[FONT=Georgia, Times New Roman, Times, serif]*Asema wakishinda watafukuzwa
*Adokeza namna atakavyopata taarifa zao
[/FONT][FONT=Georgia, Times New Roman, Times, serif] NA PREMI KIBANGA, SHINYANGA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameonya kwamba, mgombea atakayebainika ameshinda kwa kutoa rushwa, atafukuzwa.
Tahadhari hiyo aliitoa jana katika mkutano wa hadhara wilayani Kishapu, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga.
[/FONT][FONT=Georgia, Times New Roman, Times, serif] Chama Cha Mapinduzi kinafanya uchaguzi wa viongozi nchini kote kwa ngazi ya wilaya, leo na kesho na Septemba 10 na 11 utafanyika uchaguzi wa viongozi ngazi ya mkoa.
"Napenda kutoa tahadhari kwa wanachama wote, hatutakuwa tayari kuwa na kiongozi aliyepata uongozi kwa kutoa rushwa, mkibainika hamtaendelea kuwa viongozi," alisema Rais Kikwete.
Alisema wapo watu wanaofuatilia mwenendo wa uchaguzi na kukusanya taarifa mbalimbali zitakazofanyiwa kazi.
"Chama hakiwezi kuendelea kuwa na wanachama wanaonunua uongozi," alisema na kuongeza kwamba ameweka vyanzo vyake vya kumpa taarifa, na kazi hiyo inafanyika.
" Na mara uchaguzi utakapokamilika, nataka kamati za siasa za wilaya na mikoa kufanya tathimini, lakini kubwa nataka taarifa ya viongozi waliopata uongozi kwa kununua," alisema.
Alisema amejipanga vyema na vya kutosha kupata taarifa hizo.
Kabla ya mkutano na wananchi, Rais Kikwete alizindua mnada wa kisasa wa ng'ombe.
Mnada huo umegharamiwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika, iliyotoa sh. bilioni 14.4.
Mradi huo umejengwa katika eneo la Muhunze lenye mifugo mingi, ili kuweka mazingira mazuri kwa wafugaji kupata faida kutokana na mifugo yao.
Rais pia alielezea azma ya serikali ya kufufua kiwanda cha nyama cha Shinyanga ambacho kilishakamilika, lakini hakijaanza kazi.
Alisema serikali imetenga sh. milioni 160 kwa ajili ya kupanua huduma ya maji wilayani Kishapu, na kuna mpango mwingine wa maji ambao umeandaliwa na utahudumia vijiji tisa wilayani humo, ili kupunguza na hatimaye kulimaliza tatizo la maji wilayani humo.
Wilaya ya Kishapu ni wilaya mpya ambayo haina hospitali, lakini tatizo hilo limeshashughulikiwa na tayari imepata kiwanja cha kujengea hospitali na fedha zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.[/FONT]