SoC03 Tatizo la ajira laweza kuisha na kubaki kuwa historia Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Maendeleo ya nchi yoyote duniani yanahitaji mambo muhimu kama ifuatavyo: Ardhi, Watu, Siasa safi na Uongozi bora. Utawala bora na uwajibikaji vipo ndani ya siasa safi na uongozi bora.

Tukiimarisha utawala bora na uwajibikaji katika nchi yetu, tatizo la ajira litaisha na kubaki kuwa historia.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu imeongezeka kutoka 12,313,469 mwaka 1967 hadi kufikia watu 61,741,120 mwaka 2022. Hii inamaanisha kuwa idadi ya watu mwaka 2022 ni mara tano ya jinsi ilivyokuwa miaka 55 iiyopita (1967). Kwa mujibu wa sensa hii (2022), watu (wanaume kwa wanawake) wa umri kati ya miaka 20 na 59 (wanaopaswa kuwa nguvu kazi ya taifa) ni zaidi ya milioni 26.

Kielelezo Na. 1: Ongezeko la Idadi ya Watu, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 1967 – 2022
Ongezeko la watu 1967 - 2022.png

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu, 2022

Nchi nyingi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na Tanzania, kilio kikubwa ni ukosefu wa ajira, hasa kwa kundi kubwa la vijana, ambao wanaongezeka hadi kufikiwa 800,000 kila mwaka kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kazi Duniani ya mwaka 2020.

Kielelezo Na. 2: Viwango vya Ukuaji wa Shughuli za Uchumi, Robo ya Tatu, Mwaka 2022
Ukuaji wa Uchumi Robo ya Tatu Mwaka 2022.png

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu, 2022

Hali Halisi ya Ajira Tanzania
Kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya Takwimu Tanzania, miongoni mwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi, ni chini ya asilimia kumi (10) wenye ajira rasmi.

Tunawezaje kutengeneza Ajira Nyingi kila mwaka?
Hapa ndipo dhana ya Utawala Bora na Uwajibikaji inapohitajika kufanya kazi! Hakuna serikali yoyote duniani inayoweza kuajiri watu wake wote; kwa kuwa ukubwa wa serikali na taasisi zake hauongezeki kila mwaka kama ilivyo kwa watu.

Fursa za Ajira Tanzania
Kuna fursa nyingi sana za ajira nchini Tanzania, ambapo watu wengi wanaweza kuajiriwa na kujiajiri. Fursa hizi zinapatikana katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kilimo, Viwanda, Madini, Utalii, na Huduma za Kijamii. Changamoto kubwa ni kwamba watu wengi wanaofanya kazi katika sekta hizi hawana ajira rasmi! Ajira rasmi, naamanisha uhakika wa mwajiriwa kuwa na uhakika wa kupata kipato cha kukidhi mahitaji yake kila siku, ikiwa ni pamoja na huduma za afya yake na ya familia yake.
Watu wengi walioajiriwa kwenye viwanda na makampuni makubwa, pamoja na waliojiajiri hawana ajira rasmi!

Kwa kutumia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, serikali ihakikishe ajira nyingi zisizo rasmi zinakuwa rasmi, na hivyo kupunguza kabisa wimbi la vijana wanaosaka ajira serikalini.

Sekta Muhimu za Uchumi
Kilimo ni uti wa mgongo wa Uchumi wa Tanzania! Lakini ukiangalia kielelezo Na. 2 hapo juu utaona kilimo kikichangia asilimia 3.4 tu katika pato la taifa, huku ikipitwa kwa mbali na sekta ya Malazi na Huduma ya Chakula ambayo inachangia asilimia 13.2. Sekta nyingine muhimu ambayo inachangia kidogo katika pato la taifa ni ya Viwanda (asilimia 4.5); na ya Madini na Mawe (asimia 9.8).

Tukianza na Kilimo, hii ni sekta inayotegemewa na karibu asilimia 80 ya Watanzania kiuchumi. Nchi imebarikiwa kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba, maziwa, mito, na misitu mingi, ambavyo vingewezesha Kilimo kutoa mchango mkubwa sana katika pato la taifa. Serikali iwezeshe wananchi kutumia rasilimali hizi kuinua Kilimo kwa kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na kuhama kwenye kilimo cha kutegemea mvua.

Serikali iinue sekta ya Viwanda, kwa kuhakikisha mali ghafi kwa kiasi kikubwa zinatokana na sekta ya kilimo.

Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, iinue sekta ya madini na mawe na kuhakikisha kiasi kikubwa kinachakatwa hapa nchini. Tuna hazina kubwa sana ya madini ambayo yanaweza kubadili kabisa Uchumi wa Tanzania. Mfano, tunayo hazina kubwa ya Gesi Asilia iliyogunduliwa karibu miaka 50 iliyopita, lakini hadi sasa, haijaweza kutumika vizuri na kuleta tija katika Uchumi wetu.

Sambamba na kuboresha sekta hizi, serikali ihakikishe zinatoa ajira rasmi na sii vibarua kama ilivyo kwa sekta nyingi hapa nchini (hususani sekta binafsi).

Mitaaala ya Elimu
Ni vyema mitaala ya elimu ikafanyiwa marekebisho makubwa ili kila mhitimu wa ngazi yoyote ya elimu, kuanzia shule ya msingi aweze kuajiriwa na/au kujiajiri. Kujiajiri ni jambo la kutiliwa mkazo, maana kwa mujibu wa Jarida la Umoja wa Mataifa la Machi 11, 2020, Kijana sii lazima kuajiriwa, kupitia mafunzo anaweza kujiajiri.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Serikali ihakikishe watu wote walioajiriwa na waliojiajiri wamejiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ikiwa ni pamoja na Bima ya Afya. Kwa viwanda na/au makampuni yalioajiri watu wengi kama vibarua, sheria zitumike kuwalazimisha waajiri kutoa ajira rasmi zitakazohakikisha waajiriwa wanapata kipato stahiki, na kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwa wale waliojiajiri, tukianzia na mfanyabiashara mdogo (maarafu kama Mmachinga), kwa kutumia kitambulisho cha taifa (NIDA) awezeshwe kufungua Akaunti Benki, na kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutumia sehemu ya kipato chake cha kila siku.

Moja ya sababu zinazofanya watu wengi kutafuta ajira taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikalini ni kuwa na uhakika wa kujiunga na mifuko hii ya kijamii. Hivyo, uwepo wa mifuko hii kwa kila mtu aliyejiajiri au kuajiriwa, kutapunguza kama sii kuondoa kabisa pengo katika mtumishi wa Umma na yule wa sekta Binafsi.

Viongozi na Watumishi wa Serikali, ngazi ya Kijiji/Mtaa
Serikali ina mtandao mkubwa sana wa watumishi wa umma, lakini kwa mtizamo wangu hutumika kwa kiasi kidogo sana katika maswala ya maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi. Kwa muktadha huu, watumishi hawa ambao sekta zote za ajira zipo maeneo yao, watumike kuhakikisha waajiriwa husika katika sekta zote (kama nilivyoeleza hapo juu) wana ajira rasmi.

Hitimisho
Kwa kutumia sheria na sera zilizopo, na pale inapobidi kutunga sheria na sera mpya kuhusiana na ajira za staha, serikali itapunguza kwa kiwango kikubwa, kama sii kumaliza kabisa tatizo la ajira nchini. Hii ina maana kuwa kila mmoja katika nafasi yake serikalini na/au wadau mbalimbali awajibike kikamilifu kufanya kazi, na hivyo kudhihirisha Utawala Bora kwa Umma.

Marejeo
Kijana si lazima aajiriwe kupitia mafunzo anaweza kujiajiri:Nyoni TYC

Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Oktoba, 2022), Muhtasari wa Pato la Taifa Robo ya Tatu (Julai – Septemba) 2022 – Bei za Mwaka Kizio 2015.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Oktoba, 2022), Sensa ya Watu a Makazi ya Mwaka 2022, Matokeo ya Mwanzo.







 
Nilizungumza na mtu mmoja kuhusu tatizo la ajira, akasema ajira ni nyingi sana, ila watu wanachagua aina za ajira; kama hazikidhi matarajio yao, basi wanasema hamna ajira. Ndio maana, naisihi serikali kurasimisha ajira, kwa maana ya kuweka viwango vinavyotakiwa na kuvisimamia sio tu katika sekta za umma, bali hata katika sekta binafsi.
 
Miaka ya 70 Wizara ya Kazi ilisimamia kwa karibu sana jambo hili la ajira; ilihakikisha sekta binafsi zinatoa ajira rasmi (au za kudumu) na sii vibarua. Kwa kutumia rasilimali tulizonazo hivi sasa, ikiwa ni pamoja na tehama, serikali ina uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia sekta zote zinazotoa ajira, na kuhakikisha zinatoa ajira rasmi nyingi.
 
Tatizo la ajira linaweza kuisha iwapo hivi vitu vitatekelezwa kwa ufasaha:-
  • Sekta ya kilimo ikiboreshwa kwa sera, na matajiri kushawishiwa kuwekeza huko kwa mashamba makubwa makubwa.
  • Unafuu wa uagizaji mitambo ya viwandani na mashambani kutoka nje ya nchi
  • Msamaha wa kodi kwa wale wote watakaowekeza kwenye viwanda na kilimo
  • Urasimu wa kupeleka bidhaa nje usiwepo
  • Urasimu wa kuanzisha viwanda usiwepo
  • Kutafutiwa masoko nje ya nchi, pale inapotokea safari ya viongozi waende na matajiri waliopo Tanzania.
  • Baada ya hapo, wengi watapata ajira na fedha za kigeni zitakuwepo za kutosha.
 
Andika ,unavyoandika,Tatizo la ajira haliwezi kuisha milele tuombeni Mungu tu....
Uasilia upo ukitazama population yetu inavyokuwa kwa Kasi na nafasi za ajira zinavyokuwa finyu... ..
Kila jambo linawezekana, ukiamini hivyo! Ukiamini haliwezekani, kweli itakuwa hivyohivyo!
 
Tatizo la ajira linaweza kuisha iwapo hivi vitu vitatekelezwa kwa ufasaha:-
  • Sekta ya kilimo ikiboreshwa kwa sera, na matajiri kushawishiwa kuwekeza huko kwa mashamba makubwa makubwa.
  • Unafuu wa uagizaji mitambo ya viwandani na mashambani kutoka nje ya nchi
  • Msamaha wa kodi kwa wale wote watakaowekeza kwenye viwanda na kilimo
  • Urasimu wa kupeleka bidhaa nje usiwepo
  • Urasimu wa kuanzisha viwanda usiwepo
  • Kutafutiwa masoko nje ya nchi, pale inapotokea safari ya viongozi waende na matajiri waliopo Tanzania.
  • Baada ya hapo, wengi watapata ajira na fedha za kigeni zitakuwepo za kutosha.
Ni kweli kabisa, kuna mbinu nyingi sana ambazo serikali na wadau wanaweza kutumia kumaliza tatizo hili!
 
Tatizo la ajira linahusiana na matumizi kidogo ya rasilimali tulizonazo. Wazungu wengi wanapata ajira kupitia rasilimali zetu!
 
Back
Top Bottom