SEHEMU YA 28
Aliwakata mapanga wanaume wengi, walimuogopa na kumuona Naseku kama ukoma, hakukuwa na mtu aliyemsogelea. Naseku alimwambia hilo Cassian lakini hakutaka kujali, hakutaka kusikia kitu chochote kile, kwake alichokuwa akikitaka ni kuzungumza na msichana huyo tu.
Wakati Naseku akiwa amepeleka ndoo ya maji ndani, mara Oscar akaanza kuonekana kwa mbali, kama kawaida yake alikuwa akija kwa kasi ya ajabu, alikwishatoa onyo kwamba hakutaka kumuona mwanaume yeyote nyumbani kwao, kitendo cha kumuona Cassian alijua kabisa alifika nyumbani hapo kwa ajili ya dada yake tu.
Alipomfikia Cassian, hakutaka kuuliza alikuwa nani, akalipandisha shati lake, akatoa panga. Watu wote waliokuwa wakimuona wakajua kabisa kwamba Oscar hakuwa akitania, hakuwa na historia ya kurudisha panga pasipo kufanya kazi.
Cassian alibaki akimwangalia mwanaume huyo aliyeonekana kuvimba kwa hasira. Hapohapo akamrushia Cassian panga, bila kukwepa lilikuwa likimpiga kichwani.
“Umekwepa! Unajiona ninja!” alisema Oscar na kuanza kumsogelea tena, kitendo cha Cassian kukwepa panga lake ilionekana kuwa kama dharau kwani tangu awe mtemi wa mtaa, hakukuwa na mtu aliyewahi kulikwepa panga hilo.