Ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika umeibua fursa nyingi na kuleta ushindi kwa pande zote mbili

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
a9d3fd1f4134970ae7849504e4196cc2a6865d00.jpeg


Sekta ya kilimo katika bara la Afrika ni muhimu sana na inapaswa kupewa kipaumbile zaidi kwani kwa hivi sasa imekuwa ikiendelea kukua na kuleta mabadiliko mengi ya kiuchumi. Sekta hii ndio inashikilia ufunguo wa siri za mafanikio ya kuondoa uhaba wa chakula, kuleta usalama wa chakula na kupunguza umasikini katika bara hili.

Utafiti unaonesha kuwa ukuaji unaotokana na kilimo barani Afrika unachangia pakubwa katika kupunguza umasikini kuliko ukuaji unaotokana na sekta nyingine. Pia inapaswa kukumbukwa kuwa kilimo ndio chanzo cha mapato kwa watu wengi wanaoishi maeneo ya vijijini barani Afrika, na kinachangia zaidi ya nusu ya ajira. Hata hivyo kwa sababu nyingi tu, uwezo wa kilimo katika Afrika bado haujafikia pale unapostahili kufikia na haujawa mkubwa. Je, ili kuinua uwezo huo China inasaidia vipi?

Tangu mwaka 1959, ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika umeweka msingi imara, na usaidizi wa China umeendelea kukua kwa kasi. Upeo wa ushirikiano huu umefika mbali na kupanuka kutoka msaada wa bure uliokuwa ukitolewa hapo awali hadi kuwepo na shughuli nyingi zaidi, zikiwemo biashara na uwekezaji kwenye kilimo.

China inainua uwezo wa kilimo wa bara la Afrika kwa kufanya mambo makuu manne: kusaidia katika ujenzi wa miradi ya ushirikiano wa teknolojia ya kilimo, kulijengea uwezo bara la Afrika katika kuendeleza kilimo, kupeleka wataalamu wa kilimo, na ujenzi wa vituo vya maonesho ya teknolojia ya kilimo. Ushirikiano huu ni sawa na ushindi wa pande mbili katika sekta ya kilimo, kwani kwa sasa biashara ya mazao ya kilimo imeongezeka sana katika miongo miwili iliyopita, hasa tangu China ianze kutekeleza sera ya kutotoza ushuru wa bidhaa kwa baadhi ya nchi za Afrika.

Hivi majuzi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Wang Wenbin, alisema China itaunga mkono na kurahisisha uingizwaji wa bidhaa bora za kilimo na chakula za Afrika katika soko la China, na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa China na Afrika. Hivi sasa aina 25 za bidhaa za kilimo na vyakula kutoka nchi 14 za Afrika zikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Benin na Misri zimeingia China, huku China ikianzisha njia rahisi ya kuagiza bidhaa hizo kutoka Afrika.

Hii yote ni katika juhudi za China kuishika mkono Afrika ili iweze kwenda sambamba na dunia hasa kuiwekea mazingira ya kuwa na kilimo cha kisasa, ambacho kitalisha watu wake wa Afrika, halikadhalika kukitumia kama biashara kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi mbalimbali za Afrika.

Katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Novemba mwaka jana, China ilitangaza kuanzishwa kwa "njia ya kijani" kwa bidhaa za kilimo za nchi za Afrika zinazoingia China, ambapo hivi sasa Idara Kuu ya Forodha imeandaa na kutekeleza kikamilifu hatua kadhaa ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa kama hizo.

Ili kutumia fursa hiyo adhimu inayotolewa na China kwa nchi za Afrika, hivi sasa nchini Tanzania wimbi kubwa la vijana wameamua kugeukia kwenye shughuli za kilimo cha bustani za mboga. Chama cha Kilimo cha bustani Tanzania (Taha) kimesema kwa sasa kinashuhudia vijana wengi wanye nia ya kutengeneza fedha za haraka, wakiongeza shauku yao kwenye kilimo cha bustani. Na wanafanya hivi, zaidi kwasababu mazao ya kilimo cha bustani yanaweza kuchukua muda wa miezi mitatu kuzaa matunda, jambo ambalo linawavutia zaidi vijana hawa kujitosa katika sekta hiyo.

Ni ukweli usiopingika kwamba Afrika ina idadi kubwa sana ya vijana, hivyo ikija kwenye suala la ajira au kujiajiri kidogo huwa unaibuka ukakasi. Kugeukia kilimo ndio njia nzuri na muafaka ya kuweza kuwakwamua kwenye maisha magumu na kuweza kujikimu kimaisha.

China tayari imeshawashika mkono na kuwaonesha wakulima wa Afrika njia ya kupita, hivyo sasa kazi iliyobaki ni kwa wakulima hawa kutumia mbinu, ujuzi na teknolojia kuzalisha mazao ya kilimo na kuyasafirisha kwenye soko la China, ambalo kwa mujibu wa takwimu ni kwamba thamani ya mazao ya kilimo yaliyoagizwa na China kutoka Afrika imeongezeka kwa asilimia 4.4 kwa miaka 4 mfululizo. Kwa juhudi za pamoja za pande zote mbili, kwa hakika biashara ya bidhaa za kilimo na chakula kati ya China na Afrika itastawi na kustawi zaidi.
 
Back
Top Bottom