..na inastahili ifanyiwe mabadiliko makubwa haraka sana
Posted Date::10/20/2007
Tuhuma: Mkapa analindwa na katiba ya Tanzania
* Inasema wazi hawezi kushtakiwa milele
* Aweza tu kujibu tuhuma kama akipenda
* Ni zile za ufisadi, kufanya biashara Ikulu
Na Andrew Msechu
Mwananchi
KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo inayompa jeuri Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kukataa kujibu tuhuma za ufisadi na kufanya biashara akiwa Ikulu zinazomkabili kwa kuwa hawezi kushtakiwa milele.
Rais huyo mstaafu tayari amewaeleza wanaomtuhumu wasitarajie majibu yoyote kutoka kwake kwa kuwa tayari yeye ameshastaafu masuala ya kisiasa, hivyo asingependa kujihusisha na malumbano yoyote ya aina hiyo kwa sasa.
Mkapa alitoa kauli hiyo Alhamisi iliyopita alipokuwa akihutubia katika mkutano wa tathmini ya mwaka ya Taasisi ya Mkapa inayoshughulikia masuala ya Ukimwi (Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation), uliofanyika katika Hoteli ya Kunduchi Beach, jijini Dar es Salaam.
Tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa ambazo zimekuwa zikichapishwa katika magazeti na pia kuzungumzwa na wanasiasa wa upinzani na wengine, akiwamo Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku zinaeleza kuwa, rais huyo mstaafu alikiuka taratibu za uongozi kwa kutumia nafasi yake kama kiongozi wa nchi katika kujitafutia mali.
Suala hilo linatafsiriwa kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka sambamba na ukiukaji wa maadili ya uongozi wa umma.
Lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa ulinzi dhidi ya mashtaka kwa rais aliyepo madarakani na aliyestaafu katika Ibara ya 46(3) ya katiba.
Ibara hiyo inasema; "Isipokuwa kama hataacha kushika madaraka ya rais kutokana na masharti ya ibara ya 46A (10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya rais kwa mujibu wa Katiba hii".
Ufafanuzi unaopatikana katika kifungu cha 46A (10), unasema kuwa rais mstaafu anayeweza kushtakiwa kwa kosa la jinai au madai ni yule aliyeondolewa madarakani kwa azimio la bunge baada ya mashtaka dhidi yake (bungeni) kuthibitika, jambo ambalo halikumtokea Mkapa.
Kifungu hicho kinasema, "Endapo Bunge litapitisha azimio kuwa mashtaka dhidi ya rais yamethibitika na kwamba hastahili kuendelea kushika kiti cha rais, spika atawafahamisha rais na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi juu ya azimio la bunge, na hapo rais atawajibika kujiuzulu kabla ya siku ya tatu tangu bunge lilipopitisha azimio hilo."
Kwa mujibu wa vifungu hivyo, Rais Mkapa hakuondolewa madarakani na bunge, hivyo anabakia na sifa ya kutoshtakiwa milele hadi Katiba itakapozungumza vinginevyo.
Hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, majibu ya Mkapa aliyoyatoa siku za hivi karibuni yalijikita katika kinga aliyonayo kikatiba, jambo ambalo inaonekana wanaomtaka kujibu tuhuma walikuwa hawajalitazama, au wanataka ajibu tu kwa misingi ya kuonyesha ustaarabu na uadilifu.
Hata hivyo, miongoni mwa wanaomtaka Mkapa kujibu tuhuma ni Mhadhiri wa Sheria katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sengondo Mvungi, ambaye alikaririwa na gazeti dada la Mwananchi jana akisema kuwa; kauli ya Mkapa kwamba hataki kujibu tuhuma hizo kwa kuwa ni za kisiasa siyo ya uwajibikaji na uungwana.
Mvungi alisema, Mkapa hawezi kukwepa kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hana kinga kisheria kuwajibika kwa mambo aliyofanya kwa utashi wake wakati wa utawala wake.
Alisema sheria inampa kinga rais kwa mambo aliyofanya kama rais na siyo aliyofanya kwa utashi wake, hivyo Mkapa anapaswa kujibu tuhuma hizo endapo zimemlenga yeye binafsi.
Kwa kuzingatia tafsiri ya Dk Mvungi, yapo baadhi ya mambo ambayo Mkapa anaweza kushtakiwa, hasa aliyoyafanya binafsi kama vile kufanya biashara akiwa Ikulu, lakini
kwa tuhuma za Wapinzani kuwa anahusika na ufisadi kwa kuwa ulifanyika yeye akiwa rais, zinalindwa na Katiba.
Mwingine aliyeeleza nia ya kumtaka Mkapa kujibu tuhuma ni Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, ambaye alisema kauli ya Mkapa inaleta hisia kuwa amesahau kuwa aliingia Ikulu kwa ridhaa ya wananchi na aliahidi kuwatumikia wananchi hao kwa ukweli na uwazi.
"Nafikiri mheshimiwa Mkapa amesahau kwamba aliomba kazi ya Urais kwa hiari yake na akaahidi kulitumikia taifa kwa ukweli na uwazi. Sasa ni busara zaidi akimaliza vizuri kwa kujisafisha tuhuma hizo," alisema Profesa Baregu.
Profesa huyo aliongeza kuwa ni muhimu sasa kwa serikali kuanzisha utaratibu wa viongozi wa umma kutangaza mali zao kabla na baada ya kuingia madarakani, ili jamii ifahamu uwezo wao kimapato na kuwaamini katika kila jambo wanalofanya.
Alisema kitendo cha Rais Mstaafu Mkapa kujibu tuhuma hizo sio tu kitamaliza mjadala unaoendelea kuhusu tuhuma za ufisadi dhidi yake, bali pia kitamjengea heshima na imani zaidi kwa wananchi.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanasema kutaja tu mali za viongozi haitoshi, bali wanatakiwa kueleza na jinsi walivyopata mali hizo, ili uadilifu wao uweze kujidhihirisha.