HOJA zimekuwa zikijengwa kuwa nchi yetu imefanikiwa kujenga utaifa ambapo hakuna ubaguzi wa kidini au kikabila. Aidha, Mtanzania yeyote ukimuuliza atakuambia kuwa serikali yetu haina dini. Kwa mtazamo huo viongozi hawaongozi kwa utashi wa dini zao kuwahujumu wananchi wasio katika dini moja.
Wanasiasa wanapotoa shutuma dhidi ya watu, wanaodai wana udini, taswira inayojengwa ni kuwa Muislamu ndiye mdini, bali Mkristo hawezi kuwa mdini.
Ndio maana japo serikali na taasisi zake zaweza kuwa imejaa Wakristo ikilinganishwa na Waislamu, haionekani kuwa ni tatizo.
Aidha, ndio maana uongozi wa juu wa CCM ulipokuwa na Wakristo wengi (!?), lakini hausikii CCM ikiambiwa ni chama cha Wakristo au kina udini. Lakini inapotokea chama hicho hicho au kingine, kuwa na viongozi Waislamu basi hubatizwa kuwa chama cha kidini.
Wananchi tunahoji, iweje? Wazandiki hao wadai kwamba baadhi ya vyama au Tassisi ni vya kidini, kwa sababu tu ya kuongozwa na Waislamu, wakati hata vyama au Taasisi wanazo ziongoza wao wenyewe, vimejaa viongozi Wakristo watupu? Au ndio tuseme sasa ndio wananchi wanatakiwa kujua kwamba ndani ya vyama vyao au Taassisi hamna Waislamu? Na kwa maana hiyo ni vyama vya wakristo? Matamshi ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa yanatia kichefuchefu. Kama ni ushahidi, sasa umepatikana kumbe yaliyokuwa yakisemwa ni kweli, udini upo tu pale ambapo Mwislamu ni kiongozi au anaposhika madaraka katika taasisi za umma.
Mayowe yote tunayosikia ya udini na mara nyingine na ukabila, yanayopigwa na walaghai, ni katika kuendeleza hila za kuwalaghai wananchi, ambao bado wanadhaniwa kuwa ni punguwani, hasa wale wanaoambiwa kwamba hawakusoma.
Wananchi wamekwisha baini kwamba, kumbe wale wanaodai kuwa wanaupiga vita udini, ndio hasa wanaouendeleza nchini. Upitizi wa makini wa kitabu "Kanisa Katoliki na siasa Tanzania Bara 1953-1985" unatoa habari za ndani zisizo za kawaida juu ya kampeni dhidi ya Uislamu.
Kwa sababu zisizoeleweka kitabu hiki kimeandikwa na kuchapishwa na waumini wa Kanisa hilo. Yaliyomo ndani ya kitabu hicho hayajakanushwa wala kubishiwa na serikali ya Muungano ya Tanganyika au CCM, huu ukiwa ni ushahidi kamili juu ya ukweli wa kukiri juu ya neno hilo.
Kwa sababu na malengo yoyote ya kutolewa kitabu hicho, na lazima ziwepo sababu za msingi za kufanya hivyo, kitabu hiki ni ufunuo mzuri juu ya mbinu za chini kwa chini za Kanisa katika medani ya kisiasa Tanzania.
Kitabu kinaeleza ni Kanisa Katoliki lililojenga njia ambazo ziliwawezesha kuwa na mahusiano ambayo kitabu hicho inaeleza yalikuwa ya karibu kabisa na TANU wakati wa miaka ya kupigania uhuru. Kinaonesha ni vipi Kanisa lilitayarisha waumini wake shupavu ambao walikuwa wameshika karibu nafasi zote muhimu katika serikali mpya ya Kiafrika ya Tanganyika. Lakini hatukusikia wanachi wakilalamika kuwa serikali ina udini, japokuwa wakristo ndio waliokuwa wamejazana kwenye nafasi kubwa kubwa za uongozi na ndio walio kuwa wengi wenye madaraka.
Kwa wale viongozi, wawe wa Kanisa, CCM au serikali ya Muungano ambao walikuwa wakijipigia kelele kutenganisha kwa siasa na dini, lakini wao wenyewe wakiwa ndio waendelezaji wakubwa wa hilo, wana kazi ngumu ya kuelezea kwa umma kwa ujumla lakini zaidi kwa Waislamu. Sivalon anaelezea juu ya mpango na njama zinazoendelea zikishirikisha Kanisa Katoliki, Chama (TANU-CCM) na serikali ya Muungano.
Tangu njama hizo ziwekwe wazi 1992 hapakuwa na kauli moja ya kupinga au kutolea maelezo juu ya hilo. Huku ni kukiri kwa dhahiri juu ya mipango na njama za Kanisa zinazofanywa hali zikiwa zinaeleweka na mkono wa chama na serikali yake.
Yafuatayo ni baadhi ya madondoo kutoka kitabu hicho:
"Mwishowe tutakuja kuonesha jinsi Rais mstaafu Nyerere alivyokuja kuwa kiungo cha pekee kati ya chama/kanisa na Kanisa Katoliki. Uhusiano huo unaelezwa kwanza kama msingi wa kuelewa jinsi gani na kwa kiasi gani viongozi wa Kanisa walivyoingilia kati maendeleo ya siasa hapa Tanzania (uk. 5).
Huo uhusiano ukawaweka viongozi wa Kanisa katika nafasi nzuri ya kuelekeza maelekezo ya siasa Tanzania. (uk. 9).
Kinyume na kampeni inayosambazwa, Waislamu sio chanzo ila wao ni waathiriwa wa mbinu za makusudi za kujenga mfumo wa uhasama ambao unawanyonya watu wa dini zote mbili na siasa ili kuwabana Waislamu na pia kupata uwezo wa kuwakandamiza.
Wananchi wamekwisha kujua kwamba, vyama vingi vya siasa hapa nchini ni matawi ya Chama Cha Mapinduzi, vilivyobuniwa makusudi, ili kuwagawa wananchi wasiwe na nguvu za kuleta mabadiliko ya uongozi wa chama cha siasa nchini.
Na kwa kumalizia wakristo hao waliokuwa wameshika madaraka makubwa na kuiongoza serikali ya Tanganyika na sasa serikali ya Jamhuri ya Tanzania ndio walio tuletea umaskini huu, tulio nao hivi leo. Wao ndio waliokuja na sera ya Azimio la Arusha na kuiba mali za wanachi, wao ndio walio kuja na sera ya vijiji vya ujamaa na kusababisha maafa makuwa kwa wanachi.
Je tukisema kuwa Wakristo wameiangamiza nchi hii ya Tanzania tutakuwa tumekosea?