Kaburi bila Msalaba

Kaburi bila Msalaba

Wakili wa shetani

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2022
Posts
2,131
Reaction score
4,008
Renew Premises_page-0001.jpg

I Mumbi ahojiwa

Asubuhi, Siku ya Ijumaa, jua lilitokea mapema na kufukuza baridi kali iliyopenya hata ndani ya mifupa ya mahabusu. Askari alipofungua mlango, mahabusu wote walitoka nje na kuota jua waliolingojea kwa muda mrefu. Hata na inzi nao walikuwa wanalingojea, na wao vile vile walitoka nje na kuliota. Mumbi alimwona inzi mmoja akitafuta chakula, na kwa macho yake akamfuata kila alipokwenda. Hata hivyo hakuwa akifikiri habari yake, kwani fikira zake zilikuwa juu ya njaa aliyoisikia tumboni mwake.

Mumbi alipokuwa akiota jua, huku akiwatazama inzi na kufikiri vile alivyokuwa na njaa, Chifu na askari wake walifika. Yeye hakuwaona mpaka Chifu alipomwuliza, "Je wewe jina lako ni nani?"

Mumbi aliinua kichwa chake na kumtazama Chifu huku akijibu, "Mumbi," "Umekula viapo vingapi?" Chifu akamwuliza.

Mumbi hakujibu. Aliinama na kutazama chini. Akiwekelea mkono wake wa kushoto juu ya tumbo lake, alianza kuumauma kucha za mkono wake wa kulia.

"Nimekuuliza umekula viapo vingapi?" Chifu akauliza tena. Askari wake waliomlinda Chifu po pote alipokwenda, walianza kuonyesha hasira walipoona kwamba Mumbi hakumjibu Chifu. Maina, mmoja wao, alianza kushikashika kiboko cha ngozi ya kifaru, alichokichukua kila mahali walipokwenda. Chifu na askari wake walikitumia kiboko hiki kwa kuwapiga wale watu walioshitakiwa kuwa ni wafuasi wa Mau Mau. Kwa mara ya tatu Chifu alimwita Mumbi tena, "Msichana we!"

"Humm," Mumbi akajibu.

"Umekula viapo vingapi?"

Mumbi aliona kwamba Maina alikuwa tayari kumchapa kiboko dakika yoyote. Hapo aliyakumbuka majeraha aliyoyaona miilini mwa mahabusu wengine waliokuwa wamepigwa. Aliogopa 'asije naye akapigwa vile. Kwa sauti ya chini akajibu, "Sikula."

Chifu kusikia hivyo alifyatuka kwa ukali na hasira akasema, "Sikula! Wafikiri tulikuleta hapa bila kujua kwamba umekula kiapo? Ninataka uniambie upesi ni viapo vingapi umekula, ama sivyo utaona wanachopata Mau Mau wengine."

Mumbi hakusema neno lolote. Alisimama tu kimya, huku akiuma kucha zake. Moyoni alijua hakuwa na lolote la kufanya, ila alijua kwamba hata kama akisema amekula au hajala kiapo, ilikuwa sawa tu. Alikumbuka rafiki yake Nyaguthii. Yeye alikubali kwamba alikuwa amekula viapo viwili. Aliwataja wote waliomlisha na wale waliokula pamoja naye. Lakini hata hivyo, alihukumiwa na kutiwa korokoroni huko Kamiti kwa muda wa miaka minne. Alipokuwa huko alipigwa na askari wa jela mpaka akafa, lakini watu wa jela wakasema alikufa baada kuugua.

Alikumbuka vile vile yaliyompata Maciira. Yeye alikuwa kijana aliyesoma mpaka darasa la kumi. Sura na tabia zake ziliwapendeza watu wote wa Lokesheni yake. Lakini Chifu alimchukia sana. Alifikiri pengine angepewa kazi ya uchifu badala yake. Kwa sababu hii, aliwachukua Maciira na vijana wengine rafiki zake, na kuwapeleka mpaka karibu na msitu wa Kabaru. Walipofika mahali palipokuwa na miti mikubwa, aliwaambia, "Hii ndiyo nchi mnayoipigania. Tokeni sasa mwende mkaishi huko."

Maciira na wenzake walikataa kutoka, na hapo Chifu akawaamrisha askari wake wawatoe kwa nguvu, kutoka juu ya motokaa. Waliposhuka chini, Chifu aliwapiga risasi na kuwauwa papo hapo. Huko kijijini, aliwaambia watu kwamba Maciira na wenzake walikuwa wakijaribu kutoroka kuelekea msituni kwa hivyo askari wakalazimika kuwapiga risasi na kuwauwa. Hakuna mtu aliyethubutu kutokubaliana na habari hii, kwani angefanya hivyo, yeye vile vile angefanyiwa kama wao.
Mumbi alisimama kimya. Chifu naye akamtazama kila sehemu ya mwili wake. Aliona vile uso wake ulivyokuwa umenyooka. Nywele zake ndefu zilikuwa zimesokotwa zikawa mfano wa nanasi. Miguu yake nayo ilikuwa mirefu na yenye kupendeza. Kusema kweli Mumbi alikuwa mzuri kweli kweli. Chifu hakuweza kujua kwa nini msichana mzuri kama vile amekula kiapo cha Mau Mau.

Moyoni alikata shauri kwamba angefanya lolote mpaka kumfanya Mumbi ageuze nia zake, na ikiwezekana, awe mmoja wa wasichana wengi waliokaa hapo kambini wakiwapikia, na mara wakitembea na Chifu na askari wake.

Mumbi naye alikuwa akifikiri jambo jingine. Moyoni alikuwa amekata shauri kwamba hata ikitokea nini hatasema amekula kiapo. Alijua akikubali kwamba amekula kiapo, ni lazima atasema ni nani aliyemlisha, na ni watu gani wengine waliokula kiapo pamoja naye. Alikumbuka usiku wa manane, na wenye giza, usiku ambao yeye, mama yake, na wasichana wengine walipokula kiapo. Alimkumbuka vile vile mpenzi wake Maciira, ambaye ni nyumbani mwao walimolia hicho kiapo. Alijua akikubali kuwa amekula kiapo, ni lazima angewatia taabuni wote waliokula kiapo siku hiyo. Alipofikiri hali ya mama yake vile alivyokuwa mnyonge kwa kuugua mifupa, alikata shauri kuwa kufa au kupona, hangekubali kuwa amekula kiapo.

Baada ya kuhojiwa hivi kwa muda bila yeye kusema kama kwamba amekula kiapo, Chifu aliwaamrisha askari wake wamshike Mumbi na kumpeleka mpaka kambi ya Githunguri. Mumbi aliposikia hivyo machozi yalianza kumtoka bila yeye kupenda.

Kambi ya Githunguri ilijulikana sana katika nchi nzima. Kati ya watu watatu waliopelekwa hapo, ni mmoja tu aliyerudi hai, na yeye vile ilikuwa ni lazima awe amevunjwa mguu, mkono au afanywe kutokuwa mwanamume tena.

Kambi ya Githunguri ndipo alipoishi Waiwai, kijana wa kizungu ambaye alikuwa mnyama kuliko vile alivyokuwa mwanaadamu. Wote waliopelekwa kwake, wakishitakiwa kula kiapo, aliwapiga risasi papo hapo. Waliokuwa na bahati, aliwapiga kwa kiboko mpaka wasijijue wenyewe.

Mumbi aliposikia kwamba atapelekwa Githunguri, alikufa moyo kwa hofu. Mwili wake ulianza kutetemeka, na machozi yakazidi kumtoka. Ingawaje, alizidi kukazana kwamba hatakubali kuwa amekula kiapo. Hata kama akiuawa, hatasema kamwe kwamba amekula. Kwa moyo mshupavu aliwafuata Maina na askari wengine wawili na wote wakaelekea upande wa Githunguri.

Kila askari alivaa fulana nyekundu yenye mikono mirefu na hali shingoni imefungwa kamba iliyofungiwa filimbi. Kiunoni walijifunga mshipi wenye upana wa inchi mbili hivi, wenye rangi nyeusi. Wote walivaa suruali fupi za kaki zilizofuliwa na kunyooshwa sawa sawa. Miguuni walivaa viatu vya buti vyenye rangi nyeusi na juu yake wakafunga patisi. Kichwani walivaa kofia ndogo nyeusi ambazo hapo upande wa mbele palitiwa nishani iliyoandikwa "On Her Majesty's Service," yaani "Katika Utumishi wa Malkia."

Askari wote walijiona wamevalia vizuri sana. Hii ilikuwa ni kweli kwa sababu watu wengine wote walikuwa wachafu na wamerarukiwa na nguo zao sana. Watu wote, waume, wake na watoto, walikuwa ni lazima kukaa vijijini mwao bila kutoka nje. Wakati huu walikuwa wameishakaa pale kwa karibu mwezi mzima. Wote walikuwa wameishakula chakula chote, na kutumia pesa zote walizokuwa nazo hapo mwanzo. Hata senti za kununua sabuni hawakuwa nazo. Maji yenyewe walikubaliwa kuteka mara moja tu kwa juma nzima, huku wakilindwa na askari. Haya ndiyo yaliyokuwa chakula chao.

Askari tu ndio waliopata chakula, maji na pesa za kununua sabuni. Hata na nguo walizipata bure kutoka serikalini. Wao tu ndio waliopata nafasi ya kuoga, kula na kulala vizuri. Hali hii iliwavutia wasichana wengine, na ikawa kwamba kila askari aliweza kujipatia wake wachanga zaidi ya mmoja. Huko vijijini, wake hawa walipewa jina la "Wake wa Hali ya Hatari." Wengine ambao hawakuolewa, walipewa jina la "Rarua" kwa vile walizoea kurarua chapati nyumbani mwa askari.

Ingawaje, kulikuwako na wasichana wengine kama Mumbi, ambao walichukia sana hali hiyo ya kutangatanga, katika kambi za askari. Ingawa walijua kwamba vijana waume walikuwa wengine wameishaingia misituni, wengine wamehamishwa, na wengine wameuawa, wao waliona ni lazima kungoja mpaka hali ya Hatari iishe. Walitumaini vijana marafiki zao watarudi, na hata wasiporudi, pengine wangepata vijana wengine wazuri na ambao wangependana. Kwa kutumaini hivi, walikaa tu nyumbani mwa mama zao, huku wakila taabu kama watu wengine. Hawakupenda kamwe kupoteza sifa zao.

Wasichana kama hawa walichukiwa sana na askari, na yeyote kati yao aliyeshitakiwa kwamba amekula kiapo, aliteswa sana.

Maina na wenzake walichukua kila mmoja bunduki ya .303, ambayo ni bunduki kubwa na iwezayo kutupa risasi mbali. Mau Mau walipenda sana bunduki hii, na kila walipopata nafasi, waliwashambulia hawa askari na kuwanyang'anya hizo bunduki. Kijana Mzungu aliyeongoza kikundi cha Askari Walinda Nyumba, aliwaonya sana wazichunge bunduki zao. Lakini askari wengi waliposhambuliwa na Mau Mau waliona ni heri kutupa bunduki wakijua kwamba Mau Mau wakishapata bunduki hawatawafuata tena.

Soma na Pakua vitabu ndani ya maktaba.co.tz

Itaendelea. . .
 
2 Jani la maji


Safari ya kutoka Konyu kwenda Githunguri ilianza kama saa tano za asubuhi. Jua kali la mwezi wa Januari liliwachoma sana askari na mahabusu pamoja. Kwa vile askari ndio waliovalia fulana zenye joto, wao ndio, walioisikia joto zaidi. Walitokwa na jasho usoni hata na mwilini, hivi kwamba walitembea pole kwa kuchoka.

Pamoja na Mumbi palikuwako na wazee wengine wawili na kijana mmoja. Wote walikuwa mahabusu na wote walikuwa wameshitakiwa kwa kula kiapo. Yule kijana alikuwa ameshitakiwa sio tu kwa kula kiapo lakini vile vile kwa kulisha kiapo na kuchukua bunduki. Haya yalikuwa mashtaka mabaya sana, maana yeyote aliyeshitakiwa na kuhukumiwa kwa makosa kama hayo, alikuwa ni lazima kunyongwa au kufungwa jela zaidi ya miaka kumi. Huyo kijana alijua hana la kufanya na asipopata njia ya kutoroka ni lazima atahukumiwa. Watu wengi watoto waume na wake, walikuwa wamesema kwamba ni yeye aliyewalisha kiapo. Hata ingawa hii ilikuwa ni kweli, hakukubali alipoulizwa na Chifu, kama kwamba alijua chochote juu ya kiapo.

Njiani walipokuwa wakisafiri kuelekea Githunguri, askari mmoja alitangulia mbele akifuatwa na mahabusu, ambao nao walifuatwa na askari wawili nyuma. Kila mmoja wao alikuwa amechoka kwa jua kali. Walipofika Tegu kijito kidogo kilicho karibu na kijiji cha Gikumbo, wote walikaa chini na kuanza kunywa maji. Hawakuwa na kikombe cha kutekea maji. Mahabusu walilala chini na kunywa maji kama ng'ombe. Maina na askari hawakufanya hivyo. Maina alimwambia Mumbi, "Nenda kaniletee jani la kunywea maji."

"Nikalitoe wapi?" Mumbi akauliza.

"Nikalitoe wapi?" Maina akarudia kwa hasira. "Kwani huna macho ?"

"Nenda kule ng'ambo shambani ukalikate."

Maina mwenyewe hangethubutu kuingia shambani kukata jani. Aliogopa pasiende pakawa na Mau Mau wamejificha hapo ndani. Lakini yeye hakujali kitu hata Mumbi akiwakuta. Fikirani mwake Mumbi alikuwa mtu asiye na maana, kwanza kwa sababu alimfikiria kuwa mfuasi wa Mau Mau na tena kwa sababu alikataa kuwa rafikiye.

"Unajivuna hivi kwa sababu wewe ni rafiki wa Mau Mau?" Maina akaendelea. "Ngoja utaona. Hakuna mtu aliyekula kiapo atakayeponyoka."

Mumbi hakusema lolote. Alijua akisema Maina huenda akampiga. Aliona heri anyamaze kimya na kufanya kama alivyoambiwa. Aliruka mto na kuingia shambani akaanza kukata jani la kunywea maji.

Huko shambani mahindi, maharagwe, ndizi, miwa, na viazi vyote vilimea pamoja. Ilikuwa rahisi sana kwa watu kujificha hapo ndani bila kuonekana. Kwa vile watu hawakukubaliwa kulima, mashamba yao kwa mwezi mzima, majani mengi yalikuwa yamemea na kulifanya shamba liwe kama kichaka.

Mumbi aliingia hapo shambani kama alivyoamriwa. Majani mengine yaitwayo "mshika kondoo" yalishikilia miguu na nguo zake. Yeye hakujali kwani alikuwa tu akitazama kila upande huku nafsi yake ikimwambia labda palikuwa na mtu hapo ndani. Alikata jani upesi na akaanza kuvuka mto kurudi kwenye wale wengine. Lakini kabla hajaruka, askari mwingine alimwambia amletee jani na yeye pia. Mumbi alirudi tena shambani na kukata jani la pili.

Mara tu alipoinama kukata jani, alisikia huko ndani sauti ndogo ya majani yaliyokauka. Upesi alitupa macho hapo mbele yake, na mara tu akaona mtu amemkodolea macho makali kama ya mnyama. Nywele zake ndefu ambazo zilifika mpaka mabegani, zilikuwa zimesukwa kama zile za wasichana. Nguo zake zilikuwa zenye uchafu na zimeraruka. Aliketi akapiga goti kwa mguu wake wa kulia, na mguu wake wa kushoto umesimama. Mkononi alishika bunduki tayari kumpiga Mumbi.

Mumbi alishituka sana alipomwona lakini hata hivyo hakutoa sauti yoyote. Alijisikia kama amekwisha kufa na hata sauti haingeweza kutoka. Yule mtu alimtazama tu bila kufunga macho. Mumbi naye alimtazama, na wote wawili wakatazamana. Hajui walisimama kwa muda gani katika hali hii, lakini alisikia hawezi kugeuka wala kukata jani. Alilishika tu huku akiitazama bunduki iliyolengwa kuelekea kwake.

Ilikuwa kama saa sita na nusu. Maina alifungua radio yake ndogo aliyoichukua kila alipokwenda, na mara sauti kutoka katika radio ikasema, "Kikundi cha askari polisi kutoka katika kituo cha polisi cha Niana, kilitupiwa risasi na magaidi wa Mau Mau karibu na mto Hombe. Na wao waliwatupia risasi lakini hakuna aliyejeruhiwa. Magaidi walitoroka na kuingia msituni.

"Kikundi cha magaidi kilishambulia kijiji cha Marigi huko pande za Fort Hall, na kuchukua mtu na mke wake, pamoja na askari wanane wa Kulinda Nyumba. Mtu na mkewe walitoroka lakini askari waliuawa. Maiti zao zilionekana maili tatu kutoka hapo kijijini.

"Kikosi cha askari wa K.A.R. kilikuta kimengojewa na kundi kubwa la magaidi wa Mau Mau upande wa Embu karibu na kijiji cha Ena. Magaidi hao ambao walichukua bunduki zitoazo risasi mfululizo, walikimbia askari wa K.A.R. walipowatupia risasi.

"Bwana Nicholson alihukumiwa kulipa faini ya shillingi mia tano, kwa kuacha bunduki ndani ya motokaa bila kufunga sawasawa, motokaa yake. Baada ya dakika tano tu alirudi na kukuta imeishaibiwa.

"Mjaluo mmoja kwa jina la Ondiek Okong'o alifikishwa mbele ya Hakimu wa Kisumu na kushitakiwa kuwa mshiriki wa Mau Mau. Alikiri makosa yake akahukumiwa kifungo cha miaka saba kufanya kazi ngumu.

"Mkikuyu mmoja alikutwa amenyongwa na magaidi karibu na shamba la Bwana Davis huko upande wa Nanyuki.

"Kikosi cha askari wa K.A.R. kilikutana na magaidi karibu na kijiji cha Gikumbo upande wa Fort Hall. Baada ya kutupiana risasi magaidi walitoroka. Yafikiriwa mmoja wao alipigwa risasi na kujeruhiwa ingawa hakupatikana."

Habari hii ilipokuwa ikitangazwa, Maina na askari wengine walisikiliza hata wakasahau kwamba Mumbi alikuwa bado hajarudi. Wao walifikiri kwamba hata na yeye alikuwa akisikiliza. Wote walishituka waliposikia jina la kijiji cha Gikumbo likitajwa. Gikumbo kilikuwa nusu maili kutoka mahali walipokuwa. Ilikuwa yawezekana kwamba magaidi hao walikuwa karibu tu na wao. Fikira kama hizi ziliwafanya kuogopa sana hata zikamfanya Maina kukumbuka kwamba Mumbi alikuwa ng'ambo ya mto. Alimtazama na kwa sauti yenye ukali akamwambia, "Haraka twende."
. . . .
 
Back
Top Bottom