Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Umesikika Shunie wangu, ngoja niongeze episodes 2...

Kizungumkuti! - 62

Na Bishop Hiluka

ASP Komba alijilaumu sana kwa kushindwa kumpata Joram Mbezi akiwa hai kwani aliamini kuwa Joram ndiye alikuwa kiungo kikubwa kati ya mtu aliyejiita Belinda Jackson na Yusuf na sasa kazi ilianza kuwa ngumu pasipo Joram.

Alikuwa amebakiwa na kazi moja tu, kumbana Yusuf ili amweleze uhusiano wake na wale watu wawili, Joram Mbezi ambaye sasa alikuwa marehemu na Belinda Jackson, ambaye hawakuwa na taarifa zake hadi muda huo. Alipaswa kupata majibu ya uchunguzi wake haraka iwezekanavyo.

Endelea...

ASP Komba alionekana kuchoka sana asubuhi ile alikumbuka kuwa baada ya kurudi tu ofisini mkuu wake wa kazi, Kamanda wa Polisi wa kanda maalumu alimuuliza, “Unadhani kuna haja ya kukuongezea mtu mwingine katika kazi hii?”

“Hapana, afande! Naamini sisi wawili tunatosha. Nikihitaji msaada, nitakujulisha,” ASP Komba alijibu.

Picha ya maiti ya Joram Mbezi iliyokuwa imefumuliwa kichwani iliendelea kumjia ASP Komba akilini mwake, baada ya uchunguzi wa mwili wa Joram Mbezi waliwahoji takriban watu watano, wakiwamo wale watoto wawili waliopewa madafu katika eneo la tukio.

Watu hao watano, watatu wakiwa watu wazima ambao kati yao mmoja alikuwa mwanamume na wawili wanawake, walichukuliwa hadi kituo cha polisi na kuhojiwa na ASP Komba, wote walieleza kuwa walimwona muuza madafu kwa mbali na wala hawakumtilia maanani, hivyo wasingeweza kumtambua endapo wangemuona tena.

Ila wale watoto waliopewa madafu walikiri kumwona kwa ukaribu yule muuza madafu akitumia bastola. Walieleza kuwa waliitambua bastola kwa kuwa waliwahi kuona zikitumika kwenye sinema walizoziangalia kwenye mabanda ya video.

Baada ya mahojiano, wale watu wazima watatu, isipokuwa wale watoto, waliachiwa. ASP Komba na Sajenti Mapambano wakabaki peke yao na wale watoto.

ASP Komba aliwatazama kwa macho ya upole wale watoto. Aliamini kuwa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kushuhudia mauaji na kufikishwa kituo cha polisi kutoa maelezo. ASP Komba alikumbuka kuwa pamoja na mambo mengi aliyowauliza wale watoto lakini alitaka kujua kama wangeweza kumtambua yule mtu aliyewapa madafu endapo wangemuona kwenye picha.

“Mkimwona tena yule baba aliyekupeni madafu mtaweza kumtambua?” ASP Komba aliwauliza wale watoto.

“Sura yake?” aliuliza mtoto mmoja aliyeonekana mjanja zaidi.

”Ndiyo, sura yake”

“Naweza,” yule mtoto alijibu pasipo hata kufikiria mara mbili.

“Hata ukimuona kwenye picha?” ASP Komba alimuuliza kwa upole huku akimkazia macho.

“Ntamjua.”

ASP Komba aliinuka akafungua kabati moja la chuma lililokuwa ukutani na kuvuta droo iliyokuwa ndani yake upande wa kulia, akatoa faili lililokuwa na picha kadhaa za wahalifu, akawawekea mbele wale watoto.

“Angalieni vizuri kama picha ya huyo mtu imo humo. Msifanye haraka,” ASP Komba aliwaeleza kwa sauti ya upole.

Pamoja na kuchukua muda mrefu kufunua na kuziangalia zile picha kwa utulivu mkubwa, wakipitia kila moja kwa msaada lakini hawakuweza kumuona mtu waliyekuwa wakimtafuta. Jambo lile likazidi kumuumiza ASP Komba.

* * * * *

I killed Kisu, he had to die…” (Nimemuua Kisu, alipaswa kufa…) maneno ya Carlos ambayo bado yaliendelea kupita kichwani mwa Jacky na kumsumbua. Baada ya kuambiwa maneno yale Jacky hakusema lolote, alijiondosha pole pole pale alipokuwa amesimama akaketi juu ya sofa.

Uso wake ulionesha mchanganyiko wa huzuni na hasira. Alimtazama Carlos huku akipumua kwa nguvu. Carlos alimtazama Jacky kwa mshangao, akapitisha ulimi wake chini ya midomo yake. Hakuweza kuelewa mara moja ni kipi kilichomkera Jacky.

Carlos alimsogelea Jacky, akaketi karibu yake huku akimtulizia macho yake usoni akimtazama kwa makini.

Why you look so serious?” (Vipi, mbona unaonekana hivyo?) Carlos alimuuliza Jacky huku akiendelea kumkazia macho.

Jacky alimtazama Carlos, akashusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani, “There was no reason to kill Kisu,” (Hapakuwa na sababu ya kumuua Kisu) alisema, uso wake akiwa kaukunja, kisha akaongeza, “We agreed to bring him here, give him his share and then let him leave the country,” (Tulikubaliana kuwa umlete hapa, umkatie chake kisha atoroke nchi).

Carlos alitazama kando akaonekana akiwaza kwa kitambo kifupi kisha akayarudisha macho kwa Jacky, “So, is this what makes you so distressed?” (Kwa hiyo, ndicho kinachokukera sana?)

“Kwani wewe hakikukeri?” Jacky alimuuliza huku aakimtulizia macho.

“Kinikere kwa vipi? Carlos aliongea kwa sauti iliyoanza kuonesha dalili za hasira. “Si alikuwa akisakwa na polisi kwa udi na uvumba, na ilibaki kidogo tu wangemtia mbaroni, sasa weweulitakaje?”

Jacky alibaki kimya akimtazama Carlos kwa makini, kisha alitazama kando, akashusha pumzi za ndani kwa ndani.

I don't understand, what are you trying to tell me, Jacky?” (Sijaelewa, unajaribu kuniambia nini, Jacky?) Carlos alimuuliza Jacky huku akimkazia macho yaliyokuwa yanawaka kwa hasira.

Listen, Carlos. We have everything that man has to have that can buy anything, I didn't see a reason to start killing people who helped us!” (Sikiliza, Carlos. Tuna kila kitu ambacho binadamu anatakiwa kuna nacho ambacho kinaweza kununua chochote, sikuona sababu ya kuanza kufanya mauaji kwa watu waliotusaidia!) Jacky alisema huku akiminya midomo yake.

Carlos aliachia tabasamu la mbali, akatingisha kichwa taratibu, “Jacky,” alisema kwa sauti ya upole. “Hivi tangu lini mwenzangu umeanza kuwa mlokole?”

“Nani mlokole?” Jacky alimuuliza Carlos huku akitoa macho. “Yaani mimi niwe mlokole, are you kidding?

“Kama si mlokole basi ni nini hiki unachomaanisha?” Carlos alisema huku akimkazia macho Jacky.

”Basi tuyaache hayo, tayari yameshatokea na hakuna namna ya kumrudishia Kisu uhai wake,” Jacky alisema huku akiinuka pale kwenye sofa. Akaingia jikoni. Carlos alimsindikiza kwa macho kisha akainuka na kutoka nje.

Baada ya kuandaa kifungua kinywa, Jacky alitoka na kuelekea sebuleni, hakumkuta Carlos, akaanza kuita akidhani labda Carlos alikuwa chumbani, kimya. Akaamua kuchukua simu yake na kumpigia simu lakini simu ilikuwa inaongea na simu nyingine na baada ya muda alipokea ujumbe mfupi, “Nimetoka kidogo, nitarudi baada ya nusu saa…

Saa tano asubuhi Jacky alikuwa amejipumzisha kwenye kochi kubwa la sofa pale sebuleni, hadi muda huo Carlos hakuwepo nyumbani. Jacky hakuwa na furaha kabisa kama alivyozoea siku zote, alijikuta akiwa na mawazo mengi yaliyokuwa yakizunguka kichwani kwake kiasi cha kutaka kumtia wendawazimu.

Jacky alikwisha anza kuchoshwa aina ile ya maisha waliyokuwa wakiyaishi yeye na mumewe Carlos, alijiona ni mtu mwenye hatia kuishi maisha kama yale, ya kuuza utu wake na hata kuhatarisha maisha kwa sababu ya kutaka kuendelea kupata mabilioni ya fedha.

Alianza kujishangaa, kwa nini aendelee kuishi maisha ya uhalifu wakati tayari walikuwa na fedha nyingi za kutosha kufanya chochote na hata kuishi nchi yoyote!

Nyumba waliyokuwa wakiishi lilikuwa kasri lililokuwa na thamani kubwa ya zaidi ya mabilioni ya fedha na walikuwa na nyumba nyingine tatu jijini Dar es Salaam, zenye thamani ya mabilioni ya fedha na miradi kadhaa iliyokuwa ikiwaingizia fedha nyingi, japo hazikufikia mabilioni. Pia walikuwa na magari kadhaa ya kifahari.

Kila alipofikiria mambo aliyokwisha yafanya na wanaume kadhaa kwa maelekezo ya mume wake Carlos, alianza kuona kinyaa na kujiona mjinga kukubali kutumika kama chambo cha kuingiza mabilioni ya fedha. Alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku akihisi thamani ya utu wake ilikwisha toweka siku nyingi na sasa alikuwa akiishi maisha ya majonzi!

Itaendelea...
Shukran mkuu, pia shukran zimfikie muihsani wetu(...)
 
Hahahhaha eti muhisani wetu
Kabwe,Liston,Yusuf,Jasmine........ Then mwisho kabisa Shunie a.k.a Belinda yaa ni mlolongo ni mrefu hatari.
Yaweza kuwa jamaa hana maana hata kidogo kama alikuwa anamuuza kwa ajili ya kupata information hawezi kushindwa kumfumbia jicho moja kisha akapotea. Ila nadhani wale watoto wanaweza kumtambua nae akaanza kusakwa kama manjagu wana rekodi yake.
 
Yaweza kuwa jamaa hana maana hata kidogo kama alikuwa anamuuza kwa ajili ya kupata information hawezi kushindwa kumfumbia jicho moja kisha akapotea. Ila nadhani wale watoto wanaweza kumtambua nae akaanza kusakwa kama manjagu wana rekodi yake.
Umemsahau muuza madafu mwenyewe ambaye kamuona kwa uzuri zaidi?
 
Kizungumkuti! - 64

Na Bishop Hiluka

ILIPOISHIA

We need to find a quick way to silence Kabwe and Liston before things get worse, and then I’ll find out how to deal with Yusuf in jail,” (Itabidi tutafute njia ya haraka ya kuwanyamazisha Kabwe na Liston kwanza kabla mambo hayajaharibika, halafu nitatafuta namna ya kudili na Yusuf kule kule mahabusu) Carlos alisema huku akiachia tabasamu.

Jacky alishtuka sana na kumkazia macho Carlos kwa hofu kana kwamba alikuwa akitazama kitu cha ajabu sana chenye kutisha.

What do you mean to silence them, Carlos?” (Unamaanisha nini kuwanyamazisha, Carlos?) Jacky aliuliza huku akionekana kuanza kuchanganyikiwa.

To kill them, like Kisu,” (Wauawe, kama Kisu) Carlos alisistiza huku akiendelea kutabasamu.

“Aah, sasa unataka kutafuta matatizo mengine. Haya bado hayajaisha unataka kuzua mambo mapya!” alisema Jacky kwa huzuni.

Endelea...

“Bila hivyo hatutakuwa salama kabisa, kwanza siamini kabisa kama tangu jana Kabwe na Liston hawajazua balaa lolote huko waliko… I don't believe at all!” Carlos alisema huku akishusha pumzi.

Jacky alimtazama kwa makini na kutaka kusema neno lakini akasita na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akabaki akimtazama Carlos kwa wasiwasi. Alimtazama kwa kitambo kisha akaamua kuvunja ukimya, “And what about Jasmine?” (Na vipi kuhusu Jasmine?) Jacky aliuliza huku akiwa bado amemtulizia Carlos macho.

I want to follow her right now and bring her here, we’ll give her the money belongs to her and ask her to leave the city completely,” (Nataka kumfuata sasa hivi nimlete hapa, tutamkatia anachostahili na kumtaka aondoke kabisa hapa mjini) Carlos alisema na kuinuka kisha akaanza kupiga hatua kutoka, mara akakumbuka jambo na kugeuka kumtazama Jacky.

By the way, be careful when you want to get out of here, because I feel like there are people going to be tracking our movements,” (Hata hivyo, kuwa mwangalifu unapotaka kutoka humu ndani, maana nahisi kama kuna watu watakuwa wanafuatilia nyendo zetu) Carlos alimwambia Jacky kisha akatoka kabla Jacky hajasema neno lolote.

Carlos aliingia kwenye gari lake aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi ya samawati kisha akabofya remote kufungua lile geti kubwa na kuliondoa gari lake kwa mwendo wa kasi, alichukua uelekeo wa barabara iliyokuwa ikielekea Kinyerezi akiwa hataki kuelekea moja kwa moja Vingunguti ili kuwapoteza watu aliodhani wangeweza kuwa wakifuatilia nyendo zake.

Aliyachunguza magari yaliyokuwa yakija nyuma yake, na kuona magari mawili miongoni mwa magari yaliyokuwa nyuma yake ambayo aliyaanza kutilia shaka.

Magari yale, moja lilikuwa ni gari aina ya Landcruiser Hardtop la rangi nyeusi na jingine lilikuwa ni gari aina ya Land Rover 110 jeupe, na yote mawili yalikuwa yakielekea upande ule ule aliokuwa akienda. Katika muda ule barabara ile haikuwa na msongamano mkubwa wa magari, hivyo mwendo wake ulikuwa wa kuridhisha.

Alipoitupia macho saa yake ya mkononi ilimuonesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa sita mchana na wakati huo jua lilikuwa limeanza kushamiri huku hali ya hewa ikiwa ya joto kama ilivyokuwa kawaida katika jiji la Dar es Salaam.

Carlos alianza kuteremsha mteremko mkali na baada ya kulivuka gereza la Segerea alikwenda mwendo wa kasi zaidi na mbele kidogo alifika eneo la Mbuyuni Njiapanda.

Hapo aliamua kuiacha ile barabara iliyokuwa ikielekea Kinyerezi na kukata kuelekea upande wa kushoto akiifuata barabara ya Mbuyuni.

Ilikuwa ni barabara ya kawaida yenye kiasi kidogo cha magari na iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu. Carlos aliendelea mbele na safari yake huku akifanya tathmini nzuri ya barabara ile iliyoonekana kuwa na watu wachache waliokuwa wanatembea kwa miguu.

Baada ya mwendo mfupi wa safari yake akayaona yale magari Landcruiser Hardtop jeusi na Land Rover 110 jeupe yakiwa nyuma yake, moyo wake ukapiga kite na kumfanya aongeze mwendo ili kuhakikisha kama yale gari yalikuwa yakimfuata.

Wakati akiendelea na safari yake na akiwa hajui afanye nini mara mbele kidogo upande wake wa kushoto akaiona gereji ya Wantong, hivyo ili kuhakikisha kama ni kweli alikuwa anafuatwa aliamua kuchepukia upande ule wa kushoto na kuliingiza gari lake kwenye eneo lile la gereji.

Lile gari jeusi Landcruiser Hardtop lilipunguza mwendo na kuonekana kama vile dereva alikuwa anajishauri kama asimame au lah, lakini akaonekana kuendelea na safari huku lile gari jingine Land Rover 110 jeupe likipitiliza bila kusimama.

Carlos aliyasindikiza kwa macho yale magari huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani na kujipa matumaini kuwa alikuwa salama. Alisubiri kwa dakika tano kisha akaliondoa gari lake kuendelea na safari yake akiifuata ile barabara.

Alipokwenda mbele zaidi alikipita kituo cha mafuta cha Meru kilichokuwa upande wake wa kushoto na mbele kidogo kulikuwa na kituo kingine cha mafuta cha Anna ATN kilichokuwa upande wa kulia kwenye kona ya ile barabara huku kushoto kwake kukiwa na MTN Bakery.

Carlos alishtuka sana alipoliona lile gari Landcruiser Hardtop jeusi likiwa limeegeshwa kando ya barabara jirani na Anna ATN Petroleum huku dereva wake akionekana kufungua boneti la gari.

Carlos aliongeza mwendo huku akilitupia jicho lile gari, na baada ya mwendo mfupi mara akamuona yule dereva akifunga haraka boneti na kuingia kwenye gari kisha gari likaingia barabara na kumfuata nyuma.

Hata hivyo, tukio lile bado lisingekuwa kigezo cha kumridhisha Carlos kuwa sasa alikuwa amefungiwa tera, hata hivyo kwa namna nyingine ile ilikuwa ni ishara mojawapo ya kumtahadharisha kuwa alipaswa kuwa makini na nyendo zake.

Hakujua lile gari jingine Land Rover 110 jeupe lilikuwa wapi muda ule, hivyo mara hii alijikuta akilitazama lile gari Landcruiser Hardtop jeusi kwa utulivu wa hali ya juu katika namna ya kutafuta hakika kama alikuwa akifuatwa au lah!

Aliongeza mwendo na kuivuka baa ya Darajani White kisha alilivuka daraja katika Mto Msimbazi, na kuzivuka baa nyingine za Ndindindii, Elegant Lodge na baadaye Kilimani Bar huku akifikira kama aingie kwenye mojawapo ya zile baa kujifanya kuwa safari yake ilikuwa inaishia pale.

Lakini akaamua kuendelea mbele na baada ya mwendo mfupi wa safari yake akakifikia Kituo cha Decent na kuiacha barabara ile kisha akachepuka na kuingia upande wa kulia akiifuata barabara finyu ya vumbi iliyokuwa ikielekea Da Prince Lodge.

Aliongeza mwendo na wakati akiifikia Da Prince Lodge, aliliona lile gari jeusi Landcruiser Hardtop nalo likichepuka na kuingia kwenye ile barabara finyu ya vumbi na kufuata uelekeo wa Da Prince Lodge likiwa katika mwendo wa taratibu.

Kitendo kile kikamfanya Carlos ashtuke kidogo baada ya kuridhishwa vizuri na tathmini za hisia zake. Sasa aling’amua kuwa lile gari Landcruiser Hardtop jeusi nyuma yake lilikuwa kazini kumfuata kama alivyokuwa amehisi pale awali.

Hivyo, aliamua kuongeza mwendo bila kujali makorongo katika barabara ile finyu ya vumbi huku kijasho chepesi kikianza kumtoka usoni. Moyo wake nao ulikuwa umeanza kupoteza utulivu, hata hivyo kwa kila hali alijitahidi kupambana kikamilifu na hali ile.

Akili yake ikiwa mbioni kupoteza utulivu sasa alikuwa makini sana kulichunguza lile gari kupitia vile vioo vya ubavuni. Hatimaye akafika mwisho wa ule mtaa na kuchepuka akiingia upande wa kushoto.

Kisha aliongeza mwendo katika barabara ile, hata hivyo hadi alipokuwa mbioni kufikia mwisho wa barabara ile lile gari halikuwa limejitokeza. Carlos hakutaka kuamini kuwa lilikuwa linaishia katika mtaa ule, aliongeza mwendo na kuchepuka tena akiingia upande wa kushoto akiifuata barabara nyingine pana kidogo ya vumbi iliyokuwa inakwenda sambamba na reli ya kati.

Itaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater, Bigjahman moneytalk marybaby, nipo2, ram, kisukari, Smart911, Madame S, carbamazepine, Astelia, culture gal , Prisoner of hope, Mine eyes, kuku mweus, Thad, hearly, Shunie, moneytalk,Tumosa, Mine eyes, Kudo, swahiba92, ludist, Toyota escudo, Clkey, macson3, Thad, boga la kiangazi, macson3, LEGE, Smart911, Richard irakunda, skfull, popie, Krizy Beat, hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Kinondoni Sweetheart SUPER EMILY
 
Kizungumkuti! - 65

Na Bishop Hiluka

Akili yake ikiwa mbioni kupoteza utulivu sasa alikuwa makini sana kulichunguza lile gari kupitia vile vioo vya ubavuni. Hatimaye akafika mwisho wa ule mtaa na kuchepuka akiingia upande wa kushoto.

Kisha aliongeza mwendo katika barabara ile, hata hivyo hadi alipokuwa mbioni kufikia mwisho wa barabara ile lile gari halikuwa limejitokeza. Carlos hakutaka kuamini kuwa lilikuwa linaishia katika mtaa ule, aliongeza mwendo na kuchepuka tena akiingia upande wa kushoto akiifuata barabara nyingine pana kidogo ya vumbi iliyokuwa inakwenda sambamba na reli ya kati.

Endelea...

Ilikuwa barabara iliyokuwa ikikatisha kwenye makazi ya watu upande mmoja na upande wa pili kulikuwa na reli, na hakukuwa na msongamano mkubwa wa magari katika barabara ile.

Hivyo mwendo wake ulikuwa wa kasi zaidi akiwa hataki mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari jeusi Landcruiser Hardtop, ambalo aliamini lilikuwa linamfuatilia ingawa hadi pale lilikuwa halijajitokeza nyuma yake, wafahamu alipokuwa akielekea.

Alihakikisha analipoteza lile gari kabla hawajajitokeza katika barabara ile, hivyo alipofika katika makutano ya barabara ile na barabara ya lami iliyokuwa ikitokea Segerea alivuka na kukunja akiingia upande wa kushoto kuifuata barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa inaelekea Kituo cha Polisi cha Stakishari kabla lile gari Landcruiser Hardtop halijatokea katika ile barabara.

Carlos alikwenda mwendo mfupi na kuiacha barabara iliyokuwa inaelekea Kituo cha Polisi cha Stakishari, akachepuka na kuingia katika uchochoro wa barabara finyu zaidi iliyokuwa ikiyazunguka maghala ya Ushirika ambayo kwa wakati huo yalikuwa yakitumiwa kama nyumba ya ibada.

Alisimamisha gari lake kwenye uchochoro ule jirani na yale maghala ya ushirika na kuchungulia nyuma yake akilichunguza kila gari lililopita kwenye ile barabara ya lami iliyotoka Segerea. Baada ya kukaa hapo kwa takriban dakika kumi, mara akaliona lile gari Landcruiser Hardtop jeusi kwa mbali likipita katika ile barabara ya lami iliyokuwa ikitoka Segerea kuelekea eneo la Njia Panda ya Segerea katika Barabara ya Nyerere.

Carlos alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kusubiri pale kwa dakika zingine kumi kisha aligeuza gari lake na kurudi hadi kwenye ile barabara ya vumbi iliyokuwa ikienda sambamba na reli ya kati. Alipofika pale alichukua uelekeo wa upande wa kushoto akiifuata ile barabara ya vumbi ambayo haikuwa na magari mengi, hivyo kumfanya kuongeza mwendo wake.

Alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi katika barabara ile iliyokuwa ikikatisha kwenye makazi ya watu bila kujali kwamba maeneo yale ya uswahilini yalikuwa na watu wengi.

Mara kadhaa alikosakosa kuwagonga watembea kwa miguu na hata waendesha bodaboda aliopishana nao katika barabara ile iliyokuwa ikielekea eneo la Vingunguti.

Baada ya mwendo wa dakika kumi alivuka katika eneo la Chuo cha Ufundi Stadi, VETA, kisha akaanza kuzivuka shule za msingi na sekondari za Ilala na Majani ya Chai.

Wakati akivuka eneo la shule kijana mmoja alikuwa anavuka barabara bila kuwa makini, Carlos aliliyumbisha gari lake huku na huko ili kumkwepa yule kijana lakini hakuweza, hivyo alimgonga na kumrusha kando ya ile barabara.

Carlos alisonya kwa hasira na kukanyaga pedeli ya mafuta, gari likafanya magurudumu yake kuchimba ardhi na kuongeza kasi licha ya baadhi ya watu waliokuwa jirani na eneo lile kumpigia kelele kumtaka asimame.

Aliendelea na safari yake huku akijitahidi kuwakwepa watu waliokuwa katika pilika pilika hadi alipofika kwenye kiwanda cha mabomba cha Pipes Industries.

Hapo alikunja na kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara finyu ya vumbi ambayo hata hivyo haikwenda mbali, akachepuka akishika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata barabara nyembamba ya lami iliyokuwa ikipita katikati ya makazi ya watu upande mmoja na viwanda upande mwingine.

Akiwa bado katika mwendo wa kasi alilivuka eneo lile la viwanda na hatimaye aliingia katika eneo la Vingunguti Sahara, hapo alipunguza mwendo kutokana na magari kadhaa yaliyokuwa yakipita eneo lile, kisha aliiona nyumba ya Jasmine mbele yake na kufunga breki akiliegesha gari lake umbali wa mita kama therathini hivi kutoka ilipokuwa ile nyumba ya Jasmine.

Aliangaza macho yake huku na kule kwa makini akiangalia kama angeweza kumuona Jasmine lakini hakumuona popote, kwa takriban dakika mbili hivi aliendelea kuangalia huku na kule bila kumuona, akapata wazo la kumpigia simu lakini wakati akitoa simu yake ili kumpigia mara akamuona Jasmine akitokea nyumba moja iliyokuwa upande wa pili wa ile barabara na kuvuka kuelekea nyumbani kwake akiwa ameshika gazeti mkononi.

Carlos alipiga honi huku akimtazama Jasmine kwa umakini. Jasmine alishtuka na kugeuza shingo yake kutazama upande ule ilikotokea ile sauti ya honi na kuliona gari la Carlos. Carlos alitoa mkono wake na kumpungia Jasmine akimwashiria amfuate kwenye gari.

Jasmine alimfuata Carlos pale kwenye gari na alipofika alimsalimia kwa heshima zote, japo alionekana kuwa na uso uliosawajika.

“Tena ilikuwa nije nyumbani kwako leo jioni,” Jasmine alimwambia Carlos baada ya kumsalimia huku akimtazama kwa umakini usoni.

“Nimekufuata, ingia ndani ya gari tuongee,” Carlos alimwambia Jasmine huku akilitupia jicho lile gazeti lililokuwa mkononi kwa Jasmine.

Jasmine hakusita, alifungua mlango wa mbele wa lile gari upande wa kushoto wa dereva na kuingia bila huku akiendelea kumtazama Carlos kwa umakini.

“Vipi, umesoma magazeti ya leo?” Carlos alimuuliza Jasmine huku akimkazia macho mara baada ya kuingia ndani ya lile gari na kuketi.

“Gazeti mojawapo ni hili hapa nimelitoa kwa shoga yangu,” Jasmine alisema huku akimwonesha Carlos lile gazeti.

“Umeshaongea na watu?” Carlos alimuuliza huku akiwa amemtulizia macho.

“Watu gani?” Jasmine aliuliza kwa mshangao huku akimkazia macho Carlos.

“Sijui, labda shoga zako ama…”

“Hmm… kwa mambo kama haya nitaongea nao nini?” Jasmine aliuliza kwa mashaka huku akishusha pumzi.

“Nilitaka tu kujua kama kuna yeyote umeongeaa naye… vipi ulishafika kazini siku mbili hizi?”

“Akah, si nilikwambia siendi tena kazini, naogopa sana…” Jasmine alisema huku akibetua mabega yake juu kukataa.

“Okay, sasa sikiliza, mambo yamekwisha haribika, hivyo nimekufuata twende nyumbani nikakupe pesa zako uondoke kabisa hapa mjini, au unasemaje?” Carlos alimwambia Jasmine huku akimkazia macho.

“Nitashukuru sana maana naogopa wasije wakanifuata hapa nyumbani,” Jasmine alisema huku wasiwasi ukizidi kujionesha usoni kwake.

Carlos aliingiza gia ili kuondoka lakini wakati Carlos akitaka kuliondoa gari lake mara akaliona gari moja aina ya Range Rover SV Autobiography LWB la rangi nyeusi lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha watu waliomo ndani likifika katika eneo lile na kuegeshwa mbele kabisa ya nyumba ya Jasmine.

Carlos alilitazama lile gari kwa umakini mkubwa huku akionekana kulitilia shaka, hakuta kuondoka, hivyo alisubiri kidogo kuona ni watu gani waliokuwemo ndani ya lile gari na walikuwa wanatafuta nini pale.

“Twende basi,” Jasmine alimwambia Carlos baada ya kumuona akiwa amezubaa akilitazama lile gari.

“Ngoja kwanza, unaliona lile pale gari, nina shaka watakuwa ni askari,” Carlos alisema huku akimwonesha Jasmine kwa kidole lilipokuwa limesimama lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB jeusi.

Jasmine aligeuza shingo yake na kuliona lile gari na hapo hapo moyo wake ukapiga mshindo kwa mshtuko mkubwa, alilitambua lile gari na kumaka kwa mshangao.

“Ha! Ni gari la bosi Nassos!” Jasmine alisema kwa mshtuko mkubwa.

Itaendelea...
 
Kizungumkuti! - 66

Na Bishop Hiluka

“Ngoja kwanza, unaliona lile pale gari, nina shaka watakuwa ni askari,” Carlos alisema huku akimwonesha Jasmine kwa kidole lilipokuwa limesimama lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB jeusi.

Jasmine aligeuza shingo yake na kuliona lile gari na hapo hapo moyo wake ukapiga mshindo kwa mshtuko mkubwa, alilitambua lile gari na kumaka kwa mshangao.

“Ha! Ni gari la bosi Nassos!” Jasmine alisema kwa mshtuko mkubwa.

Endelea...

“Unamaanisha ni gari la bosi wako, wa kampuni ya The Jacarandah…” Carlos alitaka kumuliza Jasmine lakini alijikuta akikatisha swali lake baada ya kuwaona watu wanne wakishuka kutoka ndani ya lile gari.

Wa kwanza kushuka alikuwa mwanadada mweupe mfupi aliyeitwa Zena Chande na kufuatwa nyuma na mwanamumke wa Kigiriki, Nassos.

“Huyo msichana ni rafiki yangu anaitwa Zena, na yule mzungu ndiye bosi wangu…” Jasmine alimwambia Carlos huku akiwaangalia Zena na Nassos kwa umakini.

Wakati wakiendelea kuwaangalia wale watu mara wakawaona maofisa wa polisi, ASP Komba na Sajenti Mapambano nao wakishuka kutoka ndani ya lile gari na kujiunga na kina Nassos na Zena. Carlos aliwatazama kwa umakini ASP Komba na Sajenti Mapambano na kuwatambua. Akahisi moyo wake ukibadili mapigo na kuanza kwenda kasi isivyo kawaida.

Wakati huo huo wakamuona Zena akimfuata mwanamke mmoja aliyekuwa amesimama nje ya ile nyumba ya Jasmine na kuonekana akimuuliza jambo. Yule mwanamke alimwonesha Zena kwa kidole lilipokuwa limeegeshwa lile gari la Carlos. Na hapo Nassos, ASP Komba na Sajenti Mapambano wakageuka kulitazama lile gari la Carlos.

Carlos alishtuka sana, akakanyaga pedeli ya mafuta na hapo magurudumu ya gari yakachimba lami huku lile gari likiondoka kwa kasi ya ajabu, muda ule ule kijana mmoja alikuwa akikatisha barabara hivyo lile gari likakosa kumgonga.

Muda ule ule ASP Komba akawaamuru watu wote waingie haraka ndani ya gari walilokuja nalo, wote wakaingia na dereva akaliondoa lile gari kwa mwendo wa kasi kulifukuza lile gari la Carlos ambalo muda ule lilikuwa limekwisha waacha mbali.

Kwa kuwa barabara ile ilikuwa finyu na ilikuwa ikipita katikati ya makazi ya watu katika eneo la Uswahilini la Vingunguti lililokuwa na msongamano mkubwa wa watu, hali ile ilimfanya Carlos asiweze kwenda kwa kasi aliyoitaka.

Hata hivyo, alifanikiwa kufikia katika makutano ya barabara ile na barabara zingine za kuelekea machinjio ya Vingunguti na ile ya kuelekea Buguruni kwa Mnyamani. Carlos alikunja kona na kuingia kushoto kwake akiifuata ile barabara iliyokuwa ikielekea machinjio ya Vingunguti.

Kwa mbali akaliona lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB jeusi likizidi kumsogelea likiwa katika mwendo wa kasi, huku taa za mbele za lile gari zikiwa zimewashwa kuashiria hali ya hatari. Carlos alijitahidi kuwakwepa watembea kwa miguu na pikipiki zilizokuwa zikija katika uelekeo wake.

Lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB jeusi nalo lilipoyafikia makutano ya barabara zile likakunja na kuingia kushoto likiifuata barabara ile iliyoelekea kwenye machinjio ya ng’ombe ya Vingunguti, na hivyo kuyafanya yale magari kuanza kufukuzana.

Purukshani za yale magari mawili zilisababisha mtafaruku mkubwa katika barabara ile huku watembea kwa miguu na watu waliokuwa wakifanya biashara pembezoni mwa ile barabara wakikimbilia mbali kabisa kukwepa kugongwa na yale magari.

Baada ya kuyapita machinjio ya ng’ombe ya Vingunguti, gari la Carlos lilianza kushusha mteremko mkali katika bonde la Mto Msimbazi na lilipokuwa likikaribia kwenye daraja la Mto Msimbazi lililounganisha Vingunguti na Tabata kuna lori moja lililokuwa limebeba mchanga lilionekana kukatisha kwa mbele, hivyo kumfanya Carlos aliyekuwa katika mwendo wa kasi ajitahidi kufunga breki huku akiliyumbisha gari lake kujaribu kulikwepa lile lori.

Kutokana na mwendo wake kuwa wa kasi mno alishindwa kuhimili na hivyo gari lake liliyumba na kuserereka huku magurudumu yakilalamika kwenye ile barabara ya lami, likaacha barabara na kupinduka likitumbukia kwenye daraja la Mto Msimbazi. Sauti ya mshindo mkubwa sana ilisikika na mara vumbi kubwa likatimka katika eneo lile likifuatiwa na yowe kubwa la hofu.

Lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB jeusi walilokuwa wamepanda ASP Komba na wenzake liliserereka huku dereva akijitahidi kuepusha ajali na kusababisha magurudumu yake yalalamike kwenye ile barabara ya lami, likayumba na kufunga breki za ghafla huku likiingia kwenye kibanda kidogo kisichokuwa na mtu kilichokuwa kando ya ile barabara jirani kabisa na lile daraja.

ASP Komba na Sajenti Mapambano walishuka haraka kutoka ndani ya lile gari, wakasimama wakiangalia kule ambako gari la Carlos lilikuwa limeangukia huku wakiwa hawaamini macho yao. Muda ule ule watu walianza kusogea na kukusanyika katika eneo lile.

* * * * *

Siku ile ilionekana kuwa ndefu sana kwa Jacky kuliko kawaida, hadi muda ule alikuwa bado ameketi peke yake pale sebuleni akijihisi upweke mkubwa, alipoitupia jicho saa yake ya mkononi alishangaa sana kuona kuwa ilikuwa imeshatimia saa saba na ushee!

Hakujua kwa nini siku ile hakuwa na furaha kabisa na alishangaa kuona kuwa tangu asubuhi alipokuwa ameamka hakuwa akihisi njaa ingawa hakutia chochote tumboni zaidi ya ile bilauri moja ya juisi ya passion ya boksi. Kwa miaka miwili na ushee aliyoishi na Carlos hapakuwa na hata siku moja aliyowahi kuwa katika wakati mgumu kama siku ile.

Alijikuta akitafakari jinsi alivyokutana na Carlos kwa mara ya kwanza kule jijini Arusha, walivyoanza uhusiano hadi walipofunga ndoa. Siku zote tangu walipooana aliishi kwa furaha na kujikuta akimsahau kabisa Jacob, mwanamume aliyewahi kumpenda sana kuliko chochote.

Kitu ambacho hakukijua ni kuwa hakuwaza kama ingetokea siku ambayo angekuja kuwa na wakati mgumu kama siku ile. Alipigiwa simu mara kadhaa na Jacob lakini hakuweza kuzipokea simu zake, na hata alipopigiwa na kuona namba ngeni bado hakupokea simu.

Akiwa bado anatafakari mara alisikia sauti ya kengele ya getini ikiita kuashiria kuwa kulikuwa na mtu nje ya uzio wa ile nyumba, moyo wake ukapasuka pah! Jasho jepesi likaanza kumtoka mwilini na hakujua kwa nini alishtuka kiasi kile, alianza kuhisi ubaridi mwepesi wa woga ukimtambaa mwilini huku mapigo ya moyo wake yakabadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida!

Aliinuka huku mwili wake ukitetemeka na kuchungulia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha lakini hakuweza kumuona mtu yeyote. Ile kengele ikaendelea kuita tena na tena, Jacky aliamua kutoka na kwenda moja kwa moja hadi kwenye lile geti, kisha akachungulia nje.

Aliwaona wanaume wawili wakiwa wamesimama pale kwenye geti huku wakiendelea kubonyeza kile kitufe cha kengele kwa fujo, Jacky alipowatazama kwa makini akapatwa na mshangao uliochanganyika na wasiwasi baada ya kuwatambua Kabwe na Liston wakiwa wamesimama nje ya ile nyumba.

“Karibuni,” Jacky alisema baada ya kuwafungulia lile geti na na kusimama kando huku akiwatazama kwa umakini, hata hivyo, uso wake ulishindwa kuficha mshangao aliokuwa nao wakati akiwakaribisha ndani. Kabwe alimtazama kwa makini na kuachia tabasamu huku akiingia ndani na kufuatwa nyuma na Liston.

“Vipi hapa?” Kabwe alimuuliza Jacky huku akimkazia macho mara baada ya kuketi kwenye sofa pale sebuleni.

Itaendelea...
 
Kizungumkuti! - 67

Na Bishop Hiluka

“Karibuni,” Jacky alisema baada ya kuwafungulia lile geti na na kusimama kando huku akiwatazama kwa umakini, hata hivyo, uso wake ulishindwa kuficha mshangao aliokuwa nao wakati akiwakaribisha ndani. Kabwe alimtazama kwa makini na kuachia tabasamu huku akiingia ndani na kufuatwa nyuma na Liston.

“Vipi hapa?” Kabwe alimuuliza Jacky huku akimkazia macho mara baada ya kuketi kwenye sofa pale sebuleni.

Endelea...

“Ah, ndo’ kama mlivyosikia!” Jacky aliongea kwa sauti ya unyonge huku akiwa amesimama akiwatazama wote wawili kwa makini.

“Kusikia nini, mbona sikuelewi, shem?” Kabwe alimuuliza Jacky huku akimkazia macho kwa mshangao.

“Kwani hamsomi magazeti, jamani au hamperuzi hata mitandao kujua yanayoendelea duniani?” Jacky aliwauliza huku akiwatazama kwa mshangao.

“Tunasoma lakini habari za magazetini hazituhusu…” Kabwe alijibu huku akionekana kupuuza kile alichokuwa akiambiwa na Jacky. Jacky alitaka kusema neno lakini Kabwe alimkatisha kwa ishara.

“Sikiliza shem, watu wa magazeti wanafanya biashara yao, watu wa mitandao wanaingiza fedha zao na sisi tunayafanya ya kwetu. Ndiyo nchi ya viwanda inavyokwenda, kila mtu na mambo yake, au siyo?” Kabwe alisema huku akicheua, na muda huo huo ile sebule ikaenea harufu ya pombe.

“Lakini habari zilizotoka leo kwenye magazeti zinatuhusu, ni kwamba mambo yetu ndiyo yamekwama…” Jacky alisema kwa huzuni na kukatishwa na sauti ya Liston aliyepiga ngumi juu ya meza huku akifoka.

“Haiwezekani! Kwani ile fedha mmeirudisha benki?” Liston alimuuliza Jacky huku macho yake yakiwaka kwa ghadhabu.

“Fedha yote ipo!” Jacky alisema huku akimtazama Liston kwa wasiwasi.

“Sasa kilichokwama ni nini? Unajua shem, usituchanganye hapa… kwanza niambie ukweli, ni kweli Kisu ameuawa maana tumesikia habari juu juu?” Kabwe alidakia huku akimkazia macho Jacky kisha akaendelea bila hata kusubiri jibu lake, “Mmemuua Kisu na sisi hatujui hatma yetu ni ipi! Naomba usituchanganye kabisa…” Kabwe alifoka.

Jacky alimtazama Kabwe kwa makini huku akijaribu kutafakari namna ya kukabiliana na hasira za wale wanaume endapo wangeamua kuanzisha vurugu.

“Kwanza mzee yuko wapi? Tunataka kuongea naye kama wanaume,” kabwe alimuuliza Jacky huku aakimkazia macho.

“Katoka kidogo lakini atarudi muda wowote kuanzia sasa.”

“Kama kakuachia mzigo wetu, tupe tusepe ili kila mtu afe na chake, maana sasa naona mnaanza uswahili,” Kabwe alimwambia Jacky huku akionekana kuanza kupandwa na jazba.

“Hajaniachia mzigo wowote wa kuwapeni leo, ninachojua kesho ndiyo mnatakiwa mje kuchukua mzigo wenu… labda nimpigie simu kumjulisha kuwa mmekuja leo,” Jacky alisema huku akiichukua simu yake iliyokuwa juu ya meza, kisha alibofya namba ya Carlos, akapiga na kusikiliza. Simu ya Carlos ilikuwa haipatikani!

Jacky alishtuka sana na kuitazama ile simu kwa mshangao kisha alipiga tena lakini bado simu ya Carlos ilikuwa haipatikani! Akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiwatazama Kabwe na Liston katika hali ya kukata tamaa. “Simu yake haipatikani,” Jacky alisema kwa wasiwasi.

“Naona sasa mnatuchanganya, Kisu ameshakufa na sijui kama mlishamkatia chake, na sisi mnaanza kutuletea ngonjera… sikiliza tunachotaka ni hela yetu ama sivyo nyumba hii itawaka moto,” Kabwe alisema kwa ghadhabu.

“Msiwe hivyo jamani, hebu jaribuni kuwa na subira kama ni hela yenu ipo…” Jacky alisema kwa sauti laini huku akiachia tabasamu na kulegeza macho yake akijaribu kuwalainisha.

“Bwana ee, usitulegeze macho yako hapa ukadhani utamrusha mtu roho. Harushwi mtu roho hata kwa nini! Tunachotaka ni mzigo wetu tu, au kama vipi tutalianzisha!” Kabwe alifoka kwa sauti kubwa huku akiinuka kutoka kwenye lile sofa alilokuwa amekalia.

Jacky alimtazama Kabwe kwa makini huku akijiandaa kwa lolote endapo wangetaka kuleta vurugu kisha akayahamishia macho yake kwa Liston ambaye muda wote alikuwa ametulia kwenye kochi akimtazama huku macho yake yakiwaka kwa ghadhabu.

“Basi naomba mvute subira tu jamani, hakawii kurudi,” Jacky alisihi huku akiupima upepo.

Liston na Kabwe wakaangaliana. “Unasemaje kamanda wangu, tumsubiri au tukautwike halafu tuwajie jioni?” Kabwe alimuuliza Liston.

“Jioni ya saa ngapi? Wanaweza kutukimbia hawa,” Liston aliuliza huku naye akiinuka kutoka kwenye sofa.

“Tuwazukie mapema tu…”

“Poa, twen’zetu!” Liston alisema na hapo hapo wakaondoka wakimwacha Jacky amepigwa butwaa.

* * * * *

Saa tisa alasiri, gari lenye maandishi ya POLISI ubavuni aina ya Nissan Patrol la rangi nyeusi liliingia kwenye lango kuu la kuingilia katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ilala ya Amana, katika eneo la Amana Ilala jijini Dar es Salaam.

Walinzi wa hospitali ile ya Amana waliokuwa nadhifu kwa sare zao za ulinzi walimwelekeza Sajenti Mapambano aliyekuwa akiendesha lile gari sehemu maalumu ya kuliegesha gari lake katika maegesho maalumu ya magari.

Baada ya lile gari kuegeshwa katika eneo lile la maegesho ya magari, ASP Komba, ambaye muda ule alikuwa amevalia sare rasmi za polisi na cheo chake cha nyota tatu kikionekana vyema kwenye mabega yake, alishuka kutoka katika lile gari.

Sajenti Mapambano naye aliteremka na hapo wakaanza kupiga hatua kikakamavu wakielekea kwenye jengo la ofisi za madaktari wa hospitali ile. Walifika na kusimama mbele ya mlango mmoja na hapo ASP Komba akagonga mlango ule mara moja kisha akakishika kitasa, akakinyonga na kuusukuma mlango.

Mlango ulisalimu amri na kumruhusu ASP Komba kuingia ndani ya ile ofisi, Dk Fadhili Masha ambaye alikuwa ameinamisha uso wake akisoma taarifa fulani za mgonjwa kwenye faili alilokuwa amelishika mkononi aliinua uso wake na macho yake yakakutana na yale ya ASP Komba, akaachia tabasamu huku akiinuka kuwalaki ASP Komba na Sajenti Mapambano.

Dk Masha alikuwa mwanamume mrefu mnene na alikuwa mweupe kama chotara, akiwa na umri wa miaka takriban hamsini alionekana mwenye nguvu na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu. Alikuwa na upara mpana uliokuwa unawaka na uso wake ulikuwa mpana huku miwani yake mikubwa ikiwa imeyahifadhi macho yake makubwa.

Alikuwa amevaa suruali ya bluu yenye mistari myeupe, shati la rangi ya samawati lililokuwa na mistari ya bluu ya pundamilia na juu ya lile shati alivaa koti refu jeupe la kidaktari na kuning’iniza shingoni kwake kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ambacho kitaalamu kiliitwa stethoscope. Miguuni yule daktari alikuwa amevaa viatu vizuri vyeusi vya ngozi.

“Naona mmeniwahi, sasa hivi nilikuwa namalizia kuisoma hii taarifa kisha niondoke!” Dk Masha alisema baada ya kuwakaribisha wale maofisa wa polisi.

“Majukumu yametubana, dokta… vipi habari za muda?” ASP Komba alisema huku akinyoosha mkono wake kumsalimia Dk Masha.

“Nzuri tu, karibuni,” Dk Masha aliitikia huku akimpa ASP Komba mkono, kisha akamsalimia Sajenti Mapambano na wote wakaketi kwenye viti. Walipoketi tu Dk Masha alivuta droo ndogo ya meza yake na kutoa humo kitabu kidogo cha kumbukumbu.

“Kitu pekee nilichokipata kutoka kwenye mfuko wa suruali ya marehemu ni hiki kitabu chake cha kumbukumbu,” Dk Masha alisema huku akinyoosha mkono wake kumpa ASP Komba kile kitabu.

ASP Komba alikipokea kile kitabu cha kumbukumbu, maarufu kama Diary na kukigeuza geuza huku akikiangalia kwa umakini. Kilikuwa kitabu kidogo cha rangi ya bluu.

“Pia kuna karatasi zingine mbili tatu, labda zitaweza kuwasaidia,” Dk Masha alisema tena huku akichukua zile karatasi na kunyoosha mkono wake kumpa ASP Komba.

Itaendelea...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom