Ubepari wa Kigeni Katika Uchumi wa Tanzania Leo

Pile F

Senior Member
Aug 15, 2020
121
170
Habari ya siku, wasomi wa kweli, nguvukazi yetu na watu mlio Imara. Poleni na shughuli na purkushani za hapa na pale. Mola awajaalie mpate afadhali zaidi. Moja kwa moja kwenye Mada:

Pamoja na Ubepari wa kibinafsi na mabwanyenye wa kienyeji hapa Tanzania, kuna utaratibu wa uzalishaji mali wa kibepari wa kigeni wenye kuwakilishwa na makampuni, shughuli na manzili zake za aina mbalimbali, na kuambatanisha uchumi wa nchi kwa mapeo haya au yale.

Inafahamika kwamba sawa na mabepari wa kienyeji wa Tanzania, wenzao wa kigeni pia wanajitahidi kujipatia faida kubwa kutokana na unyonywaji wa kazi za ujira. Lakini bila ya shaka hawa wa kigeni wako mbele zaidi kwa viwango vya ukuaji wa nguvu za uzalishaji mali, ufundi na teknolojia, njia za matengenezo ya kazi na mapeo yenyewe ya uzalishaji.

Mara nyingi shughuli za kibepari zimekuwa ni sehemu za makampuni makubwa ya kuhodhi mali na yavukayo mamlaka ya kitaifa.

Kujiingiza kwa haya makampuni katika uchumi wa nchi kunayanufaisha sana kwa pande mbalimbali. Kwa mfano, ni katika nchi yetu ndiko yanapohamishia mara kwa mara sehemu 'chafu' za utaratibu wao wa uzalishaji mali, na kwa hivyo, kuokoa mali chungu nzima ambazo ingeyalazimu kuzitumia kwa ajili ya kuzuia kuchafuliwa kwa mazingira kutokana na uendeshwaji wa shughuli hizo huko kwao.

Miongoni mwa sehemu nyingine zenye kuyavutia makampuni haya kuingiza na kupanua mirija yao katika uchumi wetu ni gharama za chini za kuajiri kazi, 'ulaini' wa sera ya kodi, udhaifu wa udhibiti wa kisheria juu ya shughuli zao, pamoja na fursa nyingine nyingine nyingi zenye kuyawezesha kujichumia faida nyingi.

Baadhi ya nyakati imesemekana kwamba ni makampuni hayo tu ya kibepari ya kigeni ndiyo yanayoweza kuhimiza maendeleo ya nchi zilizozorota kiuchumi. Katika upande huo, serikali fulani za nchi zimefika mbali hadi kutangaza "sera ya kufungua mlango wazi" na kutoa nafasi zote kwa kukaribisha rasilimali za kigeni.

Watetezi wa mwongozo huo wanadai kwamba ilivyokuwa makampuni ya kibepari ya kigeni yamejipatia ufundi na teknolojia ya daraja ya juu, wataalamu wenye maarifa mengi, njia bora za matengenezo ya kazi, vyanzo vikubwa vya fedha na vifaa, basi ni makampuni hayo tu ndiyo yanayoweza kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ya nchi, ambayo Ubepari wake wa kienyeji ungali bado haujapata nguvu ya kuishughulikia.

Inapasa kusisitiza kwamba utetezi huo huzingatia tabia za kiufundi-kiuchumi tu za huu utaratibu wa Ubepari, wala haugusii madhumuni ya kijamii-kiuchumi, na lililo muhimu zaidi hausaidii kufafanua matokeo yake ya baadae katika maendeleo ya kijamii-kiuchumi ya nchi yetu.

Kwa mfano, inajulikana kwamba kima cha faida zipatikanazo na makampuni ya kibinafsi ya kigeni katika nchi changa kama yetu huwa ni asilimia 300 - 400 na hata zaidi! Kwa hakika tunalipa gharama kubwa mno kwa uingizwaji na utumiaji wa rasilimali kutoka ng'ambo.

Hata hivyo, haja ya kujibebesha mzigo mzito kama huo ingeliweza kuchukuliwa kama ni ya kukubalika laiti kama Ubepari wa kigeni ungelidhaminia nchi yetu kuendeleza uchumi wake wa kitaifa upesi na bila ya kusita, na lililo muhimu zaidi, kwa pande zake zote kabisa, pamoja na kuiwezesha nchi yetu kujitoa kwenye hali ya Umaskini.

Walakini hiyo siyo madhumuni ya matajiri walioko ng'ambo. Wala si bure utaratibu wa Ubepari wa kigeni unazidi kukabiliwa na malalamiko. Sababu kuu ya malalamiko yao ni:
  1. Ubepari wa kigeni, kama kawaida, huwa hauingizi rasilimali zake katika miradi itokanayo na mipango ya maendeleo ya uchumi wa kitaifa.
  2. Makampuni ya kigeni yanasafirisha ng'ambo sehemu kuu ya faida yanazochuma, wala hayakubali kuingiza tena katika uchumi wa kitaifa.
  3. Matarajio ya nchi yetu ya kujipatia ufundi na teknolojia ya kisasa kutoka kwa makampuni haya hayakusibu. Nchi nyingi zinazoendelea hazijajipatia msingi wa kitaifa wa maendeleo ya sayansi na ufundi. Mnamo miaka ya karibuni tegemeo la kiufundi kwa makampuni ya kibeberu si kama halikupungua, bali hata limezidi kuongezeka.
  4. Ubepari wa kigeni hutumia kidogo sana kazi za ujira na vyanzo vya kienyeji vya mali na vifaa. Shughuli zake zenye kuandaliwa kwa ufundi na teknolojia ya hali ya juu, huwa hazihitaji wafanyakazi wengi. Wakati huohuo makampuni haya huingiza katika nchi si kama mashine na vyombo tu, bali pia aina nyingi za vifaa na malighafi zilizopo kwa kutosha huko kwao.
  5. Kwa kumudu kulipa mishahara yenye kupita kima chake katika nchi yetu makampuni haya yanajitahidi kujivutia kwao MAKADA wa kitaifa wa nchi, jambo ambalo hutia hasara kubwa uchumi, na hasa kwenye sekta yake ya kiserikali.
  6. Makampuni haya hutumia mara kwa mara mifuko yao maalum 'ya uwakilishi' kwa kuwahonga wafanyakazi wa chombo cha serikali katika nchi, jambo ambalo linapelekea katika kuzidisha ulaji rushwa na upotofu wa aina nyingine.
Bila shaka wote tunaweza kuendeleza zaidi orodha hiyo ya matokeo ya uingizwaji na ukuzwaji wa shughuli za kibepari za kigeni katika nchi yetu, ambayo yana madhara sana kwa maendeleo ya kijamii-kiuchumi ya nchi.

Lakini pia ifahamike kuwa, sababu ya kuligusia tatizo hili si kukomeshwa kwa mahusiano yoyote yale baina ya nchi yetu na rasilimali za kigeni bali ni kuainisha haja ya utekelezwaji wa madai muhimu tunayoyatoa kama nchi katika kupigania kuanzishwa kwa mfumo mpya wa mahusiano ya kiuchumi ya kimataifa.

Ushirikiano wa mataifa yote lazima utegemezwe juu ya msingi wa faida na haki sawa.

Nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza ikaiachia rasilimali ya kigeni nafasi maalum katika uchumi wake wa kitaifa kwa kipindi fulani cha maendeleo yake. Lakini tuna uhakika kwamba utaratibu huo wa Ubepari wa kigeni hautaweza abadan kuchukua jukumu la kuamua na kuongoza mwendo wa ukuaji na uimarikaji wa uchumi wa nchi yetu.
 
Back
Top Bottom