Tanzania: Utawala bora vs Rushwa

Tanzania: Utawala bora vs Rushwa

Serikali ya ccm imekosa Mwelekeo hivyo imepotoka. Sijawahi kuona tamko la kihuni tangu nizaliwe kama hili
 
Wazee muda wao umekwisha chumvi nyingi walo ila imekomaza mishipa ya fahamu sasa wanaropoka ovyo.

Zaidi nahisi wakati wa ku square difference na wasure wetu wote umefika (Y-x)^2.

kazi ni kwetu Generation X na wadogo zetu ni lazima tutwae madaraka ya Bunge tubadiri sheria na kunusuru nchi yetu.

Huu moto heshima yake ni kubuni njia mpya na za kisasa za kuuendeleza ili usizime.

Sisi Generation X ndiyo watawala wapya, ni lazima tutwae sehemu kubwa madaraka ya uongozi wa kisiasa ili kuipeleka njia kwenye mkondo wa maendeleo halisi.

Wenzetu kule Kigali wana Plan ya New Kigali City. Wanajenga majengo ya Kisasa na kuimarisha mifereji mikubwa ya maji machafu,barabara na usafi wa Jiji la kwa ujumla.

Sisi vijana vile vile ni lazima tutwae madaraka ya kisiasa na kuweka mipango ya Ujenzi wa MODERN DAR ES SALAAM CITY. Na mipango mingine ya kuendeleza ukuaji wa mji wa Dar na Vitongoji vyake. Kutatua tatizo la msongamano wa magari kwa kutandaza reli sambamba na Barabara.

Mawazo haya hata ukiyaingiza leo hayawezi fanikiwa mpaka tuung'oe mzizi wa Ufisadi.

Gx kazi kwenu.
 
Dhamira ya Rais Kikwete kuvalia njuga rushwa ni dhati, isibezwe

Na Mhariri

Mapambano dhidi ya rushwa ni moja ya ahadi muhimu alizotoa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete mara tu alipoingia madarakani.

Rais akaainisha kuwa rushwa ni moja ya maradhi mabaya yanayoitafuna jamii ya Watanzania, hivyo juhudi za dhati yafaa zifanyike kupambana nayo hatimaye kuyatokomeza.

Katika kuonyesha dhamira ya dhati katika kuwaongoza Watanzania, alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza Desemba 30,2005 alisema ataongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake na kuziba mianya yake.

Kwa kuanzia, mapema mwaka 2006 Rais akaelekeza jicho lake katika kukiimarisha chombo kikuu cha mapambano hayo, yaani Taasisi ya Kuzuia Rushwa wakati ule kikijulikana kama TAKURU na sasa kinaitwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).

Chombo hicho kiliongezewa wafanyakazi na zana, vitendea kazi na rasilmali za kukiwezesha kutekeleza vizuri zaidi majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Kadhalika, Rais kwa kuonyesha jinsi alivyolivalia njuga tatizo la rushwa nchini, serikali yake ilipotimiza mwaka mmoja madarakani, ikawa imeandaa rasimu ya Sheria Mpya ya kupambana na rushwa ambayo aliamini itakiongezea upeo na nguvu chombo hicho.

Rasimu hiyo ilifikishwa Bungeni na kupitishwa kuwa sheria Aprili 16, mwaka huu na kusainiwa na Rais Kikwete mwenyewe Juni 11, mwaka huu. Hii ni Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya 2007 iliyoanza kazi Julai mosi.

Hata alipokutana na viongozi wa chombo hicho Jijini Mbeya mwanzoni mwa mwaka huu, aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na kujiamini na kwamba wasikubali kutishwa na kuingiliwa na mtu yeyote, kwani hata yeye(Rais) hatawaingilia hivyo wasimhofu mtu mwingine yeyote katika utekelezaji wa shughuli zao.

Katika kuonyesha kukerwa na rushwa hata katika uchaguzi wa CCM unaoendelea amekemea vikali viongozi wanaochaguliwa kwa rushwa, akawaambia wakibainika wataondolewa.

Juhudi hizi zote za Rais wetu hakika, zimelenga katika kuhakikisha kuwa mapambano haya yanapewa msukumo na nguvu za kisheria ili wala rushwa waweze kuadhibiwa kulingana na makosa yao bila kuonewa.

Lakini badala ya kumuunga mkono na ushiriki wa kila mwananchi, viongozi, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kufanikisha jambo hili, wapo baadhi ya watu wanaomzunguka Rais wetu na kumpaka matope kwa kumhusisha na ufisadi.

Hawa ni watu wanaotapatapa ambao wanaona fika kuwa mianya yao ya ufisadi imefikia ukingoni kwa jinsi Rais Kikwete alivyoweka dhamira yake ya dhati kupambana na wakumbatia rushwa. Kumhusisha Rais ni mbinu za mafisadi ambao tayari wamewekewa ndoano na TAKUKURU ziwanase kukomesha uoza wao.

Ni vema wakaelewa kwamba Rais ni chaguo la wananchi. Kama alikuwa fisadi katu wasingemchagua kuwa kiongozi wao.

Usafi na uadilifu wake ndio uliovuta hisia za Watanzania kumchagua kuwa jemadari wao na siyo wenye husuda wachache waliopoteza mwelekeo.

Huu ni wakati wa kuungana naye kushughulikia kero za maendeleo ya wananchi na siyo kumvunja moyo.

SOURCE: Nipashe
 
Pamoja na matatizo yote ya JK, SI FISADI wa kuwekwa kundi moja na kina EL na RA, hata kidogo. Pamoja na kuwa ni rafiki zake na watu ambao anawalinda na pengine anawaogopa, si wa kuchanganywa nao hata kidogo. Lakini pia kumchanganya JK na watu hao kwa sasa si mbinu nzuri ya kupambana na mafisadi kwani baada ya kumtaja JK katika hiyo LIST unategemea nani achukue hatua? Nadhani kuna udhaifu mkubwa kama SI MKONO wa mtu katika sehemu ya kwanza ya LIST OF SHAME. List ya kwanza ilikua na majina manane tu, ambayo JK alikuwamo bila ya kuwamo watu watatu, LOwasa, Rostam Aziz na Kamaragi. Siamini kwamba ilikua ni bahati mbaya kwa kundi hili ambalo LINAITWA UTATU MTAKATIFU (ISOMEKE UFISADI MCHAFU). Haiwezekani watu kama Rutabanzibwa ambaye alikataa rushwa ya IPTL akawekwa katika list wakaachwa Karamagi ambaye hata mtoto mdogo leo hii anamtaja kutokana na hoja ya BUZWAGI. Kuna maneno kwamba ilikua ni mkakati wa kutaka kufanya hoja nzima ya BUZWAGI na MAFISADI ionekane ni ya kitoto kama ilivyofanyika kwa orodha ya majengo ya kihistoria ikiwamo Salamander iliyonunuliwa na MANJI. Waziri Dialo aliingizwa mkenge kwa kuweka orodha ya majengo zaidi ya 100 na matokeo yake maana nzima ikaonekana ya kukurupuka na baadaye serikali wakapata sababu ya kulifuta tangazo la serikali na majengo yakawa huru kuvunjwa ikiwamo SALAMANDER alilonunua MANJI. Lazima tuwe makini sana, vinginevyo hii vita ni ngumu inahitaji mikakati ya kupambana na mikakati ya MAFISADI. HAWALALI HAWA, tumuondoeni JK ili awe sehemu ya wapiganaji na akishindwa kuchukua hatua ndio tuanze kwa kumshambulia na kumshinikiza kwa hilo kwani liko ndani ya uwezo wetu. Tukifanikiwa ndio tuanze kujiandaa kufanya mabadiliko 2010 kwa kuwaandaa wapiga kura kufanya CHAGUO MAKINI kuanzia MADIWANI, WABUNGE hadi RAIS
 
Hayo ni maoni ya mhariri tu na wala hawakilishi maoni ya walal hoi. Yeye hapo anajaribu kukipaka mafuta kitumbua chake.
Katika vita dhidi ya UFISADI hapalaliki mpaka kieleweke.
 
Nimesoma kwa makini sana maoni ya Mhariri lakini kwa kiasi kikubwa sijaona hoja nzito kwenye maoni yake. Hapo ndipo ninaposhawishika kuona kwamba kweli kuna wahariri ambao inawezekana wanatumiwa kwa maslahi fulani (sipendi nimhukumu, lakini inawezekana ndiyo upeo wake wa kutoa maoni yake au upande wa shilingi anao uangalia uko tofauti na upande ninaouangalia mimi).

Maoni yake yamejikita kwenye uimarishaji wa TAKUKURU ili kuweza kupambana na kuzuia rushwa. Lakini TAKUKURU hiyo hiyo ina kasoro zifuatazo ambazo nadhani Mhariri wa Gazeti ameshindwa kuziona au kwa makusudi kabisa ama kwa maslahi yake. Mhariri anapigia debe kitu ambacho waandishi wa gazeti lake wamekuwa wakikipigia kelele kwamba kimeshindwa kufanya kazi.

Kuimarishwa kwa TAKUKURU kwa kuongezewa wafanyakazi na vitendea kazi bila kuona matunda ya kazi yao, sioni kama kuna haja ya kuwasifia. Wakati Balozi wa US akiondoka hapa nchini alilalamika kwamba TAKUKURU imejikita kwenye kushika wala rushwa ndogondogo, ina maana wala rushwa kubwa kubwa za mabilioni hawazioni?

Sheria ya TAKUKURU anayoiongelea, waandishi kibao na wananchi wameiponda kwamba bado haiko madhubuti yaani iko "weak" na pia kwa njia fulani imeweka uzio kwa tuhuma ambazo TAKUKURU wakishaanza kuzichunguza vyombo vya habari haviruhusuwi kuandika habari za kasheshe hizo na wakimaliza kufanya kazi ya kuchunguza Hoseah ataenda pale Maelezo na kusema wamechunguza na mambo ni safi! Lakini kama vyombo vya habari vingeendelea kuandika juu ya scandal hizo tungeweza kupata upande wa pili wa shilingi na hivyo kupata picha kama TAKUKURU imeficha baadhi ya mambo. Kwa hiyo kwa sheria hiyo, madudu ambayo serikali haitaki yajulikane kwa wananchi ndipo utasikia vitisho vya sheria ya TAKUKURU kwamba swala likishaanza kuchunguzwa halitakiwi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari. Is that a credit to the new PCCB Act?

Mhariri anasema kwamba JK akiwa Mbeya alisema kwamba hawezi kuiingilia TAKUKURU. Lakini tumejionea wazi kwenye swala la Mh. Mkapa ambapo JK alisema aachwe apumzike na hawezi kuchunguzwa. DG wa TAKUKURU akasema kwamba hawezi kwenda kinyume na Boss wake. Je hilo siyo kuiingilia TAKUKURU? Ndiyo maana nimekuwa nikisema kwamba TAKUKURU ina macho, inaangalia nani achunguzwe na nani asichunguzwe. Hivi kweli Mhariri huyu yuko makini na hoja zake??

Kiini cha Maoni ya Mhariri ni sakata la Dr. Slaa kuanika orodha ya mafisadi na lengo la Mhariri ni kumsafisha Muungwana. Hayo ameyasema yeye mwenyewe kwenye maoni yake mwishoni mwa maoni hayo. Maoni yake yamepinda au hoja yake imeshindwa kusimama yenyewe hasa aliposema hivi:

Hawa ni watu wanaotapatapa ambao wanaona fika kuwa mianya yao ya ufisadi imefikia ukingoni kwa jinsi Rais Kikwete alivyoweka dhamira yake ya dhati kupambana na wakumbatia rushwa. Kumhusisha Rais ni mbinu za mafisadi ambao tayari wamewekewa ndoano na TAKUKURU ziwanase kukomesha uoza wao.

Ina maana Dr. Slaa anatapatapa kwa kuwaanika mafisadi? Slaa nondo zake amezitoa kwenye Report ya CAG ya BoT. Rais alikuwa na report hiyo, pia wasaidizi wake nao walikuwa nayo tangu ilipotoka. Je, waliifanyia kazi report hiyo? Mbona report ya ukaguzi wa hesabu za serikali ilipotoka tu aliwaita watendaji wakuu wote na kuwaambia kwamba hajafurahishwa na report hiyo. Kwanini hawakumhoji Gavana atoe maelezo hizo hela zimekwenda wapi? Wakasubiri mpaka Dr. Slaa aanike hoja yake ndipo sasa wanakuja na majibu nusu nusu ambayo haya-add up. Kwa maneno mengine kwa muda wa zaidi ya mwezi mzima na nusu tangu vielelezo vya Slaa vilipopelekwa serikalini walikuwa bado "wanapika" majibu ambayo hata hivyo yako nusu nusu. Wakimaliza kutoa majibu wanasema wataendelea kutoa majibu ya hoja nyingine, which means, bado "wanapika" majibu na wanahisi "hayajaiva" kwa ajili ya kuwapatia wananchi majibu "yaliyopikwa".

Huu ni mwaka pili tangu JK aingie madarakani, kauli ya kupambana na rushwa imebaki kuwa ya maneno tu bila matendo. Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 alisema kwamba atapambana na rushwa kwa nguvu zote na kwamba kutuhumiwa kula rushwa inatosha kumuondolea kiongozi wa serikali sifa ya uongozi na hivyo asingesita kumuondoa kwenye uongozi. Hayo yalibaki kuwa maneno matupu bila vitendo. Leo hii baada ya miaka 10 pale Ikulu tumeona alifanya ujasiriamali wa hali ya juu na kujiuzia baadhi ya mali za umma kimya kimya bila ya wananchi kujua nini kinaendelea nyuma ya mapazia. Kitu gani kitatufanya tuamini kwamba JK kweli kadhamiria kuwashughulikia wala rushwa? Kwanini anapata kigugumizi kuwasimamisha wanaotuhumiwa na rushwa ili uchunguzi ufanyike na baada ya hapo ukweli ujulikane? Halafu Mhariri anasema tusibeze juhudi za maneno matupu ya kupambana na rushwa ambayo yamebaki kwenye makaratasi.

Ujumbe wa Mhariri uko hapa:

Ni vema wakaelewa kwamba Rais ni chaguo la wananchi. Kama alikuwa fisadi katu wasingemchagua kuwa kiongozi wao.

Usafi na uadilifu wake ndio uliovuta hisia za Watanzania kumchagua kuwa jemadari wao na siyo wenye husuda wachache waliopoteza mwelekeo.

Huu ni wakati wa kuungana naye kushughulikia kero za maendeleo ya wananchi na siyo kumvunja moyo.

Ni kweli Rais alichaguliwa na wananchi na tena kwa kishindo cha 80% ya wapiga kura. Sura aliyokuwa nayo wakati ule ilionyesha matumaini kwamba angeweza kuleta mabadiliko katika uchumi kwa kuwa hata Mwalimu Nyerere (RIP) hakuwahi kumhusisha na ufisadi, ni EL pekee aliyeulizwa swala la utajiri wa haraka haraka na aliupata wapi. Sura ya JK ya uadilifu ilianza kupotea pale watu walipoona EL ameteuliwa kuwa PM na huku akiwa kwenye rekodi za Mwalimu kamba utajiri wake una walakini. Jamii haina imani tena uswahiba uliopo kati yake na watu ambao wanahisiwa kwamba ni mafisadi. Kwa hiyo kwa kifupi ni kwamba leo hii wakisema waitishe uchaguzi tena sijui kama JK anaweza kupata hizo 80% ya kura alizopata mwaka 2005!

Ninazidi kushawishika kwamba wahariri wanatumika kwa maslahi, itafika mahali tuanze kusema ... hata Nipashe nao wamenunuliwa??? Kwa mwendo huu Taaluma ya Uandishi wa Habari inaelekea shimoni na ule umuhimu wa mhimili wa nne usio onekana unapotea taratibu maana nao umekuwa ni sehemu ya serikali. Tumebaki na mihimili 2 tu, serikali na labda "mahakama", Bunge lilijidhalilisha juzi na tumeishaliona liko upande gani!
 
Katika kuonyesha dhamira ya dhati katika kuwaongoza Watanzania said:
Haya ni maoni ya mhariri, na mimi nadhani hakuna haja ya kumhukumu, lakini maoni kama haya unaona kuwa yana walakini. Kuna mawaziri wangapi ambao walichaguliwa na wabunge lakini ni wafisadi na watoa rushwa. Kuna wabunge wangapi wamechaguliwa na wananchi ambao wanajihusisha na vitendi hivyo. Sababu kubwa ya rushwa inayoliathiri vibaya taifa letu yaani inayofanywa na wanaosaini mikataba au wanaotoa kandarasi, ni uchu wa fedha na kujitajirisha haraka haraka. Sasa toka Desemba 30, 2005 amelifanyia vipi kazi hilo. Nadhani kama kweli mwandishi angekuwa na la kuwaambia watu angetuambia amefanya nini. Kubadilisha jina la PCP hakumaanishi kuwa sasa ina nguvu kuliko mwanzo, it same wine in a different bottle. A different bottle is not going to make it any better.
Labda hajatumia ofisi yake kufanya mambo yanayoweza kumfanya aonekane yumo kwenye kundi hilo, na hata Slaa hakusema rais ni fisadi. Amezungumzia vitendo vyake vya nyuma aliposhika nyadhifa mbalimbali za uwaziri.
Nadhani cha muhimu ni kupuuza tu anayosema huyo mhariri. Labda na yeye anataka apewe nafasi Ikulu kama Salva.
 
Halisi Kula 5 Mzee!

Ninakubaliana na wewe kwa 100% kwamba inawezekana kuna mchezo mchafu ulichezwa. Kule kwenye thread ya orodha ya mafisadi nimeuliza zaidi ya mara 3, mbona orodha iliyowekwa hapa JF ina majina 8 tu? Katika orodha hiyo EL, RA na NK hawamo, na nilikuwa interested kuona tuhuma zao. Kwa hiyo inawezekana kama ulivyosema, ile version ya kwanza kabisa ndiyo iliyowekwa hapa JF na ile yenye majina 11 sijui imeenda wapi.

Sasa umenifumbua macho, nina mashaka makubwa sana na hawa mafia wa UTATU BADHIRIFU kwamba wanaweza kuwa na nia mbaya kwa kuwa tayari uchafu wao uko wazi na inawezekana wanahofia kwamba JK anaweza kuwatosa na hivyo mambo yakawa magumu. Njia pekee ya ku-survive ni kuvuruga mambo kwa njia uliyoisema. Anyway, ngoja tusubiri JK akirudi atakuja kusema nini, maana nimesoma utetezi wa serikali wala sioni kama una add-up. Na kuna watu wanasema kwamba EL aligoma kujisafisha kwenye hiyo kashfa, labda anasubiri JK akija ndiyo atumie mgongo wa JK kujisafisha. Lakini ni wakati muafaka kwa JK kuanza kufikiria namna ya kuwaondoa hao watu ambao ni kero katika uongozi wake!

Hivi ni kwanini JK anapata kigugumizi kuwatosa? Kama wanamharibia wazi wazi kabisa inakuwaje awaache? Kuna thread moja nimesoma kwamba RA alichota hela za kampeni ya uchaguzi toka BoT na sasa anatakiwa kurudisha lakini tayari kaisha mgeuzia kibao Ballali na kwamba anachongewa ili apoteze mkate wake. Kwanini JK aendelee kuwakumbatia watu kama hao ambao wanaonekana ni hatari na wanaweza kukugeuka wakati wowote??????
 
Nimesoma kwa makini sana maoni ya Mhariri lakini kwa kiasi kikubwa sijaona hoja nzito kwenye maoni yake. Hapo ndipo ninaposhawishika kuona kwamba kweli kuna wahariri ambao inawezekana wanatumiwa kwa maslahi fulani (sipendi nimhukumu, lakini inawezekana ndiyo upeo wake wa kutoa maoni yake au upande wa shilingi anao uangalia uko tofauti na upande ninaouangalia mimi).

Keil,

nakubaliana na wewe kwa asilimia mia moja kwani baada ya kusoma kwa makini, nimebaini kwamba Mhariri hapa alikurupuka. Pamoja nna nia nzuri ya kuwasilisha ujumbe, hakuwa na facts za kuwafanya watu wamjuamini anachotaka kusema. Kwa bahati mbaya sana Mhariri hajui TANZANIA inakwendaje, na badala yake alikwenda katika kusoma magazeti yake ya nyuma na kuweka na kisha kuandika maoni. Nadhani kama alimpa hiyo kazi KIJANA wake kwa kuwa ni WEEKEND, basi nadhani siku zijazo ataandika mwenyewe MAONI
 
Maelezo yenu mazuri sana lakini mtu unafika katikati uelewe mnaongelea nini. Rushwa na ufisadi ni vitu viwili tofauti. Mla rushwa ni fisadi lakini fisadi siyo lazima au mla rushwa. Orodha ya Dr. ni ya mafisadi na yeye ameeleza ni vigezo gani ametumia kumuita mtu fisadi. Rejea maelezo yake. Kwa mfano RA siyo mla rushwa labda kama kuna mtu hapa anaweza kunieleza kitu ambacho sifahamu. Kwa maelezo ya Dr. rais JK hajawekwa kwenye kundi ya wala rushwa wala hajamuita moja kwa moja fisadi kama alivyomuita BWM. JK amewekwa kwenye list hiyo kama mtu aliyehusika kutoa maamuzi ya kifisadi kwa hiyo ni fisadi kwa vigezo vyake. Hata Ndugu Rutabanzibwa, kwa maelezo tuliyonayo ni mtu ambaye anapinga sana vitendo kwa rushwa lakini hiyo haimuondoki kwenye ufisadi kutokana na vigezo alivyotumia Dr. Slaa.
Hawa watu wanaomjibu Dr. Slaa wanakurupuka tu nadhani bado wanaweweseka kwani hawaamini kwamba siku moja tungefika sehemu kama hii. Nadhani Mgonja pekee ndiye aliyejitahidi kujibu hoja za Dr. Wangeanza na vigezo alivyotumia kabla ya kurukia kwenye orodha ya mafisadi ingeweza kuwasaidia sana. Mambo mengi aliyoeleza Dr. Slaa ni ya kweli sasa ni kifipi utageuza True to be False? Huo ni uendwazimu. Kama wanahitaji msaada wa kujibu hoja ni nafuu waseme.
 
Haya sio majibu kwani mbona hawasemi ni kwa nini Tangold ikasajiliowa nje ya nchi kama kweli na kampuni la serikali.

Mbona wanasema kuwa kuhusu madini ni nyeti na watatoa taarifa rasmi hapo baadae.

Duh, kilio cha samaki.........Remmy......the handsome.
 
Nenda kamwambie mh.Rais kuwa dhamira bila vitendo haina maana hata kidogo.

Kusema ni rahisi mno kuliko kutenda, kwa nini awache hao mafisadi kwa kiasi hicho, mbona amesema mengi tu kuwa urais wake hauna ubia hapa ndio maahali pa kuonyesha kwa vitendo .

Nenda kamwambie waziri mkuu kuwa wanaokula pesa za maendeleo ni haoa haoa wanaoichangia ccm kila kukicha wakiacha kuzila watapata wapi za kuchangia.
 
Propaganda za Magazeti kuhusu dhamira ya JK kupambana na rushwa
Dhamira ya Rais Kikwete kuvalia njuga rushwa ni dhati, isibezwe


Unajua kuna kitu kimoja muhimu, kuanzia magazeti mpaka wanazi wa vyama hawaelewi kuhusu hii forum, ni kwamba no matter how much spin you present hapa, ni kazi ya bure tu,

Maana hii forum ina vichwa safi sana katika ku-read betweeen the lines, tena kwenye kila ishu ndio maana huwa mra nyingi tunaandika tu na kuwaachia wananchi waamue hapa, maana ninajua kuwa hakuna aliyelala hapa forum,

Shukrani mkuu Halisi!
 
Bado tutaendelea kushikia bango suala la Takukuru kuwa huru. Kama wanataka taasisi hii iwe na meno basi waiondoe kutoka katika ofisi ya raisi, ili iweze kujitegemea na kufanya kazi bila vitisho. Hosea hawezi kumchunguza JK ama EL kamwe, tusahau hili!
 
Kama dhamira zingekuwa muhimu kiasi hicho, nguruwe wangeota mbawa! Haitoshi kuwa na dhamira na nia nzuri kwani hata barabara ya kwenda motoni inatengenezwa kwa dhamira safi..
 
i dont care kama yumo au hayumo kwenye hiyo list...lakini ukweli Jk anatuangusha sana maana hakuna kitu anafanya na anajua nchi inaliwa sana tuu na sasa kwanini naye wasimwite fisadi tuu hata kama haibi direct...huyu mtu ana tabia za kiswahili za kishkaji shikaji ambazo zinatuumiza
 
i dont care kama yumo au hayumo kwenye hiyo list...lakini ukweli Jk anatuangusha sana maana hakuna kitu anafanya na anajua nchi inaliwa sana tuu na sasa kwanini naye wasimwite fisadi tuu hata kama haibi direct...huyu mtu ana tabia za kiswahili za kishkaji shikaji ambazo zinatuumiza

Vile vile tusisahau waswahili wasemae ukishindwa jua tabia ya mtu 'mwangalie rafiki yake'

-Haiwezekani Jk awe safi wakati kazungukwa na mafisadi
-Haingii akilini kwamba yeye ni safi wakati ana simama kidete kuwatete mafisadi ( Mfano ANBEM)
-Haiwezekani awe msafi ashindwe kujitenga/kujitofautisha na mafisadi kwa kutumia maneno mepesi kwamba hawezi msimamisha mtu kwani hizo ni tuhuma ( rejea Balali)

Ili tumtenganishe na hao mafisadi basi afanye kweli vinginevyo kigugumizi chake kinatushawishi tuamini kwamba huu ni mwendo wa waswahili wa pwani wajuanao kwa vilemba.. pengine anapanga timu anawambia fanyeni mie nitawalinda!

Hatujasahau tetesi za hoteli inayo jengwa kwenye mbuga gani vile??.... unadhani ni bure??
 
Hii ndio Tanzania, na hivi ndio vyombo vya habari vya Tanzania.

--
From : Ansbert Ngurumo
Sent : 9/28/2007 1:40:29AM
To : tamwa@raha.com
Cc :
Subject : FW: Mkutano wa wahariri wape wahariri salamu hizi

Dada Nkya na wapambanaji wote wa TAMWA,

Salaam.

Nasoma sana habari za nyumbani. Nawapongeza kwa mapambano makali mnayoshiriki katika ukombozi wa
taifa letu. Kufanya kazi mnayofanya sasa, katika sheria dhalimu kadhaa tulizonazo, ni ujasiri
unaopaswa kupongezwa.

Leo nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba mtakutana na wahariri wapato 50 kujadili ufisadi.
Hili nalo ni tukio lenye uzito wake. Nawapongeza pia kwa kuandaa mjadala huo, na nawatakia
mafanikio mema. Sijaalikwa, na sababu zinaeleweka, lakini nipo nanyi kiroho na kiakili katika
mkutano huo.

Kwa sababu hiyo, naona bora niandike mawili niliyonayo, ambayo ni mchango wangu katika
kufanikisha mjadala huo.

1. Wahariri dhaifu

Ni vema mjadala huu utumike pia kuwakumbusha wahariri wenyewe kwamba miongoni mwao wamo mafisadi. Hakuna haja ya kutajana majina hapa, lakini inajulikana kwamba baadhi ya wahariri wamekuwa mafisadi ama kwa sababu ya tamaa au kwa kutumiwa bila kujua. Bahati mbaya, jamii iliyotuzunguka inatujua na inatusema kichini chini, inatudharau na itafika mahali itatupuuza au kutuadhibu. Bahati mbaya, hata baadhi ya 'wanaotutumia' wakishafanikisha malengo yao, au mambo yakiharibika, wanatudharau na kutusema vibaya. Wanadhani kwamba kwa sababu wao waliweza kututumia tukatumika, ndiyo tabia yetu, hivyo tunaweza kutumiwa na wengine dhidi yao kwa njia hiyo hiyo. Hawatuamini.

Tusikubali kufika huko. Habari zilizonifikia ni kwamba kuna magazeti kadhaa hapo nchini yanaongozwa na wahariri 'dhaifu' ambao wamelainishwa na mmoja wa vinara wa mtandao - Rostam Azizi -kiasi kwamba wako tayari kuacha kuandika habari zinazoigusa serikali hata kama zina maslahi ya kitaifa, wako tayari kupotosha habari au kufifisha mapambano ya kifikra yanayoendelea ili kutumikia maslahi yao. Sina haja ya kuyataja hapa. Mnayajua,na wahariri hao wanaosubiri serikali 'iwafikirie' wanafahamika.

Tutumie fursa hii kukumbushana hilo, uhariri wa kizazi hiki umekuwa kama uongozi wa sasa wa CCM; kwamba tusipojisafisha sisi wenyewe, mjadala huu dhidi ya ufisadi hautakuwa na maana.

2. Haja ya uasi

Amri za Mungu zinatufundisha kuwatii wakubwa na wenye mamlaka. Lakini zinatufundisha pia kwamba hatuna sababu ya kuwatii watakapotutaka tuzivunje amri hizo. Tuna haki ya kuasi amri zao kwa ajili ya maslahi makubwa zaidi. Kwa msingi huo huo, wahariri tunapaswa kuzitupia macho sheria dhalimu tunazozitumikia na zinazosimamia taaluma yetu. Zipo nyingi, na 'mama yao' ni Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Tumekuwa tunapiga kelele ziondolewe au zirekebishwe. Serikali imekaa kimya.

Serikali hii ilipotaka kuonyesha uhodari, ikaibuka na muswada dhalimu zaidi wenye jina zuri na malengo mabaya, ambao tuliupinga na kufanikiwa kuusitisha 'kwa muda.' Serikali yetu haina dhamira ya kuwatumia wananchi kama inavyosema; ndiyo maana haiondoi sheria mbovu wala haizirekebishi,lakini inazidi kutunga sheria dhalimu nyingine tunazoripoti. Nasikia hata sasa wanapeleka muswada wa sheria mpya ya uchochezi.

Hiki ni kitanzi ambacho waathirika wa kwanza ni sisi tunaojipendekeza kwa serikali hiyo hiyo. Kumbuka, ni majuzi tu serikali hiyo hiyo (kwa kutumua Bunge letu) imetunga sheria ya TAKUKURU ambayo ni dhaifu kama iliyokuwapo.

Tufanye nini? Wahariri tunapaswa kuwa chachu ya mabadiliko ya kitaifa. Tunapaswa kusimama upande wa wanyonge wa Tanzania. Tunapaswa kuwa jasiri na kusimamia ukweli, uhuru na uhai wa taifa hata kama itabidi tutoe sadaka ya maslahi yetu na maisha yetu. Napendekeza wahariri tuanzishe uasi mtakatifu dhidi ya sheria dhalimu. Hata kama sheria hizi hazitaondoka leo, tukiendelea kuziasi tutazipunguza nguvu na hatimaye itakuwa rahisi kuwashawishi watawala kuzifuta.

Mshikamano tuliouonyesha dhidi ya Omar Mapuri, ulikuwa sehemu ya uasi wetu dhidi ya sheria dhalimu ya magereza - maana ni kweli waandishi waliopigwa walivunja sheriai hiyo! Hivyo, Mapuri alikuwa sahihi lakini alikuwa anatetea sheria ya kihuni. Kazi iliyofanywa na gazeti la MwanaHALISI wiki iliyopita kuwataja watuhumiwa wa ufisadi ni uasi mtakatifu dhidi ya sheria hizi za kikoloni.

Laiti magazeti yote nchini yangeandika hivyo na kushitakiwa, ungekuwa mwanzo mpya wa mageuzi ya maana. Kingekuwa kishindo kikuu kama kilicholetwa na maandamano ya wafanyakazi na wananchi waliompokea Zitto Kabwe, au hata wanaowazomea viongozi mikutanoni wanapohisi wamehadaiwa.

Hatuwezi kujikomboa kwa kujikomba. Wahariri wakijikabidhi kwa watawala kwa sababu ya safari, mishiko na ahadi za kuteuliwa; wakizitii sheria dhalimu na kuwanyima wananchi kile wanachostahili kwa sababu tu ya kuenzi mawazo ya kikoloni, hata wakikaa na kujadili ufisadi kwa wiki nzima, stori za ufisadi zitafia kwenye madawati yao, isipokuwa kama zitakuwa zile ambazo baadhi yetu wanaziita 'zinazowahusu wale wanaopigwa vita na wanamtandao.'

Bila ujasiri na uasi huu, mjadala kuhusu ufisadi utapungua makali. Maana tutakuwa watu wa maneno yasiyo vitendo, na tutakosa dhamira halisi na mamlaka ya kuwasema mafisadi au watuhumiwa wa ufisadi. Nasi tutakuwa waigizaji na wasanii kama hao tunaowaandikia. Kimsingi, tutakuwa watumwa wanaotumia kalamu zetu kutetea uhuru wa wengine bila kufikiria ukombozi wetu wenyewe.

Dhamana tuliyobeba kwa nyadhifa zetu ni kubwa. Inaweza kulitosa au kulibomoa taifa. Tujikomboe kutoka kwenye minyororo ya ufisadi, ili mjadala wetu juu ya ufisadi uweze kuwa na maana. Tuuondoe uandishi kwenye 'ukarani' uwe zana ya uchambuzi, harakati na mapambano ya kuleta haki, usawa, heshima na tunu zote walizopigania waasisi wa uhuru wa Tanzania. Woga na uzembe viwekwe pembeni, tuvae uzalendo, tutimize wajibu wetu.

Naamini tuna wahariri makini. Naamini walio dhaifu wa dhamiri na tabia ni wachache. Ndiyo maana nina imani kubwa na mkutano wenu huo na mjadala utakaotokana nao. Yawezekana huu ni mwanzo wa matengenezo mapya ya wahariri na taaluma ya uandishi wa habari; na mwendelezo wa vita kali dhid ya ufisadi. Nawatakia mafanikio.

Kwa unyenyekevu mkubwa,

Ndugu yenu,

Ansbert Ngurumo
 
Najua Ngurumo ni mwana JF na kwamba pengine hakutaka barua hii ichapishwe kwani anajua walengwa wameipata. Lakini baada ya kuisoma barua hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHalisi, nimeona kwa faida ya wana JF na Watanzania, barua hii niiweke hapa ili isomwe na wengi zaidi japo nafahamu baadhi ya yaliyoandikwa si mapya sana kwa kuwa WATANZANIA WANAJUA. WATANZANIA SI WAJINGA.
 
Back
Top Bottom