Utajiri wa damu

Utajiri wa damu

UTAJIRI WA DAMU - 8-

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Chepriska baada ya kupokea simu ya polisi akajiona ni mnyonge sana hali iliyomfanya mzee Mitimingi kuwa na wasiwasi.
"Kwani hiyo simu imetoka wapi? Maana baada ya kuipokea umekuwa mnyonge, kulikoni?," Akamuuliza.
"Hii simu imetoka polisi. Wananiita ."
"Polisi wanakuita? Tafadhali sana usiwaambie kuhusu huyu mbwa mtu, ukiwaeleza tu, umeniua, umeelewa?" Mzee Mitimingi alisema huku akiwa ametoa macho.
SONGA NAYO...


"Lakini mzee umeniambia kuwa utaniambia jambo zito, kabla ya hujasema simu imeingia, kwani huwezi kuniambia kwa kifupi?"
Aliniangalia akiwa amekunja sura kisha akasimama.
"Nilichokuambia hukielewi, kwamba nimekuongezea shilingi laki moja kwa ajili ya kuficha siri hii. Mbwa huyu hajawahi kuonwa na mtu yeyote isipokuwa wewe na mimi."
"Ni hilo tu?"
"Wee mtoto, kwani katika maisha yako umewahi kumuona mbwa kama huyu?"
"Sijawahi, kwani huyu ni mbwa au jini?"
"Swali gani hilo unauliza? Nilichokueleza umeelewa?" Alifoka huku akifuta jasho usoni.
"Samahani mzee."
"Nimepata wazo jipya. Hebu wapigie hao polisi na uwaambie kuwa leo huna nafasi kwa kuwa kuna dharura, waombe uende kesho."
"Lakini mzee nikifanya hivyo wanaweza kudhani kuwa nataka kutoroka?"
"Wewe waombe kama watakataa basi, nitakupeleka mimi."
"Sawa."
Nilichukua simu na kuipiga namba ya yule mpelelezi, baada ya kuita ikapokelewa.
"Inspekta Ado hapa."
"Aaah, nilifikiri ni simu ya mpelelezi wa kesi ya marehemu Mpepechere."
"Nani anaongea?"
"Ni mimi Chepriska."
"Aaah binti, ni mimi niliagiza wakuite, nahitaji kukuona."
"Nilikuwa nampigia mpelelezi wangu ili kumuomba nije kesho kwa sababu saa hizi nampeleka mzee wangu hospitali anaumwa," nilimdanganya.
"Kwani sasa hivi upo wapi?"
"Nipo Mtaa wa Mizambarauni nyumba namba kumi na mbili."
"Sawa lakini mpelelezi atakuja kukuona jioni nyumbani kwako."
"Sawa mzee na nashukuru kwa kuniruhusu."
Nilikata simu na kumuangalia mzee Mitimingi.
"Wanasemaje? Wamekuruhusu?" aliuliza mzee Mitimingi huku akinikodolea macho.
"Wameniruhusu. Nimeongea na bosi wao."
"Mbona umeitaja namba ya nyumba yangu?"
"Nimewaambia wewe mzee wangu unaumwa, nakupeleka hospitali."
"Una akili sana binti wewe na ndiyo maana napenda sana uwe unafanya kazi zangu na safari hii ni lazima nibadili maisha yako yawe ya kifahari."
Alifikiri kwa dakika kama moja hivi kisha akachukua juisi na kuinywa, akaniangalia, akasema:
"Kumbe ulikuwa na namba ya bosi wa wale wapelelezi?"
"Nilikuwa sina kumbe yule mpelelezi alitumia simu ya bosi wake kunipigia."
Wakati wanaendelea na mazungumzo yao walipigwa butwaa baada ya kuliona gari la polisi ‘Defender' likipiga honi kwenye geti.
Bahati nzuri mlinzi ambaye sikujua awali alikuwa wapi, alifungua geti na taratibu gari likaingia ndani.
"Jifanye mgonjwa," nilimnong'oneza mzee Mitimingi.
Naye kisanii akawa ameegesha shingo yake upande pale kwenye kiti cha sofa alichokuwa amekalia.
Lile gari lilisimama hatua chache kutoka pale tulipokuwa tumeketi na mzee Mitimingi.
"Karibuni sana," nilisema huku nikijifanya sina hofu nao. Askari watatu walishuka, miongoni mwao alikuwepo askari wa kike. Nilihisi kwamba wamekuja kunikamata kwa sababu kwa sheria za polisi mwanamke hukamatwa na askari wa jinsia yake.
"Huyu ni mzee wangu, lakini siyo baba yangu mzazi ni wa kunilea."
"Sawa. Mimi ni Sajenti Mbegu na hawa ni wapelelezi bila shaka huyu wa kike unamkumbuka."
"Namkumbuka, ndiye aliyekuwa akinihoji pale kituo cha polisi."
"Huyu mzee wako anaitwa nani?"
"Ni mzee Mitimingi."
"Haah kumbe mzee Mitimingi ndiye huyu? Ni maarufu sana kwa sababu huwa naona mabasi na malori yake sehemu mbalimbali hapa mjini yakiwa yameandikwa jina lake."
"Bahati mbaya mmekuta anaumwa."
"Siyo mbaya kwa sababu yote ni mipango ya Mungu."
"Karibuni, sijui mnatumia kinywaji gani?"
"Wewe tuletee juisi tu, hakuna mnywaji wa pombe hapa."
Niliingia katika nyumba ya mzee Mitimingi japokuwa sikuwa mwenyeji mle ndani lakini nilikwenda moja kwa moja jikoni nikakuta friji.
"Khaaaa" nilisema kwa sauti. Nikafunga mdomo kwa mikono yangu kushangaa kile nilichokiona ndani ya friji.Niliona kuna kiganja cha mtu!!
Nilitaka kutimua mbio kurudi walipo askari lakini nikaona nikifanya hivyo tutakuwa tumejipalia mkaa maana hata mimi nitajiingiza katika matatizo.
Nilishika boksi moja la juisi nikaipasua na kumwaga kiasi chini kisha nyingine nikaweka kwenye trei na kuwaletea wageni.
"Vipi mbona tumesikia ukisema khaa?" aliniuliza yule askari wa kike.
Kabla sijajibu chochote nilimuona mzee Mitimingi akitetemeka, bila shaka alijua polisi wakikagua wataona maajabu ya mbwa-mtu na kiganja kwenye friji.


Je, nini kitatokea? Fuatilia leo jioni tena
 
Haya nasubiri jioni ifike

Sent from my BlackBerry 9300 using JamiiForums
 
UTAJIRI WA DAMU - 9-

Niliingia katika nyumba ya mzee Mitimingi japokuwa sikuwa mwenyeji mle ndani lakini nilikwenda moja kwa moja jikoni nikakuta friji.
"Khaaaa" nilisema kwa sauti. Nikafunga mdomo kwa mikono yangu kushangaa kile nilichokiona ndani ya friji.
Niliona kuna kiganja cha mtu! Nilitaka kutimua mbio kurudi walipo askari lakini nikaona nikifanya hivyo tutakuwa tumejipalia mkaa maana hata mimi nitajiingiza katika matatizo.
Nilishika boksi moja la juisi nikaipasua na kumwaga kiasi chini kisha nyingine nikaweka kwenye trey na kuwaletea wageni.
"Vipi mbona tumesikia ukisema khaa?" aliniuliza yule askari wa kike.
Kabla sijajibu chochote nilimuona mzee Mitimingi akitetemeka.
"Naona mzee amezidiwa, tumuwahishe hospitali," alisema askari mmoja.
SONGA NAYO...


"Nilifungua friji kwa nguvu nikaangusha boksi la juisi, likapasuka. Nitakunywa mimi hii, hizi juisi zingine ni zenu." Nilidanganya.
Kila mmoja nilimpa pakiti lake na glasi na wakaketi wakawa wanakunywa nami nikaenda alipoketi mzee Mitimingi nikawa namgusa shabu kuona kama ana homa kali (nilikuwa ‘naekti') .
"Vipi mzee ana homa kali?" aliuliza yule askari.
"Siyo sana."
"Bila shaka Afande Ado alikueleza kuwa tutakuja kwako."
"Ni kweli, lakini kwani hapa ni nyumbani kwangu?"
"Tulitumia akili za kipelelezi tukaona kuwa kabla ya kuja kwako tuanze kwanza kuja hapa kwa mzee maana ulisema upo hapa."
"Mmefanya vizuri maana mtanisaidia hili janga."
"Janga gani?"
"Hili la kuugua mzee wangu."
Askari hao walikunywa juisi yao haraka haraka kisha kunipa pole kwa kuuguliwa na mzee.
"Sasa tukupe lifti ya kumkimbiza mzee hospitali?"
"Hapana, sasa hivi ataingia dereva wake na tutatumia hilo gari."
"Basi kama ni hivyo ni sawa."
"Lakini ningeomba basi nije kituo cha polisi kesho asubuhi kwani sijui hospitali madaktari watasemaje au watachukua muda gani kumtibia."
"Subiri nimjulishe Afande Ado kwa sababu yeye ndiye aliyetutuma."
Baada ya kusema hayo askari aliyekuwa kiongozi wao alichukua redio yake ya upepo na kumpigia afande wake.
"Halooo deka mbili."
"Nakusoma, sema."
"Tumefika kwa huyu binti Chepriska."
"Mmefika nyumbani kwake?"
"Hapana tumefika kwa mzee wake. Si alikuambia kuwa mzee wake ni mgonjwa?"
"Ndiyo."
"Baada ya kusema hivyo tulitumia akili yetu tukaamua kuja moja kwa moja hapa kwa mzee wake, mzee Mitimingi."
"Ehee… endelea."
"Ni kweli tumemkuta huyu mzee wake ana hali mbaya sana, ni mgonjwa."
"Anaumwa nini?"
"Anatetemeka mwili wote, hawajui hasa anasumbuliwa na nini?"
"Kwa hiyo mmekubalianaje?"
"Hatujakubaliana chochote isipokuwa ameniomba aje hapo kituoni kesho nami nikamuambia kuwa siwezi kutoa uamuzi ndiyo maana nikaona ni vyema tuongee humu kwenye redio nisikie ushauri wako."
"Kama mmehakikisha baba yake ni mgonjwa ni vyema mkamkubalia. Asije akafa mzee wake akatusingizia polisi, sawa?"
"Sawa afande."
Wakati anazungumza na kiongozi wake nilikuwa nikimuangalia mzee Mitimingi aliyekuwa amekaa kwenye kochi akiwa amejilegeza.
Wakati hayo yakiendelea, kule nyuma yule mbwa mwenye sura ya mtu akawa analia kwa sauti ya juu.
Uliaji wa mbwa huyo ulimfanya mzee Mitimingi azidi kutokwa na machozi. Bila shaka alikuwa anadhani kwamba polisi wanaweza kwenda kibandani na kumuona mbwa huyo wa ajabu ambaye dunia nzima hakuna.
"Huyo mbwa kwa nini analia?" aliuliza yule askari wa kike.
"Ngoja nikamuangalie," nikasema.
Nilizunguka nyumba na kwenda kibandani. Nilikuta amejifunga kamba shingoni, hivyo kushindwa kugeuka na ndiyo maana alikuwa akilia kuomba msaada.
Nilijitahidi kuikunjua kamba aliyokuwa amefungwa shingoni na kuiweka sawasawa. Aliniangalia kwa huruma mno na kuachia tabasabu.
"Usiwe na wasiwasi nitakusaidia." Nilisema polepole bila kusikia mtu mwingine yeyote isipokuwa mbwa huyo.
Ajabu ni kwamba mbwa mtu yule aliitikia kwa kutikisa kichwa huku akitokwa na machozi. Nilijisikia vibaya sana.
Kwa jinsi alivyokuwa na sura ya binadamu, nilihisi kwamba inawezekana huyu mzee amemgeuza mtu kuwa katika hali ile.
"Chepriska, huyo mbwa ana nini?" aliuliza yule askari polisi wa kike.
"Ahaa, alikuwa amejifungafunga shingoni na kamba, hivyo akawa anashindwa kugeuka." Nilijibu.
"Hajapata madhara makubwa?"
"Hajapata," nilimjibu.
"Tuje kukusaidia kumfungua?" alizidi kuhoji askari yule wa kike huku akiangalia kwa mbali.


Je, siri ya mbwa mtu huyo itafichuka? Fuatilia baadae usikonde tu.
 
Je, siri ya mbwa mtu huyo itafichuka? Fuatilia baadae usikonde tu.

Mzizi....mie nimeshakonda tayari. Lete ingine ili ninenepe.
 
Back
Top Bottom