SEHEMU YA 13
“Kama ni furaha, muonyeshee, usimfanye ashtukie kitu chochote kile, halafu huo ujumbe wake ulioingia, ufute. Halafu kesho nitakupeleka katika hospitali ya swahiba wangu akakufanyie vipimo tena,” alisema Osman.
“Sawa. Nitashukuru!”
Hicho ndicho alichoambiwa, hakutaka kuonyesha tofauti yoyote ile. Hakutaka kuondoka muda huo, alikaa mpaka ilipofika usiku ambapo akajiandaa na kuelekea nyumbani.
Alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbatia Evelyne kwa furaha tele, alimletea unafiki, hakuonyesha tofauti yoyote ile machoni mwake, kama ilivyokuwa juzi na jana ndivyo ilivyokuwa siku hiyo kiasi kwamba msichana huyo akahisi hakukuwa na jambo lolote baya na inawezekana ujumbe ule haukuenda, na kama ulienda basi hakuuona.
Wakati Cassian akiwa amekwenda bafuni kuoga, haraka sana Evelyne akachukua simu ya mpenzi wake huyo na kuanza kuangalia. Akaenda sehemu ya meseji na kuangalia katika uwanja wa kuwasiliana naye, hapo, hakukutana na ujumbe wowote mpya kuonyesha kwamba kumbe meseji hakuwa ameipata.
Kidogo moyo wa Evelyne ukarudi kwenye amani, furaha ambayo ilikuwa imepotea ikarudi tena. Cassian alipomaliza kuoga, akarudi chumbani, akamnyanyua Evelyne na kumtupa kitandani ambapo akaanza kumvua nguo moja baada ya nyingine na kuanza kufanya mapenzi.