Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

SEHEMU YA 94

Waliwaulizia lakini madaktari hawakutaka kuzungumza kitu chochote kile, kila walipokuwa wakiulizwa, waliruka na kuliacha swali hilo kitu kilichowafanya kuwa na hofu kwamba inawezekana walikuwa wamefariki dunia ila madaktari hawakutaka kuwaambia ukweli.

Waliendelea kubaki hospitalini hapo, mtu aliyekuwa akiwajulia hali zaidi alikuwa msichana Catherine ambaye hakukuwa na siku iliyokuwa ikipita pasipo kufika katika chumba walichokuwa wamelazwa na kuzungumza nao.

Hakuwaambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea, alijua kwamba ni Edmund ndiye ambaye alisababisha hayo yote, alihofia kuwaambia ukweli kwa kuwa alihisi kwamba wangemchukia kwa kuwa mwanaume huyo alikuwa karibu naye.

Kila siku walikuwa wakiwaulizia wazazi wao, walitaka kujua ukweli kama walikuwa wamekufa au walikuwa hai, na kama walikuwa hai walikuwa mahali gani.

Hakukuwa na mtu aliyewaeleza ukweli mpaka pale ambapo walipopewa taarifa kwamba wazazi wao nao hawakuwa katika hali nzuri, walikuwa hapo hospitalini kwani sumu iliyokuwa imewapata, ilikuwa mbaya sana.

“Sumu?” aliuliza Walker huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Mliwekewa sumu!” alijibu Dk. John.
“Nani alifanya hivyo?”

Hakukuwa na mtu aliyejibu hilo, kila mtu alihofia kwamba kama wangejibu basi wangewafanya mapacha hao wamchukie Catherine ambaye alionekana kuwa karibu na mwanaume aliyekuwa amesababisha hayo yote.

Siku ziliendelea kukatika mpaka pale walipoanza kupata nafuu. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha na baada ya siku mbili, wazazi wao ambao hawakujua mahali walipokuwa kipindi cha nyuma, wakakutana nao hospitalini hapo na kuanza kuzungumza nao.

Sumu ile haikuwapata sana kama ilivyowapata wao, katika kipindi chote hicho hata nao walikuwa wakifichwa juu ya hali waliyokuwa wakiendelea nao watoto wao.

Walipokutana, wakashindwa kuvumilia, wakakumbatiana kwa furaha, kila mmoja hakuamini kwamba hatimaye familia hiyo iliungana kwa mara nyingine.

Watu wakapewa taarifa kwamba hatimaye mapacha hao walikuwa wameinuka kitandani, kila mtu aliyeziangalia picha zao alibaki na furaha tele kwani kwa kipindi hicho hakukuwa na watu waliokuwa wakipendwa kama ilivyokuwa kwa Walter na Walker.
 
SEHEMU YA 95

Hawakuambiwa juu ya mtu aliyewafanyia hivyo ila baada ya kusikia habari na kuona matangazo, wakajua kwamba mwanaume aliyekuwa amefanya hivyo alikuwa Edmund.

Hilo liliwasikitisha, walimfahamu mwanaume huyo kwa kumuona tu, hawakuwa wamezoeana sana, sasa ilikuwaje mpaka kuamua kuwafanyia unyama mkubwa kiasi hicho?

“Kisa?” aliuliza Walter na hapo ndipo Catherine alipoanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea kati yake na mwanaume huyo.

Hapo ndipo wakajua ukweli kwamba Edmund alidhamiria kufanya mauaji hayo kwa sababu tu alihisi kwamba Walter alikuwa mpenzi wa Catherine. Hilo lilimuumiza mno, hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angeweza kufanya jambo kama hilo kwa ajili ya mapenzi tu.

Waliendelea kukaa hospitalini hapo huku kila siku wakifuatilia kuhusu kufuatiliwa kwa Edmund. Kidogo dunia ikatulia, kitendo cha mapacha hao kupona kilimfanya kila mmoja kuwa na furaha tele.

Nchini Marekani, kila mtu akatamani kuwaona watu hao wakielekea huko. Kulikuwa na mashindano makubwa ya America Got Talent ambapo waliombwa kuwa majaji katika shindano hilo lililokuwa kubwa duniani ambalo lilikuwa maalumu kwa watu kuonyesha vipaji vyao mbalimbali.

Ilikuwa nafasi kubwa kwao, hawakuwa na jinsi, kwa kuwa walikuwa watu wa watu, wakapanga kwenda huko ambapo wangekuwa katika siku zote za shindano hilo ambalo lingechukua miezi mitatu.

Wakapanda ndege, Catherine hakutaka kubaki nchini Uingereza, maishani mwake, hakukuwa na mwanaume aliyekuwa na thamani kubwa kama Walter, alimpenda mwanaume huyo, kwake, ngono halikuwa tatizo, alichokuwa akikifikiria ni kumuona mwanaume huyo kila wakati kitu alichoamini kingemfanya kuwa mwanamke mwenye furaa duniani kote.

“Are you going to Las Vegas?” (utakwenda Las Vegas?) aliuliza Walter.

“Yeah! I lost you, I don’t wanna lose you again,” (ndiyo! Nilikupoteza, sitotaka kukupoteza tena) alisema Catherine huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.

Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 96

Siku nzima polisi walikuwa barabarani kuhakikisha kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa, Edmund anapatikana kwa hali na mali. Hakukuwa na polisi aliyejua kwamba gari moja miongoni mwa magari yaliyotaka kuingia nchini Wales lilikuwa na mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.

Kila mmoja alichoka, hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikuwa njiani kuelekea huko, walichokijua ni kwamba aliendelea kuwa Uingereza hivyo hata kwa jinsi walivyokuwa wakiyakagua magari mpakani hapo, hawakukagaua kama ilivyotakiwa kuwa.

Edmund akapewa kofia kama ya Malboro na dereva yule, akaivaa na kuanza kulisogeza gari kule walipokuwa polisi. Kila mmoja alichoka, walihitaji kuondoka kuelekea nyumbani kwani tangu asubuhi walikuwa mahali hapo, walizikumbuka familia zao, umakini wa kupekua magari uliwatoka na hivyo kuruhusu magari hata kama hawakufanya ukaguzi ambao ulitakiwa kufanyika.

Polisi alimuona Edmund akiwa na kofia, hakumjua, hakutaka kumkagua sana, ilikuwa ni usiku na mwili wake ulichoka mno. Hata kumwambia kuvua kofia ile ili amwangalie vizuri hakuwa na muda huo, akamulika tochi ndani ya gari kizushi, tena kwa haraka na kuliruhusu gari hilo kupita.

Edmund mwenyewe hakuamini, alihisi kama yupo ndotoni, alimwangalia polisi yule kwa makini, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyeliruhusu gari hilo kupita pasipo kufanyika ukaguzi kwa makini kama ambavyo ulitakiwa kufanyika.

Wakapita kirahisi kabisa, na baada ya dakika kadhaa gari likasimishwa nje ya hoteli kubwa ya Wales King ambapo Edmund akateremka, akaelekea mapokezi na dereva yule, akachukua chumba kwa ajili ya kwenda kupumzika.

“Utachukua chumba nikulipie?” aliuliza Edmund huku akimwangalia dereva, bado alimuhitaji, walikuwa na safari ndefu ya kuelekea katika Kituo cha Treni cha Bravein kwa ajili ya kupanda treni na kuelekea nchini Ireland.

“Haina shida. Nichukulie cha chini kabisa, ila kwanza ngoja niende baa kunywa,” alisema dereva huyo na Edmund kufanya hivyo.
 
Sehemu ya 97

Dereva yule akaelekea baa na kuanza kuunywa, nusu ya kiasi cha pesa alicholipwa kama malipo kilimfanya kujiona tajiri, aliamini kwamba kama angemfikisha mwanaume huyo huko alipokuwa akienda basi angepata kiasi kikubwa zaidi.

Kulikuwa na watu wengi ndani ya baa hiyo, kila mmoja alikuwa na chupa ya pombe, wengine waliongea kilevi, wapo walikuwa bize kuwashika makalio wahudumu, na wengine kuwa bize na mambo yao.

Macho ya dereva yule yalikuwa yakiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Baada ya dakika chache alipoyahamishia macho yake kwenye televisheni, akashangaa kuiona sura ambayo haikuwa ngeni kabisa machoni mwake.

Haraka sana akasimama na kuisogelea televisheni ile ili kuiangalia vizuri. Ilikuwa ni sura ya Edmund ambayo ilikuwa kwenye tangazo lililosema kwamba alikuwa akitafutwa na dau la paundi milioni moja iliandaliwa kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.

Moyo wake ukamlipuka, hakuamini kile alichokuwa akikiona. Akaisogelea televisheni zaidi, kile alichokiona akiwa mbali ndicho alichokiona akiwa karibu. Haraka sana akatoka ndani ya baa, nje, kulikuwa na walinzi wawili waliokuwa wakihakikisha usalama mahali hapo, akawasogelea.

“Oya! Mnataka pesa?” aliuliza dereva huku akiwaangalia mabaunsa hao.
“Ndiyo! Kiasi gani?”
“Paundi elfu kumi kila mmoja!”
“Ndiyo! Zipo wapi?” aliuliza, kiasi hicho kilikuwa kikubwa mno.

“Twendeni. Mnamjua yule jamaa anayetafutwa kwenye televisheni?”
“Nani? Edmund? Yule aliyewafanyizia mapacha?”
“Ndiyo!”
“Yupo huku!”
“Wapi?”

“Nyie twendeni acheni presha!” alisema dereva na kuwachukua mabaunsa hao na kuanza kuelekea nao katika hoteli ambayo haikuwa mbali kabisa kutoka hapo.

Aliamini kwa kutumia nguvu za watu watatu, wasingeshindwa kumkamata Edmund ambaye kwa kuwangalia tu alionekana kuwa goigoi.

Wakavuka barabara na kuanza kuelekea katika hoteli hiyo ambapo baada ya kufika, wakawaambia polisi waliokuwa mahali hapo pia kuongozana nao kwenda katika chumba alichokuwamo kwani kila waliposikia jina la Edmund, waliziona akaunti zao benki kujaa pesa.
 
Sehemu ya 98

Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Edmund alikuwa ndani ya hoteli hiyo hivyo kuanza kupandisha juu, polisi mmoja na dereva walipanda kwa kwenda huko kwa kutumia lifti huku wengine wakienda kwa kutumia ngazi.

Tayari walikwishazungumza na dada wa mapokezi ambaye aliwaambia kwamba mwanaume waliyekuwa wakimuulizia ambaye aliingia na dereva huyo muda mchache uliopita alichukua chumba namba 62 kilichokuwa katika ghorofa ya saba.

Walikwenda mpaka katika ghorofa hiyo aliyokuwa mwanaume huyo katika chumba hicho, wakaanza kuangalia huku na kule kabla ya kwenda katika chumba hicho. Walipohakikisha kwamba hakukuwa na mtu yeyote yule, wakamtaka mhudumu waliyekuwa naye kuufungua mlango kwa kutumia kadi ya masta.

"Mna uhakika yupo humu?' aliuliza mhudumu yule.
"Ndiyo dada. Fungua haraka asije kuruka dirishani," alisema dereva huku akiwa na presha kubwa.

Yule mhudumu akaufungua mlango huo kwa kutumia kadi ile, wakaingia ndani kwa pamoja huku polisi wale wakiwa na bunduki zao mikononi.

Wakaanza kuangalia huku na kule kwa lengo la kumuweka chini ya ulinzi mwanaume huyo lakini kitu cha ajabu kabisa, Edmund hakuwepo chumbani.

"Au chooni," alisema dereva na hivyo kwenda huko.
Hakukuwa na kitu walichoambulia, huko napo hawakufanikiwa kumuona, kila kona chumbani humo palikuwa peupe kitu kilichomfanya dereva yule kushangaa kwani si muda mrefu mwanaume huyo alikuwa ameingia ndani ya hoteli hiyo.

"Au alibadilisha chumba?" aliuliza polisi.
"Sidhani! Hakubadilisha chumba, nina uhakika huo," alisema dereva huku akionekana kuwa na presha kubwa.

Kwa maelezo ya dereva yaliwapa uhakika kwamba bado Edmund alikuwa ndani ya hoteli hiyo, hawakutaka kuishia hapo, walichokifanya ni kuomba ruhusa kwa uongozi wa hoteli na kuanza kuingia kwenye kila chumba.

Ilikuwa kazi kubwa sana lakini hawakuwa na jinsi, walikwenda kila chumba na kuangalia kama mwanaume huyo alikuwepo huko lakini hawakupata jibu.
 
Sehemu ya 99

Baada ya dakika arobaini na tano wakateremka mpaka chini, walishangaa, hawakujua mahali alipokuwa Edmund, wakamuuliza mlinzi kama alimuona mtu yeyote aliyetoka ndani ya hoteli hiyo, wakaambiwa kwamba hakukuwa na mtu yeyote.

"Au waulizeni wale vijana," alisema mlinzi huku akiwaonyeshea wanaume wawili waliokuwa wakiingiza takataka kwenye gari la taka.

"Hatujamuona. Kwani alikuja huku? Labda alitoka wakati tumekwenda kuchukua takataka kule," alijibu jamaa mmoja.

"Basi sawa. Popote mtakapomuona, tupeni taarifa," alisema polisi huku akiwaachia namba yao.

Hakukuwa na mtu aliyechanganyikiwa kama dereva, hakuamini kile kilichotokea, alikaa chini huku akiwa ameshika kichwa chake. Kilichomuuma ni kwamba Edmund alikimbia huku akiwa hata hajammalizia malipo yake.

Alikasirika, hakutaka kuondoka, aliamini kwamba mwanaume huyo alikuwa ndani ya hoteli hiyo, kwa kuwa yeye ndiye alikuwa amempeleka mule, akaelekea ndani ya gari na kusubiri humo kwa kuamini kwamba Edmund angerudi na kuendelea na safari kwa kutumia gari lake.

*** Edmund alikuwa chumbani kwake hotelini, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi yaliyopita, hakuamini kama alifanikiwa kuwamaliza mapacha wale kwani hata alipokuwa akiangalia kwenye televisheni, taarifa pekee ambayo aliipokea kipindi hicho ni kwamba walikuwa kwenye hali mbaya sana.

Moyo wake ulifarijika, hakuamini kama kweli alifanikiwa katika hilo. Hakuwa tayari kupoteza penzi lake, alimpenda sana Christina kiasi kwamba alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini si kumuona mwanaume mwingine akimchukua na kuondoka naye.

Alitulia kwa muda, alijiuliza maswali mengi kama alifanya jambo la maana sana kujificha ndani ya gari kwa kisingizo cha kutafutwa na baba yake.

Alikuwa na machale, ni kweli alikuwa amezungumza na dereva yule kuhusu kutafutwa kwake na baba yake lakini kwa upande mwingine alikuwa na hofu kubwa kwamba inawezekana dereva huyo akataka kutafuta kile kilichokuwa kimetokea mpaka kuamua kujificha wakati polisi walipokuwa wakipekua kila gari lililokuwa likipita.
 
Sehemu ya 100

Wakati akiwa anafikiria hayo yote akiwa ndani ya chumba kile, akasimama na kwenda dirishani, alitaka kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa salama na hata pale ambapo alipokuwa kunakuwa salama kabisa.

Akiwa hapo, bado alikuwa akijifikiria mambo mengi mno na baada ya dakika kumi nzima, akamuona kijana mmoja akiwa na mabaunsa wawili wakivuka barabara kuelekea kule hoteli ilipokuwa.

Alimfahamu dereva yule, alipomwangalia, alikuwa na uhakika kwamba alikuwa yeye. Alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea katika upande kulipokuwa na hoteli ile.

Hofu ikamjia, akahisi kabisa kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kujiuliza, hapohapo akatoka dirishani, kwa haraka sana akachukua kila kitu alichokuwa nacho kwa lengo la kuondoka mahali hapo.

Alijua fika kwamba kama angepitia mapokezini basi kungekuwa na urahisi wa kukutana na watu hao, alichokifanya ni kupanda ngazi na kuelekea juu ya ghorofa kabisa na kupanga mikakati ya kuondoka hotelini hapo.

"Nitaondoka kwa kuruka! Hapana! Nitaweza kuvunjika! Au nishuke kule kule mapokezi? Hapana! Nitakamatwa," alisema huku akizungukazunguka huku na kule.

Alikuwa akitafuta njia ya kuteremka kutoka ghorofani mpaka chini. Hakuona sababu ya kuendelea kubaki kwani hapo hotelini hakukuwa salama tena.

Wakati akiwa hapo, akaona bomba kubwa la maji machafu likiwa limeshuka mpaka chini nyuma ya hoteli hiyo, bomba hilo lilikuwa na kazi ya kukusanya mamji ya mvua yaliyokuwa yakikaa huko juu na kuteremka chini.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake, kitu cha kwanza kabisa akalishika bomba hilo na kulitikisa kuona kama lilikuwa imara, halikuonekana kuwa na tatizo na hivyo kuanza kuteremka kuelekea chini.

Alilidandia na kuanza kuteremka kwa kasi kubwa, hakutaka kuchelewa, alijua dhahiri kwamba kama watu wale wangemkosa kule chumbani basi ilikuwa ni lazima kwenda kumtafuta katika vyumba vingine na hata kujaribu kupanda kule ghorofani.
 
Back
Top Bottom