Uzi wa vyakula tu

20201120_202909.jpg
 
Na Esther Karin Mngodo
@Es_Taa

Mwanamke Chapati?





Kuna namna unajisikia ukimsikia mwanaume akimsifia mwanamke anayejua kupika chapati. Ni sifa ambayo inamtenganisha na wanawake wengine na kumfanya aonekane bora machoni pa jamii. Zipo sababu zisizopungua mbili kwa nini mwanaume anaweza kumsifia mwanamke mwingine kwako kwa namna hiyo.



Aidha, anampenda huyo mpika chapati, na anajiona ana bahati kwamba kapata atakayempikia hizo chapati zake anazozitaka. Au, anakupenda wewe lakini hujui kupika chapati na anakulinganisha na huyo mpishi ambaye anaweza kuwa hata ni mama aliyekuzidi umri na uzoefu, ili kukuambia bila kukuambia kuwa inabidi ujiongeze.



Tofauti na mapishi mengine mengi, chapati imepewa hadhi ya kipekee. Kuna tofauti mtu akikuuliza “unajua kupika?” na kama akikuuliza, “unajua kupika chapati?”



Ukweli ni kwamba, sikuwahi kujua kwamba hili swali limeambatana na hisia nyingi hasi kwangu mpaka hivi karibuni ambapo niliamua kupika chapati baada ya muda mrefu.


View attachment 1609106

Chapati ni pishi lenye tabia ya kubadilika badilika matumizi yake. Unaweza kula chapati kama kitafunwa cha kusukumia chai asubuhi. Iwe nyepesi, ukipenda uipake asali kama mimi. Au utandaze yai la kukaanga juu yake, ukalikunjia kwa ndani. Waganda wanaiita hii, rolex.

Wengine wanapenda kuweka soseji badala ya yai, nayo inakwenda pia. Lakini chapati pia inaliwa kama chakula kamili, na maini au mchuzi wa nyama, harage lenye nazi, kabichi na kadhalika. Nje ya Afrika Mashariki, chapati inajulikana kama chakula kinachopatikana kwenye migahawa ya wahindi, ikiwa ni binamu yake mikate ya naan na paratha.
Sidhani kama pishi hili huwa linaleta raha kwa mpishi mithili ya ile raha unayojisikia ukipika keki kwa mfano, walau sio kwangu mimi. Chapati bwana ina ufundi. Ndiyo, kila chakula kina ufundi. Lakini chapati ina mambo mengi. Na ukikosea hatua moja, ni ngumu kuja kuiokoa hatua nyingine.
Kwanza ukandaji. Ukikosea kukanda, umekosea chapati. Ukikosea vipimo, maji mengi kuliko unga, unga mwingi kuliko maji, mafuta si ya kutosha, umekosea chapati. Hupati laini. Na kukanda sio kama kukata vitunguu, mikono inabidi iwe na nguvu, ukande haswa ikandike. La sivyo, itakuzodoa mwisho wa safari.

Haya, halafu sasa kuna hatua nyinginezo kama kusukuma. Hapa wengine wanapata kichwa cha ng’ombe na mapembe yake, wengine wanapata mstatili, duara kulipatia nayo changamoto. Unaweza kudhani kwamba umepatia kukanda, chapati kweli ikatoka laini kwa hiyo mradi iingie tumboni, hapana.

Mwonekano wa chapati ni wa muhimu sana kama ladha yake. Chapati yenye mapembe, mtu anaweza akaacha kuichukua kisa umbo lake. Chapati sharti iwe duara. Ndiyo hivyo yaani.

View attachment 1609107




Kuchoma chapati nalo ni jambo lingine. Moto ukiwa mkali sana, unaunguza nje ndani haiivi. Ukiwa mdogo napo inanyonya tu mafuta, zinadoda.

Na kikaango chako nacho ni jambo lingine. Una kikaango kizito? Chepesi? Kinashika moto haraka au taratibu? Huwezi amini, lakini hata cha kugeuzia nacho kina sehemu yake.

Niliwahi kuambiwa kwamba ukitaka chapati iive vizuri, tumia kipande cha gazeti kuigeuza geuza. Ni kwa nini, mi sijui. Sasa hapa nilipo ughaibuni, sikumbuki lini mara ya mwisho nimenunua gazeti, majanga. Nyumbani hata kama huna la kwako, unaenda dukani, unanunua hata kibiriti, unamwambia nifungie kwenye gazeti. Tayari unalo.

Sikumbuki mara ya mwisho ni lini nilipika chapati, sikumbuki. Wala maandazi. Inawezekana ikawa zaidi ya miaka kumi.

Ninachokumbuka, nikiwa O-Level Jangwani Sekondari, tulipika sana sambusa kama mradi wa shule. Tena tulikuwa hatupewi hata senti tano. Tunauziana wenyewe kwa wenyewe, hela tunarudisha. Ila leo ukiniambia nipike sambusa, itabidi kwanza nigugo.

Nakumbuka wakati huo, mama yangu mdogo alikuwa anatusimamia tupike maandazi na chapati nyumbani, tena kwa umakini mkubwa sana. Kwa sababu tuliishi ndugu wengi nyumba moja, ilikuwa kawaida mimi na binamu zangu kuwa na zamu ya kupika chakula na vitafunwa kama maandazi. Tungepika kama maandazi 100 – 120 hivi tukaweka kwenye mifuko na kuyahifadhi kwenye jokofu. Maana mkiwa wengi ndani ya nyumba, inabidi na vitafunwa viwe vingi.

Lakini pia, mkiwa mabinti wengi nyumba moja ni aibu kama wenzako wanajua kazi au mapishi, na wewe hujui. Kwa hiyo, hilo nalo lilichangia kuongeza ujuzi. Na kama unataka kuongeza manjonjo na kuweka nazi, nazi nakwambia, unasimamiwa uikune inavyopaswa kukunwa. Hapo kaja bibi kutoka Tanga, unaambiwa legeza mkono itoke laini, sio kama siku hizi ni kuchukua tu nazi za pakiti haraka haraka mradi liende.

Chapati nazo, zilikuwa hazinipi shida. Mikate ndio usiseme. Mpaka namaliza sekondari, tulikuwa hatununui mikate nyumbani. Tulikuwa na utaratibu wa kupika mikate yetu wenyewe. Kila siku ilikuwa na mtu wake mwenye zamu ya kupika mkate. Na mikate ya kupika nyumbani ilivyo mitamu sasa, imeshiba ndani. Hadi raha.

Lakini najiuliza, leo mimi ni mtu mzima. Ni mama. Nina elimu na mengineyo. Kweli kabisa kweli, uanamke wangu hautoshei mpaka niwe nimefuzu kupika chapati?

Sijui kwa nini niliacha kupika chapati. Lakini najua kila mara nilipomsikia mtu (na hasa mwanaume) akiniuliza kama najua kupika chapati, nilihisi kama niko kwenye mtihani ambao sitaweza kuushinda. Na wapo wanaume ambao walilisema hili wazi wazi kwangu, pengine hapo ndipo hiyo hofu ilipoanzia.

Kwamba, “Ooh wadada wa siku hizi bana” hamjui kupika chapati, ooh sio kama mama zenu, au mama fulani. Dooh! Basi ukijilinganisha na huyo mama fulani anayejulikana hapo kanisani kwa chapati zake anazopika, unahisi viatu vyake havikutoshi.

Kichwani kwangu, nilishajiambia kwamba kamwe sitakaa nipike chapati. Sio jambo nililolisema wazi wazi hata kwangu mwenyewe; ni sasa ndio nagundua kuwa hayo yalikuwa mawazo yangu. Hata nilipofika ughaibuni, nikiwa naishi na familia moja ya Kitanzania kipindi cha nyuma, waliniuliza kama naweza kuwapikia chapati na maandazi. Nikawaambia, mimi nitapika chochote kile mnataka lakini siyo hivyo vitu viwili.

Ukisikia mtu anakuuliza kama unajua kupika chapati, ni kama anakuuliza, wewe ni mwanamke? Chapati imekuwa kama kipimo cha uanamke. Yaani kuna wanawake, halafu kuna wanawake wanaojua kupika chapati.

Ukikutana na mwanaume anayejua kupika chapati napo, heshima kwake inakuwa ni ya tofauti. Hata hivyo, uanaume wake haupimwi kwa ujuzi wake jikoni. Ni nyongeza tu ya wasifu wake.

Lakini mwanamke, anapewa heshima fulani ya kiutofauti. Unaweza kuwa unajua kupika chakula kingine chochote kitamu. Iwe ni biriani, pilau, ndizi, na mikaango yote. Lakini ukisema najua kupika chapati, hadhi inapanda. Shikamoo Dada.




Ugali nao, na vyakula vya kimakabila kutegemeana na ni wapi unatokea, hupewa hadhi hii. Lakini kwa leo, naongelea chapati kama chapati. Siasa za chapati.

Mji wa Dar es Salaam unalishwa na wanawake. Ukiamka asubuhi, akina mama wamekaa chini na majiko yao ya mkaa au kuni, wanakaanga mihogo, maandazi, chapati, vitumbua n.k. Wana vibanda vidogo vidogo nje ya maofisi na viwanda, wakiuza chai asubuhi na vyakula siku nzima.

Unaweza kununua maandazi na vitumbua popote. Lakini chapati, utasikia, “Mi nataka chapati za Mama nanihiu, kama hayupo, basi.” Halafu wakina mama wa Dar wenye ufundi wa kupika, walipogundua kwamba wanaweza kuuza chapati kwa wingi na kufahamika kuwa hiyo ndiyo biashara yao, basi wakatupumzisha wenzao ambao tunataka kukimbia hilo jukumu kwa sababu mbalimbali. Maana kuna suala la muda pia.

Chapati haihitaji papara. Hata kama ni chapati mbili, kama ni za kusukuma inabidi uzipe walau saa moja kuziandaa. Basi ndo wakaibuka dada wa chapati Kinondoni, Kijitonyama, Mwenge na kwingineko. Chapati kubwa mia tano, laini. Ukitaka za shughuli, haya. Ukitaka za kula nyumbani, sawa. Kwa nini tabu yote ya kujipikilisha mwenyewe? Agiza tu.

Basi chapati ikabadilika. Sio kama wali, ambao hamna atakaekuelewa kwa nini unaagiza wali ukaulie nyumbani. Bali kama chipsi mayai, ambazo lazima uwe na sababu maalumu ya kuzipika mwenyewe. Kwanza za nyumbani siyo tamu.
Sasa nilipoingia jikoni hii juzi, kupika maandazi na chapati kwa sababu nilikuwa nimemisi vya nyumbani, nilijishangaa mimi mwenyewe. Na nilishangaa hisia na mawazo yaliyokuwa yameambatana na kitendo hicho cha kishujaa. Pengine ningekuwa Dar, au kama wangekuwepo watu karibu yangu, nisingekuwa na ujasiri. Maana hakukuwa na wa kuchungulia na kunipima kwa kusema, “Hapo umekosea, hapo fanya hivi, fanya vile.”




Na nisidanganye, niligugo sana tu. Nikamtumia meseji dada yangu Diana yupo Tanzania, mtaalamu wa vitafunwa vyote. Nikamtumia meseji wifi yangu Tuma yupo Marekani ana biashara ya vitafunwa.

Lakini wote walichelewa kunijibu. Kwa hiyo nilipomaliza kuangalia maelekezo YouTube, nikabaki mwenyewe hapo jikoni nahaha. Kupika napika mwenyewe, kula nakula mwenyewe, lakini nahaha.

Nikasema, nikipika mara mbili, tatu mwenyewe, nitarudi kuwa fundi tena. Pengine nitashinda vipimo vilivyowekwa na wanajamii. Hatimaye nami pia nitakuwa sio tu “mwanamke” bali “mwanamke anayejua kupika chapati”.
Hongera sana,

Mwanamke asiyejua kupika ni mzigo mzito sana kwa mumewe na jamii kwa ujumla.
 

Similar Discussions

64 Reactions
Reply
Back
Top Bottom