Nchi sasa inayumba
Mwandishi Wetu Aprili 16, 2008
Lowassa, Rostam, Chenge, Mkapa moto
Kikwete, CCM, Bunge watishwa
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) na Serikali zake vinasukwasukwa kiasi kwamba kuna hofu kwamba kama hali haitabadilika nchi itafika pabaya, imeelezwa.
Watu mbalimbali waliozungumza na Raia Mwema wiki hii wanalitaja suala la kuzuiwa kwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kujitetea kuwa dalili za mwisho za jinsi hali ilivyo mbaya ndani ya CCM, hali ambayo inaigusa pia Serikali.
Watu hao wanataja pia tukio la Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye ana fedha nyingi za kigeni nje ya nchi kuwa ufa mwingine ndani ya CCM na Serikali ambako Chenge anaheshimiwa sana.
Yanatajwa pia matukio kama ya wizi ndani ya Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mikataba mibaya ya uchimbaji madini na kushindwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua thabiti juu ya watuhumiwa, wengine watu wa karibu naye, kuwa ambayo yanatia doa katika mchakato wa nchi kujiletea maendeleo.
Ni mambo hayo, habari zinasema, ambayo yameibua mgawanyiko kwenye CCM na serikalini katika makundi ya wanasiasa wenye nguvu upande mmoja kiasi kwamba sasa mazungumzo ya wazi yameibua mjadala wa kuanza kutafuta mrithi wa Rais Kikwete, miaka miwili kabla ya kipindi chake cha kwanza kwisha.
Anasema mwanasiasa mmoja kuhusu mjadala huo: Katika mfumo wa vyama vingi tulioiga kwa wenzetu kama mnakuwa na kipindi mlichojiwekea basi mnamuacha huyo aliyepo amalize kipindi hicho. Lakini mkianza kumjadili hata kabla ya kipindi chake cha kwanza kwisha, hiyo ina maana kwamba kwenye chama chenu kuna matatizo makubwa.
Lakini vyanzo mbalimbali vya habari vinasema sababu kubwa ya kukua kwa mtikisiko huo ni jinsi Kikwete alivyoliachia gurudumu la kile kinachoitwa mapambano dhidi ya ufisadi, huku likiwakumba watu waliokaribu naye na hata wasaidizi wake ndani na nje ya serikali.
Matuko ya hivi karibuni yakiwamo yale yaliyotokea bungeni mjini Dodoma na baadaye katika vikao vya CCM kijijini Butiama, yamechochea moto wa mtikisiko huo ndani ya CCM na serikali yake.
stori inaendelea