SoC03 Upotoshaji wa kiuandishi unavyorudisha nyuma maendeleo ya lugha ya Kiswahili

Stories of Change - 2023 Competition

DON YRN

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
474
999
Lugha ya Kiswahili, ni lugha inayokua kwa kasi ikiwa ni miongoni mwa lugha zenye wazungungumzaji wengi duniani. Ni lugha inayozungumzwa sana kwenye nchi za Afrika mashariki na baadhi ya nchi kuifanya kuwa lugha rasmi katika shughuli za kiserikali na katika mazungumzo ya watu yaani lugha ya kwanza kama Taifa. Nchi kama Tanzania, Kenya, na Uganda, lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi. Kiswahili ni lugha ya Kimataifa. Lugha ya Kiswahili huzungumzwa pia nchini Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda. Inakadiriwa kuwa lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji zaidi ya milioni mia mbili(200m) duniani kote.

Nchini Tanzania, kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuifanya lugha ya Kiswahili iendelee kukua zaidi ikiwa ni pamoja shughuli mbalimbali za Kiserikali, Mahakama na Bunge kutumika kwa lugha ya Kiswahili, kuanzishwa kwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili(TATAKI) kwanye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA), Baraza la Kiswahili Zanzibar(BAKIZA), Tume ya Kiswahili(TUKI), Kuanzishwa kwa vyombo mbalimbali kama ITV TANZANIA, TBC, RFA, WASAFI TV/FM, STAR TV, AZAM TV, n.k. Magazeti kama Mwananchi, Nipashe, Mwanaspoti, Jamhuri, Tanzanite, nk. ambavyo vinachochea zaidi ukuaji wa lugha ya Kiswahili kwenye nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisayansi.

Juhudi za Kimataifa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) kuitambua na kuanzisha siku maalum ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili ambayo ni tarehe 07 Julai ya kila mwaka tangu 2022.

Vilevile Kuidhinisha kwa Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi kwenye vikao vya Bunge la Afrika Mashariki tangu 2016, Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano(2018). Lugha ya Kiswahili inatumika kusambaza habari katika vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa kama BBC, DW, RFI, SAUTI YA AMERIKA, n.k.,
Screenshot_20230606_080407_Google.jpg

Idhaa ya kiswahili ya DW. Chanzo: DW.
Screenshot_20230606_080540_Google.jpg
Chanzo:Dw Swahili.
Screenshot_20230606_081301_Google.jpg
Chanzo: BBC Swahili.
Screenshot_20230606_080626_Google.jpg


Chanzo: RFI Kiswahili.

Pamoja na juhudi zote hizi za kueneza lugha ya Kiswahili, kumekuwa na upotoshaji mkubwa mno hasa kwenye suala la UANDISHI wa maneno ya Kiswahili hasa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kama Facebook, Twitter, Instagram, WhatsApp, n.k..

Hali hii inaweza kuonekana kama ni kawaida au kustaarabika kwa watu lakini ni hatari mno katika mustakabali wa lugha ya Kiswahili. Upotoshaji huu upo hadi kwenye vyombo vya habari kama magazeti na televisheni.

Kama tujuavyo, kwa sasa Dunia ni kijiji hivyo hii inatoa fursa hasa kwa jamii au watu mbalimbali kuweza kujifunza lugha yetu pendwa ya Kiswahili kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Kwa mfano badala ya mtu kuandika neno "Hebu njoo" anaandika "Emu njoo", neno "Hauna" anaandika "Auna", neno "Hapana" anaandika "Apana", neno "Uzima wa milele" anaandika "Huzima wa milele", n.k. Na huyu mtu anaweza kuwa ni mtu maarufu kama Mwanasiasa au Mwanamuziki au Kiongozi na anayefuatiliwa na watu kutoka sehemu mbalimbali za Dunia, hii inafikirisha sana kwamba huyu mtu kafundishwa na Walimu wa aina gani?, alifaulu vipi hadi kufikia hapo kielimu au ni ile janjajanja na njia za mkato?.

Anaweza kuwa Mwalimu wa shule ya Sekondari au shule ya Msingi na anafudisha wanafunzi, hebu fikiria hao wanafunzi anawakaririsha maneno ambayo hayapo na matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona kwenye mitandao ya kijamii kuandikiwa vitu visivyokuwepo.

Kwa dalili hizi, kuna hatari kubwa sana ya watu au kizazi chetu cha sasa na kijacho kujifunza maneno yasiyokuwepo kwenye lugha yetu pendwa ya Kiswahili hivyo kuharibu taswira nzima ya Kiswahili ikiwepo watu kujua na kuelewa kuzungumza lugha ya Kiswahili na wasijue kuandika.

Screenshot_20230605_145501_Samsung Internet.jpg

Chanzo: Jamii Forum. Moja ya bandiko la mdau wa Jamii Forum likiwa na makosa ya kiuandishi.
Screenshot_20230605_150201_Instagram.jpg
Chanzo: Istagram. Moja ya bandiko la mdau wa mtandao wa Instagram likiwa na makosa ya kiuandishi.
Screenshot_20230606_075741_Instagram.jpg
Chanzo: Instagram: Moja ya bandiko la ndugu Steven Nyerere kwenye mtandao wa Instagram.
Screenshot_20230606_080849_Facebook.jpg
Chanzo: Facebook. Bandiko la ndugu Thantalo Thantalo kwenye mtandao wa Facebook.

Mambo matatu(3) yafuatayo yafaa kuzingatiwa ili kuepusha upotoshaji huu wa maneno ya Kiswahili hasa nchini Tanzania ambapo ndipo kitovu cha lugha,
Moja, ni kuandaa mfumo maalum au mchujo maalum wa kupata walimu bora wa lugha ya Kiswahili hasa kutoka Chuo kikuu watakaonza kufundisha kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu tofauti na ilivyo sasa kwamba unakuta mwanafunzi alifeli kidato cha nne halafu anaenda kusoma chuo cha Ualimu kisha huyu mtu anapewa jukumu la kufundisha darasa la awali(chekechea) hadi Shule ya Msingi, hii ni hatari sana kwa mustakabali wa lugha ya Kiswahili.

Pili, Serikali kuongeza mishahara na kuzingatia maslahi ya Walimu kuanzia Shule za awali hadi Chuo Kikuu. Hii ina maana ya kwamba Mwalimu anastahili kuwa na mshahara kuliko mfanyakazi yoyote kulingana na majukumu mazito aliyonayo kwenye ujenzi wa Taifa hili la Tanzania lakini ni tofauti kwa nchi yetu kwamba Mwalimu ni mfanyakazi anayedharaulika sana. Maslahi yakiboreshwa huenda hili wimbi la makosa ya kiuandishi yanaweza yakapungua kama siyo kuisha maana huenda walimu wanalipa kisasi kwa kufundisha vitu visivyokuwepo kwenye lugha yetu pendwa ya kiswahili.

Tatu, kuandaa warsha na semina mbalimbali za kuwajengea uwezo na kuwahamasisha hawa watu wanaohusika na masuala ya mitandao wakiwemo watu maarufu, viongozi na wadau wengine ili wawe wawakilishi na balozi wazuri wa lugha ya Kiswahili kwenye mitandao ya kijamii. Kama bidhaa zingine, kiswahili pia ni bidhaa na ili iwe na wateja ni lazima inadiwe na kuwasilishwa vyema pasipo kuwa na makosa ya kiuandishi.

Wako katika ujenzi wa Taifa,
DON YRN.
 
Back
Top Bottom