na Sauli Giliard
LICHA ya Rais Jakaya Kikwete kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuachana na ununuzi wa mitambo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans, kauli hiyo sasa inaonekana kutotekelezeka, Tanzania Daima Jumapili imebaini.
Machi 31, mwaka jana akitoa hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alihitimisha mvutano uliokuwepo kati ya TANESCO na Bunge juu ya ununuzi wa mitambo ya Dowans.
Ripoti ya Wizara ya Fedha na Uchumi imeainisha gharama ambazo serikali inaingia katika uendeshaji wa mitambo ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kutoa mapendekezo kuwa sasa umefika wakati mitambo ya Dowans ikanunuliwa kuliko kuendelea na mitambo ya IPTL.
Ripoti ya wizara hiyo, iliyowasilishwa kwa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ya Bunge wiki hii, imebainisha kuwa serikali inaweza kutumia sh bilioni 6.4 pekee iwapo itanunua mitambo ya Dowans kuliko gharama inazoingia sasa kuiendesha IPTL.
IPTL iliyoingia nchini mwaka 1997 wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, inaligharimu taifa kiasi cha sh bilioni 20 kila mwezi, zikiwa ni gharama za kununulia mafuta lita 14,125 za mafuta mazito pamoja na kuwalipa wafanyakazi.
Ripoti hiyo imetoa mchanganuo wa gharama hizo unaoonyesha kila mwezi serikali inalazimika kununua kiasi hicho cha mafuta kwa gharama ya sh bilioni 13.6 kila mwezi, kununua mafuta mengine kwa sh milioni 996 na sh bilioni 2 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi.
Katika mchanganuo huo, Tanzania Daima Jumapili imebaini kuwa iwapo serikali itanunua mitambo ya Dowans, inaweza kuokoa kiasi kisichopungua sh bilioni 13 kila mwezi na kukielekeza katika huduma nyingine za kijamii ambazo zinalegalega.
Katika kile kinachoonekana kuitiisha serikali na kuona hakuna mbadala mwingine zaidi ya Dowans, ni kuwa iwapo mitambo ya IPTL haitatumika, taifa litagharamika mara sita zaidi ya kiasi kilichopo kwa sasa.
Kwa mantiki hiyo, taifa linaweza kuingia gharama zaidi na kufikia takribani bilioni 60 kwa mwezi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kuwa hata vyanzo vya maji vikijaa na kutumia umeme kutoka kwenye mabwawa mbalimbali bado IPTL itaendelea kulipwa kutokana na mkataba uliopo hivi sasa.
Ripoti hiyo imeweka bayana kuwa pamoja na Dowans kuonekana kuwa ahueni kuliko IPTL, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha umeme wa uhakika wa megawati 105 kwa gharama ya sh bilioni 6.4 kwa mwezi badala ya takribani sh bilioni 20 zinazolipwa kila mwezi kwa IPTL inayozalisha megawati 100.
Kupanuka kwa shughuli za kiuchumi huku idadi kubwa ya watu ikiingia katika kundi la watu wenye kipato cha kati, taifa lina upungufu wa megawati 225 huku takwimu zikionyesha ni asilimia 14 tu ya Wanzania takriban milioni 40 ndiyo wanaotumia umeme majumbani mwao.
Ripoti hiyo ilibainisha, iwapo itasubiriwa kununua mitambo mingine huku taifa likikabiliwa na kiasi hicho cha nishati, italichukuwa taifa miaka miwili kuipata na kutabiri uchumi kuingia katika hali mbaya zaidi..
Tanzania Daima Jumapili ilifanya jitihada za kumtafuta kwa simu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Fedha na Uchumi, Abdallah Kigoda, kuona iwapo imeridhia mapendekezo ya kununua mitambo ya Dowans, simu yake iliita bila kupokelewa.
Alipopigiwa mara ya pili, Dk. Kigoda alipokea na kukata sumu mara moja: Siwezi kuzungumza sasa, niko kwenye kikao.
Kwa upande wake Waziri Mkulo, alikiri kuwepo ripoti hiyo na kusisitiza hawezi kuzungumzia lolote kwa vile aliyeiwasilisha kwenye kamati ya Bunge ni naibu wake.
Niko Kilosa, siwezi kuzungumzia lolote maana sijui wabunge waliipokeaje na kuizungumzia vipi.
Ni vizuri ukawasiliana na Naibu Waziri, Jeremia Sumari, ama Katibu Mkuu utapata maelezo zaidi, alisema Waziri Mkulo.
Ripoti hiyo ya wizara inaiweka serikali katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi kwani mwaka jana Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, alishauri serikali kununua mitambo hiyo lakini wazo lilitupiliwa mbali.
Nawapongeza viongozi wa TANESCO kwa uamuzi wao wa busara wa kuachana na nia yao ya kununua mitambo ya Dowans. Wameyasoma vizuri mazingira na nyakati na kufanya uamuzi muafaka.
Pili, niwaombe wanasiasa wenzangu kuwa maadam waliokuwa na nia ya kununua mitambo hiyo hawanayo tena, suala hili limemalizika, alisema Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi iliyorushwa kwenye vituo vya runinga Machi 31, mwaka jana.
Baada ya hapo, Aprili mwaka jana, serikali ilitangaza zabuni ili kumtafuta mzabuni wa kuleta mitambo mipya na kuachana na ya Dowans iliyochukuliwa kuwa ni chakavu lakini hadi kufikia Septemba, hakukuwepo dalili zozote za kuipata mitambo mipya.
Kitendo hicho, pamoja na mitambo ya Kihansi na Pangani kushindwa kufanya kazi kutokana na uchakavu wake na kupungua kwa kina cha maji, kilichukuliwa kama hujuma inayofanywa na watendaji wa TANESCO kwa lengo la kufanikisha azma yake ya kununua mitambo ya Dowans.
Wabunge hasa wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini walipinga kununuliwa kwa mitambo ya Dowans kwa kuwa ilirithi mitambo ya kampuni ya Richmond Development iliyoshindwa kuzalisha umeme licha ya kulipwa sh bilioni 152 kila siku.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, alifikia hatua kusema ni bora taifa likaingia gizani kuliko kununuliwa kwa mitambo hiyo ya Dowans.
Hata hivyo baada ya mwaka jana taifa kuingia kwenye mgawo mkubwa wa umeme kwa saa 14 hadi 16, kamati hiyo na serikali kwa ujumla ilikubaliana mitambo hiyo iiuzie TANESCO umeme ila kutoka kwa mtu binafsi.
Baada ya kutokuwepo dalili za kufikiwa makubaliano ya kupata umeme wa uhakika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma, alimtaka Rais Kikwete kufanya maamuzi magumu kwa kuitaifisha mitambo hiyo.
Serikali kuanza kutumia umeme wa IPTL mwishoni mwa mwaka jana licha ya pande hizo mbili kuwa na kesi, ilitokana na uamuzi alioufanya rais kwa kumwamuru Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, kushughulikia masuala yote ya kisheria dhidi ya kampuni hiyo. Aidha, Waziri Mkulo aliambiwa ahakikishe wizara yake inatoa fedha zinazohitajika, wakati Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akitakiwa kuhakikisha masuala yote ya kiufundi yanashughulikiwa baina ya TANESCO na IPTL.