Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Kizungumkuti! - 68

Na Bishop Hiluka

ILIPOISHIA

“Nzuri tu, karibuni,” Dk Masha aliitikia huku akimpa ASP Komba mkono, kisha akamsalimia Sajenti Mapambano na wote wakaketi kwenye viti. Walipoketi tu Dk Masha alivuta droo ndogo ya meza yake na kutoa humo kitabu kidogo cha kumbukumbu.

“Kitu pekee nilichokipata kutoka kwenye mfuko wa suruali ya marehemu ni hiki kitabu chake cha kumbukumbu,” Dk Masha alisema huku akinyoosha mkono wake kumpa ASP Komba kile kitabu.

ASP Komba alikipokea kile kitabu cha kumbukumbu, maarufu kama Diary na kukigeuza geuza huku akikiangalia kwa umakini. Kilikuwa kitabu kidogo cha rangi ya bluu.

“Pia kuna karatasi zingine mbili tatu, labda zitaweza kuwasaidia,” Dk Masha alisema tena huku akichukua zile karatasi na kunyoosha mkono wake kumpa ASP Komba.

Endelea...

ASP Komba alizipokea zile karatasi na kuzitupia jicho mara moja kisha akayarudisha macho yake kwenye kile kitabu cha kumbukumbu. Akakifungua na macho yake yakatua kwenye ukurasa wa kwanza tu ambapo alikutana na jina la mmiliki wa kile kitabu, “Carlos Mwamba” likiambatana na taarifa zingine binafsi ikiwemo mawasiliano yake.
ASP Komba akaonesha kushtuka kidogo kwa kuwa alimfahamu vyema Carlos Mwamba, ni wiki chache tu zilizokuwa zimepita walikutana wakaongea na Carlos Mwamba alimuahidi kuwa alitaka kulisaidia Jeshi la Polisi kiasi cha shilingi milioni 100 katika operesheni zake mbalimbali.
ASP Komba alishusha pumzi kisha akaanza kuangalia kurasa mbili tatu na hapo macho yake yakatua kwenye karatasi mbili zilizokuwa zimepachikwa kwenye ukurasa mmoja wa kile kitabu cha kumbukumbu.
ASP Komba alizitoa zile karatasi na kuzitazama kwa umakini, karatasi moja ilikuwa ni nakala kivuli (photocopy) ya hundi ya The Jacarandah Group iliyokuwa na saini na karatasi nyingine ilikuwa imeandikwa namba kadhaa za simu.
ASP Komba alizitazama zile namba kwa umakini mkubwa na kugundua kuwa namba mbili kati ya zile zilikuwa ni namba alizokuwa ameziona kwenye simu ya Yusuf, moja ikiwa ni namba ya Joram Mbezi, ambayo pale ilipewa jina la Kisu na namba ya Belinda Jackson, ambayo pale ilipewa jina la beloved coordinator.
Pia katika orodha ile kulikuwa na namba aliyoifahamu kuwa ni ya Yusuf na namba nyingine mbili ambazo hakuweza kuzifahamu. ASP Komba alijikuta akiachia tabasamu pana ambalo baadaye lilitengeneza kicheko hafifu na hivyo kuwafanya Dk Masha na Sajenti Mapambano wapate shauku ya kutaka kujua kilichokuwa kimeandikwa kwenye zile karatasi.
“Vipi, afande, kuna lolote umegundua?” Dk Masha alimuuliza ASP Komba kwa shauku huku akijitahidi kurefusha shingo yake ili ajionee kilichokuwemo kwenye zile karatasi.
“Huwezi kuamini, umenisaidia sana, dokta… nilikuwa nina hamu kubwa sana ya kukutana na huyu mtu,” ASP Komba alisema huku akiendelea kutabasamu.
“Nani, huyu marehemu?” Dk Masha alimuuliza ASP Komba kwa mshangao.
“Naam! Lakini tayari kajihukumu mwenyewe…” ASP Komba alisema na kusita kidogo, kisha kama aliyegutuka akauliza, “Na hali ya yule binti aliyekuwa na marehemu ikoje?”
“Yule binti kama atavuka kesho jioni basi ataweza kuongea,” Dk Masha alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
ASP Komba aliinuka kutoka kwenye kiti chake huku akiendelea kutabasamu kisha akampa ishara fulani Sajenti Mapambano ambaye pia aliinuka, wakamuaga Dk Masha.
“Nakushukuru sana, dokta, huwezi kujua ni kwa kiasi gani umeifanya kazi yangu kuwa rahisi mno, nitakutembelea kesho au keshokutwa kutegemea na hali ya yule binti itakavyokuwa, maana nina hamu kubwa ya kutaka kuongea naye.”
“Karibuni sana,” Dk Masha alijibu huku akiinuka kutoka kwenye kiti chake na kuwasindikiza ASP Komba na Sajenti Mapambano. Wakatoka nje na kuelekea walikokuwa wameegesha gari lao.
Waliingia kwenye gari lao na dereva akaliondoa, waliamua kurudi ofisini. Walipofika ofisini ASP Komba aliketi kwenye kiti chake, akaanza kupitia maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwenye kile kitabu cha kumbukumbu cha Carlos Mwamba, ukurasa mmoja baada ya mwingine.
Kuna wakati alijikuta akisisimkwa mwili wake kutokana na kusoma mipango ya hatari iliyokuwa imeandikwa kwenye kile kitabu cha kumbukumbu ikionesha tarehe ya kutekeleza mipango ile na aina ya watu ambao wangetumika kufanikisha mipango ile.
ASP Komba hakuamini kabisa kile alichokuwa akikisoma kwenye kile kitabu cha kumbukumbu cha Carlos Mwamba, mtu aliyekuwa rafiki yake, yeye na mkewe Jackline Mgaya Mwamba. Siku zote ASP Komba aliamini kuwa Carlos ni mfanyabiashara mwenye mafanikio na raia mwema aliyependa kusaidia wengine kwa hali na mali, kumbe ni mbwa mwitu ndani ya ngozi ya kondoo!
Hadi wakati ule ASP Komba alikuwa bado akikkikodolea macho kile kitabu cha kumbukumbu akiwa haamini kama ni kweli Carlos Mwamba alikuwa nyuma ya uhalifu ule, akaamua kuingiza jina la Carlos Mwamba kwenye ile kompyuta maalumu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kanda Maalumu iliyokuwa pale ofisini ili kutafuta taarifa zake.
Alipoingiza tu lile jina zilikuja taarifa nyingi zilizoonesha kuwa Carlos Mwamba alikuwa mfanyabiashara wa madini mwenye mafanikio makubwa akimiliki kampuni mbili, Mwamba Mines iliyojihusisha na biashara ya madini na Jaco Investment (ikiwa ni kifupi cha Jackline na Carlos) iliyokuwa ikihusika na ujenzi wa majumba (estates), na hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu.
Taarifa zile zilibainisha kuwa jina lake kamili aliitwa Carlos Michael Mwamba, mzaliwa wa jijni Mwanza, umri wake ulikuwa miaka arobaini na mbili, alikuwa na mke Jackline Mgaya Mwamba na aliwahi kupata mafunzo na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya System Analysis and Design katika Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza na baadaye alifanya mafunzo ya shahada ya uzamili katika masuala ya takwimu (Statistics) huku huko Oxford nchini Uingereza…
ASP Komba alishusha pumzi ndefu huku akimtazama msaidizi wake, Sajenti Mapambano, kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake huku akizitazama kwa makini picha kadhaa za Carlos zilizokuwa zimeambatana na taarifa ile.
“Niseme wazi, taarifa hizi zimenishtua sana, sikutegemea kama Carlos Mwamba anaweza kuwa ndiye Master Planner aliye nyuma ya uhalifu huu!” ASP Komba alisema huku akishusha pumzi.
Kisha alitoa paketi ya sigara na kuiweka kwenye pembe ya mdomo wake na kuchukua kiberiti kutoka mfukoni, akawasha ile sigara kwenye pembe ya mdomo wake na kusimama, akaelekea dirishani.
Alisimama pale dirishani na kutazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha akiyatazama mandhari ya jiji la Dar es Salaam yaliyokuwa yakipendeza katika muda ule wa alasiri. Hata hivyo, hakuwa na tashwishwi yoyote katika sura yake.
Alivuta sigara yake kwa utulivu huku akiutoa moshi mwingi na kuutazama kwa makini kisha akapiga mkupuo mwingine mkubwa wa moshi na alipoitoa sigara mdomoni akapuliza moshi wake pembeni huku akiutazama kabla ya macho yake kuweka kituo kwenye magari machache yaliyokuwa yameegeshwa katika sehemu maalumu ya kuegesha magari yaliyokuwa na kesi au matatizo katika lile jengo la polisi.
Alilitazama gari la Carlos Mwamba aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi ya samawati lililokuwa limeharibika vibaya baada ya kupata ajali kule kwenye daraja la Mto Msimbazi katika eneo la Vingunguti.
Wakati akiwa bado amesimama pale dirishani akitazama chini mara mlango wa kile chumba ukagongwa na kufunguliwa, ASP Komba na Sajenti Mapambano wakageuza shingo zao kutazama kule mlangoni na kumuona askari mmoja aliyekuwa na cheo cha Koplo akiingia na kutembea kwa ukakamavu hadi pale dirishani kisha akasimama karibu na ASP Komba na kupiga saluti ya ukakamavu.
“Afande, kuna mtu mmoja amepiga simu akijitambulisha kama raia mwema anayeishi Tabata Segerea, amesema kuwa amesikia mzozo mkali kwenye nyumba ya jirani yake anayeitwa Carlos Mwamba kuhusiana na mgao wa fedha,” yule askari mwenye cheo cha Koplo alisema.
Maneno yale yakawafanya ASP Komba na Sajenti Mapambano waangaliane kwa makini. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, kisha ASP Komba akashusha pumzi za ndani kwa ndani.

Itaendelea...

Cc the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater, Bigjahman moneytalk marybaby, nipo2, ram, kisukari, Smart911, Madame S, carbamazepine, Astelia, culture gal , Prisoner of hope, Mine eyes, kuku mweus, Thad, hearly, Shunie, moneytalk,Tumosa, Mine eyes, Kudo, swahiba92, ludist, Toyota escudo, Clkey, macson3, Thad, boga la kiangazi, macson3, LEGE, Smart911, Richard irakunda, skfull, popie, Krizy Beat, hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Kinondoni Sweetheart SUPER EMILY
 
Kizungumkuti! - 69

Na Bishop Hiluka

“Afande, kuna mtu mmoja amepiga simu akijitambulisha kama raia mwema anayeishi Tabata Segerea, amesema kuwa amesikia mzozo mkali kwenye nyumba ya jirani yake anayeitwa Carlos Mwamba kuhusiana na mgao wa fedha,” yule askari mwenye cheo cha Koplo alisema.
Maneno yale yakawafanya ASP Komba na Sajenti Mapambano waangaliane kwa makini. Kikatokea kitambo kifupi cha ukimya, kisha ASP Komba akashusha pumzi za ndani kwa ndani.

Endelea...

“Mzozo huo umetokea lini na saa gani?” ASP Komba alimuuliza yule askari mwenye cheo cha Koplo.
“Leo kama dakika therathini au therathini na tano hivi zilizopita zimesikika sauti za vitisho kutoka kwa vijana fulani wawili wakimweleza mke wa Carlos Mwamba kuwa wanataka fedha yao vinginevyo nyumba itawaka moto, pia wamesikika wakilaumu kuhusu kifo cha mwenzao anayeitwa Kisu…” yule askari mwenye cheo cha Koplo alisema huku akimkazia macho ASP Komba.
“Huyo jirani amepata kuwaona hao vijana?”
“Ndiyo, afande! Anasema ni vijana wawili ambao kimuonekano wanaonekana kabisa kuwa ni wahuni, na jinsi alivyowaelezea ninadhani wanashabihiana sana na wale walioonekana kwenye tukio la wiza pale benki kama ambavyo picha za video za CCTV zimewaonesha…” yule askari mwenye cheo cha Koplo alisema na kuongeza, “Amesema wale vijana wametoka lakini wameahidi kurudi tena jioni…”
ASP Komba alishusha pumzi ndefu na kuweka sigara yake mdomoni, alivuta akipiga mkupuo mkubwa wa moshi kisha aliutoa ule moshi huku akiutazama kwa umakini, alionekana kuzama katika lindi la mawazo.
“Kwa hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba fedha iliyoibwa pale Benki ya Biashara ipo ndani ya nyumba ya Carlos,” ASP Komba alisema huku akiendelea kuutazama moshi aliokuwa akiutoa mdomoni, kisha aligeuza shingo yake kumtazama yule askari mwenye cheo cha Koplo na kuachia tabasamu.
“Koplo!” ASP Komba alimwita yule askari mwenye cheo cha Koplo.
“Ndiyo, afande!” yule askari mwenye cheo cha Koplo aliitikia kwa ukakamavu.
“Kawaite kachero Haji na Seba wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kanda Maalumu, kisha na wewe uje ili muwe watatu, nataka kuanzia sasa muanze kufuatilia kwa siri nyendo zote zinazoendelea kwenye hiyo nyumba, na mhakikishe hakuna mzigo wowote unaotoka katika nyumba hiyo, sawa?” ASP Komba alimpa amri yule askari mwenye cheo cha Koplo.
“Sawa, afande!” yule askari mwenye cheo cha Koplo alijibu kwa ukakamavu.
“Okay, unaweza kwenda,” ASP Komba alisema na hapo hapo yule askari mwenye cheo cha Koplo alipiga saluti ya ukakamavu kisha akaondoka haraka kwa ukakamavu.
“Sasa, tunahitaji tena kumhoji Yusuf,” ASP Komba alimweleza Sajenti Mapambano.
* * * * *
Jacky aliitazama saa yake ya mkononi kwa mara ya mia moja. Alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kutingisha kichwa chake kwa huzuni huku akisonya. Alishangaa sana kwa kuwa hadi muda ule wa saa kumi jioni Carlos alikuwa hajarudi na wala simu yake ilikuwa haipatikani.
Alitamani sana atoke nje akamtafute lakini aliogopa, hasa alipokumbuka kauli ya Carlos alipomuonya kuwa makini. Akaanza kuhisi kuwa huenda labda Carlos alikuwa amekamatwa na polisi. Hata hivyo, wazo la kukamatwa kwa Carlos likamfanya aogope sana, akawaza kutoroka lakini akajikuta akijiuliza angekimbilia wapi!
Alijiuliza, akimbilie kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi jijini Tanga ambako Jacky alifanikiwa kuwajengea nyumba kubwa ya kisasa na kwa kumtumia Carlos, walikuwa na maisha mazuri wakimiliki kiwanda cha kusindika majani ya chai mkoani Tanga na miradi mingine kadhaa!
Hata hivyo, aliona isingekuwa busara kukimbilia Tanga kwa wazazi wake, hakutaka kuwaingiza kwenye matatizo, hivyo akajiuliza, akimbilie kwa jijini Mwanza, ambako pia yeye na mumewe Carlos walikuwa wamejenga nyumba kubwa ya kisasa iliyowagharimu mabilioni ya fedha? Ni huko huko jijini Mwanza ambako pia dada wa Carlos na wifi yake, Anita Mwamba alikuwa akiishi.
Au achukue fedha zote walizoiba katika Benki ya Biashara kisha akimbilie nje ya nchi akaanze maisha mapya?
Mawazo hayo na mengine mengi yalipita kichwani kwa Jacky kisha akayapuuza, alijipa moyo kuwa Carlos hakuwa mtu wa kukamatwa kirahisi namna ile, kwani alikuwa na mtandao mkubwa wa marafiki wakiwemo viongozi wakubwa serikalini na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa polisi. Hivyo isingewezekana kukamatwa kwa muda ule.
Swali likabaki, Carlos alikuwa wapi muda wote ule na kwa nini simu yake ilikuwa haipatikani? Simanzi ilimjaa Jacky moyoni mwake, hata hivyo alipiga moyo konde na kuamua kusubiri majaliwa ya Mungu.
Muda wote aliokuwa akiwaza hili na lile simu zilikuwa zinapigwa kwa fujo, alipozitazama namba zilizokuwa zikimpigia aliweza kuona namba ya Jacob, baadhi ya namba za rafiki zake na namba zingine ambazo hakuzifahamu kabisa.
Na wakati mwingine uliingia ujumbe mfupi wa maandishi lakini vyote hivyo Jacky alivipuuza, hakutaka hata kusoma ujumbe uliokuwa ukiingia kwenye simu yake. Ilifikia wakati ile simu iligeuka kuwa kero kubwa kwake na hata kuna wakati alitamani kuizima.
Kwa kweli siku ile ilionekana kuwa ndefu sana kwa Jacky. Ile simu haikuacha kuita, ikafika wakati sasa Jacky aliichukua ile simu kwa kusudi moja tu, la kuizima kabisa, kwani alishachoshwa na zile simu zilizokuwa zikipigwa mfululizo.
Lakini alipoichukua na kuiangalia vizuri namba iliyokuwa inaita akakutana na jina la mama yake mzazi. Jacky akashtuka kidogo, ingawa hakujua kwa nini alishtuka kuona mama yake akimpigia simu. Jacky aliikodolea macho ile simu wakati ikiita hadi ikakatika pasipo kupokea.
Akiwa bado anatafakari akijiuliza mama yake alitaka kumwambia kitu gani, mara ile simu ikaanza kuita tena, Jacky alijishauri kama aipokee au aachane nayo lakini kuna sauti ndani yake ikawa inamsisitiza kuipokea ile simu, hivyo alishusha pumzi na kuipokea kisha akaiweka sikioni.
“Hello, mama, shikamoo!” alisema kwa sauti tulivu ya chini iliyokuwa na kitetemeshi.
“Marhaba, mwanangu, pole sana kwa msiba, mwanangu! Tupo pamoja nawe…” sauti ya majonzi ya mama yake ilisikika kutokea upande wa pili wa simu na kumfanya Jacky apate mshtuko mkubwa.
“Msiba wa nani, mama?” Jacky aliuliza huku akiitazama ile simu kwa makini, na hapo hapo akaanza kuhisi kizunguzungu.
“msiba wa nani! Kwani aliyekufa siyo mumeo?” sauti ya majonzi ya mama yake ilisikika tena ikiuliza kwa mshangao na kumfanya Jacky ahisi kama ile nyumba yake ilikuwa ikizunguka kama tufe kubwa lililokuwa likining’inia angani. Kwa sekunde chache Jacky alibaki kimya akiwa ameganda kama sanamu.
Jasho lilianza kumtoka, alijiona kama aliyekuwa amepigwa na shoti mbaya ya umeme huku akiuhisi mwili wake wote ukiwa mzito sana kama uliogeuka kuwa kipande cha chuma na moyo wake ukisahau mapigo yake kwa sekunde kadhaa.
Aliitazama ile nyumba yake na kujiona kama aliyekuwa yumo ndani ya pango kubwa lililotisha sana. Hakuwahi kuwaza hata siku moja kwamba nyumba yake aliyoipenda ingeweza kuwa kitu cha kutisha kiasi kile na hata kufikia hatua ya kumfanya kupagawa na kuogopa mno. Ilikuwa ni siku ambayo hangeweza kuisahau kabisa katika maisha yake!
Kwanza alidhani kuwa labda alikuwa kwenye usingizi wa mang’amung’amu kwa sababu tangu alipoamka asubuhi alikuwa na mawazo mengi yaliyokuwa yanapita kichwani kwake kiasi cha kumchosha, na kwamba yote aliyokuwa ameambiwa na mama yake kwenye simu yalikuwa ni mambo yaliyotendeka wakati akiwa yupo ndotoni.

Itaendelea...
 
Kizungumkuti! - 70

Na Bishop Hiluka

Kwanza alidhani kuwa labda alikuwa kwenye usingizi wa mang’amung’amu kwa sababu tangu alipoamka asubuhi alikuwa na mawazo mengi yaliyokuwa yanapita kichwani kwake kiasi cha kumchosha, na kwamba yote aliyokuwa ameambiwa na mama yake kwenye simu yalikuwa ni mambo yaliyotendeka wakati akiwa yupo ndotoni.

Endelea...

Hali ile ikasababisha jasho jingi lizidi kumtoka sehemu mbalimbali za mwili wake, huku akihisi joto fulani ambalo alishindwa kulitafsiri likimtambaa mwilini mwake na mapigo ya moyo wake yakibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida!
Wakati akiwa katika hali ile mara hisia zake zikamtanabaisha kuwa ile haikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi kilichokuwa kimetokea na muda huo mama yake alikuwa akimfikishia taarifa zile. Hisia za kifo cha mumewe Carlos zikasababisha koo lake likauke ghafla huku nywele zake zikimsimama kichwani kwa hofu.
Hata hivyo, mara hii milango yake ya fahamu ilikuwa makini zaidi huku akijaribu kuishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika ili kujaribu kubaini endapo tukio lile lilikuwa katika mlolongo wa yale matukio ya ndotoni au la!...
“Jackline!” sauti ya upole ya mama yake ikamzindua Jacky kutoka kwenye yale mawazo. Jacky alishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Mama, kwani wewe taarifa hizi umezipata wapi?” Jacky alimuuliza mama yake huku akiwa bado haamini kile alichokisikia kwenye simu.
“Mbona zimesambaa kila mahali kwenye mitandao ya kijamii! Kuna mfanyakazi mmoja wa baba yako kule kiwandani ndiye aliyeanza kutupa habari hizi kuwa Carlos Mwamba amekufa kwenye ajali ya gari eneo la Vingunguti, sijui alikuwa anawakimbia polisi… tena wameweka hadi picha ya gari lake likionekana jinsi lilivyoharibika… Inamaana wewe hufahamu kama mumewo amekufa?” sauti ya mama yake ilisema maneno yale yaliyomfanya Jacky azidi kuchanganyikiwa.
Jacky aliuma midomo yake, akataka kuongea neno lakini akashindwa, kwani aligundua kuwa sauti yake ilikuwa haitoki, hivyo akaamua kukata simu.
Alipokata tu, mara simu ikaanza kuita tena, alipoitazama akaiona namba ya wifi yake Anita Mwamba. Jacky hakujiuliza tena, alibonyeza kitufe cha kupokelea na kuiweka ile simu sikioni, mara akasikia sauti ya Anita aliyekuwa akilia kwa uchungu mkubwa huku akiongea maneno ambayo Jacky hakuweza kuyasikia vizuri. Hakuona sababu ya kuendelea kuisikiliza ile simu, akaikata na kuitupia kando.
Hadi hapo hakuweza kuamini kama kweli Carlos alikuwa amekufa kwenye ajali, akafumba macho na kujiegemeza kwenye sofa huku akihema kwa nguvu, kisha kama mtu aliyekumbuka kitu, akaichukua ile simu na kuwasha data, na haikuchukua muda akaona ujumbe wa kifo cha Carlos Mwamba uliokuwa ukisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya WhatsApp na Instagram ukiambatana na picha ya gari aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi ya samawati lililokuwa limepondeka vibaya.
‘Mfanyabiashara maarufu wa madini ambaye pia anamiliki biashara kadhaa jijini Dar es Salaam amepata ajali eneo la Vingunguti wakati akiwakimbia askari, ajali hiyo imetokea mchana wa saa sita baada ya gari lake kupinduka na kutumbukia katika daraja la Mto Msimbazi, eneo la Vingunguti jijini Dar es salaam… pia ndani ya lile gari kulikuwa na binti mmoja ambaye bado haijulikani kama naye alikufa au alinusurika…’
Jacky alishtushwa sana na taarifa ile, alijikuta akisimama wima, mikono yake ikiwa kichwani huku akili yake ikikataa kabisa kukubali kile alichokuwa akikisoma. Ilikuwa ni habari mbaya sana aliyowahi kuisikia maishani kwake. Jacky aliendelea kusimama wima huku akiikodolea macho ile simu yake akiwa bado haamini, mawazo mengi yalizidi kupita kichwani mwake hukusu hatma yake.
Simu ziliendelea kupigwa, Jacky hakutaka kupokea simu yoyote, aliitupia kando ile simu huku ile picha ya gari BMW X6 xDrive 50i la rangi ya samawati lililokuwa limebondeka vibaya baada ya kupata ajali ikikataa kufutika akilini kwake.
Alianza kuhisi kuchanganyikiwa, sebule yote ilienea hali ya hewa ya joto kali sana ambalo lilianza kutambaa mwilini na kumfanya atamani kuvua nguo zake ili abaki mtupu. Kisha kama mtu aliyezinduka kutoka usingizini, akaanza kulia kwa uchungu mkubwa.
* * * * *
Saa kumi kasoro dakika tano jioni, kwenye chumba maalumu cha mahojiano cha Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kanda Maalumu katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, Yusuf alikuwa ameketi kwenye kiti mbele ya meza ndefu yenye umbo mstatili. Alikuwa mnyonge sana huku akimtumbulia macho Ibrahim Komba kwa wasiwasi.
“Hii inaweza kuwa mara ya mwisho kukuita hapa na kukuhoji kuhusiana na wizi uliotokea pale Benki ya Biashara, kuwa makini sana katika majibu yako, umenielewa?” ASP Komba alisema huku akimkazia macho Yusuf.
“Nimekuelewa,” Yusuf alisema kwa unyonge huku akiwa bado anamtumbulia macho ASP Komba.
“Je, unamfahamu mwanamke mmoja anayeitwa Belinda?” ASP Komba alimhoji Yusuf huku akiwa amemkazia macho.
Yusuf alisita kidogo na kuangalia chini kwa kitambo, alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akainua uso wake, “Belinda! Wa wapi?” aliuliza huku akionesha kushangaa kidogo.
“Belinda Jackson,” ASP Komba alimjibu Yusuf huku akiendelea kumkazia macho.
Yusuf akainamisha tena kichwa chake chini huku akishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani, “Simkumbuki mtu mwenye jina hilo,” hatimaye alijibu huku akiangalia kando kuyakwepa macho makali ya ASP Komba.
“Ni kweli humkumbuki Belinda Jackson?” ASP Komba aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Yusuf. Yusuf alitingisha kichwa chake kukataa. ASP Komba alimwangalia kwa makini kwa kitambo kifupi na kuachia tabasamu pana.
“Nilikwambia uwe makini sana katika majibu yako, ukasema umeelewa,” ASP Komba alisema huku akiendelea kutabasamu, lakini tabasamu lake lilikuwa limeficha ghadhabu aliyokuwa nayo.
“Ndiyo nimekuelewa sana, afande. Huyo Belinda Jackson simkumbuki kweli,” Yusuf alijaribu kujitetea.
“Unasema uongo, nimelikuta jina lake na namba yake ndani ya simu yako. Unaweza kuniambia vimefikaje?” ASP Komba alimuuliza kwa sauti tulivu huku akimtulizia macho usoni bila kupepesa.
Yusuf alishtuka, jasho jepesi lilianza kumtoka sehemu mbalimbali za mwili wake huku mapigo ya moyo wake yakienda mbio isivyo kawaida. ASP Komba alizidi kumkazia macho.
“Nijibu, vimefikaje?” ASP Komba aliuliza kwa ukali.
“Alinipa mwenyewe,” Yusuf alisema kwa unyonge huku akiangalia chini.
“Alikupa lini?”
“Muda mrefu.”
“Muda mrefu… lini?”
“Kama wiki mbili hivi zilizopita.”
“Wiki mbili zilizopita, eh?”
“Ndiyo afande.”
“Mlikutana wapi?”
Yusuf alitaka kusema neno lakini akasita, na hapo machozi yakaanza kumlenga lenga machoni. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya huku Yusuf akifuta machozi, “Tuli… tulikutana hotelini,” hatimaye alisema huku akifuta machozi.
“Mlikutana katika hoteli gani?” ASP Komba alizidi kumsaili Yusuf.
“Kwanza tulikutana Southern Sun na baadaye tukakutana Amariah Hotel,” Yusuf alijibu kwa unyonge.
ASP Komba alivuta droo ndogo na kutoa picha kadhaa za Carlos na Jacky alizokuwa amezipakua kutoka kwenye mtandao, kisha akachukua picha ya Jacky na kumuonesha Yusuf, “Belinda Jackson ndiyo huyu, siyo?”
Yusuf aliitazama ile picha ya Jacky kwa kitambo kirefu pasipo kusema neno lolote huku midomo yake ikimtetemeka kwa hofu. Machozi yalizidi kumlenga lenga machoni.
“Nijibu, huyu ndiye Belinda Jackson, siyo?”
“Ndiyo, afande,” Yusuf alijibu kwa unyonge.

Itaendelea...
 
Lakini bado kizungumkuti kinaendelea...
Tukisubiri cha jacky. Sijui ataendelea kutumia mwili wake maana yusuph anamjua kwa sura. Labda atasaidiwa na ex wake au ndio sijui wapenzi. Na yasmine na yeye atatapika yote. Jacky juu ya yote yeye sio muuaji. Yeye kinga yake kubwa ni papuchi
 
Aisee tamaa mbaya utajiri wote huo bado hutosheki.mke anaishia kulala tu na wanaume ili madili ya hela yakae sawa. Wakati una utajiri wa kutosha tu
Hata mimi nilimshangaa sana Carlos, pesa alishakua nayo ya kutosha, bora angeachana na mambo ya kupiga dili akaendelea na mishe zake za halali kwa amani

the Legend☆
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom