Utajiri wa damu

Utajiri wa damu

UTAJIRI WA DAMU - 6-
ILIPOISHIA
Ghafla yule mbwa aliyekuwa akipigwa akawa amesimama nyuma yangu, ajabu ni kwamba alikuwa na sura ya binadamu na muda wa sekunde yule mzee alirudi na baada ya kumuona mnyama huyo akawa anatetemeka. Mbwa naye akawa analia kama afanyavyo binadamu! Nilishituka sana...
ENDELEA KUJIMWAGA


Baada ya sekunde chache yule mbwa alionekana kama kwamba alikuwa akihitaji huruma fulani. Katika maisha yangu sikuwahi kuona mbwa akimwaga machozi kama yule.
Mzee Mitimingi aliingia ndani na kutoka na bakora, haraka sana mbwa yule baada ya kuona bakora alitimua mbio huku akilia na kwenda kwenye banda lake.
Huku fimbo ikiwa mkononi na kuonekana mwenye hasira, mzee Mitimingi alimfuata hukohuko mbwa huyo na alikuta amekwisha ingia kwenye banda lake.
Niligeuza shingo yangu na kumuona mzee huyo akiinama, nilijiuliza anainama kuchukua nini chini ya ardhi. Kumbe alikuwa akichukua kamba ambayo mbwa yule amefungiwa shingoni lakini ilikuwa ndefu na kubaki nje ya banda.
Mzee Mitimingi alianza kuivuta kamba hiyo na mbwa akawa analia kwa sauti kubwa iliyofanya anga lote eneo lile kuwa na kelele zake.
“Nimekuambia kwa nini umekuja pale kwa yule binti?” akamchapa bakora na mbwa akawa analia sana.
“Nilishawahi kukuambia kwamba ni marufuku kujitokeza mbele za watu, wewe leo umekiuka, una maana gani? Alimchapa tena bakora.
Niliingiwa na moyo wa huruma nikajifanya nakohoa kama vile nimepaliwa na mate hivyo nikatoka pale nilipokuwa nimeketi na kwenda katikati ya uwanja wa mzee Mitimingi.
Mzee yule aliniona na akaacha kumchapa yule mbwa kisha akamfungia ndani ya banda.
Nilijifanya nakohoa sana. Akaja karibu yangu.
“Vipi tena Chepriska?”
“Nimepaliwa na mate Koh koh kohooo.” Nikawa natema vitu kama mlenda, hakika moyoni nilijiona ni msanii lakini mzee yule aliamini kuwa nilikuwa nimepaliwa mate lakini nia yangu ni kumuokoa yule mbwa-mtu asiendelee kupata kipigo.
“Ngoja nikakuletee maji usukutue,” alisema na kuingia ndani baada ya sekunde chache akaja na jagi lilokuwa na maji.
Nilisukutua maji na mengine kunawa usoni kisha nikamrudishia jagi. Akaniambia nikaketi pale nilipokuwa nimekaa awali.
Wakati nakwenda kukaa niliingiwa na mawazo mbalimbali nikawa najiuliza huyu mzee kwa nini anamkung’uta yule mbwa tena huku akimsemesha?
Kwa nini mbwa yule ana macho na sura kama ya binadamu? Na nini kilimfanya mzee Mitimingi atetemeke baada ya kumuona mbwa akiwa nyuma ya mgongo wangu?
Ni maswali ambayo sikuwa na majibu na nilikuwa naogopa sana kumuuliza mzee huyo.
Tangu nimfahamu mzee Mitimingi sikuwahi kumuona mwanamke pale nyumbani kwake au mtoto hali iliyonifanya niwe na mashaka naye. Ni mara chache sana huwa namuona mlinzi tu wa getini. Niliacha wazo la kumuuliza kuhusu mbwa niliona hilo nilifanye siku nyingine, hivyo nikaamua kurudi katika suala lililonifanya niende pale, la kudai fedha zangu.
“Mzee naona sasa niondoke hivyo naomba zile fedha maana nyumbani kwangu sijafika tangu jana.”
Aliingiza mkono mfukoni akatoa fedha kama alivyoahidi awali. Shilingi elfu thelathini za kinyozi aliyenipa nywele za watoto na shilingi laki moja yangu kwa ajili ya kazi ya kukusanya nywele za watoto.
Wakati ananipa fedha hizo waliingia madereva wake wawili wanaoendesha malori yake mawili kati ya sita aliyoyamiliki. Kila mmoja alikuwa ameshika bunda la noti.
“Mzee safari yetu tulikwenda salama na tumerudi salama. Tulikwenda na mzigo na tumerudi na mzigo kwa tajiri yuleyule. Lakini pale Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda tulitaka kukwama kwani tulikuta bei ya kupitisha lori la Tanzania ni kubwa,” alisema mmoja wa wale madereva wa malori.
Alichukua mabunda yake ya fedha na kwenda kuweka ndani kisha akatoka na bahasha akawapa wale madereva kila mmoja na yake.
“Vipi mzee mama hayupo?” alihoji mmoja wa wale madereva ambao mpaka dakika hiyo nilikuwa sijajua majina yao.
Swali hilo lilinishangaza kwa sababu sikuwahi kumuona mkewe.
Nilijisemea moyoni kuwa kama ni mama yake mzazi basi atakuwa mzee sana kwa sababu kwa kumkadiria tu mzee Mitimingi alikuwa na miaka sitini.
“Mama yenu mgonjwa.”
“Tangu lini?” mmoja wa madereva alihoji.
“Wiki moja sasa!” Mzee Mitimingi alijibu.
“Anasumbuliwa na nini?”
“Ana presha ya kupanda na analalamika miguu inamuuna sana asubuhi na jioni.”
Madereva hao waliahidi kwenda kumuona siku iliyofuata kwani walichoka sana kisha wakaaga na kuondoka.
Nilibaki na mzee Mitimingi na nilipomuaga kwamba naondoka akasema anataka kuniambia jambo gumu.
“Kuna jambo gumu sana na zito nataka kukuambia kuhusu yule mbwa mwenye sura ya mtu, nataka uitunze siri hiyo.”


Je, ni siri gani hiyo? Fuatilia usiku mwingi baadae.....
 
Hivi Mbuzi mzee , yuko wapi siku hizi? kuna story alituonjesha kisha akaingia mitini.
 
Last edited by a moderator:
UTAJIRI WA DAMU - 7-

“Mama yenu mgonjwa.”
“Tangu lini?” mmoja wa madereva alihoji.
“Wiki moja sasa!” Mzee Mitimingi alijibu.
“Anasumbuliwa na nini?”
“Ana presha ya kupanda na analalamika miguu inamuuma sana asubuhi na jioni.”
Madereva hao waliahidi kwenda kumuona siku iliyofuata kwani walichoka sana kisha wakaaga na kuondoka.
Nilibaki na mzee Mitimingi na nilipomuaga kwamba naondoka akasema anataka kuniambia jambo gumu.
“Kuna jambo gumu sana na zito nataka kukuambia kuhusu yule mbwa mwenye sura ya mtu, nataka uitunze siri hiyo.”
ENDELEA


Niliwaza, ni nini anataka kuniambia mzee huyo, lakini akili ikagonga kuwa ni lazima itakuwa kuhusu mbwa-mtu.
Katika maisha yangu sijawahi kuona mbwa akiwa na sura ya binadamu. Niliwahi kusoma katika vitabu kitu kama hicho na nilikuwa nadhani ni mambo ya utunzi tu lakini sasa nimejionea laivu.
Mzee Mitimingi aliingia ndani na kutoka na begi jeusi, aliketi kisha akalifungua.
Alitoa noti nyekundunyekundu na kuzihesabu kisha kunipa.
“Chepriska, shika hizi ni fedha zako,” alisema. Niliona kama amechanganyikiwa kwa sababu alikwishanipa shilingi laki moja na shilingi elfu thelathini za kinyozi aliyekuwa akinikusanyia nywele za watoto wadogo.
“Mzee ulishanipa fedha zangu na za kinyozi, sikudai chochote,” nilimkumbusha.
“Hapana, si nimekuambia kuwa nataka kukuambia jambo gumu na zito? Chukua kwanza huu mzigo.”
***
Katika kituo cha polisi, Inspekta Ado alikuwa amejifungia akichambua majalada lakini yote yalihusiana na vifo vya watu mbalimbali.
“Huyu Josefu Kumusi, alinyongwa kwa kuning’inizwa mtini, Paulo Gunia naye hivyohivyo lakini Hamisi Mpepechere yeye kifo chake siyo cha kunyongwa kwa kuning’inizwa bali aliuawa huko alikokuwa na kuning’inizwa mtini ili ionekane alinyongwa,” alijisemea Inspekta Ado kama vile kulikuwa na mtu aliyezungumzanaye.
Kifupi mezani kwake kulikuwa na majalada tisa na yote yalikuwa yakihusu watu kuuawa na watu wasiojulikana.
Mbaya zaidi ni kwamba hakuna hata mtuhumiwa aliyetiwa mbaroni.
“Hili ni tatizo sana. Kwa nini wahusika hawapatikani? Ina maana wapelelezi wangu wana walakini?” aliendelea kujihoji.
Baadaye alichukua jalada la mauaji ya Mpepechere na kuanza kulisoma.
“Huyu Chepriska anaweza kujua kitu, kwa nini hawa wapelelezi wamemuachia?” alijiuliza na kuamua kupiga simu chumba cha wapelelezi.
“Haloo. Inspekta Ado hapa. Naomba mpelelezi anayeshughulikia kesi ya kifo cha Mpepechere aje ofisini kwangu,” aliamuru.
Baada ya dakika tatu hivi, askari mpelelezi aliingia katika ofisi yake na kunyooka huku akiwa amekakamaa.
“Jambo afande?” akasalimia.
“Jambo. Keti.”
Askari yule aliketi na kusubiri bosi wake atampa maelekezo gani.
“Nilikuwa napitia hili jalada la kesi unayoipeleleza nikaaona yule binti Chepriska umemuachia.”
“Ndiyo afande.”
“Kigezo gani kilikufanya umuachie?”
“Kama umesoma vizuri afande maelezo yake, sijagundua lolote la kumhusisha ndiyo maana siku iliyofuata tukaamua kumuachia lakini tulimuambia kuwa tukimhitaji tutamuita.”
“Kwani hukufanya uamuzi huu peke yako?”
“Ndiyo afande tulikaa jopo la wapelelezi na tukagundua kuwa huyu binti alikuwa mlevi tu ambaye alikuwa akikutana na marehemu baa lakini alikuwa hakujui nyumbani wala kazini kwake.”
“Mlifuatilia huko baa?”
“Nilifuatilia usiku uleule na mwenye baa ya Chambilecho alinihakikishia kuwa wote hao ni wateja wake ambao hawana uhusiano wowote.”
“Uliaminije hilo?”
“Niliamini kwa sababu mwenye baa alisema marehemu siku nyingine alikuwa akija na mkewe au mpenzi wake na kukutana na msichana Chepriska na kukawa hakuna malumbano wala ugomvi na binti huyo naye kwa siku kadhaa alikuwa akija na boifrendi wake na marehemu hakuwa akionesha kuchukia.”
Inspekta Ado aliuma kalamu yake akawa anamuangalia yule askari wake wa upelelezi kisha akafunua jalada la kesi na kutoa simu yake ya kiganjani. Akabofya namba kadhaa, simu ikawa inaita kwani aliitegesha kwenye spika ya nje.
“Akiipokea mwambie anahitajika hapa polisi.”
“Sawa afande.”
“Haloo, ni Chepriska anayeongea?”
“Ndiyo.”
“Tafadhali sana unahitajika hapa kituoni.”
“Sawa nakuja lakini nipe dakika ishirini kwa kuwa siko nyumbani na ni lazima nifike nyumbani kufunga mlango maana nyinyi polisi hamuaminiki.”
“Hatuaminiki kwani sisi wezi?”
“Hapana. Naweza kuja hapo mkanishikilia.
***
Chepriska baada ya kupokea simu akajiona ni mnyonge sana hali iliyomfanya mzee Mitimingi kuwa na wasiwasi.
“Kwani hiyo simu imetoka wapi? Maana baada ya kuipokea umekuwa mnyonge sana, kulikoni?,” akamuuliza.
“Hii simu imetoka polisi. Wananiita .”
“Polisi wanakuita? Tafadhali sana usiwaambie kuhusu huyu mbwa mtu, ukiwaeleza tu, umeniiua, umeelewa?” Mzee Mitimingi alisema hayo huku akiwa ametoa macho.
Je, nini kitatokea?

Fuatilia baadae usiku mwingi......
 
Stori yako ya ukweli lakini mikatisho mikatisho inatufanya tusahau tunako toka na tunako kwenda ehm fanya sote tumeipenda itupie yote hapa au twambie huirushi basi tusipoteze muda kusubiria! Ya ni nzuri sana!
 
Back
Top Bottom