wanaume,” alisema Mwajuma.

Maneno ya rafiki yake huyo hayakumuingia kichwani, bado alikuwa na hofu kwa kuhisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea upande wa pili.

Muda ulizidi kusogea, hakupata usingizi, ilikuwa ni heri kukosa kitu chochote kile lakini si kuikosa ndoa ambayo iliutesa moyo wake, ndoa ambayo aliamini piga ua ilikuwa ni lazima kuyabadilisha maisha yake.

Ilipofika saa kumi na moja na kuona kimya, hakutaka kuendelea kubaki hospitali, haraka sana akatoka na kuanza kwenda katika hospitali zilizopo karibu, alihisi kwamba mwanaume wae huyo alikuwa huko. Alikwenda kwenye hospitali tatu lakini huko hakufanikiwa na ndipo akapata wazo la kwenda nyumbani kwa Cassian.
 
SEHEMU YA 20

Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani hapo. Hali aliyoikuta ikamtia hofu, nje kulikuwa na walinzi kadhaa waliokuwa na bunduki, hakujua sababu ya watu hao kuwa mahali hapo, kitendo cha wao kuwa hapo kikampa majibu kwamba kulikuwa na tatizo, inawezekana Cassian alikuwa amekamatwa na polisi.

“Unakwenda wapi wewe mwanamke?” aliuliza mlinzi mmoja huku akimsogelea Evelyne.
“Naingia kwangu!”
“Humu kwako?”
“Ndiyo!” alijibu huku akimwangalia mlinzi yule.
“Nyumba yako hii?”

“Ni kwa mume wangu mtarajiwa, na leo tunafunga ndoa!” alijibu Evelyne kwa mbwembwe zote, alikuwa akimwangalia mlinzi huyo kwa jicho la dharau, jicho lililoonyesha moyo wake kusema ‘nikiingia ndani utanikoma mshenzi wewe’.

“Wewe si ndiye Evelyne?”
“Ndiyo!”
Wale wenzake waliokuwa pembeni waliposikia jina hilo, nao wakajisogeza kule alipokuwa msichana huyo na kumwangalia. Evelyne alishangaa, hakujua kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, akahisi kulikuwa na tatizo.
“Hutakiwi kuingia humu!” alisema jamaa mwingine.

“Siruhusiwi kuingia humu?”
“Ndiyo!”
“Na nani?”
“Huyo unayejidaia ni mpenzi wako!”
“Cassian?”
“Ndiyo!”

“This is insane! I gonna get inside,” (huu ni uwendawazimu! Inabidi niingie ndani) alisema Evelyne kwa Kiingereza cha harakaharaka.

“No! You have to leave!” (hapana! Unatakiwa usepe) alisema mwanaume mwingine, hakuishia hapo, akaanza kukoki bunduki yake.

Mara ya kwanza msichana huyo alifikiri ni utani lakini baada ya kuwaona watu hao wakimwangalia huku wakionekana kumaanisha walichokuwa wakimwambia, akahisi kabisa hapo hakukuwa na utani wowote ule.

Akanywea ila kitu pekee kilichomjia kichwani ni kwa sababu gani Cassian hakutaka aingie ndani.
Akaona hilo halitoshi, akawaomba walinzi hao wamuitie mlinzi wa kila siku nyumbani hapo, hilo halikuwa tatizo, mlinzi huyo akafika na kuanza kuzungumza naye.

“Jamaa ndiyo aliagiza usiingie ndani! Hata huu ulinzi umeongezwa kwa ajili yako,” alisema mlinzi huyo kitu kilichompelekea Evelyne kuhisi kama akimwagiwa maji ya baridi kabisa.
 
SEHEMU YA 21

Machozi hayakutaka kusubiri, hapohapo yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake, akaanza kusikia maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, alihisi kwamba alikuwa ndotoni akiota kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

Hiyo ilimaanisha kwamba Cassian hakutaka kuwa naye, ilimaanisha kwamba hakukuwa na ndoa tena, yaani alichwa siku ya harusi. Lilimuumiza moyoni, alitamba sana kwamba alikuwa akienda kuolewa, mitandaoni, gumzo lilikuwa ndoa hiyo, kila kona ilizungumziwa harusi hiyo.

Akarudi ndani ya gari, kabla ya kuondoka akalalia usukani, mbele yake akayaona maisha yake yakiwa yamejaa giza, hakujua sababu iliyomfanya Cassian kuchukua uamuzi ule na wakati mpaka mara ya mwisho mwanaume huyo alipokuwa akiagana naye alionyesha sura ya tabasamu, penzi zito lilionekana kupitia macho yake, sasa iweje abadilike ghafla hivyo?

Akaanza kuifikiria mitandao ya kijamii, alitumia kiasi kikubwa cha pesa kutamba huko, kama kila mtu alikuwa akijua kwamba alikaribia kufunga ndoa na mwanaume huyo siku hiyo ilimaanisha kwamba hata hapo alipoachwa kwenye mataa basi kila mmoja angejua kwamba ameachwa solemba.

Alilia sana, hakutaka kumpigia simu Mwajuma na kumwambia, alichokifanya ni kuwasha gari na kumfuata huko. Mawazo juu ya Cassian yalikuwa makubwa mno, hakuamini kama kweli mwanaume huyo alimuacha katika kipindi kigumu kama hicho.

Aliendesha gari huku akiwa na mawazo hayo ya kuachwa yakimsumbua kichwani mwake. Kila alipokuwa akipita na kupishana na watu, aliona kama wote hao tayari walijua kama aliachika.

Alipofika Sinza Makaburini, akakata kulia ambapo aliendesha mpaka katika nyumba moja iliyokuwa na wanawake wengi kwa nje, akasimamisha gari na kuwafuata wanawake hao, akawasalimia na kuingia ndani.

Alikijua chumba alichokuwa akikaa Mwajuma, moja kwa moja akaelekea mpaka katika chumba hicho na kugonga, mlango ukafunguliwa na msichana huyo ambapo baada ya kumuona tu, akaanza kulia.
 
SEHEMU YA 22

Mwajuma alishangaa, ilikuwa ni asubuhi sana hata kutoka ndani hakuwa ametoka, alijiuliza sababu ya msichana huyo kulia namna hiyo, alionekana kuumia, alionekana kuwa na kitu moyoni mwake, ilikuwaje alie kwa uchungu namna ile na wakati siku hiyo ilikuwa ni ysiku ya kufunga ndoa na bilionea mkubwa Afrika Mashariki.

Alijaribu kumbembeleza anyamaze lakini Evelyne hakunyamaza, alikuwa akilia mfululizo, tena kilio kikali kilichojaa kwikwi. Aliendelea kulia kwa dakika ishirini nzima ndipo akanyamaza na kuanza kumwambia Mwajuma kilichokuwa kimetokea.

“Haiwezekani!” alisema Mwajuma huku akimwangalia rafiki yake huyo.
“Ameniacha! Cassian ameniacha,” alisema Evelyne huku kila wakati akiyafuta machozi.

Huo ndiyo ulikuwa ukweli, aliumia mno moyoni mwake, kilichokuwa kimetokea hakukiamini, aliona kila kitu kilichokuwa kikiendelea kama ndoto fulani ambapo baada ya dakika chache angeshtuka kutoka usingizini.

Hawakujua sababu ya Cassian kuchukua uamuzi wa ghafla namna hiyo kwani usiku uliopita tu alikuwa na furaha tele na alimuonyeshea msichana huyo mapenzi yote, sasa iweje abadilike namna hiyo?

“Au ile meseji uliyomtumia ndiyo chanzo?” aliuliza Mwajuma.
“Hapana! Haikumfikia?”

“Una uhakika? Kwako ilionyeshaje? Kama meseji haikwenda inakuonyeshea kwa kuweka kialama chekundu, sasa kama ile ilikwenda, kwa nini kialama hakikuonekana?” aliuliza Mwajuma maswali ambayo yalianza kumpa jibu Evelyne.

“Mmh!”
“Nahisi meseji aliipata ila aliifuta na hakutaka kukuonyeshea dalili zozote zile!” alisema Mwajuma huku akimwangalia msichana huyo.
“Inawezekana!”

“Kwa hiyo utafanyaje?”
“Nimeaibika Mwajuma. Cassian ameniumiza. Kwa pesa nilizokuwa nazo kwenye akaunti yangu, nitazitumia hata zote kumuua mwanamke yeyote atakayekuwa naye, kama kuumia, na yeye aumie kwa kumuua msichana ampendaye!” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na hasira kali.

“Wewe tu! Na mimi nitakusaidia. Ukiua kwa kisu, nitaiweka maiti kwenye gunia, sitokuacha ila huyu mbwa lazima tumkomeshe,” alisema Mwajuma huku naye akionekana kuwa na hasira sana kwani mafanikio ambayo angeyapata rafiki yake yangekuwa sawa na mafanikio yake.
 
Sio hatupendani huyo ana hasira za kuachwa na acha avune tu alichopanda alifanya dhambi sana kumsingizia baba wa watu bora angemwambia ukweli tatizo lake
Kinachosikitisha ni kwamba...

Evelyne na rafiki yake wanachotaka kumfanyia Cassian... kwamba kila mwanamke atakayekua nae watamtoa roho... kweli wanawake hampendani kabisa...


Cc: mahondaw
 
Back
Top Bottom