Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni haki ya msingi kwa kila mtu; usimamizi sahihi wa ulinzi huo ndio mfumo fanisi wa kuilinda haki hiyo

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
ULINZI WA TAARIFA NA DATA BINAFSI.jpg

Haki za Kidigitali kimsingi ni haki ya binadamu katika enzi hizi za mtandao. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuwatenganisha binadamu na mtandao ni ukiukaji wa haki hizi na ni kinyume na sheria za kimataifa.

Kadiri tunavyoendesha maisha yetu mtandaoni - kununua, kushirikiana kijamii na kushirikishana habari - haki zetu za kidigitali, hasa haki za faragha na uhuru wa kujieleza, zinazidi kuwa muhimu.

Tunahitaji kuelewa jinsi taarifa/data zetu zinavyotumiwa na taasisi, serikali na makampuni. Je, zinashughulikiwa kwa haki na kwa uangalifu au zinauzwa au kusambazwa bila idhini zetu? Hivi karibuni tuliona suala la faragha lililoihusu kampuni ya Tigo lilivyoibua mijadala mizito hapa nchini. Hii ni baada ya wakili wa kampuni ya Tigo kueleza mahakama wakati akitoa ushahidi kuwa usiri wa taarifa za wateja kwao si kipaumbele bali utii kwa mamlaka, akimaanisha utayari wa kampuni hiyo kutoa taarifa za wateja bila idhini yao.

Katika nyakati hizi taarifa kuhusu programu za uchunguzi na udukuzi wa kidijitali nazo zinaendelea kuzua mizozo kote duniani. Edward Snowden, whistleblower wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) amewahi kutoa wito wa kuwepo kwa sheria mpya za kimataifa kulinda faragha ya data, akisema kwamba sasa kuna ufuatiliaji wa data kwa wingi na ni wakati wa "kudai haki zetu za kidijitali ili tuweze kuzilinda".

Kwa mujibu wa ripoti ya Freedom House inayoitwa Freedom on the Net, 2021, uhuru wa matumizi ya mtandao wa kimataifa umepungua kwa mwaka wa 11 mfululizo. Ripoti hiyo inaonesha kuwa mazingira ya haki za binadamu mtandaoni yamezorota katika nchi 30 mwaka 2021, wakati ni nchi 18 pekee zilizorekodi ustawi. Uzorotaji mkubwa zaidi ulitokea Myanmar ikifuatiwa na Belarus na Uganda, huku Ecuador ikirekodi ustawi mkubwa zaidi, ikifuatiwa na Gambia.

Mamlaka katika angalau nchi 45 zinashukiwa kupata programu za udukuzi (spyware) za teknolojia juu kwaajili ya uvunaji wa data/taarifa binafsi.

Katika nchi 88 zilizogusiwa katika ripoti hiyo, 39% zipo katika hali ya kutokuwa huru (not free), 28% zipo katika hali ya uhuru kiasi (partly free) huku 21% zikiwa katika hali ya kuwa na uhuru (free). Tanzania si miongoni mwa nchi zilizopo katika ripoti ya Freedom on the Net - 2021, hivyo katika jedwali letu hapa chini inadondokea katika sehemu ya “not assessed”.

Untitled-1 copy (3).png

Chanzo cha Data: Ripoti ya Freedom House ya Uhuru Mtandaoni, 2021 (Freedom on the Net, 2021)

Hata hivyo, nchini Tanzania kumekuwepo azma ya kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection). Julai 2, 2021 wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Muhtasari wa Mfumo wa Dijitali, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndungulile alisema serikali inathamini jambo hilo ambalo linachochewa na ukweli kwamba kwa sasa shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi zinafanyika mtandaoni.

Serikali kupitia Wizara hiyo pia imesistiza suala hilo ambapo imewataka wanaokusanya na kutumia taarifa za watu binafsi, taasisi na Serikali kupitia mitandao kutimiza wajibu wao kwa kuzilinda kwa kufuata kanuni, taratibu, sheria, maadili na nidhamu ya kulinda taarifa hizo kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuzilinda taarifa hizo.

''Matumizi ya mtandao ni haki kwa watu wote ila yazingatie nidhamu, maadili na kufuata kanuni na taratibu”, alisema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habar Dk. Jim Yonazi wakati akifungua mkutano wa nane wa wa masuala ya usimamizi wa mtandao Tanzania (TZIGF) mwezi Novemba 2021.

Mapema mwaka huu, naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Sheria ya Ulinzi wa Taarifa ni ya msingi katika Tanzania ya kidijitali, ili watu wajiamini na kuwa huru.

Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kupitia Ibara ya 16 imeweka bayana umuhimu na Haki ya Faragha, mpaka sasa Tanzania haina Sheria inayosimamia haki hiyo. Bado kuna sheria zingine zinatumika kuingilia faragha na uhuru wa mawasiliano.

Akizungumza kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Data katika maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu mwaka 2019, Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo, alisema suala hilo ni muhimu sana kwani imegundulika kuwa hata kiasi cha Shilingi 50,000 au 100,000 kinaweza kununua taarifa binafsi za watu kutoka mitandao ya simu.

Jamii Forums na wadau wengine wamekuwa mstari wa mbele kutetea uundwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Data ili pamoja na mambo mengine, kuwezesha kutengenezwa kwa mifumo inayofaa ya kukusanyia data binafsi, kuhakikisha usalama wa data hizo pamoja na kuwa na chombo huru kitakachosimamia.

Bado muda upo kwa serikali za kidemokrasia kuchukua hatua ili kulinda haki za watumiaji wa mtandao. Sheria za faragha za data zinapaswa kuzingatia kulinda watumiaji wa mtandao na usimamizi wake unapaswa kuhakikisha kuwa nguvu hazihodhiwi kwenye mikono ya watendaji wachache wakuu, iwe serikalini au sekta binafsi.
 
Back
Top Bottom