Hoja kuchunguza mkataba Buzwagi yatibua Bunge
*Waziri, Mbunge watunishiana misuli
*Hoja yageuzwa ya kisiasa
*Wabunge wengine wavutana
*Baadhi watishiana, wengine walalama
Na Ndyesumbilai Florian, Dodoma
HOJA binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) kuhusu utaratibu uliotumiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini haraka mkataba wa mradi wa madini wa Buzwagi, Wilayani Kahama, umeligeuza Bunge kuwa kikao cha mapambano ya kiitikadi na kupunguza uzito wa hoja na mjadala wenyewe.
Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, hatma ya hoja hiyo ilionyesha zaidi kufuatiwa na kurushiana vijembe na kejeli kutoka miongoni mwa wabunge wa chama tawala, CCM dhidi ya wale wa upinzani ambao kwa kiasi kikubwa walionekana dhaifu, kushindwa kuhimili vishindo, hususan katika kujibu mapigo ya Waziri Karamagi dhidi ya hoja ya msingi ya Kabwe.
Matokeo yake, karibu kila mchangiaji aliyesimama, alikuwa akionyesha kuegemea zaidi kwenye itikadi au fungamano la kambi yake kisiasa, kuliko uzito wa hoja hiyo iliyoibuliwa na kujengwa na mwanasiasa huyo kijana, hasa ile inayohusu matatizo kuhusu mikataba katika sekta ya madini na sheria zinazosimamia sekta hiyo.
Akiwasilisha hoja hiyo, Kabwe alilitaka Bunge likubali kuunda kamati hiyo teule ili kuchunguza mwenendo mzima wa kusainiwa kwa mradi huo kulikofanyika jijini London, Uingereza Februari mwaka huu. Alidai kuwapo kwa ukiukwaji katika baadhi ya taratibu zinazosimamia, kuongoza sekta ya madini nchini.
Miongoni mwake ilikuwa ni haraka iliyomfanya Waziri Karamagi ausaini mkataba huo akiwa nje ya nchi bila kusubiri kwanza ripoti ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) kuhusiana na mradi huo ambazo kwa kawaida hutolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc).
Katika hoja yake yenye vipengele 11, Kabwe alitaka kamati hiyo iundwe kwa lengo la kujiridhisha na kuondoa utata huo ambao alidai umejitokeza zaidi na kugubika mchakato mzima wa kusainiwa kwa mkataba huo, akidai kuwa ilikuwa kinyume na Sheria ya Madini ya mwaka 1998.
Pia, alihoji sababu za kuendelea kuiita miradi wakati Kampuni ya Barrick imewekeza mtaji mkubwa katika mradi huo, kiasi cha dola za Kimarekani milioni 400, ikiwa ndio mradi mkubwa wa pili baada ya ule wa Bulyankhulu, pia ulioko Kahama, ambao umewekezwa dola milioni 600 na kampuni hiyo.
Hata hivyo, aliposimama, Waziri Karamagi alianza kuzipangua hoja hizo moja baada ya nyingine, huku akishangiliwa kwa makofi na wabunge wa CCM.
Kama vile hiyo haitoshi, Karamagi alionyesha dhahiri kukejeli hoja za Kabwe kuwa hazikuwa na msingi na zaidi zilitokana na ukosefu wa uelewa wa masuala yanayosimamia sekta ya madini na kuongeza kuwa hakukuwa na uvunjaji wowote wa sheria za nchi.
Badala yake, alisema alichokifanya akiwa katika ziara ya kikazi ya muda mrefu nje ya nchi, ni kupata habari kuhusu kuwapo kwa nafasi ya uwekezaji katika mradi huo wa madini na hivyo kuichangamkia.
Alisema alichoshindwa kuelewa Kabwe ni kushindwa kutofautisha na kisha kuchanganya sheria zinazohusu utafutaji na uwekezaji katika madini na uchimbaji halisi.
Aliongeza kuwa hilo ndilo limemfanya afikirie suala la EIA kwa mradi wa Buzwagi, ambalo kwa kawaida huwagusa zaidi wachimbaji ambao tayari wamepewa leseni za uchimbaji katika migodi ya madini na siyo wale wanaoendelea na uwekezaji kama ilivyo kwa kampuni ya Barrick kupitia mradi wa Buzwagi.
Kwa maana hiyo, Karamagi alieleza kuwa hakukuwa na sababu ya kuhitaji kwanza ripoti hiyo ambayo itafikiwa wakati wawekezaji hao watakapoanza shughuli rasmi za uchimbaji wa dhahabu katika mgodi huo.
Kuhusu manufaa ambayo Watanzania wataweza kupata kutokana na mradi huo, Karamagi alieleza kuwa ni kupatikana kwa ajira zaidi ya 600 kwa Watanzania, zikiwamo zile za maafisa wa vyeo vya juu.
Aliongeza kuwa mradi huo utaweza kuwekeza kiasi cha zaidi ya dola milioni 800 baada ya kukamilisha uwekezaji wake na kuongeza kuwa kamwe serikali isingeweza kuacha nafasi hiyo ipotee bure na ndiyo maana ikasaini mkataba huo mapema Februari kabla ya tarehe ya mwisho ya Machi mwaka huu.
Karamagi ambaye alizipangua hoja za Kabwe kwa umakini mkubwa, hatimaye alionyesha kuteleza na kutumbukia katika mtego wa kiitikadi alipodai kuwa hoja hiyo iliibuliwa na Kabwe na sasa imechukuliwa kama ajenda na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anayeipigia debe majukwaani huku akivishambulia vyombo vya habari kuwa vimetumika kumchafua na kumpaka matope.
Wakichangia hoja hiyo, wabunge wa kambi ya upinzani, Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), Mhonga Ruhwanya (Viti Maalum-Chadema), Chacha Wangwe (Tarime-Chadema), Maulida Anna Kome (Viti Maalum-Chadema) na Margareth Sakaya (Viti Maalum- CUF), wao waliunga mkono hoja ya kuundwa kwa kamati hiyo.
Hata hivyo, alikuwa Komu aliyewaacha hoi wabunge kwa kudai kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere pekee, ndiye anayeweza kukemea mambo yanayoendeshwa na serikali ya CCM ikiwamo wizi na ubadhirifu wa rasilmali za umma, yakiwamo madini.
Waliochangia kwa upande wa CCM, walikuwa Ruth Msafiri (Muleba Kaskazini-CCM), Suleiman Kumchaya (Lulindi), Adam Malima (Mkuranga), ambao walionyesha dhahiri kuungana na msimamo wa serikali na hata kuwabeza wapinzani.