Riwaya ya Kijasusi Mabaduni wa serikali

Sonko Bibo

JF-Expert Member
May 24, 2019
267
279
Riwaya hii ni ya kubuni, hivyo mfanano wa matukio wa ndani ya Riwaya na maisha halisi unayoyaishi ni shabaha tu ya fikra za Mtunzi. Karibuni nyote kwa wingi


MABADUNI WA SERIKALI

Utangulizi

Kila serikali ya taifa lolote hapa ulimwenguni ni lazima iwe na kikosi cha watu maalumu kwa ajili ya kutekeleza majukumu Fulani Fulani ambayo huwa ni magumu na ya siri sana.

Mara nyingi serikali hizi zimejikuta katika migongano mikubwa sana na hivi vikosi ambavyo vimesheheni watu wenye uwezo na ustadi wa hali ya juu sana katika mikakati mbali mbali kama vile hujuma na mauaji .

Hii hupelekea vifo vyenye utata kwa baadhi ya watu wenye nyadhifa serikalini na kuacha sintofahamu kwa jamii za watu wa taifa husika.


Sehemu ya 1

Pilika za uchaguzi wa viongozi mbali mbali nchini Songomo zilikuwa zimepamba moto.

Wagombea mbali mbali walikuwa wakijinadi ipasavyo kwa wananchi ili wapewe ridhaa ya ama kuendelea na nyadifa zao au kuingia kwa mara ya kwanza katika jopo la watawala.

Wagombea Uraisi nao walikuwa na shughuli pevu ya kulishawishi baraza la Seneti ili yapatikane majina mawili ya watu watakaochuwana vikali kukiwania kiti hicho.

Raisi Mwibale Moha ambae alikuwa anahitimisha ngwe yake nae alikuwa mgombea,

Japo hali ilionesha kuwa baadhi ya wajumbe katika seneti walikuwa hawamuhitaji kuendelea kutawala taifa hili lenye ukwasi wa kutisha, na ilionekana wazi angeanguka katika kura za wajumbe.

Lakini yeye aliamini ana karata ya ushindi ambayo ingempitisha na kufanikiwa kuwa Raisi tena .

Mbinu hii hakuwashirikisha hata watu wake wa karibu, ila mara kadhaa alisikika akisema kuwa kama atapoteza katika kura basi labda ni kwa wananchi lakini sio kwenye seneti.

Aliamini kuwa sehemu ambayo hatakiwi kuanguka ni kwenye kura za seneti, maana za wananchi hazimsumbui kamwe,

Ana uwezo wa kubadili nyeusi kuwa nyeupe. Mh!! Ogopa sana.

Basi siku zilikatika na kusalia majuma mawili kabla ya kikao cha baraza la Seneti kuwapigia kura wagombea.

***** ******* ******

Katika jengo moja kubwa sana la SHATOTO COMPLEX, mali ya kampuni ya MUKUNI INVESTMENT, kulikuwa na kikao cha siri sana.

Maana hata wageni waalikwa hawakutambua dhumuni la kikao hiki licha ya kupokea mualiko wenye muhuri wa Ikulu.

Saa mbili kamili asubuhi watu walianza kuwasili maeneo ya jengo hili na kuingia moja kwa moja kwenye hoteli moja kali sana iliyomo ndani ya jengo hili,

Niwaelezee kwa ufupi tu kuhusu hili jengo la SHATOTO COMPLEX.

Limejengwa likiwa na upana wa kilomita tano kuelekea kusini na kilomita kumi Mashariki,

Likiwa limejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa Kilomita 50 za mraba.

Lina mabwawa makubwa yasiyopungua themanini ya kisasa ya kuogelea,

Uwanja wa ndege wa kisasa wenye uwezo wa kutua ndege kubwa zaidi ya ishirini kwa wakati mmoja.

Hoteli za kisasa tano zenye ghorofa arobaini na tano kila moja zikiwa zimejengwa kwa maumbo ya tofauti kila moja

Kuna mitaa ishirini yenye barabara za wastani za kisasa,zilizotenganisha viunga vya hili jengo.

Kuna kumbi nyingi sana za kisasa za mikutano mbali mbali na kuna chemba za siri sana kwa ajili ya vikao nyeti zenye usalama na ulinzi wa mitambo ya kutisha sana.

Hivyo siku hii kikao hiki kiliikuwa kimeazimiwa kufanyika katika chemba moja yenye jina Black chamber 17.

Ni chemba isiyoweza kulipuliwa hata kwa bomu la aina yoyote ile,

na kuikodi hii chemba iligharimu pesa nyingi sana sio chini ya Dola millioni kumi, hivyo basi ilihitaji uwe na ukwasi wa kutisha ili uweze kuingia katika chemba hii.

Vyumba vya kulala vyenyewe viligarimu Dola laki moja kwa usiku mmoja tu.

Bila kusahau kulikuwa na utitiri wa maduka makubwa sana maarufu kama super markets zisizo na idadi,

Mandhari ya jengo hili yaliwavutia matajiri wazawa na wa kigeni kuja kuwekeza katika viunga hivi, ikiwa ni pamoja na mayadi makubwa na maduka yaliyojaa hapo.

Ndilo jengo kubwa na lenye hadhi nchini Songomo lenye mzunguko wa kila aina ya watu kutoka mataifa mbali mbali duniani.

Inakadiriwa kuwa idadi ya watu wanaofika katika jengo hili kwa mahitaji mbali mbali kwa siku inafika watu laki saba, maana kuna viwanja vya michezo ya aina zote.

Hata mechi muhimu nchini Songomo na matamasha makubwa ya kimataifa hufanyikia hapo.

** ** ** ** ** **

Kufikia saa tatu na nusu tayari wageni wote waalikwa walishafika na kuketi katika nafasi zao, na iliwashangaza maana kila meza ilikuwa na jina kamili la mhusika.

Utofauti mdogo tu ndio uliokuwepo hapo, viti viwili bado vilikuwa wazi.

Nafasi hizi mbili wengi walijua kuwa waliobaki ni Raisi mwibale moha, na nafasi nyingine ya mmiliki wa makampuni ya GIMONCHY GROUP OF COMPANIES.

Ambayo ndio baba wa makampuni ya,

Mukuni Investment,

Morigha Techs & media,

Junior Intelligence & security Agencies,

Super water Fishing & Marines,

P&G mining Company na

ONE OIL Refinery company.


Ambae alijulikana kama mkwasi wa hali ya juu sana nchini Songomo Bw. Fanton Mahal.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa,

mara aliingia Rais Mwibale Moha na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye nafasi yake, baada ya salamu fupi ya kunyanyua mkono wa kulia kwa wageni wote waliofika hapo ndani.

Baada ya Raisi kuketi tu, ndipo mlango uliokuwa ardhini ulifunguka kuja juu, akaonekana mtu wa mwisho, Bw. Fanton Mahal.

Aliingia akiwa na tabasamu pana usoni mwake,

Pesa ilimkubali sana mtu huyu, yaani hata tabasamu lake, kuna muda lilijenga hisia kama vile linataka kudondosha pesa.

Baada ya salamu na minong’ono ya hapa na pale, ukimya ulitanda kwa muda ili kuruhusu kikao kuanza, huku kila mmoja akiwa na shauku ya kujua lengo ama dhumuni la kikao hiki kizito.

Raisi Mwibale Moha akiwa ndiye mwenyekiti wa kikao hiki, alianza kuunguruma kwenye kipaza sauti, akiwakaribisha wageni wote waalikwa na kuwashukuru pia kwa muitikio wao juu ya hili.

Ninayo furaha kubwa na shukrani za dhati kwa nyote, maana muitikio wenu juu ya mualiko huu si tu kwamba unaonyesha umakini wenu, bali unadumisha umoja wetu tukiwa kama watu wenye maono na ndoto kubwa za pamoja katika kuhakikisha kuwa tuliyoyaazimia siku za nyuma yanabaki kuwa kipaumbele cha kwanza na muhimu Zaidi katika kupiga hatua itakayofanikisha malengo yetu ya pamoja.”



Kisha akapiga funda mbili za kinywaji kilichokuwa kwenye glasi nakutulia huku akiwatazama wenzake, ni kama alikuwa anajaribu kuyasoma mawazo yao,

lakini wengi walionekana kutaman aendelee ili wajue lengo la kikao kile. Baada ya kuona utulivu wao akaendelea.



“Hakuna asiejua hatua tulizopiga na imetugharimu juhudi nyingi na muda kuwa katika nafasi tulizopo.

Tumewekeza muda na pesa nyingi sana kufika hapa na sidhani kama kun ahata mmoja wetu anaetamani juhudi hizi zote kubaki kuwa hewa.

Kila mmoja hapa ndani ana mafanikio makubwa ambayo yametoka na utekelezwaji wa mipango kwa pamoja nah ii imezekana kutokana na undugu wetu tulioujenga wa kusaidiana ili kuhakikisha hakuna anaebaki nyuma.


Kuna jambo liko mbele yetu na ili tuweze kufikia malengo yetu ni muhimu kila mmoja wetu ahakikishe kuwa nafasi tulizonazo zinaendelea kubaki kwetu, tofauti na hivyo maana yake ni kuwa tutapoteza.

Mmoja wetu akipoteza maana yake wote tutakuwa tumepoteza, na hapo ndipo kutaibuka usaliti na hisia za chuki miongoni mwetu.




Nimewaalika hapa ili kuwakumbusha juu ya umuhimu wenu katika ushindi wangu ili kukitetea kiti changu ambacho pia ni msingi wa viti vyenu maana ninyi ndio wajumbe wa seneti.

Lakini kwa wale ambao hawahitaji kuendelea na mipango yetu ya awali sio vibaya pia wakaweka wazi nia yao juu ya hilo maana utawala wangu ni wa haki na uhuru kwa kila mwananchi wa Songomo, na ndio lengo la kuitana hapa leo.”

Alimaliza na kupiga funda tatu za kinywaji huku akiwatizama mmoja baada ya mwnine.

Kwa ufupi ni kama aliwaita kuwaambia kuwa mipango yao baadhi alikuwa akiitambua hivyo anawaonya wasifanye yale wanayoyafikiria wao bila kujali na kuangalia ni wapi wametoka wakiwa kama kikundi cha wanandugu hivyo kuwatishia pia kuwa kiti chake ni muhimu sana na ni kama jiwe kuu katika msingi way ale wanayotegemea kuyafanikisha mbeleni.

Hakika lilikuwa ni tishio kubwa sana kwa wajumbe hawa maana wengi wao walikuwa wafanyabiashara wakubwa nchini Songomo viongozi wakubwa wakiwemo mawaziri mbali mbali wakuu wote idara za usalama na vyombo vyote vya Dola kuanzia majaji wanasheria mbali mbali waliokwisha kustaafu mabalozi wa nchi tofauti Viongozi wa juu kabisa wa taasisi za kidini walikuwepo.

“Hongera sana Bw. Mwibale Moha, kwa mafanikio na hatua uliyoifikia .

Sikuwahi kufikiri kwamba itauja siku ambayo utasimama na kututishia ili tubaki katika himaya yako,

Ni kweli mafanikio yetu yamejengwa juu ya umoja wetu, tukilindana na kusaidiana Kipesa pale inapohitajika. Lakini hii haimpi mtu yeyote yule kibali cha kuwa na mamlaka juu ya mwingine, ila tunategemeana.”


Kauli hii nzito na ya aina yake ilitoka kwenye kinywa cha Bw. Fanton Mahal.

Ni kauli iliyoleta mchafuko wa hali ya hewa ndani ya ukumbi ule.



Watu walionekana kuteta huku wakiwa kama wanaopingana maana misimamo ilianza kuonekana wazi wazi.

Raisi Mwibale Moha alionekana kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa kwa wajumbe baadhi ambao walikuwa watiifu kwake.



Maana wengi ni wale ambao aliwapa madaraka kama zawadi ili kujiwekea kinga pindi kiti chake kinapokuwa hatarini

Lakini pia nguvu aliyokuwa nayo Bw Fanton Mahal haikuwa ya kawaida, maana wengi wa viongozi waliopo kwenye madaraka yeye pia alihusika kuwaweka kwenye nafasi zao kulingana na mafungamano yake na viongozi mbali mbali wa taifa waliokwisha kupita na baadhi waliokuwepo katika awamu ya Bw mwibale Moha.

Inasemekana hata Mwibale Moha mwenyewe kufikia kuwa Raisi ilitokana na sapoti ya Fanton Mahal.

Kwa ufupi kauli ya Bw Fanton Mahali iliibua wasi wasi mkubwa sana kwa watu wote waliokuwa mle ndani.

Hii ilileta picha kamili ya mpasuko ndani ya huu umoja,

Miongoni mwa watu ambao Raisi hakuwategemea kwenda kinyume ni Bw. Fanton Mahal,

Lakini baada ya kauli ile hata yeye kwa namna Fulani aliingiwa ganzi mwilini mwake, na aliona tishio la wazi juu ya nafasi yake.

Lakini hakutaka kuonesha hilo kwa watiifu wake, maana angewavunja moyo wa kuendelea kupambana na kwa wapinzani angewapa kete na asilimia za ushindi jambo ambalo hakuwa tayari kuliona likitokea, hivyo alitulia kimya akimtupia jicho la kiaina Bw. Fanton Mahal

Ni jicho lilobeba ujumbe ambao ungesomeka “ Hata wewe unanigeuka mtu muhimu kwangu leo unakuwa ngazi ya kunitelezesha kwenda chini?’”



Baada ya vurumai hii Raisi aliunguruma tena kwenye kipaza, awamu hakuwa na tabasamu wala kule kujiamini kama mwanzo, bali alikuwa na hasira iliyochanganyikana na hali ya maumivu ya kuhisi usaliti wa moja kwa moja.



Kuna muda inabidi wote tutambue kuwa, hakuna juhudi zinazopaswa kubezwa na hakuna haja ya kuwa na misuguano isiyojenga

Siku zote alieshiba hunyanyuka taratibu na kunawa kisha bila kuwabugudhi wengine wanaokula hutoka mahali pale” Aliongea kwa mafumbo.



“Hatuwezi kuendelea kuumwagilizia maji mti wa kujinyongea na ingekuwa bora kama mti huo ungekauka tangu mwanzo kabla haujakomaa na kupeleka mizizi maana chaguo la mwisho ni kuung’oa ili usije ukachipua na kuacha mbegu za kumbu kumbu zitakazosumbua vizazi na vizazi” Ilimalizia sauti ya Fanton Mahali , kauli kinzani na ile ya Raisi mwibale Moha, awamu hii ikiwa imebeba taswira halisi juu ya maandalizi ya mapambano dhidi ya Raisi. Mmh!!! Ogopa sana.

Baada ya Fanton mahal kukaa kimya Raisi nae aliunguruma tena,

“Ndugu yangu Fanton Mahal, kumbuka nafasi uliyonayo kiuchumi imechangiwa na ulinzi kutoka kwangu. Maana mara kadhaa umehujumu Uchumi na kukwepa kodi bila Bughudha kutoka kwa vijana wangu na hata washirika wako wengi nimewalinda na unalitambua hili”

Alimalizia Rais awamu hii akimchimba Fanton juu ya utajiri wake kuwa na makando kando pia ikiwa ni kama onyo kuwa akivuka mipaka huenda akakutana na vikwazo vya kiuchumi na madhira ya aina nyingi pia.

Mwibale Moha Raisi mtukufu wa wanasongomo,

Unadhani unaimiliki serikali kwa asilimia ngapi? Aliuliza Bw. Fanton Mahal.

Asilimia themanini, alijibu Mwibale Moha kwa kujiamini ni kama vile alikuwa amefanya utafiti



Baada ya jibu lile la kujiamini aliambiwa na Fanton kauli ambayo ndiyo kwanza ilimzindua kutoka kwenye usingizi aliolala miaka mingi.



“Kwenye hizo asilimia zako toamo sitini na zile ishirini hata nikikuachia huwezi kushinda.

Sisi ndio msingi wa hili taifa tuondolee giza kwenye njia zetu, tulikubeba mgongoni haujui umbali wa safari tuliotoka hadi kufika hapa. Usituone tuko kwenye hivi viti ukadhani ilikuwa rahisi, hatukuamka usingizini na kujikuta hapa. Ni vyema ungekaa kimya na kuyaacha haya yapite, pengine huko mbeleni Mbingu zingekuwa upande wako, ungepata tena nafasi ya kuja kutawala.

Utailaani sana hii siku maishani mwako, lakini si ni mpaka tukupatie hiyo nafasi ya kuilaani?”




Alimalizia kwa swali Bwana Fanton Mahal, swali ambalo halikuhitaji kujibiwa.

Kisha akanyanyuka toka kwenye kiti chake na kuanza kupiga hatua kuondoka kwenye hii Black chamber 17 huku nyuma aliachia harufu ya mauti iliyozifikia pua za kila mmoja pale ndani kuonesha kuwa hakuwa mtu wa kawida kabisa,

Nyuma yake alifuatwa na wafuasi kama robo tatu ya wajumbe wote waliohudhuria kikao kile na kuyafanya maneno yake kuwa na maana aliposema Raisi aondoe asilimia sitini katika asilimia zake.



Raisi mwibale Moha aliangalia namna wajumbe wanavyoondoka kwa wingi wakimwacha akiwa amesimama huku mikono kaiweka mezani akiwa haamini, yaani ni kama alieandaa sherehe kisha watu wakaja wakala na kumwachia yeye aondoe vyonbo.

Alichukia sana, tena alichukia mchukio mpya.



Mara alipotupa macho yake katika skrini za mle ndani zilizokuwa zikionesha mazingira ya nje kwa chini kulizunguka lile jengo, aliona ghafla walinzi wake wanavyouawa kinyama na vikosi vya wauaji walioficha sura zao kwa vinyago .

Hapo ndipo alijua kuwa kumbe ni kweli ile miamba ilyoondoka ndio msingi wa hili taifa na hakuwa na cha kuwafanya,

Mwili wake uliishiwa nguvu na kujikuta akidondokea juu ya kiti chake mithili ya mtu ambae hakuwa tayari kuketi.

Akiwa amekata tamaa asijue nini cha kufanya maana hata akili yake haikuwa hapo ndani kwa wakati huo, mambo mengi yalikuwa yakipita kichwani mwake.



Kauli ya mwisho ya Fanton Mahal ilikuwa ikijirudia kichwani mwake, alichanganyikiwa na kufadhaika kwa wakati mmoja.

Ni kama mtu aliyezinduka kutoka usingizini,

Na hii ni baada ya kuhisi uwepo wa mtu mwingine pembeni yake maana anakumbuka alikuwa amebaki peke yake.

Baada ya kuinua sura yake ili amtazame ndipo alipopigwa na butwaa baada ya kumuona mtu aliekuwa amekaa pembeni yake bila wasi wasi wowote ule. Je ni nani huyo? Usikose sehemu inayofuata.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom