Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

SEHEMU YA 15

Evelyne alikuwa na presha kubwa, alitaka kuona akifunga ndoa na mwanaume huyo bilionea ili aweze kufanikisha ile adhma yake aliyokuwa ameipanga. Alimpigia simu Mwajuma na kumwambia kwamba alitaka harusi yake iwe bab’kubwa hivyo kuendelea kuwaambia watu wengine.

Akaona hiyo haitoshi, akazungumza na waandishi wa habari wa mitandaoni na magazetini, aliwalipa kiasi kizuri cha pesa kwa ajili ya kutangaza harusi hiyo ambayo ingefanyika siku ya Jumamosi inayofuatia.

Waandishi hao na wale waliokuwa na kurasa zao katika mitandao yao wakaanza kuwataarifu watu wengi kwa kuposti matangazo kuhusu harusi hiyo kubwa ambayo ilitarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Ni ndani ya siku chache tu, gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii ilikuwa harusi hiyo, kila mtu alitaka kuona ni kitu gani kingetokea kwani kwa jinsi ilivyokuwa ikitangazwa kwenye mitandao hiyo, kila mmoja akahisi kwamba ingekuwa harusi kubwa na ya kifahari hata zaidi ya ile ya Beckham alipomuoa Victoria.

“Hii harusi kiboko! Inafungwa ndani ya boti!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushtuka sana, hakuamini kama kungekuwa na Mtanzania ambaye angeamua kufunga ndoa ndani ya boti ya kifahari badala ya kanisani.

“Kaka hiyo ni pesa. Unachotakiwa ni kuiamkia pesa, hilo tu,” alisema jamaa mwingine.

Wakati hayo yote yakiendelea, Cassian hakuwa na furaha hata kidogo, alikuwa mtu wa mawazo tele, alipokuwa akikaa ofisini kwake, hakuamini kama Evelyne angemfanyia mambo kama yale aliyomfanyia lakini wakati mwingine alibaki akimshukuru Mungu kwa muujiza alioufanya.

Alikuwa na kila kitu, alikosa mtoto tu, alikata tamaa kwa kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kila kitu lakini mwisho wa siku daktari akabainisha kwamba hakuwa na tatizo lolote lile kitu kilichomfanya kumshukuru Mungu sana.

Mapenzi yote aliyokuwa nayo kwa Evelyne yakaanza kupotea na chuki kuanza kuingia moyoni mwake.

Alihitaji kuwa peke yake, alihitaji kuwa na msichana mwingine, asingeweza kuendelea kukaa na msichana huyo, alitaka kumuondoa maishani mwake na kumuingiza mwanamke mwingine.
 
SEHEMU YA 16

Alimuumiza mno, hakutaka kumuacha hivihivi pasipo kumuumiza kama alivyokuwa amefanya.

Alipanga kumuacha siku moja kabla ya kufunga ndoa. Alijua jinsi Evelyne alivyokuwa akihaha huku na kule kuhakikisha kwamba harusi inafungwa haraka iwezekanavyo hivyo alichokitaka ni kumuumiza kwa kukataa kumuoa msichana huyo.

Akapanga na Osman kila kitu ambacho walitakiwa kufanya, ilikuwa ni lazima Cassian apange kwenda kulala na msichana huyo hotelini siku moja kabla ya kufunga ndoa hiyo halafu amtelekeze hukohuko na kuondoka hotelini hapo, hilo wala halikuwa tatizo lolote lile, wakapanga hivyo na kukubaliana na mwanaume huyo kwamba hicho kilitakiwa kufanyika haraka sana.

Bado Cassian hakutaka kuonyesha tofauti yoyote kwa Evelyne, alimuonyeshea mapenzi ya dhati kwamba bado alikuwa akimpenda mno, kila alipokuwa naye, uso wake ulikuwa na tabasamu pana na muda wote alikuwa akikenua japokuwa moyoni mwake kulikuwa na maumivu makali.

Hakuacha kumsisitiza msichana huyo kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alimharakisha sana kwani siku zilibaki chache na kama asingeweza kukamilisha kwa kipindi kifupi basi kila kitu kingeharibika.

“Waandishi umewaandaa kuja harusini?” aliuliza Cassian huku akimwangalia mpenzi wake huyo.

“Ndiyo! Tena niliwasiliana na waandishi wa habari wa BBC nao wamesema watakuja,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha tele.

“Safi sana. Nakupendea hapo tu. Hakuna mwanaume asiyependa kuwa na mwanamke mwenye kasi ya kufanya mambo kama wewe mpenzi,” alisema Cassian, hapohapo akamvuta msichana huyo na kumkumbatia.

Uso wake ulikuwa tofauti na kile kilichokuwa moyoni mwake, alikuwa na hasira kali, alimchukia mno msichana huyo japokuwa hakutaka kumuonyeshea ni jinsi gani alikuwa na chuki kali dhidi yake.

“Nakupenda mpenzi!” alisema Cassian huku akimwangalia Evelyne usoni.
“Nakupenda pia mume,” alisema msichana huyo.

Siku ziliendelea kukatika, ilipofika Ijumaa, Cassian akampigia simu Osman na kumwambia kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kufanya mpango waliokuwa wameupanga.

Akamwambia kwamba kila kitu walichokuwa wamekubaliana kilikuwa juu ya mstari na kilichobaki kilikuwa ni wajibu wa kufanya hicho walichokuwa wamepanga.
 
Kwahiyo ndio ukaamua kuniumiza macho
Ahsante Shunie ila riwaya za aina hii huwa sizipendelei sana mimi mambo yangu ni kama ya malkia sandarus ama brian na helo na za upelelezi
hizi huwa naona kama zinanichosha
 
SEHEMU YA 17

Ilipofika majira ya saa moja usiku, Cassian akampigia simu Evelyne na kumwambia kwamba siku hiyo walitakiwa kulala hotelini ili asubuhi wajiandae na harusi iliyokuwa imepangwa kufanyika siku hiyo.

Hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa alimwamini sana Cassian na aliamini kwamba hakuwa akifahamu kitu chochote kile, akaondoka nyumbani na kuelekea katika Hoteli ya Twiga iliyokuwa Masaki na kukutana huko.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kukumbatiana kwa furaha, wakaenda bafuni kuoga, walipomaliza, wakatupana kitandani na kuanza kuvuana nguo.

Akilini mwa Evelyne aliyaona mapenzi mazito ya mwanaume huyo, aliamini kwamba kusingekuwa na mwanamke yeyote ambaye angemtoa katika ulimwengu wake.

Walipomaliza kufanya mapenzi, simu ya Cassian ikaanza kuita, alipoliona jina la Osman wala hakujiuliza, akaipokea simu ile na kuanza kuzungumza naye.

“Umekwishafika? Ndiyo...ni kesho...ooh! mchungaji ndiyo amefika! Umempeleka hoteli gani? Serena...safi sana...anataka kuniona...basi sawa nakuja...” alisema Cassian na kukata simu.

“Nani?”
“Osman! Anasema kwamba mchungaji Mark ameingia kutoka Ufaransa! Hivyo anataka nikamuone mara moja,” alisema Cassian.

“Sawa. Ila usichelewe kurudi mpenzi!”
“Usijali!” alisema Cassian, hakuishia hapo tu, akamvuta Evelyne na kumbusu mfululizo kisha kuondoka.

Msichana huyo akabaki na amani moyoni mwake, hakuamini kama kweli siku inayofuata ndiyo ilikuwa ya kufunga ndoa na kuwa mke halali wa mwanaume huyo.

Alikuwa na tamaa ya utajiri, alijitahidi kuficha siri ambayo hatimaye alijua ndiyo ilikuwa imedumu pasipo kugundulika mpaka hapo alipokuwa akitaka kufunga naye ndoa.

Hapohapo akampigia simu Mwajuma, akajisifia sana kwamba alikuwa mwanamke wa shoka aliyemkamata vilivyo Cassian na mwisho wa siku kutaka kufunga naye ndoa huku akiwa amemdanganya vya kutosha kuhusu kuzaa watoto.

“Shoga kesho ndiyo naanza safari! Nikitoka hapo, ni kuleta vituko, akiniacha kesi inakwenda mahakamani tunagawana utajiri,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha ya ajabu.

“Jamani shoga mpaka nakuonea wivu! Unakwenda kuuchukua ubilionea hivihivi!” alisema Mwajuma.
“We acha tu! Ndiyo tayari nishatajirika!” alisema Evelyne.
 
SEHEMU YA 18

Cassian akashuka mpaka chini ya hoteli, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka mahali hapo. Mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa mlinzi wa nyumbani kwake, akamwambia kwamba Evelyne hakutakiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo na kama angemruhusu kuingia basi angemchukulia maamuzi magumu mno.

Mlinzi huyo hakuleta ubishi, alimheshimu bosi wake, tena baada ya kuona kwamba mlinzi mmoja asingetosha, Cassian akapiga simu mpaka katika kampuni ya ulinzi ya Knight na kuwaambia kwamba alihitaji ulinzi wa watu watano nyumbani kwake ambapo bila tatizo lolote walinzi watano waliokuwa na bunduki wakaelekea huko.

“Osman upo wapi?” aliuliza Cassian.
“Nyumbani!”
“Hebu twende Albert Lounge tukale bata kidogo!” alisema Cassian huku akiendesha gari kwa kasi kuelekea Albert Lounge. Msasani kwa ajili ya kuonana na mshikaji wake huyo.

**** Muda ulikuwa ukisonga mbele, msichana Evelyne alikuwa ndani ya chumba cha hoteli, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu Mwajuma na kuzungumza naye, alikuwa akimtambia kwamba hatimaye alikuwa akienda kufanikiwa kwa kile alichokuwa amekipanga.

Cassian alikuwa na utajiri mkubwa, makampuni mengi ambayo aliamini kwamba kama wangekuwa mume na mke kisha kuachana basi akaunti yake ingesoma zaidi ya bilioni kumi za Kitanzania.

Hakuwa radhi kuona akikikosa kiasi hicho cha pesa na ndiyo maana alipambana kuhakikisha anaolewa na kufanya uchafu huo akiwa ndani ya ndoa.

Hapo chumbani, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi, alitaka kuona kila kitu kikienda harakaharaka kama alivyokipanga, alitaka kuona asubuhi ikiingia, aende saluni na mpambe wake na baadaye aende kwenye boti ambayo walitakiwa kufungia ndoa.

Aliiamini simu aliyopigiwa Cassian na kuambiwa kwamba tayari mchungaji kutoka nchini Ufaransa alikuwa amekwishaingia nchini na kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni kufunga ndoa tu.

Pale chumbani hakutulia, kila wakati alikuwa akiishika simu yake na alipoona muda unazidi kwenda na mwanaume wake harudi chumbani hapo, akaanza kumpigia simu.
 
Back
Top Bottom