SoC02 UKIMWI siyo ugonjwa tishio tena, magonjwa yasiyoambukiza ndiyo tishio kwa sasa, tuchukue tahadhari

Stories of Change - 2022 Competition

Kingsmann

JF-Expert Member
Oct 4, 2018
4,448
16,314
Nikiwa kama askari niliye mstari wa mbele kwenye sekta ya afya, nasikitika kusema UKIMWI siyo tishio tena kama ilivyokuwa zamani, bali magonjwa yasiyoambukiza ndiyo tishio kwa sasa. Jamii inabidi iamke kutoka usingizini maana ubaya wa haya magonjwa ni kwamba hayana dalili za mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine mengi.

Magonjwa yasiyoambukiza yamebatizwa jina la "Wauaji Wakimya (Silent Killers)" kutokana na sifa ya kutoonesha dalili yoyote ile mpaka pale ugonjwa unapofikia hatua mbaya au ya mwisho. Mara nyingi wakati dalili zinaonekana unakuwa tayari uko kitandani hujiwezi, mfano Kiharusi.

Pia magonjwa haya yana gharama kubwa sana kwenye matibabu kwani yanahitaji vipimo na matibabu ya hali ya juu ili mgonjwa aweze kupona au angalau aweze kurudi kwenye hali ya uzima kwa asilimia kadhaa. Hivyo haya magonjwa ni mzigo mkubwa kwa jamii na serikali kwa ujumla kwani baadhi ya wagonjwa wasioweza kumudu gharama za vipimo na matibabu serikali hubeba jukumu hilo.

Magonjwa hayo ni pamoja na:​
1. Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu​
2. Kufeli kwa Figo​
3. Kisukari​
4. Saratani​

NCD.jpg
Photo: IRIN: Mwanamume wa miaka 46 aliyekatwa mguu kutokana na kisukari, moja ya magonjwa yasiyoambukiza.

1. MAGONJWA YA MOYO NA MISHIPA YA DAMU

Magonjwa ya moyo yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na:​
  • Kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye misuli ya moyo (ugonjwa wa moyo), ubongo (magonjwa ya ubongo) na mikono na miguu (magonjwa ya kiateri). Kuziba huku naweza kutokana na kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu au kulundikana kwa mashapo ya mafuta kwenye kuta za ndani za mishipa ya damu ambayo husababisha mishipa hiyo kuwa minene na kubanwa kwa njia ya kupitisha damu.​
  • Kutoka damu kutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo.​
  • Shinikizo la juu la damu kutokana na kupungua kwa mnyumbuko wa mishipa midogo ya damu.​
  • Misuli dhaifu ya moyo - moyo unashindwa kutimiza kazi yake ya kusukuma damu.​
Kwa kawaida, kuziba huku kwa mishipa au kutoka damu ni hali mbaya inayodhihirika kama shambulio la moyo au kiharusi.

Visababishi vya Magonjwa ya Moyo
NCD1.jpg


Dalili zilizozoeleka za Magonjwa ya Moyo
Mara nyingi huwa hakuna dalili zozote za ugonjwa wa mishipa ya damu.
Dalili za shambulio la moyo ni pamoja na:​
  • Maumivu au adha maeneo ya kifuani​
  • Mpapatiko wa moyo​
  • Maumivu kwenye mikono, bega la kushoto, kiwiko, taya au mgongo​
  • Kupumua kwa tabu au kuishiwa kabisa pumzi​
  • Kujisikia kuumwa au kutapika​
  • Kusikia kizunguzungu au kuzimia na kupata baridi ya mwili​
Dalili za kiharusi:
  • Kudhoofika kwa ghafla kwa uso, mkono, au mguu, na mara nyingi hii hutokea kwa upande mmoja wa mwili​
  • Kupatwa ganzi ghafla kwa uso, mkono, au mguu, na mara nyingi hii hutokea kwa upande mmoja wa mwili​
  • Kuchanganyikiwa, kuongea au kuelewa kinachoongelewa kwa tabu​
  • Jicho moja au yote mawili kushindwa kuona vizuri​
  • Kutembea kwa tabu, kupoteza uwiano au uratibu wa mwili​
  • Maumivu makali ya kichwa bila sababu ya msingi​
  • Kuzimia au kupoteza fahamu.​
Dalili za shinikizo la juu la damu:

Mara nyingi huwa hakuna dalili za wazi.
Maumivu ya kichwa, kizunguzungu na mpwito wa moyo kama shinikizo liko juu sana

Dalili za kuwa na magonjwa ya ziada:
  • Moyo kushindwa kufanya kazi - kupumua kwa jitihada kubwa, kuvimba vifundo au tindi za miguu​
  • Kiharusi​
  • Kushindwa kufanya kazi (kufeli) kwa figo – kujisikia dhaifu, kichefuchefu.​
2. KUFELI KWA FIGO

Figo huwa na kazi nyingi sana kama kutoa uchafu na maji kwenye mwili, kuzuia shinikizo la damu, kusawazisha kemikali mwilini , uzalishaji wa chembechembe za damu nyekundu mwilini na kadhalika. Hivyo kutegemea matatizo yaliyoko kwenye figo, dalili huwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine katika ugonjwa sugu wa figo.

Kati ya damu yote inayosukumwa na moyo, takriban moja ya tano ya damu hiyo hupita kwenye figo. Figo lina mamilioni ya mishipa midogo ya damu ambamo damu hulazimishwa kupita na baadhi ya uchafu wa mwili huchujwa kwenda kwenye mkojo. Hivyo, magonjwa yanayoathiri mishipa midogo ya damu (shinikizo la juu la damu, kisukari) pia huathiri figo na matokeo yake yanaweza kuwa ni kushindwa kufanya kazi kwa kiungo hicho muhimu, na hatimaye kushindwa kuondoshwa kwa uchafu mwilini.

Kisukari na shinikizo la juu la damu ni vyanzo vikuu vya kufeli kwa figo kwa idadi kubwa ya watu duniani kote, kunakopelekea uhitaji wa hatua mbadala (usafishaji damu kwa mashine ya figo au kupandikiza figo).

Dalili za kufeli kwa figo
Mapema katika ugonjwa huu,(CKD) wagonjwa wengi hawana dalili zozote za ugonjwa.

Katika hali hii ya ugonjwa sugu wa figo, figo huanza kushindwa kufanya kazi polepole, kwa miezi hata miaka kwa hiyo mwili huzoea hatari za hali hii. Pia, figo huwa na uwezo mkubwa wa kujisaidia katika shida ya kazi zake.kwa sababu hizi mbili, watu walio na ugonjwa huu usiopona huwa hawana dalili zozote hadi wakati figo zimeharibika sana.

Dalili hutofautiana kulingana na kiwango cha ugonjwa. Ili kuelewa vyema na kukabiliana na hali hii vizuri,ugonjwa wa figo umegawanywa katika viwango vitano kulingana na kiasi cha utoaji uchafu kwenye figo (Glomerular Filtration Rate - GFR), ambacho ndio kiwango cha kuonyesha jinsi figo zinavyochuja uchafu kutoka kwenye damu. GFR huhesabiwa kulingana na kiasi cha Creatinini kwenye kipimo cha damu. Kipimo cha GFR ni kipimo sahihi cha kuonesha utendaji wa figo: Utendaji mzuri wa figo ni wakati GFR ni zaidi ya mililita tisini kwa kila dakika (90 ml/min).
NCD2.jpg


Ishara kuu za ugonjwa wa figo ni:
  • Kukosa hamu ya chakula, kichefuchefu na kutapika.​
  • Kuwa mdhaifu, mwili kuchoka na kupungua uzito.​
  • Kuvimba miguu, mikono au/na usoni karibu na macho.​
  • Shinikizo la damu lisilozuilika hasa kwa umri mdogo.​
  • Kukosa nguvu kunakosababishwa na upungufu wa damu mwilini (anaemia), hali inayosababishwa na figo kutotengeneza homoni ya erithropoyetini inayosaidia kutengeneza chembechembe za damu.​
  • Kushindwa kulala, kizunguzungu na kushindwa kuwa makini.​
  • Kujikuna, mkakamao wa misuli (muscle cramps), kuhisi uchovu kwenye miguu na kushindwa kufikiria kitu kwa makini.​
  • Maumivu mgongoni hasa chini ya mbavu.​
  • Kuhisi kutaka kukojoa mara kwa mara hasa wakati wa usiku (nocturia).​
  • Maumivu, Urahisi wa kuvunjikavunjika mifupa kwa watu wazima na watoto kutokukua kwa sababu ya upungufu wa vitamini D inayotengenezwa na figo.​
  • Kukosa hamu ya kufanya mapenzi kwa wanaume na kukosa hedhi kwa mwanamke.​
NB: Kukosa nguvu, kukosa hamu ya chakula, kichefuchefu na kuvimba ni dalili za mapema za ugonjwa wa figo.

Ni wakati gani ushuku ugonjwa wa figo kwa mtu mwenye matatizo ya shinikizo la damu?
Shuku ugonjwa wa figo ikiwa:​
  • Umri wa mgonjwa ni nchini ya miaka thelathini (30) au zaidi ya miaka hamsini (50) shida ya shinikizo la damu inapotambuliwa/ inapogundulika.​
  • Iwapo shinikizo la damu liko juu sana(zaidi ya 200/120mm /Hg).​
  • Shinikizo la damu la juu sana hata baada ya matibabu kuzingatiwa.​
  • Kushindwa kuona kwa sababu ya shinikizo la damu.​
  • Kuwepo kwa protini kwenye mkojo.​
  • Shinikizo la damu kuhusishwa na dalili za ugonjwa wa figo kama vile kuvimba,kukosa hamu ya chakula, kuchoka/kukosa nguvu na kadhalika.​
3. KISUKARI

Kwa kawaida kabohaidreti hugeuzwa kuwa sukari za mwili, hususani glukosi. Mabadiliko haya hufanyika kwenye utumbo. Sukari hiyo hunyonywa kwenye mkondo wa damu na kuzungushwa mwilini kote kwa ajili ya kuzalisha nishati ya mwili.
Wakati wa kula:
  • Kabohaidreti iliyopo kwenye chakula hugeuzwa kuwa glukosi​
  • Glukosi husababisha kongosho kuzalisha insulini kwa wingi zaidi na kupunguza kuzalisha glukagoni​
  • Insulini hushusha sukari ya mwili kwa njia zifuatazo:​
  • Kuchochea uhifadhi wake kama glaikojeni kwenye ini na misuli ya mifupa (kwa kiwango kidogo tu)​
  • Kuruhusu itumiwe na misuli ya mifupa na,​
  • Kuruhusu ihifadhiwe kama mafuta.​
Wakati hamna chakula:
  • Kongosho huzalisha glukagoni kwa wingi zaidi na insulini kwa kiwango kidogo zaidi​
  • Glukagoni huongeza glukosi kwenye damu kwa njia zifuatazo:​
  • Kubadili glaikojeni na protini kuwa glukosi kwenye ini na​
  • Kuchochea kutolewa kwa asidi kutoka kwenye mafuta mwilini.​
Mara tu inapokuwa kwenye mkondo wa damu, sukari huweza kutumiwa na ubongo, moyo, mapafu na figo, ambapo viungo vyote hivi huihiitaji kwa muda wote. Lakini, misuli ya mifupa huhitaji insulini ili iweze kupata na kutumia glukosi. Insulini huwezesha glukosi kuingia kwenye seli za misuli hii na kudhibiti matumizi yake ndani ya seli hizo.

Uzito mkubwa wa mwili na kiribatumbo hupunguza uwezo wa insulini kuruhusu glukosi kuingia kwenye seli za misuli. Kutoshughulisha mwili hupunguza uwezo wa seli za musuli wa kutumia glukosi, hata pale inapokuwa tayari imeingia kwenye seli hizo.

Kisukari husababishwa na:
  • Uzalishaji usiofaa wa homoni za Insulini na Glukagoni unaofanywa na kongosho na/au​
  • Kupungua uwezo wa insulini katika viungo mbalimbali vya mwili​
Kuna aina kuu mbili za Kisukari zilizoenea: Aina ya 1 na Aina ya 2.
  • Katika Aina ya 1 ya Kisukari (huathiri zaidi watu wenye umri chini ya miaka 30) huwa hakuna uzalishaji wa insulini kwa sababu ya kuharibika kwa seli kwenye kongosho (kwa mfano, na virusi).​
  • Katika Aina ya 2 (huathiri zaidi sana watu wazima) kuna ukinzani dhidi ya insulini (kupungua uwezo) na/au uzalishaji wa insulini usio sawa. Takribani 90% ya wagonjwa wote huwa na Aina ya 2 ya Kisukari.​
Kukosa insulini na kuzidi kwa glukagoni hupelekea kutotumika ipasavyo kwa virutubisho vyote muhimu na hivyo kusababisha kiwango kikubwa cha glukosi kwenye damu, kiwango kikubwa cha mafuta kwenye damu, kutokua na kutorekebishwa ipasavyo kwa seli za mwili na kuwa na kinga magonjwa duni.

Visababishi vya Kisukari
Hivi ni pamoja na:

1.Kutoshughulisha mwili hupelekea:​
  • Ukinzani dhidi ya insulini (misuli ya mifupa kuitikia insulini kwa kiwango cha chini, kuchukuliwa na kutumika kwa glukosi kwa kiwango kidogo).​
  • Uzito mkubwa wa mwili hupelekea ukinzani dhidi ya insulin.​
  • Kumbuka imeandikwa: "Kila mtu atakula kutokana na jasho lake": misuli ya mifupa imeumbwa ikitegemewa itatoka jasho kwa angalau dakika 150 kila wiki.​
2. Uzito mkubwa wa mwili - ukinzani dhidi ya insulin.​
  • Kiwango cha uzito mkubwa wa mwili kinachohitajika kutibua Kisukari kinaweza kuwa chini endapo kulikuwa na lishe duni kwa mtoto wakati wa ujauzito. Kwa hiyo, Waafrika wengi hupata kisukari pale tu wanapokuwa na uzito mkubwa wa mwili usiofikia kiribatumbo na hali hii inaweza hutokea wakiwa na umri mdogo.​
3. Glukosi kuzidi kuongeza sukari, vyakula vya kabohaidreti vilivyotakaswa, na kiwango kidogo cha ufumwele kwenye chakula hivyo kupelekea kupita kwa haraka kwa chakula kwenye utumbo mkubwa na hivyo kuingiza kiwango kikubwa cha glukosi kwenye mfumo wa mwili. Kiwango cha juu cha glukosi kwa muda mrefu huharibu kongosho na kuchochea ukinzani dhidi ya insulini.

4. Katika idadi kubwa ya wagonjwa, kuna historia ya ugonjwa huu kwenye familia na hivyo uwezekano wa tatizo hili kuwa la kurithi.

Dalili za Kisukari
Kisukari hupelekea kuwepo kwa glukosi kwenye mkojo. Kuongezeka kwa glukosi kwenye damu na glukosi kwenye mkojo kunaweza kusababisha:​
  • Kusikia sana kiu​
  • Kuongezeka kwa idadi ya kwenda haja ndogo na kukojoa mkojo mwingi​
  • Kusikia sana njaa​
  • Kujisikia dhaifu, kuchoka mwili​
  • Kupoteza uzito (bila jitihada ya kupunguza uzito na licha ya hamu kubwa ya kula) na,​
  • Maambukizi kwenye mkojo (kuungua ha maumivu wakati wa kukojoa)​
Mara nyingi kisukari huwa hakina dalili ya kuongezeka kwa glukosi kwenye damu na hivyo wagonjwa wanaweza kuishi kwa vipindi vya muda mrefu (hata miaka kadhaa) wakiwa na kiwango kikubwa cha glukosi kwenye damu. Kuwa na kiwango kikubwa cha glukosi kwenye damu huharibu viungo vingi vya mwili na wagonjwa wanaanza kutafuta matibabu pale tu dalili zitokanazo na magonjwa haya ya ziada zinapoanza kuonekana.
4. SARATANI

Saratani ni ugonjwa uliosambaa sana na ni wa pili baada ya magonjwa ya moyo kwa kusababisha vifo duniani. Ni ukuaji usio wa kawaida wa seli mwilini na huweza kuvamia maeneo ya jirani na kusambaa mpaka kwenye viungo vya mwili vilivyo mbali kabisa na eneo ulipoanzia kwa njia ya mkondo wa damu au mishipa ya limfu.

Kuna aina nyingi za saratani. Baadhi hujidhihirisha mapema huku baadhi hukaa kwa muda mrefu bila kubainika.

Visababishi vya Saratani
Baadhi ya visababishi vya saratani ni pamoja na:​
  • Kuvuta sigara - saratani za mapafu, mdomo, na tumbo​
  • Kutumia vilevi kupita kiasi - saratani ya ini​
  • Ulaji wa vyakula vilivyotakaswa - saratani ya utumbo mkubwa​
  • Maambukizi ya virusi - saratani za tishu za limfoidi, mlango wa kizazi, ini na tumbo​
  • Tiba ya mionzi ya ioni - saratani za tishu za limfoidi na damu (leukaemia)​
  • Kutoshughulisha mwili.​
Dalili hutegemeana na mfumo husika.
1. Dalili za jumla:​
  • Kupoteza ladha ya kula​
  • Kupungua uzito​
  • Kuchoka mwili​
  • Maumivu ya viungo au maumivu ya fumbatio​
2. Uvimbe usio wa kawaida (kwenye ngozi, matiti)
3. Kutoka damu kusiko kwa kawaida na kunakojirudia (uke, mkojo, njia ya haja kubwa, makohozi, matapishi)
4. Mabadiliko ya tabia ya kawaida ya uchengelele (matumbo)
5. Choo cheusi.
TUCHUKUE TAHADHARI SOTE KWANI MAGONJWA MENGI YASIYOAMBUKIZA YANAEPUKIKA.
 
Back
Top Bottom