SEHEMU YA 10
Hakutaka kugundulika, hivyo akachukua miwani yake ya jua na kuvaa kisha kuanza kupiga hatua kwenye sehemu ya kulia chakula ambayo ilikuwa maarufu Kinondoni nzima kwa kupika ugali mzuri na nyama ya kuchoma.
“Karibu bwana. Umebadilika! Hiyo miwani kama komando,” alisema Osman, ndiyo ilikuwa kawaida yake, kila walipokuwa wakikutana, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtania kutokana na muonekano wowote aliokuwa nao.
Wakakaa na kuagiza chakula. Macho ya Cassian hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule, hakuonekana kujiamini, swali lililokuwa kichwani mwake ni nini kingetokea mahali hapo kama tu watu wangegundua kwamba alikuwa yeye.
Wakati akiangalia macho yake huku na kule, yakatua usoni mwa msichana mmoja, mrefu kidogo, msichana aliyekuwa na sura nzuri, kifua kidogo huku uso wake tu ukiwa na tabasamu la asili.
Cassian akabaki kimya, akamwangalia msichana huyo kwa muda. Aliuona uzuri wake lakini tatizo kubwa alilokuwa nalo ni umasikini uliokuwa ukimwandama.
Alibalia khanga moja iliyoonekana kuchoka, kwa ndani alikuwa na gauni lake refu na blauzi ya rangi nyekundu.
Japokuwa alionekana kuwa masikini kwa muonekano wake tu lakini msichana huyo alikuwa mchangamfu mno, aliongea na wateja kana kwamba alikuwa akimjua kila mtu.
“Mbona unamwangalia sana Naseku?” aliuliza Osman mara baada ya kumuona rafiki yake akimwangalia sana msichana huyo.
“Naseku! Ndiye nani?”
“Si huyo msichana unayemwangalia. Ngoja nimuite aje kutuhudumia,” alisema Osman na hapohapo kumuita msichana huyo.
Bila hiyana, huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana Naseku akaanza kupiga hatua kuelekea kule walipokuwa wanaume hao. Macho yake Cassian hayakutoka kwa msichana huyo, alikuwa akimwangalia mpaka alipofika mahali pale.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu, alisahau kwa muda kwamba nyumbani alimuacha msichana ambaye kila siku alimwambia kwamba alikuwa akimpenda kuliko wanawake wote katika dunia hii.
“Naseku! Kutana na mshikaji wangu huyu,” alisema Osman huku akimtambulisha Cassian kama rafiki yake. Cassian alipovua miwani na kumwangalia vizuri msichana huyo, Naseku akashtuka.