hii nimeisoma na kujiuliza maswali mengi sana:
jee kuna ukweli kuwa wako vigogo ndani ya CCM wanawafadhili wapinzani kwa pesa au njia nyengine ili kujiweka sawa 2010?
jee kuna wafanyabiashara ambao wanataka kuwania urais kwa kupitia umoja wa upinzani na sasa ndio wanaoufadhili upinzani kuzunguka nchi?
jee fedha inayotumika ikiwa suala A na B sio zinatokea wapi?
jee ni sahihi kutembea nchi nzima na kuwapandish hasira takatifu wananchi?
na baada ya kuwapandisha hasira jee kuna lipi ambalo laweza kutokea kutokana na hasira hizo?
jeee litakalotokea ni faida kwa taifa?
ni maswala ni mengi huenda na wenzangu mkisoma yataongezeka na pengine tutapata majibu ya haya na hayo
Wapinzani wadaiwa kufadhiliwa na 'mtu anayetaka urais 2010'
Mrema akana, asema yeyote ni mfadhili wao
Adai helikopta gharama rahisi kuliko shangingi
Waziri Chenge asema hawezi kujibu 'utumbo'
Na Reuben Kagaruki
VYAMA vinne vilivyoanzisha umoja wa kushirikiana vya Tanzania Labour Party (TLP) NCCR-Mageuzi, CHADEMA na Chama cha Wananchi (CUF) vinadaiwa kufadhiliwa na mfanyabiashara mmoja maarufu mwenye malengo ya kugombea urais mwaka 2010 ili viongozi wa vyama hivyo wazunguke nchi nzima kusaidia kumwekea mambo yake sawa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, alikana na kusisitiza kuwa wanafanya kazi hiyo ili kuamsha Watanzania wapate hasira 'takatifu' waondokane na undondocha unaowafanya wanyamaze kimya huku nchi ikitafunwa na kikundi cha wachache.
Alikana madai hayo huku kukiwa na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari kuwa kuna mfanyabiashara anayefadhili vyama hivyo vianze kazi ya kumsafishia njia asiweze kupata shida ya kuingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Bw. Mrema alisema wao kazi wanayoifanya ni takatifu na mtu yeyote mwenye uchungu na nchi hii anaweza kuwasaidia kufanikisha lengo hilo.
"Lengo ni kuwahamasisha Watanzania wapate 'hasira takatifu' kwani wamezidi mno kuwa ndondocha wakati ufisadi unazidi kuwa mkubwa," alisema na kuwaomba watu waadilifu wakiwemo viongozi wa dini wajitokeze kusaidia vuguvugu la ukombozi dhidi ya watu walioamua kupora nchi.
Alisema mbali ya kutumia helikopta, ikiwezekana watatembea kwa miguu au mikokoteni kueneza hasira takatifu ili watu wagomee kigenge alichoita ni cha walaji wachache wanaoendeleza ufisadi huo.
Alipobanwa zaidi amtaje mfadhili wao alisema; "Ni mapema mno kusema kuna mfadhili. Sisi hatuna hela za rushwa, wala bangi, wala dawa zakulevya ...kama kuna mtu mwema ajitokeze atusaidie,".
Alipoulizwa kama hawana fedha wamepata wapi uwezo wa kukodi helikopta, Bw. Mrema alisema; "Nimegundua gharama za kuendesha shangingi ni kubwa kuliko helikopta. Mfano tulikwenda Sumbawanga (Rukwa) kwa saa. Tulitumia fedha kidogo kuliko tungetumia shangingi," alisema.
Alisema ni jambo la kusikitisha kusikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro, akihaha kutafuta sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 822 wakati huo kuna watu hapa nchini wanajitangaza kwenye vyombo vya habari wanapata kipato zaidi ya fedha anazohitaji.
Alisema hayo wakati akirejea agizo la Bw. Kandoro kutaka wakazi wote wa Dar es Salaam kuchangia sh. bilioni 10 za ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi watakaomaliza darasa la saba mwaka huu watakaofaulu kwenda sekondari mwakani.
Wakati huo huo, Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge aliyekuwa Mwanasheria Mkuu katika Serikali ya awamu ya tatu aliyetajwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa kama mmoja wa viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwa kuishauri vibaya Serikali katika mikataba alisema hana muda kujibu 'utumbo huo'.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili kutoka Sengerema, Mwanza aliko kwenye ziara, Bw. Chenge alisema kwa kifupi: "Mimi nakagua barabara huku bwana. Sina muda wa kujibu utumbo huo na kukata simu yake ya mkononi.
Bw. Chenge anakuwa mtu wa pili kujibu hadharani tuhuma zilizoelekezwa kwake na Dkt. Slaa. Wa kwanza alikuwa mwanasheria, Bw. nimrod Mkono.
Bw. Mkono juzi alikanusha tuhuma zilizoelekezwa kwake kwa kutoa vielelezo kutoka wakala wa Usajili wa Makamouni BRELA vinavyoonesha makampuni aliyodaiwa kuwa Mkurugenzi si yake na akachanganua malipo yake ya mabilioni ya fedha anayolipwa kihalali katika kesi ya Benki Kuu (BoT).
Source : majira