Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

Sehemu ya 101

Aliteremka, baada ya dakika tano, akafanikiwa kufika chini kabisa huku akiwa hoi. Hakusimama, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea sehemu iliyokuwa na parking ya magari ambapo hapo akaliona gari kubwa la takataka likiwa limefika hapo kwa kuondoa taka usiku huo.

"Nitakwenda nalo hilihili," alisema Edmund na kuingia ndani ya gari hilo ambapo kulikuwa na mifuko mingi myeusi, akaichambua na kujificha katikati ya mifuko hiyo na kutulia.

"Nahisi nitaondoka salama mahali hapa," alijisemea huku akiendelea kujichimbia zaidi.

*** Watu walijaa katika Uwanja wa Ndege wa JFK uliokuwa jijini New York nchini Marekani.

Watu wote waliokuwa mahali hapo walitaka kuwaona mapacha walioungana ambao walikuwa na vipaji vya aina yake, Walter na Walker waliokuwa wameiteka dunia kwa kipindi hicho.

Watu waliwaona sana kwenye televisheni, walitaka kuwaona tena na tena. Walijua kwamba siku chache zilizopita walikuwa nchini humo kabla ya kwenda nchini Tanzania, siku hiyo walitaka kuwaona zaidi, kwa wale ambao hawakuwahi hata kuwagusa, walitaka kuwagusa na hata wale ambao hawakuwa wamesainiwa vitabu vyao, walitaka kuona hilo likitokea.

Muda wote watu hao walikuwa wakiangalia saa zao, waliambiwa kwamba ndege hiyo ingewasili mahali hapo majira ya saa tisa jioni lakini cha ajabu, kila mmoja aliona kama muda ulikuwa umefika ila watu hao hawakuwa wameingia nchini humo.

“Jamani! Mbona wanachelewa hivi?” aliuliza msichana mmoja huku akiangalia saa yake, ndiyo kwanza ilikuwa saa 8:17 mchana lakini waliona kama saa tisa ilikuwa imekwishafika.

Uwanjani hapo hawakuwa peke yao, walikuwa na Waziri Mkuu, Bwana Gordon na mkewe ambao nao walitaka kuwaona mapacha hao ambapo kila kona duniani walikuwa wakizungumziwa wao tu.
 
Sehemu ya 102

Dakika zilizidi kwenda mbele na ilipofika majira ya saa tisa jioni, ndege ndogo ya kukodi, Flight 1789 WC ikaanza kuonekana angani, watu wakaanza kujiandaa kwani walijua fika kwamba hiyo ndiyo ilikuwa ndege iliyokuwa imewabeba watu waliokuwa wakiwasubiri uwanjani hapo, ndiyo ilikuwa ndege iliyowabeba watu waliowafanya kuacha shughuli zao na kufika uwanjani hapo.

Ndege ikasimama na watu hao kuanza kuteremka, kila mmoja akaanza kupiga kelele za shangwe, waandishi wa habari waliokuwa na kamera zao wakaanza kusogea kule ndege ile ilipokuwa na kuanza kupiga picha kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

Kila mmoja alitaka kuwagusa, hakukuwa na kipindi ambacho walinzi walipata wakati mgumu kama kipindi hicho. Ni kama shughuli zote za ndege zilikuwa zimesimama mahali hapo kwani kitendo cha kuwaruhusu watu kuingia katika ardhi ya uwanja wa ndege tu ilikuwa shida tupu.

“Please Walter! Sign my book,” (naomba usaini kitabu changu Walter!) alisema msichana mmoja huku akikiweka kitabu chake mbele.

Kila mmoja kipindi hicho alitamani kuwa karibu na watu hao, kila mmoja alitaka japo kuguswa na mapacha hao. Hakukuwa na mtu aliyetamani kuwaona watu hao wakiondoka pasipo kufanya jambo lolote lile kwa ajili yako.

Kwa kuwa kila mmoja alikuwa na kiu nao, walichokifanya ni kusaini vitabu vyao na kisha kuingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo.

Bi Naseku na mumewe, Cassian walikuwa hawaamini walichokuwa wakikiona, hawakuamini kama vijana wao walikuwa mastaa kiasi hicho, walifurahi, muda mwingine walikuwa wakimshukuru Mungu kwani waliamini kwamba bila watoto wao kuungana namna hiyo basi wasingekuwa mastaa kama walivyokuwa.

Wakafikia katika Hoteli ya Nyota Saba ya 3 Pyramids iliyokuwa hapo New York. Chumbani, kila mmoja alikuwa na furaha, mbali na umaarufu waliokuwa nao lakini pia walikuwa na utajiri mkubwa wa dola milioni 600 katika akaunti yao.

“Shindano no keshokutwa! Nini cha kufanya baada ya hapo?” aliuliza Walker huku akimwangalia ndugu yake.
 
Sehemu ya 103

“Ni kurudi Tanzania! Baada ya hapo, tutafanya mambo mengine mengi,” alisema Walter.

“Na vipi kuhusu Catherine?”
“Nitamuoa. Ila nitaona siku ukioa, tutafunga ndoa pamoja. Umekwishapata msichana wa maisha yako?” aliuliza Walter.

“Bado.”
“Na vipi kuhusu Jackline? Bado hujafikiria kumtafuta?”
“Bado! Ila kuna siku nitamtafuta.

Kuna mambo mengi sana. Kuna mchoro nitahitaji kuuchora, wa yule msichana Patricia!” alisema Walker.

“Yupi? Nikuumbushe!”
“Tuliyekutana naye kwenye ndege. Umemsahau?”
“Ooh! Yule Mfaransa?”
“Yeah! Ninatamani sana nimchore kisha nimtumie. Ni msichana mzuri sana.

Kiukweli nimetokea kumpenda,” alisema Walker huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Safi sana. Sema naye.”

Japokuwa alikuwa amekutana na wasichana wengi wauzri lakini Walker alikuwa amekufa na kuoza kwa msichana mmoja tu, Patricia ambaye alikutana naye ndani ya ndege katika kipindi walichokuwa wakitoka nchini Tanzania kwenda Marekani.

Alizoeana na msichana huyo na mara nyingi walikuwa wakichati, walikuwa wakizungumza mengi na kushauriana mambo mengi mazuri.

Hakukuwa na mtu aliyemwambia mwenzake, kila Walker alivyotaka kufanya hivyo, alijiona akishindwa kabisa na kitu pekee ambacho aliamini kwamba kingezungumzia hisia zake juu ya msichana huyo kilikuwa ni kumchora tu.

Alikuwa na mawazo tele, hakumfikiria rafiki yake wa utotoni, Jackline ambaye hakujua kipindi hicho alikuwa wapi, mtu pekee aliyekuwa akimfikiria sana alikuwa msichana Patricia tu.

Alimwambia ndugu yake, alitamani sana kuona akiwa na msichana huyo zaidi na zaidi ili hata kama ingetokea siku ndugu yake, Walter angekuwa anaona, basi waweze kuoa pamoja.

“Ukichelewa, nitaoa kabla yako!” alisema Walter.

“Huwezi kuoa kabla yangu. Tutaoa pamoja. Wala usijali,” alisema Walker huku akiwa na uhakika wa kumpata msichana huyo.
 
Sehemu ya 104

Maisha yalikuwa tofauti, kile alichokuwa amekifanya hakikuleta matokea chanya, akawa mtu wa kuhangaika huku na kule.

Edmund alikuwa ndani ya gari la takataka, alifunikwa na taka hizo na kulisikia gari likianza kuondoka mahali hapo.
Hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akiishi maisha hayo ya digidigi, yaani kisa mapenzi tu leo hii alikosa amani kabisa, na mbaya zaidi kile alichokuwa amekikusudia hakikuwa kimetimia.

Alijuta lakini wakati mwingine aliamua kusonga mbele, alikuwa tayari kuendelea kuishi hivyo na ndiyo maana alikuwa ameondoka kuelekea nchi nyingine kabisa kwa kuamini kwamba angekuwa salama hapo Wales.

Aliikumbuka familia yake, alimkumbuka mpenzi wake, aliwakumbuka marafiki zake, kila kitu alichokiacha nyuma yake huo ndiyo ulikuwa wakati wa kukikumbuka.

Safari ille iliishia katika sehemu iliyokuwa na jumba kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na eneo maalumu pa kuchomea takataka.

Wakati gari likiwa limesimama kwa lengo la watu kuja kutoa takataka, naye akatoka na kuanza kuelekea sehemu iliyokuwa na mlango mkubwa wa kutokea.

Hakukuwa na watu wengine, humo ndani, watu waliokuwa na zamu ya kuleta gari hilo ndiyo waliokuwa wakiingia humo kwa ajili ya kuzichoma moto taka hizo. Alipofika nje ya jengo lile, akaanza kupiga hatua kuelekea mitaani.

Hapo palikuwa Stonford Pelrr, sehemu iliyokuwa karibu na pori dogo la kutengenezwa la Jumanji.

Alitembea kwa mwendo wa haraka katika kipori hicho mpaka alipofika sehemu iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kucheza.
Alichoka, alihitaji muda wa kupumzika, pale, hakukuwa na mtu yeyote, palikuwa pamefungwa kwa muda, akayafuta mabenchi yaliyokuwa mahali hapo na kutulia.

Moyo wake ulikuwa na mawazo tele, hapo alipofika, akatamani kuwasiliana na wazazi wake, alitaka kuwaomba msamaha kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea kwani hakuwa amekusudia bali kulikuwa na nguvu kubwa iliyokuwa imemuingia ambayo ilimuongoza kufanya jamboo la kipumbavu kama lile.
 
Sehemu ya 105

Akaichukua simu yake iliyokuwa mfukoni mwake ambayo aliizima kitu kiitwacho location na kuizima kabisa, akaiwasha na kuanza kumpigia simu baba yake ambapo baada ya sekunde chache, simu ikapokelewa.
“Baba! Aliita baada ya simu kupokelewa!
“Edmund! Upo wapi?”

“Nimeondoka nyumbani. Baba! Naomba unisamehe, nimefanya jambo la kijinga sana, ninajutia kile nilichokifanya, naomba unisamehe, najua umeumia, sikuwa na cha kufanya, nilifanya hivyo kwa kuwa nilihitaji kulilinda penzi langu, nilimpenda sana Catherine, sikuwa na sababu ya kumpoteza na ndiyo maana niliamua kufanya hayo yote kwa kuamini kwamba ningeweza kulilinda penzi langu kwake,” alisema Edmund huku akitokwa na machozi ya uchungu, aliusikia moyo wake ukichomwa na kitu chenye ncha kali.

“Pole sana. Usijali! Upo wapi?”
“Nimeondoka! Nimekuja huku....” alisema Edmund lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akasikia vishindo vya watu wakija kwa kasi kule alipokuwa, hapohapo akageuka, macho yake yakatua kwa polisi waliokuwa na bastola viuononi mwao na virungu mikononi mwao.

“Mikono juu! Weka mikono tuione vizuri,” alisema polisi mmoja huku wakimsogelea, hapohapo Edmund hakuwa na jinsi, akaiachia simu na kunyoosha mikono juu huku machozi yakimtoka.

“Halo...halo..” ilisikika sauti ya baba yake kwenye simu. *** Kiuhalisia huo ulionekana kuwa mwisho wa Edmund, alinyanyua mikono yake hewani huku akiwa na hofu kwamba hatimaye alikuwa amekamatwa na polisi waliomfikia hapo bustanini na kumnyooshea bastola huku wakimtaka kutulia kama alivyokuwa.

Baba yake aliyekuwa upande wa pili aliendelea kuita pasipo mafanikio yoyote yale. Polisi wale wakazidi kumsogelea, walipomfikia, wakamuweka chini ya ulinzi na kumuuliza maswali juu ya kitu alichokuwa akikifanya mahali pale.
"I was looking for my wife," (nilikuwa namtafuta mke wangu) alisema huku akilala chini.

Walikuwa na taarifa ya mtu aliyejulikana kwa jina la Edmund kutafutwa nchini Uingereza lakini hawakujua kama yule waliyekuwa naye ndiye kijana aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
 
Sehemu ya 106

Mahali hapo kulikuwa na mwanga hafifu hivyo hata walipomwangalia usoni iliwawia vigumu sana kugundua kwamba alikuwa yeye na maneno ambayo aliwaambia kwamba alikuwa akimtafuta mke wake yaliwafanya kumuonea huruma kwamba alikuwa kwenye matatizo makubwa.

"Where is she?" (yupo wapi?)
"She came here with my son, I don't know where they are!" (alikuja hapa na mwanangu, sijui wapo wapi) alisema Edmund huku akiwa amelala chini, sauti yake kwa jinsi ilivyosikika ilikuwa ni kama ya mtu aliyetaka kulia.
"Did you try to call here?" (ulijaribu kumpigia simu?)

"I tried many times but I didn't reach her!" (nilimpigia mara nyingi lakini sikumpata) alijibu.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza, ni mara nyingi watu waliokuja wakija mahali hapo walikuwa na malalamiko mengi kuhusu kupotea kwa watoto wao na hata mume na wake zao.

Kitendo cha Edmund kuwaambia hivyo, hapohapo wakamfungua pingu na kumuweka kwenye benchi.
Hakutaka kugundulika hivyo kujifanya kulia huku akiuinamisha uso wake.

Alijifanya kuwa kwenye tatizo kubwa kiasi kwamba wote wawili wakaanza kumuonea huruma kwa kuona kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa kwenye matatizo makubwa hivyo kuhitaji msaada.
Wakamwambia achukue simu yake, akajiandikia namba na kupiga.

Simu haikuwa ikipatikana, akawaambia polisi kwamba namba haikuwa ikipatikana hivyo alitakiwa kurudi nyumbani kuona kama mkewe huyo alikuwa amefika nyumbani.

Hawakuwa na jinsi, wakamruhusu, akaondoka mahali hapo kinyonge. Polisi wale walibaki wakimsinidkiza kwa macho mpaka alipopotea na kutokomea zake huku akiwa amenusurika kukamatwa na polisi hao.

Moyoni mwake akajiona kuwa na bahati, alimshukuru Mungu zaidi na zaidi kwamba alimuokoa kutoka katika mikono ya polisi hao.
Alipofika barabarani, akasubiri basi la abiria na kuondoka mahali hapo.

Alipokuwa akielekea, hakuwa akipafahamu, basi liliendelea mpaka alipofika sehemu ambapo alihisi ndiyo mwisho wa basi hilo, akateremka na kuelekea katika kitu kupumzika. Wakati akiwa hapo, simu yake ikaanza kuita. Haraka sana akaipokea.
 
Sehemu ya 107

"Edmund...You are a superstar," (Edmund...wewe ni supastaa mkubwa) alisikika mwanaume aliyekuwa upande wa pili.
"How?" (kivipi?) akajifanya kuuliza.

"I see you in my television! You about to win an Oscar award!" (nakuona kwenye televisheni yangu, unakaribia kutwaa Tuzo ya Oscar) alisikika mwanaume wa upande wa pili.
Huyo alikuwa rafiki yake wa karibu, Mark aambaye mara nyingi sana walikuwa wakitaniana pasipo kujua ni kwa namna gani mtu fulani alikuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha yake.

Baada ya kumtania ndipo akauliza kilichokuwa kikiendelea, Edmund hakutaka kumficha, alimwambia kwamba kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni ndicho kilichokuwa kimetokea hivyo kutaka msaada kwani alikuwa nchini Wales.
"Hakuna tatizo! Ngoja nimpigie mjomba wangu akusaidie kukupokea," alisema Mark.

Hilo halikuwa hata tatizo, kipindi hicho kitu alichokuwa akikihitaji Edmund ni msaada wa hali na mali kwani ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba anaondoka salama na kwenda mbali kuishi maisha yake. Mark akawasiliana na mjomba wake huyo ambaye alimwambia kuhusu rafiki yake aliyekuwa akihitaji msaada mkubwa.

Akamwambia sehemu alipokuwa kisha kumpigia simu Edmund na kumwambia juu ya msaada aliokuwa akiuhitaji kupatikana. Akamshukuru rafiki yake huyo na kumsubiri mjomba huyo ambaye aliingia hapo baada ya dakika kadhaa.
"Wewe ndiye Edmun?" aliuliza mjomba huyo.

"Yeah! Ndiye mimi!"
"Ingia twende!"
Hakuwa na hofu yoyote ile, akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo.

Kidogo moyo wake ukawa na furaha mno, akaamini kwamba kwa kitendo cha rafiki yake huyo kuwasiliana na mjomba wake na hatimaye kumsaidia, kwake ilimfanya kumuona Mark mtu wa maana mno.

Hawakuchukua dakika nyingi wakafika mahali kulipokuwa na nyumba chache ambapo hapo ndipo alipokuwa akiishi huyo mjomba, wakateremka na kuingia ndani, akamuonyesha chumba cha kulala na kumwambia kwamba kuanzia siku hiyo angelala mahali hapo mpaka pale ambapo angetaka kuondoka mwenyewe.
"Nashukuru sana!" alisema Edmund, akaingia ndani na kupumzika.
 
Sehemu ya 108

Mjomba aliyeitwa Vonn alitulia sebuleni. Kitendo cha kwenda kumpokea Edmund na kumuona, hakuamini kabisa kama huyo ndiye alikuwa yule mwanaume aliyetakiwa kwenda kumpokea.
Alimjua, hiyo haikuwa mara ya kwanza kumuona, alimuona kwenye televisheni na kipindi chote hicho mwanaume huyo alikuwa maarufu mkubwa, alionekana kwenye kila kituo cha televisheni huku kukiwa kumetolewa donge nono la pesa ambalo angepewa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake.

Sebuleni hakutulia, alikuwa akihangaika, moyo wake ulikuwa ukifukuta, hakutulia, alitamani sana kuwa mwaminifu kwa Mark lakini kila alipokuwa akizikumbuka zile pesa alizokuwa ameahidiwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake, udenda wa tamaa ukamtoka.

"Ni pesa nyingi sana! Hizi zitanifanya kutoa mizigo Ujerumani na kuileta hapa kuendelea na biashara zangu! Siwezi kuziacha pesa hizi," alijisemea huku akiwa sebuleni hapo.

Hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima kwenda kituo cha polisi na kutoa taarifa kwamba mwanaume aliyekuwa akitafutwa kila kona alikuwa nyumbani kwake. Akaelekea chumbani, akabadilisha nguo zake, kila kitu alichokuwa akikifanya chumbani humo aliona akifanya taratibu sana kwani alitamani kuondoka haraka sana na kuelekea polisi na kutoa taarifa juu ya mwanaume huyo aliyekuwa chumbani.

Alipomaliza, hakutaka kuchelewa, hapohapo akaelekea sebuleni, akachukua simu yake, akaufuata mlango, alipoufungua tu, macho yake yakakutana na bunduki zaidi ya kumi zilizoshikwa na wanaume waliokuwa wamevalia mavazi meusi ambapo usoni mwao walikuwa wameficha sura zao na kwa nyuma kukiwa na gari lililoandikwa S.W.A.T.

"Don't movie! Hands on your head," (usitingishike! Mikono kichwani mwako) alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya chini ambayo hakutaka mtu yeyote ndani asikie chochote kile, hapohapo Vonn akafanya kama alivyoambiwa.
"Where si he?" (yupo wapi?) aliuliza.

"Who?" (nani?)
"Edmund!"
"Who is that?" (ndiye nani huyo?) aliuliza huku akiwaangalia wanaume hao.

Hawakutaka kumwambia ukweli, walichokifanya ni kuanza kuelekea ndani kwa ajili ya kumtafuta mwanaume huyo huku wakiwa na uhakika kwamba alikuwa humo.
 
Sehemu ya 109

Vonn alibaki pale mlangoni, hakuamini kilichokuwa kimetokea, ilikuwa watu hao wajue kama Edmund alikuwa nyumbani kwake na wakati hakumwambia mtu? Wakati mwingine alihisi kwamba Mark alikuwa amewataarifu polisi kwamba mwanaume huyo alikuwa nyumbani kwake.

Zile pesa zilizokuwa kichwani mwake, zikaanza kupotea na kuona kuwa hao polisi wangemuona Edmund ambapo wangemchukua na kuondoka naye bila yeye kupata kitu chochote kile kwani hakuwa ametoa taarifa kama mwanaume huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo.

"Freeze...freeze...frezeeeeee..." ilisikika sauti za watu hao huko ndani.

Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 110

Patricia alikuwa msichana mrembo aliyekuwa akiishi katika Jiji la Lyon nchini Ufaransa.

Alikuwa msichana mwenye mchanganyiko wa rangi, sura ya kitoto na kila alipokuwa akitabasamu au kucheka vishimo vilionekana mashavuni mwake kitu kilichomfanya kuonekana mzuri maradufu.

Katika kipini ambacho alikuwa na mapacha walioungana kwenye ndege alikuwa akitoka Dubai kuelekea nchini Marekani.

Walikutana ndani ya ndege na kuzungumza na Walter, kwa jinsi alivyokuwa akiwaona kila siku katika mitandao ya kijamii na hata magazeti, kitendo cha kuonana nao na kuzungumza pamoja kilimchanga.

Alifurahi na mwisho wa siku kupiga nao picha. Hakutaka kuondoka pasipo kuwaomba namba ya simu, alipoomba, mtu wa kwanza kabisa kutoa alikuwa Walker. Alichukulia kila kitu kuwa kawaida japokuwa kwa upande mwingine alijiona kuwa mtu mwenye bahati kubwa mno.

Aliwajua masupastaa, walikuwa watu waliojiona, walioishi maisha yao ambapo hawakuwa radhi kutoa namba zao za simu. Kwa Walker, alishangaa, ilikuwaje mwanaume huyo awe mwepesi kumpa namba ya simu, kuweka ukaribu kitu ambacho kilionekana kuwa kama ndoto katika maisha yake.

Njia nzima alikuwa akijibaraguza kwa Walker, walikuwa wakizungumza mambo mengi huku Walter akiwa amechuna kabisa, yeye alikuwa bize na Catherine aliyekuwa katika upande mwingine kabisa.

Ndege ilipofika Marekani, akateremka huku akimwambia Walker kwamba kesho yake alitakiwa kuondoka kuelekea Ufaransa alipokuwa akisoma ambapo huko ndipo alipokuwa akiyaendesha maisha yake.

Kitendo cha kubadilishana namba za simu kikawafanya kuwasiliana mara kwa mara. Walker alijua kuzungumza na mwanamke, alijua kusifia, alijua kubembeleza kitu kilichomfanya Patricia kujiona kama malkia wa mbingu aliyeshushwa duniani kwa bahati mbaya.

“Unajua kama wewe ni mzuri sana?” aliuliza Walker kwenye simu.
“Mmh! Mimi?”

“Ndiyo! U mzuri sana. Kama ungekuwa gari, basi wewe ungekuwa Lamborghini au Ferrari,” alisema Walker.
“Mmh! Una maneno wewe!”
 
Sehemu ya 111

“Kweli tena. Nilipokuona kwa mara ya kwanza, moyo wangu ulibabaika, nilishindwa kukuangalia mara mbili. U mzuri sana, unapokasirika, uzuri wako haupotei, unapokuwa kimya, bado u mzuri mno, unapokasirika, uzuri wako unazidi kuonekana maradufu.

Patricia, hivi ulizaliwa muda gani?” aliuliza Walker baada ya maneno mengi yalimfanya msichana huyo kutabasamu kila wakati.

“Hahah! Unanichekesha!”
“Sidhani kama ulizaliwa hospitalini! Nahisi ulizaliwa supamaketi, tena karibu kabisa na friji lililokuwa na chokolate.

U mrembo sana, sina mtu wa kukufananisha nawe,” aliendelea kusema Walker huku akichukua maneno mengi kutoka katika Kitabu cha Romeo And Juliet kilichoandikwa na mwandishi wa Kiingereza, William Shakespear.

“Walker! Hujakutana na wazuri!”
“Nimekutana nao, ila moyo wangu umekukubali zaidi wewe! Unajua kutabasamu, unajua kuringa, unajua kupetika, kwa kifupi wewe ni malkia wa nyuki, acha kidume niwe mtafuta maua.”
“Hahah! Nashukuru sana!”

“Hebu rudia tena! Nataka niisikie sauti hiyo tena!” alisema Walker huku akitoa kicheko cha mbali kabisa.

“Kwani sauti yangu ipoje?”
“Hebu rudi kwanza. Kidogo tu!”
“Niambie kwanza ikoje!”
“Jamaniiiii! Rudi basi mpenzi! Rudia basiiiii...”

“Nashukuru!”
“Patricia, nimekwambia una sauti nzuri sana, kwa sauti yako ina uwezo wa kulifungua daraja la London, kwa sauti yako ina uwezo wa kuufanya mnara wa Eifel jijini Paris ukapinda na hata kuanguka,” alisema Walker.

“Hahah! Utanifanya nisikie aibu!”
“Hakuna bwana! Unajua nashindwa kuvumilia, nashindwa kuongea lolote lile. Nahitaji nikuchore, picha moja matata sana,” alisema Walker.

“Kweli?”
“Haswaa! Nitakuchora. Haiwezekana nikutane na msichana mrembo kama wewe halafu niache kumchora. Patricia, ninakupenda mno!” alisema Walker huku simu ikiendelea kuwa sikioni mwake, Waltr alishindwa kuzungumza lolote lile kwani kwa jinsi ndugu yake alivyokuwa akiendeshwa kwa nguvu kubwa ya mapenzi, hata kwake ilikuwa hivyohivyo.

Walizungumza mengi, Patricia akajisikia raha moyoni mwake, alipenda kupendwa, alijihisi kuwa msichana aliyekuwa na bahati kubwa mno maishani mwake.
 
Back
Top Bottom