THE MODERN WAR: Simulizi ya kijasusi mapenzi na upelelezi

THE MODERN WAR
(Vita ya kisasa)
Sehemu ya.............35
Mtunzi: Saul David
Email: saulstewarty@gmail.com
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Hakuwa mwingine bali Mheshimiwa Profesa Cosmas Kulolwa, Rais mstaafu wa awamu iliyopita.
"Mheshimiwa...!!" Osward aliita kwa sauti ndogo iliyoambatana na mshangao.
"Karibu Osward, kijana wangu mtiifu" Alisema Profesa Cosmas Kulolwa.

SASA ENDELEA...
"Kwa nini uko hapa mheshimiwa?"aliuliza Osward huku akipiga hatua kusogea karibu zaidi na Profesa Kulolwa
"Nimekufuata wewe Osward"
"Kuna usalama kweli mheshimiwa?"
"Hapana, ndio maana niko hapa kuna kazi nataka kukupatia"
"Kazi gani? Mbona mimi bado nashikiriwa na polisi itawezekanaje labda usubiri nitoke kwanza mheshimiwa"
"Hapana utaifanya ukiwa huko huko na kama ukifanikiwa basi nitakupa vitu muhimu sana unavyovitaka Osward"
"Mheshimiwa....!!"
"Sikiliza Osward nayajua mahitaji yako yote muhimu kwa sasa, kwanza unataka kuwa huru yaani ushinde kesi yako mahakamani na huwezi kishinda kama Inspekta Aron ataendelea kuwa hai, pili najua unampenda sana Najma binti wa Dokta Gondwe. Sasa kama utaifanya vizuri kazi yangu basi nitakupa hivi vyote kwa wakati mmoja, unasemaje?" alieleza Profesa Cosmas Kulolwa huku akimalizia kwa swali

Osward alibaki kimya kwa muda, ni kweli kati ya vitu alivyokuwa akivitamani sana kwa wakati ule kwanza ilikuwa ni uhuru, atoke gerezani pili ilikuwa ni kumuua Inspekta Aron mtu aliyesababisha asote gerezani kwa kipindi chote lakini ndio huyo huyo pia aliyemuua bwana Big' mtu wake wa karibu sana na tatu Osward alikuwa akimpenda sana Najma binti wa Dokta Gondwe Waziri wa afya.

"Mheshimiwa ni kazi gani hiyo? Alafu kwa nini mimi? Mbona unavijana wengi tu wazuri wako huko uraiani" Aliuliza Osward, Profesa Kulolwa akatabasamu kisha akapiga hatua karibu zaidi na Osward akamshika begani.

"Kijana wangu, nakupa wewe kazi kwa sababu tayari ni mmoja wetu. Hili si agizo langu ni agizo kutoka juu kwa wakubwa zetu, ni kuhusu mpango wa vimelea vya V-COBOS najua ulikuwa mshirika chini ya Dokta Gondwe lakini kuanzia leo utakuwa chini yangu"

"Unamaana gani mheshimiwa?"
"Dokta Gondwe ameharibu kazi, anatakiwa kuuwawa na wewe ndio utakayetekeleza jukumu hilo Osward"
"Nini?"
"Ndio hivyo kijana wangu usishangae, shukuru mungu hawa watu hawajataka wewe ufe isipokuwa Dokta Gondwe pekee, wewe utaendelea kuwa mshirika wetu kama kawaida. Kwa ajili ya usalama wetu mimi na wewe na Najma mwanamke umpendae ni lazima Dokta Gondwe afe"
"Lakini nawezaje kufanya hivyo, Dokta Gondwe ni rafiki yako wa mda mrefu, mtu mkubwa serikalini, alafu pia ni baba wa mwanamke nimpendae"
"Osward kwa ajili ya kumuua Inspekta Aron, kwa ajili ya uhuru wako, kwa ajili ya Najma mwanamke wako, na kwa ajili ya kulinda vimelea vya V-COBOS Dokta Gondwe anatakiwa kufa kabla ya jua la leo kuzama"
Kauli hii ilimfanya Osward atulie kwa muda akawa anatafakari ofa hiyo aliyopewa na Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa, baada ya kuwaza sana mwisho akaongea.

"Sawa nimekubali, lakini itawezekanaje leo ndio siku yangu ya hukumu sijui nini kitatokea kule mahakamania nitashinda kesi au laa! sijui Inspekta Aron ameandaa nini huko, nitawezaje kufanya kazi yako mheshimiwa"

"Muhimu umekubali Osward,najua unacho kikosi chako cha kazi, nimeshaandaa mpango mzima na hivi tunavyoongea tayari tupo kwenye utekelezaji wa mpango huo, mimi ndio nikiyepeleka mbele siku ya kusikilizwa kesi yako sasa mpango mzima uko hivi..." Alisema Profesa Cosmas Kulolwa na hapo akaanza kueleza jinsi alivyosuka mpango wa kumuondoka Dokta Gondwe Dunia, kushinda kesi ya Osward mahakamani na kumdhibiti Inspekta Aron. Osward akawa anatikisa kichwa akiashiria anaelewa vizuri maelezo anayopewa.


Usiku huo huo katika hospitali ya Mountenia ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi alicholazwa Sultana anaeigiza kuwa mgonjwa, kwa mara nyingine tena anakutana na kijana wake wa kazi Jasusi Shadow.
"Mnh! Niambie Shadow, umefanikiwa kumjua aliyemrekodi Dokta Gondwe na Jesca wakiwa chumbani?" Aliuliza Sultana akiwa amesimama nyuma ya dirisha kubwa akitazama jiji kwa nje. Jasusi Shadow alikuwa amesimama nyuma yake na kuinamisha kichwa chake kwa unyenyekevu mkubwa. Kama kawaida yake alikuwa amefunika sura yake kwa maski.

"Hapana ila kunakitu ninahisi Madam"
"Enhe! Nini unahisi"
"Baada ya kufanya uchunguzi nimegundua mtu aliyesambaza hizi picha mtandaoni anajaribu kumtisha Dokta Gondwe na lengo lake kubwa anavitaka vimelea vya V-COBOS, Dokta Gondwe asipompatia ataachia mtandaoni video yote ya ngono inayomhusisha Jesca na Dokta Gondwe" Alieleza Jasusi Shadow
"Hii inawezekanaje? Ni nani huyo mtu?"
"Nahisi huenda akawa mwanao Tino, japo sina uhakika" alisema Shadow kauli iliyomfanya Sultana ageuke nyuma kwa kasi na kumtazama.
"Tino? Yaani Tino awe na video ya mke wake akimsaliti alafu akae kimya mpaka sasa, unawaza ujinga gani Shadow?"
"Madam inawezekana, kwa kuwa Tino anavitaka sana vimelea vya V-COBOS basi anaweza kuitumia hiyo kama njia ya kuvipata bila kujali ndoa yake na Jesca,"
"Hapana Shadow hawezi kuwa Tino, ataitoa wapi video kama hiyo? Alafu hujui ni jinsi gani Tino anampenda Jesca, asingeweza kukaa kimya hata chembe acha kuamini huo ujinga" Alisema Sultana, akili yake iligoma kabisa kukubaliana na hisia za Shadow.
Kimya kilitawala kwa sekunde kadhaa.

"Sikia Shadow, haijarishi anaevitaka vimelea kutoka kwa Dokta Gondwe ni Tino au ni mtu mwingine tofauti lakini sisi lazima tupige hatua moja mbele yao, tumefanya uzembe mara ya kwanza hatuwezi kuendelea kukaa na kusubiri. Kama Dokta Gondwe atavitoa vimelea maabara kuu ya serikali na kumkabidhi huyo mtu basi tutapoteza kila kitu na mimi siko tayari kuona hilo linatokea. Wasiliana na Jesca kuna watu nimewaandaa mtashirikiana kwa pamoja kuvamia maabara kuu ya serikali, hakikisha mnarudi na sanduku la vimelea"
"Hapana Madam hii kazi nitaifanya mwenyewe usijali"
"Hauhitaji watu wa kukusaidia?"
"Ndiyo Sultana"
"Una hakika?"
"Ndiyo, nikiwa mwenyewe itakuwa rahisi" Jasusi Shadow alijibu kwa kujiamini
"Kumbuka mara ya kwanza ulishindwa shadow"
"Ni kweli Madam, lakini hata hivyo sikutoka mikono mitupu nilitoka na ile chupa ya kijivu yenye kinga na tiba dhidi ya vimelea vya V-COBOS, safari hii lazima nifanikiwe"
"Sawa nasubiri taarifa njema kutoka kwako hapo baadae"
"Sawa, lakini madam!"
"Nini, niambie?"
"Vipi kuhusu ile chupa ya kijivu iko wapi?" Jasusi Shadow aliuliza swali muhimu sana, hiki ndio kitu alichokuwa amebakiza kutoka kwa Madam Sultana, tayari alishajua mama huyu anazo tamaa za kuvitaka virusi vya COBOS kwa ajili ya masirahi yake binafsi tofauti na mipango waliyokuwa nayo awali hivyo Shadow aliendelea kubaki karibu naye ili tu kuweza kumdhibiti.

"Kwa nini umeuliza?" Sultana aliuliza huku akimtazama Shadow kwa macho ya udadisi.
"Nataka tu kujua kwa sababu za kiusalama, tangu mzee afariki sijui chupa hiyo iko wapi, mambo ni mengi Madam lolote linaweza kutokea"
"Mmmh"
"Ndiyo Madam"
"Fanya kazi Shadow, tambua mipaka yako" Sultana aliongea kauli ambayo iliuvunja kabisa moyo wa Shadow.
"Sawa madam, samahani kama nimekosa kuuliza"
"Sawa kafanye kazi, nasubiri taarifa nzuri hakikisha ukirudi hapa baadae uwe na sanduku lenye vimelea vya V-COBOS baada ya hapo nitakwambia ni wapi tulihifadhi ile chupa ya kijivu"
"Sawa Sultana"
Shadow aliitikia kwa unyenyekevu mkubwa kisha akatoka na kuondoka tayari kwenda kuifanya kaz aliyoagizwa, kuvamia maabara kuu ya serikali na kuviiba vimelea vya V-COBOS virusi hatari vilivyohifadhiwa ndani ya maabara hiyo pasipo serikali kujua. Hii inabaki kuwa siri ya viongozi wachache sana serikali ambao wanashirikiana kwa ukaribu na maabara ya ZMLST kutoka nchini Mexico ambao ndio wahusika wakuu wa vimelea hivyo.


Muda ulizidi kwenda masaa yakazidi kusogea, usiku ulikuwa ni mrefu kwa Najma ambae wakati wote alikuwa akiilaumu nafsi yake baada ya kushindwa kumwambia Inspekta Aron ukweli anaoujua kuhusu vimelea vya V-COBOS, angefanya nini sasa? Aseme kila kitu na kumuweka baba yake matatizoni zaidi? au akae kimya alafu baadae mamilioni ya watu wafe kwa ugonjwa hatari utokanao na kirusi cha COBOS? Najma bado hakuwa na chaguo sahihi.

Usiku ulikuwa mrefu pia kwa Inspekta Aron ambae alikuwa amelala juu ya kochi sebureni ndani ya nyumba ya Inspekta Jada akisubiri kwa hamu kupambazuke ili ashuhudie haki ikitendeka dhidi ya muuaji Osward kule mahakamani. Inspekta Aron aliwaza pia kuhusu lile neno V-COBOS aliloambiwa na Najma alafu baadae tena akalikuta kwenye karatasi aliyoachiwa na jasusi Shadow kabla hajatoroka.

Annah nae alikuwa ameamka kitambo sana, alimtoroka chumbani Inspekta Jada kisha akasogea hadi kwenye kona moja jirani na sebure alikolala Inspekta Aron. Annah alikaa hapo akawa anamuangalia mwanaume huyo ambae alikuwa akijitoa kwa hali na mali kuhakikisha anamlinda. Annah alijikuta anampenda sana Inspekta Aron, hakujali tena kuhusu hatima ya maisha yake baada ya kubaki yatima, moyoni alidhamilia jambo moja tu muhimu kwake akisema iwe mvua iwe jua lazima aunase moyo wa Inspekta Aron kama yeye alivyounasa moyo wake.

Bado usiku huu ulikuwa ni mrefu pia kwa Rais mstaafu mheshimiwa Profesa Cosmas Kulolwa, tayari kila kitu alichopanga kilikuwa kikienda sawa saawia sasa lilibaki ni suala la muda tu, akisubiri kusikia kifo cha Dokta Gondwe, kifo cha Inspekta Aron na kuachiwa huru kwa Osward.


Hatimaye kukapambazuka, ikiwa ni majira ya saa 12 asubuhi, Osward ambaye tangu usiku alipotoroshwa gerezani hakuwa amerejea tena. Wakati huu alionekana yeye pamoja na wanawake watatu wakiwa katikati ya msitu mmoja mnene. Wote walikuwa wamebeba mabegi makubwa mno mkononi mwao. Wanawake hawa hawakuwa wakionekana sura zao, walivaa baibui zenye rangi nyeusi zilizowafunika vizuri kuanzia juu mpaka chini, kisha usoni wajitanda na kitambaa cheusi(nikabu), ikiwa ni vazi linalojulikana maarufu kama ninja.
Walikuwa ni wanawake waliotembea kikakamavu sana Osward akiwa katika yao, walitembea na kuingia ndani ya helikopta iliyokuwa ikiwasubiri. Mara tu baada ya wote kuingia rubani alifanya kazi yake na mara helkopta ile ikazunguusha panga zake na taratibu ikaachia ardhi na kupaa hewani.


0756862047,(WhatsApp)
Je, nini kitafuata?
Ni Osward huyu huyu mwenye kesi inayotakiwa kusikilizwa mahakamani leo?
Ni Osward huyu huyu anaetakiwa kumuua Dokta Gondwe?
Lakini pia ni Osward huyu huyu anaetakiwa kumuua Inspekta Aron?

Ni upi mpango aliosuka Profesa Cosmas Kulolwa?
ITAENDELEA...
 
THE MODERN WAR
(Vita ya kisasa)
Sehemu ya...............36
Mtunzi: Saul David
Email: saulstewarty@gmail.com
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Walikuwa ni wanawake waliotembea kikakamavu sana Osward akiwa katika yao, walitembea na kuingia ndani ya helkopta iliyokuwa ikiwasubiri. Mara tu baada ya wote kuingia rubani alifanya kazi yake na mara helkopta ile ikazunguusha panga zake na taratibu ikaachia ardhi na kupaa hewani.
Je, nini kitafuata?
SASA ENDELEA...


"Mama yako anarudi leo kutoka marekani, atafika saa saba mchana. Nahitaji kukamilisha ratiba zangu mapema kisha twende uwanja wa ndege tukampoke"
"Sawa baba, nitakuwa hapa nakusubiri twende wote"
"Vipi hauendi kusikiliza kesi ya mchumba wako Osward?"
"Ooh! Nilishasahau baba hivi ni leo?"
"Mmh! Mwanangu inaelekea huyo Inspekta Aron anakuchanganya sana mpaka umeanza kusahau mambo muhimu"
"Hapana sio hivyo baba mbona nimeshakuelekeza kila kitu kuhusu Inspekta Aron, yule ni rafiki yangu tu"
"Haya sawa, kesi yake inasikilizwa leo kwa mara ya mwisho na hukumu itatolewa nina imani atashinda na kuachiwa huru, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kama yeye ndiye aliyeua"

Haya yalikuwa ni maongezi kati ya Najma na baba yake Dokta Gondwe ikiwa ni asubuhi na mapema majira ya saa moja.

"Basi sawa nitaenda"
"Ndio mwanangu ni muhimu sana ukawepo pale ili msherehekee ushindi kwa pamoja"
"Sawa baba, vipi wewe hautokuwepo?"
"Mmh! Nikipata muda nitakuja ila asubuhi hii nakutana na waandishi wa habari kwanza baada ya hapo nitaenda kuonana na Rais ikulu, kama muda utakuwepo nitakuja mahakamani" alieleza Dokta Gondwe

"Waandishi wa habari unakuta nao mda gani?"
"Sio mda, saa mbili na nusu pale nje ya jengo la Maendeleo CFC"
"Sawa ni kuhusu ile kashfa si ndio baba"
"Ndiyo mwanangu, baba yako nimechafuliwa sana mitandaoni mimi na serikali yangu, nahitaji kutumia nguvu kubwa kusafisha jina langu na kuweka mambo sawa, mama yako amekasirika sana naongea naye hataki kabisa kuelewa"
"Ndio maana anarudi bila hata kuniambia?"
"Ndiyo Najma, ki ukweli mama yako ana hasira sana"
"Usijali baba kila kitu kitakuwa sawa, naamini hakuna ukweli wowote hapo tunaimani na wewe baba" Najma alijaribu kumpa maneno ya faraja baba yake, mwisho wakaagana Dokta Gondwe akaingia kwenye gari yake akiongozana na walinzi wake wawili safari ya kuelekea ukumbuki wa Maendeleo CFC sehemu aliyopanga kukutana na waandishi wa habari ikaanza.

Huku nyuma Najma nae alijikuta anatamani kuona namna baba yake atakavyokuwa akiongea mbele ya waandishi wa habari, alichukua fungua ya gari la familia aina ya Noah akaingia na kuanza safari akimfuata baba yake nyuma taratibu.


Wakati Dokta Gondwe akiwa bado njiani mara simu yake iliita alipoitazama namba ya mpigaji ilikuwa ni ile ya mtu aliyekubaliana nae kumpa vimelea vya V-COBOS mtu mwenye video yake chafu. Ilikuwa ni namba ya ajabu ambayo inapiga tu lakini yeye hawezi kupiga wala kutuma ujumbe wa maandishi, ni namba ambayo hutoweka hewani na kuwa namba ambayo haipo mara tu baada ya simu kukata.

"Hallo"
"Ndiyo Dokta Gondwe" sauti ya ajabu iliyojaa mwangwi na kitetemeshi kikubwa ilisikika upande wa pili, Tino ndiye aliyekuwa akizungumza lakini haikuwa rahisi kwa Dokta Gondwe kumtambua.
"Nakusikia ndugu yangu"
"Sisi tumeshamaliza kazi yetu, umebaki wewe tu. Tulikubaliana ndani ya siku tatu uwe umetupatia virusi vya COBOS la sivyo basi tusije kulaumiana"
"Naelewa ndugu yangu siwezi kuwageuka, mmenisaidia sana kupost ile picha ya pili isiyo na sura yangu hivi naenda kuongea na waandishi wa habari kwa mara nyingine baada ya hapo nitaanza mpango wa kuwaletea vimelea vya V-COBOS" Dokta Gondwe alijieleza kwa unyenyekevu mkubwa.
"Lini sasa"
"Leo jioni, nipigie simu leo jioni nitawambia ni wapi pa kukutana niwakabidhi vimelea"
Kauli hii ilimfurahisha sana Tino, alijiona kabisa namna anavyokwenda kushinda vita hii kwa kuvipata vimelea vya V-COBOS, hakujua kuwa mtu anaemtegemea tayari yupo hatarini kuuwawa ikiwa ni agizo kutoka ZMLST ya Mexico wamiliki wakuu wa vimelea vya V-COBOS. Ukiachilia mbali kuhusu hao wazungu wanaotaka kumuua waziri wa afya Dokta Gondwe lakini pia kulikuwa na balaa la Sultana na kijana wake wa kazi Jasusi Shadow ambaye alipanga leo hii kuvamia maabara kuu ya serikali na kuviiba vimelea vya V-COBOS, swali linabaki kuwa ni nani ataibuka mshindi.

Nyumbani kwa Inspekta Jada..
"Jada, vipi Annah bado amelala?" Aliuliza Aron
"Mmh! Nikikwambia kitu basi unaweza kuamini" alisema Inspekta Jada huku akitabasamu na kuangalia pembeni
"Nini hicho?"
"Huyu binti ndio ameingia sio mda kulala"
"Eeh! Una maana gani usiku wote alikuwa wapi? Au alikuwa analia?"
"Walaa"
"Alikuwa wapi sasa?"
"Alinitoroka chumbani akaja akakaa hapo"
"Hapo wapi?"
"Kwenye kona hapo ameshinda anakuangalia wewe usiku kucha"
"Nini? Annah huyu... Hebu acha utani wako basi"
"Wallah nakuambia ukweli Inspekta Aron, huyu binti naona anakupenda tena sio kidogo sana tu"
"Acha masihara yako basi Jada"
"Kweli tena"
"Haya hebu tuachane na hayo basi, ratiba imekaaje!?"
"Kesi itaanza kusikilizwa saa tano asubuhi, itakuwa sapraizi kubwa sana watakapomuona Annah yuko hai mtu wanaeamini kuwa walimuua"
"Sana tuombe mungu tu kila kitu kiende vizuri" alisema Aron
"Vipi kwani unawasiwasi Aron?"
"Yeah kiasi, unajua mpaka sasa sijui ni kwa nini kesi haikusikilizwa jana na badala yake wakataka iwe leo"
"Mmh! Kwa hiyo unahisi kuna kitu hakipo sawa?"
"Ndiyo hisia zangu zinaniambia hivyo"
"Sawa, muhimu ni kuongeza umakini tu Inspekta Aron, Annah ndio kete yetu ya muhimu kuliko vingine vyote, huyu ndio atakayefanya Osward afungwe lakini pia kumuweka hatiani Dokta Gondwe"
"Sawa Jada, kwa hiyo tunafanyaje twende na Annah ofisini tukae nae hadi mda utakapofika ndio twende mahakamani au tumuache huku tutamfuata baadae?"
"Mmmnh! Hapo mimi nawaza tumuache huku hadi muda utakapofika ndio tumfuate"

Walikubaliana hivyo lakini kabla ya kuondoka Inspekta Aron aliingia chumbani akitaka kwanza kufanya mazungumzo na Annah.
"Samahani nimekuamsha"
"Usijali Aron, niambie"
"Sisi tunatangulia kazini muda wa mahakamani ukifika nitakuja kukuchukua" alieleza Inspekta Aron
Annah alitulia kwa muda kisha akaongea...
"Aron"
"Yes Annah usijali naona kama unawasiwasi, niamini mimi kila kitu kitakwenda sawa nitahakikisha wote waliohusika na mauaji ya wazazi wako wanawajibishwa ipasavyo, leo tunaanza na Osward alafu baada ya hapo Dokta Gondwe na wengine watafuata"
"Tatizo sio hilo Aron"
"Ni nini Annah" aliuliza Inspekta Aron huku akimtazama Annah usoni, Annah naye akainua uso wake na kumtazama Aron wakatazamana.
"Ukweli siwezi tena kuendelea kujizuia Aron, haijarishi nini kitatokea huko mahakamani kushinda au kishindwa lakini sitoweza kuondoka na ndugu zangu, nataka kubaki na wewe Aron nakupenda, nakupenda sana. Nina hisia za kimapenzi kwako moyo wangu umeshindwa kabisa kuvumilia najua utaniona mwanamke wa ajabu lakini sio kosa langu Aron ni moyo, Nimekupenda" Annah alijieleza huku akiwa ametazama chini na kuchezea chezea vidole vyake.

Inspekta Aron alibaki ameduwaa kwa muda hakuwahi kuwaza kama siku moja Annah angekuwa na ujasiri wa kuongea maneno kama yale mbele yake licha ya kuona dalili za Annah kumpenda lakini hakuwahi kuwaza kama siku moja angekuja kutamka mwenyewe kwa kinywa chake.

"Annah" Inspekta Aron aliita
"Tafadhali usiseme neno lolote Aron, nilikuwa tu naeleza hisia zangu kwako najua haukuwa ukitegemea, nimeongea mimi leo wewe utaongea siku nyingine sawa baba" Alisema Annah huku akitembea na kwenda kukaa kwenye kona ya kitanda, Aron akataka kuzungumza lakini mara Inspekta Jada akaingia ghafula.

"Aron tuwahi kazini tafadhali kuna mambo mengi ya kufanya kabla ya kwenda mahakamani" alisema Jada huku akichukua koti lake refu kabatini, akalivaa na kutoka.
Aron alimtazama Annah usoni, Annah akampa ishara kuwa aende. Taratibu Aron alisogea karibu yake akamkumbatia kwa sekunde kadhaa...

"Nitarudi kwa ajili yako Annah, usijali" Alisema Aron kisha akamuachia na kuondoka.
Waliongozana na inspekta Jada kuelekea lilipokuwa gari lake.
"Si nilikwambia" alisema Jada
"Kuniambia nini?" Aliuliza Aron
"Kuwa haka ka binti kanakupenda"
"Aah! Kwa hiyo ulikuwa unasikiliza?"
"Hahah ndo maana nikaingia kukusaidia, mwanaume mzima unajiumauma unashindwa kutoa jibu, mtoto mbichu yule shauri ako, au usharusha nyavu kwa Najma nini?"
Alisema Inspekta Jada na hapo wote wakacheka kwa pamoja wakati huo tayari safari ya kuelekea kituo cha polisi cha kati Morton ilianza.


Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa alionekana amesimama juu kabisa ya nyumba yake yenye urefu wa ghorofa nne, alikuwa akilitazama jiji ikiwa ni asubuhi ya mawio wakati jua likichomoza, alichukua simu yake akapiga namba fulani na kuiweka simu sikioni.

"Hallo mkuu" sauti ya Osward ilisikika upande wa pili wa simu ile
"Nambie mambo yanaendaje"
"Kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa mheshimiwa, nitamuua Dokta Gondwe wakati anafanya mazungumzo na waandishi wa habari, Inspekta Aron atashughulikiwa na wale mabinti Malaika weusi tayari wapo kazini, baada ya hapo nitarudi gerezani kisha nitapelekwa mahakamani" Osward alisikika akieleza
"Sawa hakikisha hakuna anayekuona ukiwa nje ya gereza, saa nne kamili uwe umerudi pale tulipokutana usiku, yule askari atakusindikiza kukurudisha gerezani kwa siri kama ilivyokuwa mwanzo. Kila kitu kipo sawa usijali"
"Sawa mheshimiwa" alijibu Osward kisha simu ikakatwa.

"Oops! Rafiki yangu kipenzi tena wa kitambo sana, tangu tukiwa shuleni, tumesoma wote nje ya nchi, tumeingia kwenye siasa kwa pamoja nikawa Rais ukawa Waziri wa afya lakini leo nalazimika kuyaondoa maisha yako mimi mwenyewe, nisamehe sana Dokta Isaack Gondwe" Profesa Kulolwa alikuwa akiwaza huku akilegeza vifungo vya shati lake na kuvuta pumzi ndefu.

Je, nini kinaendelea kwenye mkutano wa Dokta Gondwe na waandishi wa habari?
Osward atamuua Dokta Gondwe?
Vipi kuhusu Najma ambaye atakuwepo eneo la tukio?
Vipi kuhusu kesi ya Osward mahakamani?
Wale wanawake watatu wanaojiita Malaika weusi watafanya nini?
Inspekta Aron atakuwa salama?

TUKUTANE SEHEMU INAYOFUATA...

Simulizi ni shillingi 1,000/= lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina saul au Airtel money namba 0788967317 jina saul kisha njoo WhatsApp inbox namba hizo hizo
 
THE MODERN WAR
(Vita ya kisasa)
Sehemu ya..............37
Mtunzi: Saul David
Email: saulstewarty@gmail.com
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA....
"Oops! Rafiki yangu kipenzi tena wa kitambo sana, tangu tukiwa shuleni, tumesoma wote nje ya nchi, tumeingia kwenye siasa kwa pamoja nikawa Rais ukawa Waziri wa afya lakini leo nalazimika kuyaondoa maisha yako mimi mwenyewe, nisamehe sana Dokta Isaack Gondwe" Profesa Kulolwa alikuwa akiwaza huku akilegeza vifungo vya shati lake na kuvuta pumzi ndefu.

SASA ENDELEA...


Kama ilivyo ada pilikapilika za hapa na pale zilikuwa zikiendelea ndani na nje ya kituo cha polisi cha kati Morton, askari walikuwa bize na kazi zao huku watu mbalimbali waliokuja kushtaki kustakiana au kuwatazama ndugu zao waliolala lumande nao wakizidi kumiminika na kufuata utaratibu maalumu uliowekwa kituoni hapo.

Katika eneo maalumu la kupaki gari za watu wasio wafanyakazi wa kituo hicho cha polisi kulikuwa na gari nyingi zimesimama na moja kati ya gari hizo ilikuwepo Noah nyeusi ambayo ndani yake walikuwa wanawake watatu waliovalia baibui na nikabu zilizofunika sura zao. Hawa walikuwa ni wale wanawake watatu ambao awali walionekana wakipanda helikopta wakiwa pamoja na Osward.
Asia, Erica na Elina haya ndio majina ya wanawake hao watatu huku Erica na Elina wakiwa ni mapacha waliokuwa wakifanana sana, haikuwa rahisi kuwatofautisha kama ndio kwanza unawatazama kwa mara ya kwanza. Wote kwa pamoja walijiita malaika weusi, kilikuwa ni kikundi maalumu cha siri cha wanawake hawa hatari ambao walikuwa wakitumika na baadhi ya vigogo nchini katika shughuli mbalimbali za kiharifu. Kila ilipotokea tajiri fulani akakwama kufanya jambo fulani lenye uhitaji wa kutumia nguvu ikiwa ni pamoja na kuua aliwatumia Malaika weusi kutekeleza jukumu hilo. Walikuwa wamejikamilisha kwa kila idara, hawakuwahu kuharibu wala kushindwa kazi yoyote. Leo kwa mara nyingine wakiwa pamoja na Osward wanapewa jukumu zito na mpango kabambe uliosukwa na Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa.

Wakiwa ndani ya gari hilo macho ya Erica na Elina yalikuwa makini kuangaza huku na huku kuangalia wafanyakazi wa kituo hicho waliokuwa wakiingia kazini asubuhi hiyo, Asia yeye alikuwa ambele kwenye siti ya dereva

"Yule pale amefika" Mara Elina aliwaambia wenzake, wote wakageuka kutazama upande ule aliokuwa anatazama Elina hapo ndipo walipomshuhudia Inspekta Aron akiwa pamoja na Inspekta Jada wakishuka kutoka ndani ya gari, ndio kwanza walikuwa wanafika.

"So?" Aliuliza Asia
"Hatuna muda wa kupoteza Erica fanya yako" alisema Elina

Hapo Erica akapandisha nikabu yake vizuri akaziba sura yake na kuacha wazi sehemu ya macho tu. Aliangaza macho huku na huku kisha akafungua mlango akashuka na kuanza kupiga hatua kumfuata Inspekta Aron na Jada ambao walikuwa wakielekea upande zilipo ofisi zao kitengo cha upelelezi.


Inspekta Aron na inspekta Jada walitembea mwendo wa taratibu huku mara kadhaa wakisalimiana na kutaniana na maaskari wengine. Akiwa amefika kwenye mlango wa ofisi yao mara kuna ujumbe wa maandishi ukaingia kwenye simu ya Inspekta Aron akasimama na kuusoma. Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa yule rafiki yake askari magereza Kanondo mahali alipo Osward.

,,,,,,,, Aisee Osward haonekani hapa gerezani tangu asubuhi, nimejaribu kufuatilia na kuuliza naambiwa alizidiwa usiku akapelekwa hospitali sidhani kama kuna ukweli katika taarifa hii inspekta Aron au wanataka kukwepa kesi isisikilizwe na leo tena,,,,,,,,

Inspekta Aron aliirudia kuusoma ujumbe huo mara ya pili, taratibu taa nyekundu ikawaka kwenye akili yake.

"Vipi kwema?" Aliuliza Jada ambaye tayari alikuwa ameshaingia ofisini lakini alishangaa kuomuona Inspekta Aron bado amesimama mlangoni yupo bize na simu yake. Kabla Osward hajajibu chochote mara kuna mwanamke aliyevaa baibui nyeusi na nikabu usoni kwake alifika na kumgusa Inspekta Aron kwa nyuma akageuka. Mwanamke huyu hakuwa mwingine bali Erica mmoja kutoka kundi la Malaika weusi.
"Samahani wewe ndio Inspekta Aron?" Aliuliza Erica kwa sauti ya chini yenye unyenyekevu
"Ndio mimi nikusaidie nini dada?" Inspekta Aron aliuliza huku akimtazama binti huyo usoni, vazi alilovaa halikumshtua hata kidogo aliamini ilikuwa ni desturi ya wanawake wengi wa kiislamu.

"Nina shida na wewe tunaweza kuzungumza?"
"Bila shaka karibu ofisini"
"Hapana naomba tuingie kwenye gari yangu iko pale parking siwezi kuzungumza kwa uhuru kukiwa na watu"
"Hapan usijali tutakuwa wawili tu ofisini sawa binti"
"Inspekta Aron ni jambo la siri na muhimu sana kwako naomba nielewe"
"Jambo la muhimu lipi kwa nini tusiingie ofisini?"
"Ni kuhusu Osward, yule mfungwa" alisema Erica na hapo Inspekta Aron akashtuka kiasi.
"Osward? Kafanyaje?"
"Nifuate" Alisema Erica huku akigeuka na kuanza kuondoka akiamini tayari ameshauteka ufahamu wa Inspekta Aron kws kulitaja jina la Osward. Ni kweli Aron alishindwa kujizuia akaanza kumfuata yule binti.
Inspekta Jada ambaye alikuwa anaweka sahihi kwenye kitabu cha mahudhurio ya wafanyakazi aligeuka na kumuona Inspekta Aron akiwa ameongozana na yule binti mwenye baibui, mwanzo alihisi hatari lakini baadae akajiaminisha kuwa haikuwa rahisi mtu kufanya uharifu maeneo ya kituo cha polisi, akaendelea kuwa bize na mambo mengine.


"Funga mlango" alisema Erica mara baada ya Inspekta Aron kuingia ndani ya ile Noah. Kabla ya kufanya hivyo Inspekta Aron aliangalia mazingira ya mle ndani ya gari akamuona mwanamke mwingine kwenye kiti cha dereva ambaye alikuwa amevaa sawa na alivyovaa huyu aliyekuja naye.
Inspekta Aron alifunga mlango taratibu na hapo akamuona yule mwanamke akibinya kitufe fulani ambacho kilikuwa ni maalumu kwa ajili ya ku-roki mlango. Hapo taa nyekundu ikawaka kwenye kichwa cha Inspekta Aron, alipogeuka kutazama nyuma akahisi kabisa kuna mtu mwingine alikuwa amejificha siti za nyuma usawa na mahali alipokaa. Inspekta Aron akajua kabisa mambo hayakuwa shwari hata kidogo ndani ya gari lile lakini akajifanya kama vile hajagundua chochote.

"Mnh! Niambie ulichotaka kusema tafadhali" alisema Inspekta Aron huku akizunguusha mkono wake nyuma akaishika bastola yake vizuri.
Kufumba na kufumbua mara kuna sehemu nne zikafunguka ndani ya lile gari, moshi wa ajabu ukatoka na kutanda kila mahali wakati huo Erica na yule dereva(Asia) waliwahi na kuvaa maski fulani maalumu ambazo ziliwapa uwezo wa kutovuta hewa ya ule moshi.
Inspekta Aron alijaribu kufungua mlango kwa nguvu lakini akashindwa akageuka kujaribu kupambana na Erica lakini mara ghafula Elina aliinuka kutoka kule nyuma alipokuwa amejificha naye pia akiwa na amevàa ile maski ya kuzuia hewa chafu akamkaba Inspekta Aron shingoni kwa sekunde chache sana. Aron akajikuta anavuta ile hewa yenye sumu na haukupita muda akalegea na kutulia kimya akiwa amepoteza fahamu.

Kwa mwendo wa taratibu Asia aliwasha gari akaanza kutoka eneo la kituo hicho cha polisi. Hakuna mtu hata mmoja aliyeshtuka wala kuhisi tukio lililokuwa likiendea ndani ya gari hiyo. Mbaya zaidi vioo vyeusi vya gari hilo vilimzuia mtu aliyeko nje kuona kilichokuwa kikiendelea ndani.

DAKIKA 20 BAADAE...
Maji ya baridi aliyomwagiwa Inspekta Aron ndiyo yaliyomzindua tangu alipopoteza fahamu akiwa ndani ya gari maeneo ya kituo cha polisi. Alifumbua macho yake taratibu huku bado akihisi mwili wake kutokuwa na nguvu kabisa. Alikuwa amesimama na kufungwa mikono yake yote miwili kisha ikainuliwa juu kwa kamba iliyounganishwa na paa la chumba hicho.
Inspekta Aron aliyatazama mazingira ya chumba hicho yalikuwa ni mageni kabisa machoni pake, kilikuwa ni chumba kikubwa na kipana chevye vitu vingi chakavu mfano wa gereji, kulikuwa pia viti na meza tv ndogo pamoja na makolokolo mengine mengi.

Inspekta Aron alitazama mbele na hapo ndipo alipowaona wale wanawake watatu yaani Asia Elina na Erica wakiwa wamesimama mbele yake huku mmoja wao akiwa na ndoo ya maji. Inspekta Aron aliwatazama kwa zamu mmoja baada ya mwingine akatamani kusema jambo lakini kabla hajafanya hivyo mara alisikia mtu anapiga makofi huku vishindo vya hatua za mtu huyo vikisikika karibu kabisa na eneo hilo na mwisho alijitokeza.
.
Inspekta Aron alitoa macho kwa mshangao mkubwa mara alipomuona mtu huyo ambaye aliingia eneo hilo, alikuwa ni Osward mtoto wa mzee Matula na mchumba wa Najma. Mwanaume anaeshikiriwa kwa kesi ya mauaji lakini anashangaa kumuona yuko nje ya gereza tena akiwa huru.

Malaika weusi walisogea pembeni na kumpisha Osward aliyesogea na kusimama mbele ya Inspekta Aron, akamtazama kwa dharau kuanzia juu mpaka chini.

"Wewe ndio unajifanya kuzijua sana sheria za hii nchi si ndio? Haya zilete hizo sheria zikutetee kutoka kwenye mikono yangu" Aliongea Osward huku akiushika shika uso wa Inspekta Aron akiupeleka kulia na kushoto. Aron hakuweza kufanya chochote kwani mikono yake ilikuwa imefungwa juu.
Ghafula Osward alianza kumsindilia Inspekta Aron ngumi za tumbo mfurulizo kiasi cha kumfanya Aron alalamike kwa maumivu makali aliyoyapata.

"Ulimuua Big'? Nakuuliza ulimuua Bigiiii!!?" Osward alipiga kelele huku akizidi kumsindilia Aron ngumu za tumbo.

"Osward! Punguza jazba kwanza" Alisema Erica huku kisogea na kumshika Osward begani.

"Niache, nimesema niache huyu ni wanguu" Osward aliongea kwa jazba
"Unatoka nje ya mpango Osward kwani wewe huoni? Dokta Gondwe amekwisha anza mazungumzo na waandishi wa habari anatakiwa kufa akiwa pale, bado kidogo mda wa kwenda mahakamani utafika pia, wewe umekazana tu kupandisha hasira zako hapo" Asia aliongea kwa ukali kidogo kauli hizi zilipenya vizuri kwenye masikio ya Inspekta Aron akajikuta anashtuka sana hasa baada ya kusikia Dokta Gondwe anatakiwa kufa, mbaya zaidi yeye pia hakuwa akiijua hatima yake.

ITAENDELEA....
Simulizi ni shillingi 1,000/= lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina saul au Airtel money namba 0788967317 jina saul kisha njoo WhatsApp inbox namba hizo hizo
 
THE MODERN WAR
(Vita ya kisasa)
Sehemu ya..............38
Mtunzi: Saul David
Email: saulstewarty@gmail.com
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
"Unatoka nje ya mpango Osward kwani wewe huoni? Dokta Gondwe amekwisha anza mazungumzo na waandishi wa habari anatakiwa kufa akiwa pale, bado kidogo mda wa kwenda mahakamani utafika pia, wewe umekazana tu kupandisha hasira zako hapo" Asia aliongea kwa ukali kidogo kauli hizi zilipenya vizuri kwenye masikio ya Inspekta Aron akajikuta anashtuka sana hasa baada ya kusikia Dokta Gondwe anatakiwa kufa, mbaya zaidi hata yeye hakuwa akiijua hatima yake.

SASA ENDELEA....
Maneno ya Asia yalimfanya Osward awe mpole akasogea pembeni ya ukuta kulikuwa na bomba la maji akalifungua na kunawa mikono yake.

"Sasa hivi ni saa tatu na nusu, tuendelee na mpango wetu" Alisema Osward huku akifungua begi kubwa lililokuwa juu ya meza moja chakavu, akatoa bunduki fulani ndogo ya masafa marefu 'sniper' akaikagua vizuri kuhakikisha kama iko kamili baada ya hapo akairudisha tena kwenye begi akageuka na kuwatazama Malaika weusi.

"Natangulia eneo la tukio, hakuna mabadiliko kila kitu kiende kama kilivyopangwa sawa" alisema Osward
"Sawaa" Asia, Erica na Elina wote waliitikia kwa pamoja baada ya hapo Osward akatoka nje kabisa ya lile jengo akiwa na begi lenye bunduki ya msafa marefu mkononi. Sekunde chache baadae sauti ya muungurumo wa pikipiki ilisikika nje ya jengo hilo, Osward alikuwa akiondoka.

Hakukuwa muda wa kupoteza, haraka Malaika weusi walifungua begi lingine kubwa lililokuwa juu meza wakachukua nguo ambazo tayari zilikuwa zimeandaliwa na kuwekwa ndani yake wakasogea pale alipo Inspekta Aron wakamvua nguo zote kisha wakamvalisha zile nyingine. Dakika chache baada Inspekta Aron alikuwa amevalishwa nguo sawa sawa na vile alivyokuwa amevaa Osward kuanzia juu mpaka chini.
Alivaa suruali nyeusi ya jeans, t-shirt na koti refu jeusi la mikono mirefu, kofia,viatu, gloves na maski nyeusi usoni pake. Hivyo vyote ilivyovaa ilikuwa ni sawa sawa na vile alivyovaa Osward pindi alipoondoka. Bado haikujulikana ni nini hasa sababu ya wao kufanya hivyo lakini hii yote ilikuwa ni ndani ya ule mpango alioutengeneza Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa.


Inspekta Jada alikuwa ndani ya ofisi ya upelelezi katika kituo cha polisi cha kati Morton, sasa zilikuwa zimepita dakika 10 bado Inspekta Aron alikuwa hajarudi tangu alipoondoka.
Uvumilivu ulimshinda Jada akainuka na kwenda kuchungulia tena pale nje cha ajabu hakuliona lile gari aina ya Noah ambalo alimuona Inspekta Aron akiingia wakati ule. Ubaridi wa hofu ulimpata Inspekta Jada haraka akatoa simu yake na kupiga namba ya Inspekta Aron simu iliita lakini haikupokelewa.

"No sio kawaida, angeniaga" aliwaza Inspekta Jada huku akijaribu kupiga mara ya tatu na ya nne lakini bado simu ilikuwa ikiita pasipo kupokelewa hapo hofu ikazidi kuongeza.

"Kuna tatizo sio bure" aliwaza tena haraka akarudi ofisini kwake akachukua simu ya mezani na kubinya vitufe kadhaa kisha akapiga na kuiweka sikioni, simu iliita upande wa pili nyumbani kwake ndani ya chumba walipomuacha Annah, Baada ya muda ikapokelewa

"Hallo"
"Hallo Annah"
"Ndio ni mimi"
"Okay fine, unaongea na Inspekta Jada vipi Aron amekuja huko?"
"Huku? Hapana mbona mliondoka wote mda ule?"
"Yeah ni kweli lakini katoka na hajaniaga"
"Ooh! Mungu wangu kaenda wapi sasa? Jada, Aron yuko wapi?"
"No! no! no! Usipaniki Annah sawa shoga angu nisikilize kwa makini usitoke humo ndani mpaka uhakikishe mimi nimekuja au Inspekta Aron mwenyewe, kuwa makini nitakutafuta tena baadae" alieleza Inspekta Jada kisha akakata simu.
Upande wa pili Annah alionekana kupatwa na wasiwasi mwingi hakuelewa haswa ni nini kinaendelea lakini sauti na maneno ya Inspekta Jada yalitosha kabisa kumthibitishia kuwa hali haikuwa shwari.

"Ee Mungu naomba utulinde dhidi ya mahasimu wanaofuatilia na kuwinda maisha yetu, naomba umlinde sana Aron usimuweke mbali na mimi Mungu wangu, pigana na adui zetu tushindie hii vita Mungu wa mbinguni" Annah aliomba akiwa amepiga magoti kitandani huku ameinua uso wake juu na kuunganisha mikono yake.


"Afadhe Chaz yuko wapi?" Inspekta Jada aliwauliza askari wenzake mara tu baada ya kumaliza mazungumzo na Annah.
"Chaz wa nini tena? Kwani hujui kama yupo likizo" alijibu askari mmoja wa kike
"Jada kwani vipi mbona uko na wasiwasi sana, unataka kudukua simu ya nani nikusaidie" askari mwingine wa kiume alidakia
"Unajua kutumia mtambo wa ku-trace?" Aliuliza Jada
"Yes! Hujasema tu twende nikakusaidie, ni nani unataka kujua alipo?" Aliuliza yule askari wa kiume
"Inspekta Aron"
"Inspekta Aron si alikuwepo hapa sio mda inakuwaje tena unataka kufuatilia simu yake kujua alipo?"
"Inspekta twende tu nitakueleza mbeleni"
Jada na yule askari walitoka na kuongozana kuelekea kilipo chumba chenye mitambo maalumu ya udukuzi na kufuatilia namba za simu.


Najma mtoto wa Dokta Gondwe alifika na kusimamisha gari yake pembeni ya barabara umbali wa mita kadhaa kutoka ulipokuwa ukiendelea mkutano wa baba yake Dokta Gondwe na waandishi wa habari. Watu walikuwa ni wengi mno waliofurika nje ya jengo la Maendeleo CFC wakimsikiliza Dokta Gondwe ambaye aliendelea kutolea maelezo juu ya tuhuma na kashfa ya picha zake za utupu iliyokuwa ikimuandama.

Najma alitamani kusogea lakini kutokana na msongamano mkubwa wa watu akaona ni bora kufuatilie mazungumzo hayo mubashara 'live' kupitia simu yake mpya ya mkononi. Alifungua mtandao na kuingia YouTube' akatafuta chaneli iliyokuwa ikirusha matangazo hayo moja kwa moja akaipata.

Wakati Najma akiwa ndani ya gari akifuatilia mazungumzo ya baba yake kupitia simu yake ya mkononi mara alimuona mwanaume mmoja akipaki pikipiki yake pembeni ya barabara kisha akatembea na kwenda kusimama nyuma ya kibanda kimoja cha simu. Najma hakuweza kuiona sura ya mtu huyo kwani alikuwa amevaa maski na kofia hali iliyofanya iwe ni ngumu kuiona sura yake, mtu huyo alikuwa ni Osward mchumba wake. Haikuwa rahisi kwa Najma kumtambua hata kwa umbo kwani hakuwa amemzoea sana. Najma alimpotezea akiamini alikuwa ni muhuni wa kawaida tu mtaani, akaendelea kutazama simu yake wakati huo mazungumzo ya baba yake yakiwa yameshika kasi haswa. Baada ya muda Najma aliinua uso wake tena kwa mara nyingine kumtazama yule mtu, hapo ndipo aliposhuhudia kitu cha ajabu ambacho hakuwa ametarajia kukiona.
Najma alimuona yule mtu nyuma ya kile kibafnay cha simu akiwa ameshika bunduki ya masafa marefu na kuielekeza kule uliokuwa ukifanyika mkutano wa Dokta Gondwe na waandishi wa habari.

"Mungu wangu nini hiki" Najma aliongea huku akiwaza haraka haraka afanye nini, hakuwahi kuiona wala kumuona mtu ameshika bunduki zaidi ya kuona kwenye muvi za kikorea alizopendelea kutazama, hii ndio ilikuwa mara yake ya kwanza. Alitamani kupiga kelele lakini aliogopa, akatamani kushuka kwenye gari lakini roho yake ikasita mwisho alipata wazo jipya. Haraka akaanza kupiga honi ya gari mfurulizo, kelele hizo za honi zilifika hadi kule ulipokuwa mkutano wa Dokta Gondwe, wale waandishi wa habari walionyeshwa kukasirishwa na kelele hizo huku baadhi yao wakigeuka na kutazama ni nani aliyekuwa akipiga honi kwa fujo kiasi kile. Mlinzi mmoja wa jengo la Maendeleo CFC akawa anasogea lilipo gari la Najma ambaye aliamini labda kwa kupiga zile honi angemzuia yule mtu kuacha kufanya kile alichokusudia kufanya.


Osward alikuwa anatafuata usawa mzuri wa kulenga shabaha kwa lengo la kutaka kumuua Dokta Gondwe kama alivyoagizwa na Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa. Mwisho alipata shabaha nzuri akawa tayari kufyatua risasi ndipo hapo aliposikia honi ya gari ikipigwa mfurulizo tena kwa fujo sana. Osward aliwaza mara mbili mbili afanye nini hapo akakumbuka kuwa kama atapoteza nafasi hiyo basi hatokuwa na nafasi nyingine tena na mbaya zaidi mda mfupi ujao alitakiwa kuwa mahakamani kusikiliza hukumu ya kesi yake.

".......Osward kwa ajili ya kumuua Inspekta Aron, kwa ajili ya uhuru wako, kwa ajili ya Najma mwanamke wako, na kwa ajili ya kulinda vimelea vya V-COBOS Dokta Gondwe anatakiwa kufa......"
Sauti hii ya Profesa Cosmas Kulolwa ilijirudia rudia kichwani kwa Osward.
mwisho akaamua kupotezea yale makelele ya honi sasa macho na akili yake yote akaelekeza kwenye bunduki na shabaha yake. Hali akiwa amefumba jicho moja na kufumbua jingine akahesabu
"moja... mbili... tatu....."

Paaaaaaaa!!!

Osward alifyatua risasi kutoka kwenye bunduki yake risasi iliyoenda moja kwa moja na kuzama upande wa kushoto wa kifua cha Dokta Gondwe akaanguka chini.
Lilikuwa ni tukio la ghafula sana hakuna mtu aliyetegemea, kelele zilisikika kwa wingi watu wakikimbia na kutawanyika eneo lile kila mmoja akielekea upande wake kuyaokoa maisha yake.
Walikimbia na kumuacha Dokta Gondwe akighaa ghaa pale chini na kutupa tupa miguu yake. Walizi walibaki wametoa macho kwa mshangao hali wakionyesha kuchanganyikiwa si kidogo.
Habari hizi kuhusu tukio hili la kusisimua ziliwafikia watu wengi ndani muda mfupi sana ukizingatia kuna baadhi ya vituo vya redio na televisheni zilikuwa zikirusha mazungumzo ya Dokta Gondwe moja kwa moja.
"Break New''.. Habari zilizotufikia hivi punde.
,,,Waziri wa afya Mheshimiwa dokta Isaack Gondwe ameshambuliwa kwa kupigwa risasi eneo la kifua na mtu asiyejulikana pindi alipokuwa akifanya mazungumzo na waandishi wa habari nje ya jengo la Maendeleo CFC,,,


"Babaaaaaaaa.....!!" Najma alipiga kelele kwa nguvu huku akishuka kwenye gari akakimbia kwa kasi kumuwahi baba yake pale chini
Baadhi ya watu walikuwa wamesimama na kumzunguuka huku taratibu za kuwasiliana na watu wa huduma ya kwanza zikiendelea.
Dokta Gondwe alikuwa amelala chini huku akitapatapa katika dakika za mwisho za uhai wake, damu nyingi ikiwa imemtoka, aliyempiga risasi alikuwa amedhamilia kumuua kwani alilenga shabaha yake katika kiungo muhimu sana cha mwili yaani moyo.

Kwa bahati nzuri walinzi wa jengo la Maendeleo CFC na walinzi wa Dokta Gondwe waliweza kumuona Osward muhusika wa shambulio hilo nyuma ya kile kibanda cha simu haraka walianza kumuandama huku wakimfyatulia risasi nyingi mfurulizo. Mji ukalindika kwa makelele ya watu na milio ya risasi.
Osward alikuwa akikimbia huku mkononi akiwa na ile bunduki yake ya msafa marefu. Kwa bahati mbaya kwake hakupata nafasi ya kupanda pikipiki yake hivyo akawa anakimbia kwa miguu huku nyuma akiandamwa na walinzi wa Dokta Gondwe na walinzi wa jengo la Maendeleo, hali ilikuwa ni tete.

Osward aliendelea kukimbia kwa kasi huku akikatiza vichochoro mbalimbali na mara akafika sehemu yenye barabara mtaa wa Aslovu.
Osward alisimama akatazama nyuma yake wale walinzi walikuwa bado hawajajitokeza upande wa pili. Ni kama Osward alijua ni nini anafanya aliendelea kusimama ndani ya sekunde chache baadae Noah nyeusi ilifika na kufunga breki kali mbele yake bila kupoteza muda mlango ukafunguliwa Osward akaitupa bunduki yake chini na kuingia haraka.
Ndani ya gari kulikuwa na wale wanawake waliojiita malaika weusi yaani Asia, Erica na Elina wakiwa pamoja na mateka wao Inspekta Aron. Mara tu baada ya Osward kuingia ndani ya gari walimsukuma Inspekta Aron nje kisha wakaondoka kwa kasi na kupotea eneo hilo. Haya yote yalitokea na kufanyika ndani ya sekunde chache sana.
Punde wale walinzi waliokuwa wakimuandama Osward wakatokea upande wa pili, ndipo walipomuona Inspekta Aron akiwa amelala pembeni ya barabara huku ile bunduki ya Osward ikiwa pembeni yake. Kwa kuwa nguo alizokuwa amevaa Osward zilikuwa ni sawa kabisa na nguo alizovaa Inspekta Aron kuanzia juu mpaka chini walinzi waliamini moja kwa moja kuwa huyo ndio yule yule mtu waliyekuwa wakimuandama tangu awali mtu aliyempiga risasi ya kifua Waziri wa afya Dokta Gondwe, hakuna aliyejua mabadilishano yaliyotokea ndani ya sekunde chache kabla ya wao kufika.

Je nini kitafuata?
ITAENDELEA....

Simulizi ni shillingi 1,000/= lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina saul au Airtel money namba 0788967317 jina saul kisha njoo WhatsApp inbox namba hizo hizo
 
Link ya simulizi nyingine nzuri ya Saul David humu Jamii forum
 
Endelea...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom