SoC02 Utamu wa ngoma...

Stories of Change - 2022 Competition

The Festival

Member
Aug 30, 2021
27
98
Nawasalimu ndugu zangu popote pale mulipošŸ¤šŸ½. Nina matumaini ni wazima wa afya, na kwa wale waliopata mtihani wa maradhi basi tunawaombea siha njema kwa MwenyeziMungu (Mtukufu, Aliye juu, Aliye mkuu).

images.jpeg

(Picha kwa hisani ya: Gift of Herbert J. Harris, 1986)

Hii ni ngoma ya kijiji chetu. Kila azaliwaye kijijini kwetu hupaswa kuwa na ufundi wa kuicheza. Ngoma hii yasifika utamu wake hasa ukiwa katikati ya kiwanja ukiicheza kufuatana na midundo yake. Wanakijiji wa vijiji jirani nao hucheza ngoma zao na hakika hunufaika. Mfano mzuri ni wanakijiji wa Uchinani, wanaicheza vizuri ngoma yao na sasa imewasaidia wako pahala poa kabisa. Wengine ni wanakijiji wa kiarabu, nao wanaicheza vizuri ngoma yao na si haba matunda ya kuserebuka kwao tunayaona. Vijiji vya Amerika na Ulaya wanaicheza kweli kweli na hatua kubwa wamepiga katika vijiji vyao. Hii inanikumbusha maneno ya bibi pale alipokua akiniambia, utamu wa ngoma uingie ucheze. Hivo kwa yeyote ambaye atakua akisifia uhondo wa ngoma basi inatupasa tufahamu ya kwamba, msifiaji huyo alibahatika kuwemo na bado yumo kiwanjani akitimbwirika kwa miondoko murua kupata utamu halisi wa midundo ya ngoma hiyo hadi kuisifia.

Lakini katika kijiji chetu hali ni tofauti kwa baadhi ya wenzetu waliopata vigoda vya kukalia. Wenzetu hao wanaonekana kutojali kabisa kujumuika pamoja nasi kiwanjani kuburudika na midundo mitamu ya ngoma hii, bali wao huona raha kutazama wachezaji huku wakihamasisha na kuipamba ngoma hii kwa mashairi na mapambio mbali mbali ili watu wasiokua miongoni mwao waingie kati kurindima na kuicheza ngoma hii.

Hali ilipofika sasa ni ya ukakasi na ninapata maswali mazito hadi ninashindwa kabisa kuyajibu: shida ni nini mpka wao wenye vigoda hawavishughulishi viungo vyao kuja kurindima na sisi? Ni kwanini hawa walio kalia vigoda kutoka pwani na bara wala hawajishughulishi kuserebuka na mdundo wa ngoma hii, ili kusudi wakiisifia wawe na uwezo wa kujenga hoja madhubuti ya kwamba ngoma ni tamu haswa na wote twaicheza kwa mitindo na mizuka mbali mbali? Au wamesahau ahadi zao kedekede kwetu, wakituaminisha ya kwamba wao ni wachezaji wazuri wa ngoma na tukiwaazima vigoda basi watatuonesha ufundi wao wa kuicheza ngoma hii ipaswavyo na wala hawatabweteka? Au wenzetu wana hofu wataanguka kama wakiicheza huku wamekalia vigoda? Au wana wasiwasi wakiicheza watanyanyuka kwa midadi na kisha kanuni ya kwenye daladala itafata, ukiinuka sisi tunakaa? Au wamesahau ya kwamba vigoda vina muda maalumu wa kukaliwa na ni dhamana na wala si miliki yao milele daima? Ni kwa nini wanaisifia sana ngoma hii na wala wao hatuwaoni kiwanjani wakijimwagamwaga kuicheza?

Naona na wenzetu wasiokua na vigoda vya kukalia kwa kiasi kikubwa wameamua kuacha kuicheza ngoma, kwa kuwa wale wenye vigoda ambao ndio walipaswa kuwa vinara wa kucheza ngoma hii hawaichezi hata thumni. Huku ni kufanya nini huku? Huku ni kuisusia ngoma ambayo ndio chachu ya mambo mazuri tuyatakayo.

Enyi mlio na vigoda kumbukeni mkataa pema pabaya panamwita. Nawanasihi muicheze ngoma. Kwani hivyo mfanyavyo, kuisifu tu na kuipamba ngoma si utaratibu tulio achiwa na wale waasisi wa ngoma hii. Waasisi kama vile Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa kijiji chetu aliicheza ngoma hii kwelikweli ndani na nje ya kijiji tangu mwaka 1922 mwezi wa 04 tarehe 13 hadi pale mauti yalipo mkuta mwaka 1999 mwezi wa 10 tarehe 14. Abeid Amani Karume, Mtu kazi, baharia mzoefu nae hakupoa kabisa katika kurindima viwanjani kwa miondoko ya kipwani tangu mwaka 1905 mwezi wa 08 tarehe 04 mpaka pale alipoaga dunia mwaka 1972 mwezi wa 04 tarehe 07. Bibi Titi Mohammed, mwanamke wa shoka asiyeimbwa na wengi, aliserebuka na kuicheza kwa mikogo ngoma hii tangu mwaka 1926 mwezi wa 06 hadi pale alipofikwa na umauti mwaka 2000 mwezi wa 06 tarehe 05. Hakika nakiri ya kwamba, ardhi imemeza watu. Hao ni baadhi tu ya wengi waliokua wamekalia vigoda na bado walidumisha kuicheza ngoma sambamba na wale wasio na vigoda. Lakini sasa mambo si shwari tena, kwani nyinyi wenye vigoda kwa kutoicheza ngoma hii kwa vitendo, munawashawishi wasio na vigoda nao kutoicheza ngoma ipasavyo. Kwa heshima na taadhima, enyi wenye vigoda naomba mjitafakari sana kwenye kuicheza ngoma hii na si kuwashawishi wengine tu nanyi mmo pembeni tulii.

Enyi ambao hamna vigoda, nawanasihi ya kwamba musiache kuicheza ngoma yetu hii, japokuwa ni ngumu sana kuicheza ngoma hii huku ukimwona alieshiba kakalia kigoda cha dhamana akikutizama wala hajishughulishi kuicheza ilihali alipaswa kuwa kiwanjani akitimua vumbi kwa kuicheza ngoma. Nafahamu baadhi yenu mwatamani kukalia vigoda lakini hilo si lengo kuu, muhimu kijiji kichangamke yaani kisipoe hata chembe. Hivyo kwa unyenyekevu nawaomba tuendelee kuicheza ngoma yetu bila kujali kama yupo mwenye kigoda ana icheza ngoma au la.

Madhara ya kutoicheza ngoma hii ni makubwa mno kwani huhatarisha maslahi mapana ya leo na kesho yetu, na pia huhatarisha maslahi ya kijiji chetu chote kwa ujumla. Naweza sema ya kwamba, kwa kuwa sisi tupo viwanjani kuicheza ngoma, wasioicheza wanaweza kupata mwanya wa kwenda majumbani mwetu ambapo tumeacha mali zetu, wakatuchukulia mali zetu bila ya ridhaa zetu. Vile vile kijiji chetu kitakosa mchezaji, hivo ngoma itadorora na kijiji kitapoa na kukosa thamani inayo stahiki.

Hamasa ya mshikamano itapungua kwani kwa kutoicheza kwetu kwa pamoja hata huo umoja tutaukosa. Masikilizano na maelewano baina yetu yatapotea kwani midundo ya ngoma hii inahamasisha umuhimu wa maskilizano na maelewano. Rasilimali za kijiji chetu zitapotea kwa kuwa ngoma hii inachochea kukipenda na kukithamini kijiji chetu.

Utamaduni utabadilika na kuharibika, hivyo vizazi vijavyo vitashindwa kufahamu namna bora ya kuicheza ngoma hii. Ulinzi na usalama utatoweka kwani ngoma hii inahamasisha wanakijiji shupavu kupenda kujitolea kulinda amani ya kijiji chetu. Vitendo vya rushwa vitashamiri kwa kuwa ngoma hii ikivuma sana haipasuki bali huelekeza watu kutokomeza tabia za ubinafsi na urasimu. Madhara ni mengi mno tutakesha kuyasema na ngoma ndio hivo tena imenoga.

Nakaribisha wanajukwaa wote kutoa maoni ya nini kifanyike kutokana na tafsiri walioipata katika bandiko hili, nami mwandishi nitatoa tafsiri hapa hapa kwenye bandiko. Pia nawaomba mpige kura kwa ajili ya bandiko letu hili. Wino umekwisha, naweka kalamu chini.

Ahsante sana & Karibu.
 
Habari ndugu zangu. Katika bandiko letu hili la "Utamu wa Ngoma..." Hizi ndizo maana za maneno yaliyotumika katika uwasilishaji wa mada husika.

Je, neno ngoma katika bandiko hili lina maana gani?
Neno ngoma lina maanisha UZALENDO. Imepigiwa mfano wa Ngoma kwa kuwa katika kipindi hiki, uzalendo umekua ni kama ngoma inayosifiwa kuwa ni nzuri na baadhi ya watu lakini wao hawaoneshi uzalendo wa kweli kwa matendo yao(hawaichezi ngoma, bali huisifia na kuipamba wengine waicheze).

Je, wenye vigoda katika bandiko hili ni kina nani?
Wenye vigoda inamaana ya VIONGOZI au WATU WALIOPATA FURSA YA UONGOZI KATIKA JAMII. Viongozi wamepigiwa mfano wa watu waliopata vigoda katika uwanja wa ngoma. Hivyo kwa kupata kwao fursa hawajishughulishi na kutenda matendo ya kizalendo bali wao husifia tu uzalendo uzalendo kwa maneno matamu bila ya wao kuonesha uzalendo huo kwa matendo yao.

Je, wasio na vigoda katika bandiko hili ni kina nani?
Wasio na vigoda inamaana ya WANANCHI WA KAWAIDA au RAIA WASIOKUWA VIONGOZI KATIKA JAMII. Wananchi wasiokua viongozi hususani kwenye uongozi wa kisiasa wamepigiwa mfano wa watu wasiokua na vigoda katika uwanja wa ngoma. Watu hawa hushajihishwa kuicheza ngoma ya uzalendo (huambiwa umuhimu wa uzalendo na hushawishiwa wawe wazalendo) na watu waliokua viongozi, ilhali wengi wao katika hao viongozi si wenye kuyatenda matendo ya kizalendo.

Je, neno kijiji katika bandiko hili lina maana gani?
Neno kijiji linamaana ya NCHI. Na neno kijiji chetu katika bandiko hili linamaana ya TANZANIA. Nchi imefananishwa na kijiji kutokana na masuala ya utandawazi ambayo yanazifanya nchi mbalimbali kua ni kama vijiji vidogo sana. Vilevile, ngoma nyingi huwa zinapigwa na kuchezwa vijijini, hivyo muandishi alitaka kuonesha uhusiano mzuri katika uwasilishaji wa mada husika.

Je, wanaoicheza ngoma ilioelezwa katika bandiko hili ni kina nani?
Wanaoicheza Ngoma inamaana ya WAZALENDO. Wazalendo wamepigiwa mfano wa watu wanaoicheza ngoma kwa kuwa neno ngoma limetumika kumaanisha uzalendo. Wazalendo hawa ndio watu muhimu katika jamii na ndio watu wanaoonesha mapenzi ya kweli kwa nchi yao na ndio watu wanaotanguliza maslahi ya nchi mbele ya maslahi yao.

Je, wasioicheza ngoma ilioelezwa katika bandiko hili ni kina nani?
Wasioicheza Ngoma inamaana ya WASIOKUWA WAZALENDO. Wale ambao sio wazalendo wamepigiwa mfano wa watu wasioicheza ngoma kwa kuwa neno ngoma limetumika kumaanisha uzalendo, hivyo wasioicheza ngoma ya uzalendo wamepigiwa mfano wa watu wasiokuwa wazalendo. Watu hawa katika jamii hawana mapenzi ya kweli kwa nchi yao na ndio watu wanaotanguliza maslahi yao mbele ya maslahi nchi.

Machache kutokwa kwa mwandishi.
Nina imani kubwa katika suala la maendeleo ya nchi kua na uhusiano mkubwa na uzalendo. Hivyo basi, nchi yetu ya Tanzania kupata maendeleo ya kweli kwanza tupambane na mioyo yetu. Hii ni kama vita ya ndani na vita ya mtu mmoja mmoja kwa ajili ya nchi. Kila mmoja wetu awe mzalendo wa kweli kwa ajili ya taifa. Lakini ili tufike huko, ni wapi uzalendo huo utapatikana?

Mosi, maamuzi ya kila mmoja wetu. Hii inamaana ya kwamba kila mmoja wetu ahamasike kuipenda na kuithamini nchi yetu kwa matendo na maneno.

Pili, ni uongozi bora ulio imara ambao utakua na ushawishi juu yetu. Hii ikiwa ina maana ya athari nzuri na ushawishi wa kimatendo na maneno kutoka kwa viongozi. Ikiwa viongozi hawataonesha matendo ya kizalendo, ikiwa wananchi wa kawaida watashuhudia ufisadi, rushwa, urasimu, ukosefu wa uwajibikaji, na ukandamizaji wa kimaneno na matendo kutoka kwa viongozi wao basi hii italeta shida kubwa kwa wananchi kuonesha mapenzi na kuthamini nchi yao hatimae maendeleo yatakua ni ya kusuasua. Mifano ipo mingi, na miongoni mwao ni utafiti mdogo nilioufanya kwa raia ambao wanatamani kuajiriwa serikalini.

Utafiti ulijikita zaidi kufatilia ni wapi vijana wengi hupendelea kuajiriwa. Njia iliyotumika kupata majibu ya utafiti ni maoni ya wasaka ajira. Matokeo ya utafiti yalionesha ya kwamba raia wengi kwa asilimia kubwa hutizama taasisi ambazo wataweza kulipwa vizuri na kupata fedha nyingi ndani ya muda mchache kwa njia zisizo halali kwa mujibu wa sheria za nchi, na ni wachache sana kati yao walionesha haja ya kuwajibika kwa ajili ya nchi kua ni kipaumbele kisha kufuatiwa na maslahi yao binafsi.

Hii ni ishara mbaya sana kwa taifa, kwani wananchi wapo tayari kutanguliza maslahi binafsi mbele ya maslahi ya nchi. Hivyo, ni muhimu kila mmoja wetu kwa nafasi yake ahakikishe anakuwa mzalendo wa kweli kimaneno na matendo.

Vile vile, kwa wale viongozi ni muhimu kuonesha uzalendo wa kweli kimaneno na matendo kwa ajili ya nchi ya Tanzania na si kwa ajili tu ya serikali inayoongoza madarakani kwa wakati huo. Ahsante sana, naendelea kupokea maoni yenu wanajukwaa. Karibuni sana.
 
Back
Top Bottom