Msanii
Platinum Member
- Jul 4, 2007
- 22,592
- 29,712
Wakuu, Nawakilisha....
=============
UPDATE
=============
LEGAL AND HUMAN RIGHTS CENTRE
Justice Lugakingira House, Kijitonyama, P. O. Box 75254, Dar Es Salaam, TANZANIA
Telephone: 2773048, 2773038, Fax: 2773037, E-mail: lhrc@humanrights.or.tz
Website www.humanrights.or.tz
TANGAZO
Maandamano ya Amani Dhidi ya UFISADI na Malipo kwa Kampuni ya Dowans Jumamosi 29/10/2011
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu nchini wameandaa maandamano ya amani Dar es salaam siku ya Jumamosi hii tarehe 29 Oktoba 2011 kupinga ufisadi na malipo TATA ya kifisadi kwa kampuni ya Dowans kama njia mojawapo ya kumuenzi baba wa Taifa. Maandamano haya yataanzia Ubungo nje ya ofisi za TANESCO mpaka viwanja vya Jangwani kuanzia saa 2.30 asubuhi.
WATANZANIA WAZALENDO SHIME TUUNGANE NA TUJITOKEZE KWA UMOJA WETU KUPINGA UFISADI HUU NA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA NA MALI ZETU.
Imetolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Francis Kiwanga (Adv.)
Mkurugenzi Mtendaji.
=============
UPDATE
=============
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
MAANDAMANO YA KUPINGA SERIKALI KUILIPA DOWANS Sh. BILIONI 111
Novemba, 2010 Mahakama ya usuluhishi ya kimataifa ilitoa tuzo dhidi ya Tanesco kuilipa Dowans shillingi billion 94. Jambo hili liliibua hisia na hasira miongoni mwa wananchi kwa kulalamika na kupinga ulipaji huo wa fedha za umma kwa kampuni tata - kutokana na taarifa za kamati teule ya Bunge.
Baada ya tuzo hiyo watu binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mawakili wa Tanesco walipinga mahakama kuu kusajili tuzo hiyo. October 2011 Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kusajili tuzo hiyo na kuamuru Tanesco ilipe shillingi billion 94 na asilimia 7.5 ya gharama hizo. Hata hivyo kabla ya usajili wa tuzo hiyo, Dowans iliuza mitambo husika kwa kampuni ya Symbion Powers kinyume cha taratibu kwa kuwa kulikuwa na amri ya mahakama ya kuacha hali ya mitambo ibaki kama ilivyo. Cha kushangaza ni jinsi ambavyo Serikali ilikuwa mstari wa mbele katika kuingia mkataba wa uzalishaji wa umeme na Symbion Powers kwa gharama ya watanzania hali ikijua mitambo hiyo iko kwenye mgogoro uliopo mahakamani.
Kwa kuzingatia haya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Asasi kadhaa za Kiraia na Wanaharakati wa Haki za binadamu tulitoa tamko tarehe 11 Oktoba 2011 kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa bila mafanikio.
Kwa kuwa serikali imeamua kudharau maoni yetu, na kwa kuwa kuna kila dalili kwa serikali kuilipa Dowans fedha za wananchi, sisi, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, serikali wakilishi za wanafunzi na raia wa kawaida wa Dar es salaam tunaitisha maandamano kwa uratibu wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu siku ya Jumamosi tarehe 29/10/2011. Kwa hapa Dar es salaam, maandamano yataanzia Ubungo, mbele ya zilipo ofisi za Makao makuu ya TANESCO hadi Viwanja vya Jangwani kuanzia saa 2:30 asubuhi.
Maandamano haya yanalenga kuitaka serikali kufanya yafuatayo:-
- Kutokuilipa kabisa Dowans kwa kutumia hela za walipa kodi wa Tanzania.
- Itoe maelezo ya kina kwanini ilipuuza ushauri wa kisheria wa kuvunja mkataba na Richmond toka awali kwani kwa mujibu wa washauri wa kimarekani Hunton & Williams LLP wakati Tanesco inaingia mkataba na Richmond Devt Co. Kampuni hiyo haikuwa imeshasajiliwa achilia mbali kuwa haikuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake chini ya mkataba huo.
- Itekeleze kwa dhati maazimio 23 yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya mlolongo mzima unaopelekea mpaka sasa tutakiwe kulipa bilioni 111. Kwa kufanya hili Serikali pia ituthibitishie kuwa itaacha kabisa kukikosea heshima chombo ambacho ni kisemaji na wakilishi cha wananchi kupitia wabunge.
- Kama sheria za kimataifa zinatubana kulipa deni hili basi malipo haya yafanyike kwa kuuza mali za wale waliotusababishia kadhia hii na kwamba malipo ya kuilipa dowans yafanyike pale tu serikali itakuwa imeshawachukulia hatua kali wahusika wa kadhia hii. Umma ni lazima ujiridhishe kwa kuona hatua hizo zinachukuliwa.
- Kuchukuwa hatua ya kinidhamu kwa wale wote walioshiriki katika kuingiza serikali katika mkataba huu hata mawakili waliotoa ushauri huu.
- Serikali ipeleke Bungeni muswada wa utaratibu mzuri na sahihi wa kushirikisha wananchi na hata wabunge katika kuingia mikataba ya kimataifa na serikali ili kuepusha hali kama hii kutokea.
Kwa hiyo tunatoa wito kwa watanzania wote tuadhimishe kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutenda yafuatayo:-
- Tujitokeze kwenye maandamano ya amani na kupinga ufisadi na malipo ya kifisadi ya Dowans siku ya Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2011.
- Kuvaa nguo za maombolezo, nyeusi, kama ishara ya maombolezo tukikumbuka msimamo wake wa kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa,
- Tuzitumie siku za ibada za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zote ndani ya muda huu, kumuomba Mungu atujalie Uzalendo na Ujasiri wa kuitetea nchi yetu, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere,
- Kuwasiliana na wanaharakati nchi nzima mahali walipo, ili kupanga na kuandaa mahali pa kukutania siku ya maandamano haya ya amani.
Mwisho, tunaomba walipa kodi (wananchi) wote ambao hawajapendezwa na mlolongo huu unaopelekea ulipaji wa deni hilo la Dowans na ufisadi mwingine wote kuwa na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kusimamia kile ambacho wanaona ni haki na stahili ya wananchi wote na taifa letu kwa ujumla.
Kwa niaba ya asasi za kiraia ncini Tanzania zinazopigania haki na kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za Umma.