SIMULIZI: "The Godfather"

Just Nana

JF-Expert Member
Jul 27, 2023
500
1,001
SEHEMU YA KWANZA:

Nyarugusu- Kigoma, Tanzania

Hofu ilikua imetanda miongoni mwetu, kina mama walikumbatia watoto wao, zaidi ya vilio vya watoto hakuna sauti nyingine iliyosikika, hata ndege pia walihofia kukaa karibu nasi, zilianza kama tetesi zilizofatiwa na hekaheka za wahudumu wa afya waliohudumu kambini pale, palikua na kila dalili kua pana jambo kubwa linaendelea na ni kama lilikua linawashinda nguvu kulidhibiti, baada ya siku chache ndio tunakuja kupata taarifa sahihi, kambi ilikua imevamiwa na gonjwa hatari la kipindupindu, msongamano wa watu ulisababisha huduma mbovu za kijamiii, vyoo vilikua havitoshelezi, maji ya kunywa yalikua ni changamoto, watu mamia kwa mamia walikua wamefululiza kuja ndani ya siku tatu zilizopita kufuatia mgogoro wa kivita uliokua unaendelea huko Kongo. Tahadhari ilitolewa ikiambatana na elimu jinsi ya kujikinga na gonjwa hilo hatari, dalili zikaelezwa pia ili atakapobainika mgonjwa mwenye dalili hizo awahishwe mara moja kwenye hema maalumu. Nilijitahidi kufumba macho japo nipate usingizi lakini kumbukumbu chungu ikapita kwenye fikra zangu, kumbukumbu ya miaka saba iliyoacha makovu mengi yasiyo na idadi mwilini na moyoni mwangu.

Ilikua ni usiku wa kuamkia jumapili, tulikua tumeshafanya maandalizi yote ya kuondoka afajiri ya siku inayofuata, hali ya usalama ilizidi kua mbaya, maelfu na maelfu ya watu walikua wameuawa kwa kukatwa mapanga ama kupigwa risasi. Hofu ilitanda kote, hakuna huduma yoyote ya kijamii iliyokua inapatikana, ni kama tuliachwa tuchinjane tumalizane wenyewe kwa wenyewe, nilikua nina miaka tisa wakati hayo yanatokea, bado naikumbuka ile siku kama ilitokea jana tuu, ni siku iliyonipa jina rasmi la mkimbizi.

Tulikua tumejificha kwa rafiki wa baba ambae alikua mwanajeshi, nyumba za jeshi zilikua hazikaguliwi labda wakipata mashaka na uungaji wako mkono katika kile walichokiita kusafisha nchi dhidi ya uchafu ulioachwa na wabelgiji. Tusingeweza kuendelea kujificha ,ilikua ni lazma tuondoke, rafiki wa baba alitoka usiku ule kwenda kuazima gari ya jeshi la kuweza kutusogeza hadi mpakani , kulikua hakuna namna tungeweza kutoka Rwanda kwa usafiri wa kawaida, magari yote yalikua yanakaguliwa, ilikua nafuu kidogo kama una gari la jeshi.

Tulisubiri kwa zaidi ya masaa manne bila ya dalili ya yule mwanajeshi kurudi, hakukua na namna hata ya kupiga simu maana simu pekee zilikua zinatumika kipindi kile zilikua ni simu za mezani tu, katikati ya kusubiri tukaanza kusikia milio ya risasi, haikua mara ya kwanza kusikia risasi ikilia ila ile siku ilikua tofauti maana milio ya risasi ilikua ni mingi na ikawa inazidi kusogea tulipo, kwa kipindi kile sikumudu kugundua aina gani ya bunduki ilitumika, ila kwa shule ya vitendo ya miaka saba porini ilinitosha kujua kila aina ya bunduki, mataifa zinapotoka na nguvu iliyonayo, kwa sasa naweza sema kua ile milio ilikua ni ya bunduki hatari sana ya kivita inayoitwa AK-47, ugunduzi wa Mrusi Kalashnikov, laiti kama huyu bwana angepata maono ya maafa ambayo bunduki yake ingeyaleta ulimwenguni hasa Africa na Mashariki ya kati , sidhani kama angeendelea na ugunduzi wake.

Tulijikusanya pamoja, mimi na familia yangu pamoja na familia ya yule mwanajeshi ambayo kwa wakati huo alikua amebaki mkewe, watoto wao wakike wawili na kijana wa kazi. Ile familia walikua wahutu, wakati sisi tulikua mchanganyiko, baba Mhutu na mama Mtutsi, watoto wawili kati ya watatu tuliozaliwa na baba na mamangu tulikua na mfanano wa kihutu wakati mdogo wetu wa mwisho alikua ana muonekano wa kitutsi. Haya yalikua ni makabila makubwa na yenye uhasama sana Rwanda.

Kilisikika kishindo cha nguvu ,gari la jeshi liliingia kwa fujo pale ndani likiwa limelizoa geti kubwa la kuingilia, yaani hawakuona kama palikua na uhitaji wa kugonga geti wakamua kuingia nalo. Kwa akili ya utoto tuliona kelele zingetusaidia, kila mtu alikua amepanick, mama alitukumbatia kwa nguvu, bado nalikukumbuka like kumbatio, bado nalikumbuka, lilikua ni kumbatio la mwisho kukumbatiwa kwa upendo wa ndani kabisa. Teke moja lilitosha kuusambaratisha mlango wa kuingilia ndani , waliingia wanajeshi wasiopungua nane wakiwa wameongozana na kundi la wanajeshi wasio rasmi maarufu Kama interahamwe.

Tuliamuliwa wote tupige magoti, mama mwenye nyumba alimtambua mmoja kati ya wale wanajeshi kua ni kati ya marafiki wakubwa wa mumewe, akawa anajitahidi kumchangamkia ili atusaidie, alipigwa teke moja takatifu akaangukia sakafu, alifikia mdomo, Sina hakika kama bado anamiliki meno yake ya mbele kama alifanikiwa kunusurika.

Walitoa amri moja tuuu, inyenzi wote kaa upande wa kulia, tukawa tunavutana na kung'ang'aniana, hakuna aliekua tayari kumuachia mwenzie, aliyempiga kofi mke wa yule mwanajeshi alietupa hifadhi kwake alikuja hadi tuliposimama na mama angu, akamnyakua mdogo angu wa mwisho wa miezi nane, alimrusha ukutani kwa nguvu ,damu ya moto ilinirukia usoni, mdogo angu alitoa sauti hafifu na kukaa kimya. Utulivu pale ndani ulipotea, ile kauli ikarudiwa tena, inyenzi pita upande wa kulia, kifo kisikie tu kwa mbali, yule kijakazi wa mwenye nyumba akawa anatusukuma mimi na familia yangu, hawa hapa inyenzi...hawa hapa inyenzi...

Ilitolewa amri ya kua mimi na kakangu tukabidhiwe mapanga, sikuwahi hata kuchinja kuku hapo kabla, nilikua naogopa sana damu, eti leo nakabidhiwa panga niue binadamu, hapana...tena mamangu mzazi,mama alikua ananisitiza nifanye wanavyotaka ili mimi na kakangu tupone, machozi hayakuacha kunitoka. Nikiwa katika kushangaa nini kinaendelea , kuipa mda akili ikubaliane na uhalisia, yule kijakazi wa mwenye nyumba alininyang'anya lile panga, kwa kasi akamrukia mama angu na kuanza kumcharanga kama nyama buchani....
 
SEHEMU YA PILI:

Nilipata fahamu baada ya masaa kadhaa, nikagundua kua nipo kwenye gari inayotembea baada ya kurushwarushwa na kujibamiza kichwani, maumivu makali ya kichwa yalizifanya fahamu zangu zirudi, hakukua na umuhimu wa kumwagiwa maji ya baridi, ni uharibifu wa maji tu, ambayo yalikua bidhaa adimu kwa wakati ule. Ukizipoteza fahamu zipoteze kwa starehe zako na pambania kuzirudisha pia kwa starehe zako.

Haikuhitaji kuambiwa na mtu kua unatakiwa ujishike kwa umakini, ubovu wa ile barabara ulinifanya nijishikirie kwa nguvu mnoo, baada ya kupata stamina ndio nilipoamua kufanya uchunguzi wa harakaharaka, kulikua na idadi ya watoto zaidi ya kumi kwenye ile gari, wote tukiwa tumejikunyata bila matumaini. Gari ilizidi kwenda na kusimama baada ya masaa kadhaa, mlango wa ile gari ulikuja kufunguliwa, tulishushwa na kupokelewa na fimbo za mgongo na kuamuliwa kulala chini.

Kuanzia ile siku tukaambiwa sisi ni mali ya jeshi la wananchi la Rwanda chini ya kamanda Bernard Munyagishari . Rasmi tukaanza mafunzo ya kutumia silaha mbalimbali ikiwemo panga, bunduki na mabomu ya mkono.Tulikaa porini kwa zaidi ya wiki mbili tukipatiwa hayo mafunzo, yakifuatiwa na mafunzo ya chuki ya jinsi gani Mtutsi ni mtu asiefaa na ambaye anatakiwa aondoke Rwanda kwa juhudi zote.

Ili kufahamu kama umefuzu masomo, unaletewa binadamu alie hai umtoe uhai, hakukua na mama wala baba wa kukutetea,ili uendelee kuishi ilibidi kufata amri. Matukio ni mengi sana siwezi kuyasimulia yote, ila ninachokumbuka ni kua nilitoa uhai wa binaadam wenzangu wengi isivyo na idadi, ili kulimudu zoezi tulikua tunapewa mirungi na bangi kuchangamsha akili zetu.

Baada ya miezi mitatu tangu tuanze kutumika kwenye vita tulivamiwa na jeshi la waasi (RPF) kwa kipindi hicho chini ya Raisi wa sasa bwana Paul kagame, risasi zilitembea sana ile siku, wanajeshi waliokua wanatuongoza wengi waliuawa na wachache walifanikiwa kutoroka, nilikua ni miongoni mwa wale wachache tuliokimbilia nchini Burundi, japo nilikua mtoto mdogo, ila kuna namna yale mafunzo yanakubadilisha unajitenga wewe mwenyewe na jamii, niliona jeshi ndio mahala pangu kwa wakati ule.

Tulikimbilia Burundi, mkuu wangu wa kazi alijiunga na waasi wa Burundi kwa sababu zilezile zilizoleta machafuko Rwanda, huku napo ilikua pia kuondoa uchafu wa wabelgiji, hizi nchi mbili zinaingiliana kwa vitu vingi sana. Nilitumika katika jeshi la waasi kwa zaidi ya miaka mitatu na kisha kuokolewa na jeshi la taifa la Burundi na kujikuta napambana tena upande wa serikali.

Hadi tunakuja kuokolewa na majeshi ya umoja wa mataifa mwaka 2004 mwishoni, nilikua nimeshapambana chini ya majeshi matatu ya nchi mbili tofauti. Tulijumuishwa miongoni mwa wakimbizi wengine na kuunganishwa kwenye safari ya kuja Tanzania. Kiumri nilikua na miaka kumi na sita wakati naokolewa, lakini nilikua nimeshiriki matukio ya kiuhalifu yasiyo na idadi ikiwemo uporaji, mauaji ya kila aina na utekaji nyara

Leo nayakumbuka haya nikiwa kambini , Nyarugusu nchini Tanzania. Nimelala bila matumaini nikisubiria kifo cha kipindupindu, nilijicheka kwa dhihaka, nimenusurika kifo cha risasi na ajali mara nyingi isiyo na idadi , haikua sahihi kuruhusu kufa tena kifo cha kishamba kama kile. Nikiwa katika kutafakari nikasikia mchakato nje ya hema ninalolala, ni kama kuna mtu aliyekua ananyata kwa siri kuelekea hemani kwangu, kuishi porini na kulala macho kwa zaidi ya miaka saba kulinifunza kulala kwa tahadhari, kelele kidogo ilinitosha kunifanya niwe macho, nilikaa kwa tahadhari nikisubiria huo ugeni usio na taarifa.

Kiliingia kipande cha mtu , nilikua mejibanza kwenye kona, niliacha nione ni kipi anataka kukifanya. Yule kiumbe aliangaza kwa machale pale nilipotandika kirago changu, watu wengine walikua wanakoroma sijui wana raha gani kukoroma katika mazingira haya, akatoa tochi yenye mwanga hafifu na kumulika pale kiragoni akaona hola, hakukaa sana, akaacha kidaftari kidogo pale kiragoni na kutokomea. Sio kama ningeshindwa kumkabili, la hasha...nimeishi maisha ya kuwindwa sana nchini Burundi maana kuna wakati tulikua tunatumika na wanasiasa kuwadhibiti maadui zao, na kujikuta unatengeneza maadui wasio na idadi. Nilichokitaka ni kufahamu, yule bwana ni nani na alikua na makusudi gani kuingia hemani kwangu usiku wa manane kwa tahadhari namna ile.

Nilijongea pale kiragoni na kumulika kale kadaftari kadogo, kalikua ni mali yangu halali, machozi yalianza kunitoka, ni Kama nilikua nimeona kitu cha thamani sana, nilihangaika kukitafuta bila ya mafanikio ile siku ambayo wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walikua wametuokoa, ilibakia kidogo nipigwe risasi nilipogundua kua nimekidondosha maana nilianza kuhaha kukitafuta na kujikuta mekiuka amri ya kulala chini.

Leo hii nimeunganishwa na kitu muhimu sana, nilikua nimeandika mtaa tuliokua tumeishi nchini Rwanda, nyumba namba , majina yangu matatu, majina ya wazazi wangu na ndugu zangu wote, shule niliyokua nasoma na pia majirani kadhaa niliokua nawakumbuka, nilijua ipo siku nitarudi Rwanda, walau niwe najua wapi naanzia kuitafuta familia yangu maana kumbukumbu ya mwisho ni lile tukio la mama kukatwa mapanga na mimi kupoteza fahamu, sikua najua wapi walipo baba na ndugu zangu wengine wawili.
 
SEHEMU YA TATU:

Nilianza kuishi kwa tahadhari ,kuwepo na mtu pale kambini anaejua kuhusu ushiriki wangu wa vita nchini Rwanda na Burundi ilikua ni hatari sana, waasi wengi walikua wanauawa katika mazingira ya kutatanisha, nilianza kukaa kwa hofu, zaidi ya hofu ya kipindupindu. Jioni moja wakati tunaota moto na kujadili mawili matatu kabla ya kulala, alikuja yule mtu alieleta kile kidaftari chenye taarifa zangu muhimu. Alikaa pembeni yangu kwa mda wa dakika tatu bila ya kuongea kitu, halafu kwa sauti ya ukimya sana akaniambia jiandae, 'General Piere Mgimba anataka kuonana na wewe...'

Nilishtuka kwa hofu, hilo jina nimelisikia sana kwa kipindi chote nilichokua naishi Burundi, alikua mtu katili sana na ambae haoni shida kuua. Nakumbuka aliamuru tuchome gari la wazungu waliompatia kazi na wakawa wanasuasua kumlipa, ndani ya lile gari walikuwepo mke wa yule mzungu na watoto wake wakike wawili, tuliwachoma moto bila ya huruma na kama haitoshi akawa anachomoa nyama za kwenye mwili wa wale wasichana anatundika kwenye mti aliochonga na kua kama mshikaki na kuanza kula zile nyama. Lilikua ni tukio baya kuwahi kulishuhudia kwa macho yangu. Leo hii napewa salamu kua General ananihitaji. Nilijionea huruma mwenyewe maana nilikua nimechoka sana na matukio hayo, kama binaadamu nilikua nimeshuhudia na kushiriki kwa kiwango kikubwa na nilikua nimechoka sana.

Kauli ya General ni amri, nikaelewa sasa maana ya kurudishiwa kile kidaftari, alikua anamaanisha kua tunajua wewe ni nani na tunajua ulipo. Nilikaa katika mkao wa kusubiri ujio wa General na hayo aliyoyakusudia dhidi yangu. Baada ya siku tatu nikafatwa tena usiku na yuleyule kiumbe, akanambia nifuate. Ilikua ni usiku wa kama saa nane hivi, nilimfata kimyakimya tukipita mahema kadhaa, baada ya umbali kiasi tulifika mahali penye uzio wa kutokea , yule kiumbe alifyatua uzio na tukapata sehemu ya kupita.

Tulitembea kwa umbali kiasi hadi tukafika usawa wa barabara kuu inayoingia kambini, kwa mbali nikaona mwanga wa taa, kwa uzoefu nikajua tu ile ni gari inatusubiria. Tuliingia garini na safari ya kuelekea kusikojulikana ikaanza. Ukimya ulitawala wakati wa safari, zaidi ya injini kuunguruma hakuna kelele nyingine iliyosikika. Tulitembea na gari kwa zaidi ya lisaa lizima, ilikua ni mara ya kwanza kutoka nje ya kambi kwahiyo sikua na namna ya kufahamu wapi tunaelekea na kuishi na waasi kulinifunza kufata amri kuliko kuuliza maswali, hapa napo niliamua kutumia utaratibu niliouzoea.

Tulifikia kwenye nyumba ya bibi mmoja ambae anayefahamika Kama bibi Ng'wazukulu...yule bibi alikua ni mganga maarufu pale Kasulu, nilikuja kufahamu baadae kupitia wateja wengine pale nyumbani kwa mganga kua pale tulipo ni Kasulu. Nilipelekwa kupikwa na kuwekwa sawa kwa kazi iliyopo mbele yangu. Nilikaa kwa takribani siku nne nikifanyiwa tiba za jadi, lengo ni kuzidi kua imara maana hii ni ardhi ya watu pana miiko yake. Baada ya kua sawa nilisafirishwa hadi Arusha kwa ajili ya kukutana na General.

Tuliingia Arusha usiku sana , niliambiwa nipumzike kwa ajili ya kuonana na general kesho asubuhi na mapema. Utaratibu wangu ni uleule, kulala kwa machale, palipambazuka na safari ya kwenda kwa general ikaanza, general alikua anaishi sehemu inaitwa Njiro, baada ya kufika niliamuliwa niingie peke angu na wale wengine waliambiwa wageuze palepale, hofu ilikua nami lakini nilijipa moyo . Nikazipiga hatua hadi ndani ya ile nyumba, kwa maelekezo ya walinzi nilitakiwa nimsubiri general bustanini.

General alikuja akiwa na muonekano tofauti na ule nilikua nauona porini, mtu katili na asie na huruma, mda wote kashikilia bunduki yake pembeni ,lakini general huyu alikua mtulivu na asie na hofu, nikaisifia amani ya Tanzania kwa muda. Kanuni za jeshi zilitembea nami popote, ingawa hapa ni uraiani lakini nilimpa heshima yake ya kijeshi na kusimama nikusubiri amri ya kukaa. Akaonesha tabasamu na kuniamuru kukaa, General akanambia anajivunia sana Mimi, katika watoto wote aliofanya nao kazi Burundi, anajivunia sana uwepo wangu, mtiifu, mwenye juhudi na msikivu sana.

General alinipa taarifa ya kile alichoniitia kua ameanzisha kundi maalumu la vijana aliowazoea na ambao ni watiifu kwake, amewakusanya vijana ishirini hadi sasa na ana kazi nyingi za kufanya kwaio tujiandae, sikutakiwa kuuliza maswali mengi sana, kanuni za jeshi ni kupokea oda na kutekeleza. Nilitafakari jinsi menusurika na kipindupindu nikaona acha nijaribu bahati yangu kwa mara nyingine ila kwa sasa natakiwa kua mbele kuliko wakati.
 
Iwe na ujasusi ndani yake km ile ya yoga 'Dark days ......' sio iwe na uongo uongo km ya INSIDER MAN watu wataikinai mapema episode za katikati usitujazie mapenzi narudia tena usitujazie watu watavurugwa maana wachambuzi wa Mapenzi ni wengi humu JF
 
Hakuna mapenzi huku rafiki, hapa Ni kazi kazi....
Haya twende kazi maana ukijaza Mapenzi story haitafika mwisho utahamisha lengo utahamia kwenye kusimulia Mapenzi Mara Eva sijui Irene na Joyce sijui Grace kufanyanini nikamshika paja
 
Haya twende kazi maana ukijaza Mapenzi story haitafika mwisho utahamisha lengo utahamia kwenye kusimulia Mapenzi Mara Eva sijui Irene na Joyce sijui Grace kufanyanini nikamshika paja
God father hana hata mda wa kulala my dear, hustle zake at 16 years si umeziona, sasa story inaenda hadi anafika age ya 50 something ambapo sasa jina la Godfather linakua limekaa mahala pale....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom