SoC02 Tutunze mazingira ya jiji la Dar es salaam ili kupunguza joto na mafuriko

Stories of Change - 2022 Competition

Khamdudulu

New Member
Aug 14, 2022
1
0
Kila mmoja atafakari,ni nini kitatokea endapo kila kaya/familia/nyumba itapanda miti miwili tu kuizunguka nyumba hiyo,nini kitatokea baada ya miaka michache tu ya kupanda miti hiyo.

Kila taasisi, iwe ya ki raia au kiserikali,ikaamua kupanda miti miwilimiwili tu kwenye kila uwazi au pembezoni mwa barabara,baada ya miaka michache nini kitatokea?

Serikali kwa ujumla wake ikaamua kusimamia upandaji wa miti kwenye kingo zote za mito bila kujali ni mto wa msimu au wa kudumu, naamini kabisa baada ya miaka mitatu Dar es Salaam yote itakuwa ya kijani yenye ubaridi wa kuvutia.

Upandaji miti maeneo yote yenye uwazi na sehemu zote zinazozunguka makazi unaweza kuwa ni rahisi sana, kinachohitajika zaidi ni utayari wa mtu mmojammoja,taasisi na nguvu ya serikali kwa ujumla, kuanzia ngazi ya kaya,mtaa hadi taifa.

Ni kweli,kuna maeneo ambayo baadhi ya miti huepukwa kupandwa kutokana na hofu ya mizizi yake kuleta nyufa katika nyumba, hata hivyo, inaweza kutumika njia nyingine ikiwa ni pamoja na kupanda miti ya matunda au miti yoyote ilimradi izalishe hewa ya kutosha katika maeneo husika.

Kadri miti itakavyopandwa kwa wingi katika mikoa yote yenye hali ya ujangwa au yenye uhaba au uchache wa miti,ninauhakika ndani ya miaka mitano tangu kupandwa kwa miti hiyo lazima kutakuwa na mabadiliko chanya ya hali ya hewa.

Tuchukulie mfano wa wenzetu,wakazi wa mikoa ya Nyanda za juu kusini,hususani, Iringa,Njombe,Mbeya na Rukwa. Mikoa hii inasifika sana kuwa na baridi yenye uwiano sawa kutokana na ari ya upandaji miti kuwa kubwa. Kwa kawaida, kila mti unapokuwa tayari kwa kuvunwa, kabla ya kukatwa mti huo, pembeni yake hupandwa mti mwingine kama mbadala wa mti unaotakiwa kukatwa.

Zoezi hili endelevu hufanya mazingira hayo kuwa oevu na yenye kutunza uasilia miaka yote. Kwa kifupi ni kwamba upandaji miti umekuwa sehemu ya utamaduni wao,na ukionekana unaharibu misitu kwa aidha kukata miti ovyo bila kupanda mingine,au kuanzisha moto porini kwa lengo la kuharibu misitu kwa maksudi huonekana kama msaliti katika jamii.

Dunia ni yetu,Tanzania ni yetu,ile sauti ya kuyatunza mazingira yetu lazima itoke ndani kabisa mwa mioyo yetu.

Baadhi tu ya faida ambazo tutazipata kwa kupanda miti ya aina mbalimbali nje faida ya hali ya hewa nzuri ni pamoja na kutengeneza mandhari nzuri ya nchi au eneo husika, matunda ya kila aina, dawa kutokana na matunda au mizizi au majani,au magome yanayopatikana kwanye miti hiyo,kivuli,mazalia ya ndege na viumbe mbalimbali,kinga dhidi ya mmomonyoko wa udongo, na rutuba kwenye ardhi husika.

Kupitia matunda biashara itaibuka na hivyo kuleta maendeleo kwenye jamii inayoyazunguka maeneo hayo, kupitia mitishamba utafiti wa tibaya magonjwambalimbali utavumbuliwa,na huenda hata kukawa na maabara kabisa kwaajili ya kufanyia utafiti huo na hivyo kutengeneza fursa za ajira kwa watu mbalimbali. Vilevile kupitia viumbe mbalimbali watakaoishi au kupumzika katika miti hiyo itakuwa ni chanzo cha utalii na furaha ya kuwatazama wanyama,ndege au viumbe hao.

Mfano halisi ni katika bonde la Kilombero mkoani Morogoro,hususani katika vijiji vya Mwaya,Mkula,Kidatu na Mang’ula nikitaja kwa uchache,maeneo haya yamezungukwa na miti ya asili na ile ya kupandwa,moja ya faida zipatikanazo katika eneo hili ni uwepo wa wanyama wa kuvutia sana wakiwemo MBEGA WEUPE na WEKUNDU ambao ni kivutio kikubwa kwa wapita njia na wakazi wa maeneo hayo. Si hayo tu,uwepo wa miti hiyo (mitiki,milingoti,na ile miti ya asili) unafanya eneo hilo kuwa na hali ya hewa ya kuvutia sana bila kujali majira husika. Uoto huo huleta mvua za kutosha na hivyo kuwezesha shughuli zingine za kiuchumi hasa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Mimi na wewe tunayo nafasi ya kuleta mabadiliko chanya ambayo yataleta tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Watu binafsi, taasisi za umma na binafsi na mashirika mbalimbali yakisimama na kuungana lazima kutakuwa na tija katika zoezi hilo. Jiji la Dar es Salaam lina wilaya tatu. Kila wilaya ikichukua nafasi yake hakika Dar es Salaam itaitwa jiji la kijani.

Wilaya ya Kinondoni pekee ikiamua kupanda miti elfu tano tu ya aina mbalimbali, ndani ya miaka mitatu kutakuwa na mabadiliko yenye faida kubwa sana kwa binadamu na viumbe vingine.

Kadhalika kwa wilaya ya Temeke na Ilala, zikiamua kupanda miti elfu kumi bila kujali aina ya mti huo ilimradi usiwe na madhara kwa afya ya viumbe hai, hakika tutakuwa mbali.

Vivyohivyo kwa wilaya ya Kigamboni, tukifanya hivyo kwa pamoja na kwa ushirika wa wadau mbalimbali, tutapunguza joto la jiji hilo na tutazuia baadhi ya magonjwa yatokanayo na mazingira au mabadiliko ya tabia nchi kwa ujumla.

Faida zingine ni kwamba uwepo wa miti au mimea hiyo utasaidia kurejesha upya viumbe hai ambavyo vilikuwa katika hatari ya kutoweka, vilevile, vitafufua vyanzo vya maji ambavyo vilikauka au kuharibiwa na shughuli za kibinadamu sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Katika umoja wetu, tuamke na tulifufue jiji letu. Kila mtu kwa nafasi yake ajione kwamba analo deni la kurekebisha mazingira yake mahali anapoishi kwa faida yake na faida ya wengine pia.

Uwepo wa miti utavutia ndege wazuri wa kuvutia, utaleta hewa nzuri,utaleta matunda yenye faida kwa binadamu na wanyama, na utaleta uvuli wenye kuburudisha nafsi zetu. Tuyapende mazingira yetu,tuupende mkoa wetu, tulipende jiji letu.
 
Back
Top Bottom