Tanzania, Uganda na Zambia ni moja ya nchi kumi zitakazopata fursa zaidi ya soko nchini China

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111409857737.jpg

Kwa mara nyingine tena China imeendelea kuonyesha udhati wake kwenye kuzipatia fursa nchi zilizonyuma kiuchumi, kwa kufungua zaidi soko lake na kupunguza masharti ya kuingia kwenye soko. Hatua mpya ya mwelekeo huu ni ile iliyotangazwa na kamisheni ya ushuru ya baraza la serikali ya China, iliyotangaza kuwa kuanzia Desemba mosi 2022, asilimia 98 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Afghanistan, Benin, Burkina Faso, Guinea-Bissau, Lesotho, Malawi, Sao Tome na Principe, Tanzania, Uganda na Zambia hazitatozwa ushuru.

Kwa wale wanaofuatilia uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya China na nchi za Afrika, uamuzi huu wa China kimsingi si jambo jipya. Huu ni mwendelezo wa juhudi za China kuongeza fursa zaidi kwa nchi za Afrika na nchi nyingine zenye mahitaji na utayari wa kutumia soko la China kujiendeleza. Kabla ya uamuzi huo kufikiwa, tayari nchi 16 zilizonyuma kimaendeleo zikiwemo Togo, Djibouti na Rwanda, zilikuwa zimepata ahadi hiyo kuanzia Septemba mosi 2022.

Hatua hii ya serikali ya China inatokana na ahadi iliyotolewa na serikali ya China mwaka jana kwenye mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC, kuwa katika miaka mitatu ijayo China itatumia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 300 kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nchi za Afrika, na kupitia uagizaji huo itaondoa kabisa ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa. Mwaka 2021 wakati China ikitoa ahadi hiyo, thamani ya uagizaji wa bidhaa za kilimo peke yake kutoka Afrika ilikuwa ni dola za kimarekani bilioni 5.03, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 18 kwa mwaka. Kama kiasi hicho kikifikia dola bilioni 300 kwa miaka mitatu, litakuwa ni ongezeko kubwa sana, ambalo litaleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na hata serikali za nchi za Afrika.

Watunga sera wa upande wa China na Afrika, wametambua kuwa biashara ndio njia muafaka na endelevu ya kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana kati ya pande mbili. Takwimu zimethibitisha kuwa kuna faida kubwa kwa pande mbili ushirikiano wa kibiashara unapozidi kuwa wa kina. Mwanzoni mwa mwezi Novemba, mamlaka ya forodha ya China ilitangza kuwa kuanzia Januari hadi Oktoba 2022, thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 236, zikiwa ni ongezeko la asilimia 14.3 kwa mwaka.

Uamuzi uliotangazwa na serikali ya China unatarajiwa kugusa aina zaidi ya 8,700 za bidhaa kutoka nchi za Afrika, ikiwa ni bidhaa za kilimo kama vile mafuta ya zeituni, unga wa kakao, bidhaa za karanga na bidhaa mbalimbali za kemikali zipo kwenye orodha hiyo. Kwa sasa China ni mwagizaji mkubwa wa pili wa bidhaa kutoka Afrika, na uagizaji huo kwa upande wa bidhaa za kilimo umekuwa unaongezeka kwa wastani wa asilimia 11.4 kwa mwaka.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa kufunguliwa kwa fursa hii kwa nchi za Afrika, kunafungua fursa nyingine za uwekezaji na ujasiriamali. Kutokana na itifaki za karantini na udhibiti wa ubora, bidhaa zinazoingia kwenye soko la China zinatakiwa kukidhi vigezo mbalimbali. Mchakato wa kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zinakidhi vigezo, unahitaji uchakataji, upimaji, ufungaji na usafirishaji. Maeneo yote hayo manne ni fursa kwa wajasiriamali. Hili tayari limeshuhudiwa kwenye bidhaa mbalimbali ambazo tayari zinaingia kwenye soko la China, ambapo wajasiriamali kwa kutumia mitambo midogomidogo wameweza kuanzisha makampuni ya kuchakata na kufunga bidhaa zinazosafirishwa nje.

Jambo la muhimu kwa sasa ni kwa wajasiriamali hasa vijana kuchangamkia fursa hizi, kwa kutafuta habari za kina kuhusu bidhaa gani zinaweza kutoka kwenye nchi zao na kuweza kuingia kwenye soko la China, na wao wanaweza kunufaika vipi na fursa hiyo.
 
Back
Top Bottom