MCL, IPP zaungana kupambana na rushwa
Na Mwandishi Wetu
Gazeti la Mwananchi
KAMPUNI za Mwananchi Communications Limited (MCL) na IPP Media zimekubaliana kuunganisha juhudi za kupambana na rushwa kwa waandishi wa habari.
Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa jana na pande zote kwenye Hoteli ya Movenpick ni kuhakikisha waandishi wa kampuni hizo hawapokei 'bahasha' kutoka kwa watoa habari.
Katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa, viongozi wa kampuni hizo walikubaliana kuwazawadia waandishi wao ambao watakuwa wanakataa fedha maarufu kama mshiko kutoka kwa watoa habari.
Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, alisema hatua hiyo inalenga kuweka mshikamano kwenye masuala yenye maslahi kwa taifa na kwamba kuanzia sasa hawatakubali mtu yeyote kuwagawa.
"Naona sisi IPP na MCL tuanze, sio kwamba tunawabagua wengine (vyombo vya habari), hapana. Wakitaka watatufuata, ila sisi lazima tuwe na mshikamano kwenye masuala yenye maslahi na taifa na kulinda hadhii ya taaluma ya habari inayozidi kuporomoka kila siku," alisema Mengi.
Mengi alisema katika ushirikiano wa aina hiyo wanaweza kupunguza gharama za uendeshaji kama kusafirisha magazeti kwa kutumia usafiri (magari) wa pamoja ili kuimarisha mshikamano na mafanikio kwa makampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Sam Shollei, alisema iwapo suala la rushwa halitaanza kupigwa vita kwenye vyombo vya habari, taifa haliwezi kufanikiwa katika harakati zake za kupambana na rushwa.
Shollei alisema biashara ya vyombo vya habari Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na Kenya na Uganda kwa idadi ya magazeti yanayochapishwa kila siku, lakini linapowadia suala la maslahi ya taifa kila chombo kinakuwa na msimamo wake.
"Ushirikiano wetu unaweza ukapanuka kwa kufanya mafunzo ya pamoja na suala la gharama za uendeshaji. Lakini taifa la kidemokrasia haliwezi kuwepo kama vita dhidi ya rushwa haiwezi kuanza kwenye vyombo vya habari," alisema Shollei.
Alisema waandishi wa habari wa kampuni hizo watakapotambua jukumu na wajibu wao kwa jamii, itakuwa rahisi kwa serikali kupambana na vita hiyo na kuongeza: " Tunatakiwa kuhakikisha tunajikinga rushwa isitugawe".
Mhariri Mtendaji wa MCL, Theophil Makunga alisema, makubaliano hayo yanaweza kubadili mwelekeo wa habari Tanzania.
Naye Mhariri Mtendaji wa This Day, Evarist Mwitumba, aliwataka waandishi wa habari kuwa na moyo wa kukataa rushwa ili waweze kupambana nayo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa The Guardian, Kiondo Mshana, alisema rushwa ziko nyingi kwenye vyumba vya habari na kwamba, baadhi huwa zinaandaliwa taratibu.
Akatoa mfano kwa kuhoji kumbwa mwandishi anapogombea ubunge anakuwa ameanzia wapi?