Kizungumkuti! - 48
Na Bishop Hiluka
ASP Komba alibetua kichwa chake huku akipiga mkupuo mkubwa wa moshi wa sigara, alitulia kidogo akionekana kutafakari kisha akapuliza moshi mwingi pembeni.
“Una mke?” ASP Komba alimuuliza Yusuf huku akiwa amemtulizia macho yake usoni.
“Ndiyo, na mtoto mmoja,” Yusuf alijibu kwa utulivu na unyonge huku akimtazama yule ofisa wa polisi kwa huzuni.
“Utaipa shida familia yako,” ASP Komba alisema huku akimkazia macho Yusuf kwa umakini zaidi kisha akatingisha kichwa chake kumsikitikia.
Endelea...
“Lakini mimi sihusiki kabisa, afande, wala sijui lolote,” Yusuf alizidi kujitetea huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Wakati huo machozi yalianza kumlengalenga kwenye macho yake.
“Sijasema kuwa wewe unahusika au unajua lolote, lakini nina kila sababu ya kuamini kwamba unaweza kuisaidia polisi katika wizi huu, kwani wewe ndiye uliyewaona vizuri hao wahalifu,” ASP Komba alisema huku akiminya midomo yake.
“Afande, naomba uniamini, mimi siwafahamu kabisa…”
ASP Komba aliizima ile mashine ya kurekodia sauti huku akitingisha kichwa chake kwa huzuni, aliendelea kuminya midomo yake na baada ya sekunde chache aliruhusu tabasamu la kifedhuli kuchanua usoni kwake, kisha aligeuza shingo yake kumtazama Inspekta Mapambano na kuonesha ishara fulani ya kichwa.
Sajenti Mapambano alisimama kwa ukakamavu na kuzunguka ile meza akimsogelea Yusuf, kisha alimshika na kumnyanyua kwa nguvu kama vile alikuwa akinyanyua kipeto cha sufi.
“Kabla hujamweka korokoroni, hakikisha unaorodhesha vitu vyake vyote,” ASP Komba alimwambia Sajenti Mapambano huku akiuma mdomo wake wa chini.
Kusikia hivyo, Yusuf aliishiwa kabisa nguvu akionekana kupatwa na mshtuko mkubwa, muda ule ule aliingiza mkono wake mfukoni na kutoa simu yake aina ya Tekno Spark K9.
“Afande, naomba nimpe jamaa yangu yupo hapo nje hii simu ili aondoke nayo,” Yusuf alisihi kwa sauti ya kubembeleza huku akimtazama ASP Komba kwa wasiwasi.
ASP Komba alimtazama Yusuf huku tabasamu la kifedhuli likizidi kuchanua usoni kwake, kisha aliangua akicheko hafifu. “Kwa hiyo sisi hutuamini, siyo?” ASP Komba alimuuliza Yusuf huku akiendelea kucheka.
“Nawaamini, afande, lakini…”
“Kama unatuamini iache hapa hapa, kwanza hatukuruhusu utoke tena nje,” ASP Komba alisema huku akikunja sura yake iliyotengeneza ndita.
Yusuf alionekana kunywea na kuishiwa kabisa nguvu, baridi nyepesi ya mshtuko wa hofu ikasambaa mwilini mwake na nywele zake zilimsimama kichwani huku koo lake likimkauka.
Sajenti Mapambano alimshika Yusuf kwa nguvu na kumuongoza akimtoa nje ya kile chumba cha mahojiano. Wakatoka wakimwacha ASP Komba akiwa bado ameketi katika kile chumba peke yake huku akitafakari kwa kina.
Kisha ASP Komba na Sajenti Mapambano waliwahoji watu wengine wanne wakiwemo wale askari wawili wa ulinzi waliokuwa zamu siku ile pale benki na wafanyakazi wawili walioshuhudia kwa ukaribu wakati wale watu watatu wakiingia mle Benki ya Biashara na kutoka.
Wakati akiwahoji baadhi ya wafanyakazi na wale askari wa ulinzi, ASP Komba alishindwa kuwahoji akiwa ameketi kitini pake, hivyo akawa anarandaranda mle chumbani.
“Nataka mkumbuke vizuri…” ASP Komba aliwaambia huku akiwakazia macho.
“Ninyi wawili, isipokuwa askari wa ulinzi, mlikuwamo mle benki wakati hawa jamaa watatu wanasimama pale kaunta na kumkabidhi Yusuf hundi kabla hawajatoka na fedha. Pamoja na kuwa kulikuwa na wateja wengi nanyi mlikuwa mkishughulika na wateja wengine, lakini mnaweza kukumbuka vitu viwili vitatu juu ya watu hawa, sura zao, kwa mfano, urefu wao, sauti zao… na vitu kama hivyo,” ASP Komba alinyamaza kidogo, akawatazama mmoja mmoja.
Kisha akaendelea, “Hebu wewe Pauline, umesema ulikuwa karibu zaidi, nieleze unavyoweza kuwakumbuka,” alimuuliza mfanyakazi mmoja wa kike ambaye wakati kina Kisu wanaingia benki alikuwa amesimama kaunta ya jirani na alipokuwepo Yusuf.
Pauline alitoa kikohozi cha chini chini, akaketi vema, “Wote watatu walikuwa wamevaa miwani myeusi iliyoonesha kuficha macho yao, walikuwa wakakamavu na yule mmoja wao aliyekuwa anaburuza begi la magurudumu ndiye alisimama karibu sana na dirisha langu.”
“Kwa hiyo ulimchunguza vizuri?”
“Alikuwa jasiri sana, afande, isitoshe sikujua kama hawakuwa raia wema,” Pauline alisema.
“Nimekuelewa, nimekuelewa,” ASP Komba alimkatiza. “Hebu jaribuni kukumbuka vitu vingine juu ya hawa watatu… kama kumbukumbu zenu ni nzuri.”
Kijana mmoja aliyeitwa Elibariki alijiinamia kwa dakika nzima bila kusema lolote. Alipoinua uso wake alionekana kukumbuka kitu. “Kuna yule mzungu, nahisi kama hakuwa mzungu ila ni mweupe tu, na hata zile nywele zake zilizokuwa zimelalia mgongoni nadhani zilikuwa nywele za bandia…”
ASP Komba alimtazama Elibariki kwa kitambo kirefu bila kukupesa macho. “Una uhakika?” hatimaye alimuuliza ili kujiridhisha.
“Ndiyo afande, nina uhakika hakuwa mzungu na inawezekana alikuwa na upara, ni kama nimewahi kumuona sehemu fulani hivi,” Elibariki alijibu bila hata kufikiria.
Baada ya mahojiano yaliyochukua takriban dakika ishirini ASP aliwaruhusu kuondoka lakini akawataka kufika kituoni kila watakapohitajika. Waliondoka na kumwacha akifikiria sana kuhusu yale maelezo. Kisha aliishika ile simu ya Yusuf na kuitazama kwa makini huku akiigeuza geuza katika namna ya kuichunguza kwa makini.
Kisha aliiwasha na kuanza kuzipitia namba za simu zilizopigwa na majina yaliyokuwa yameorodheshwa kwenye ile simu. Wakati akiyapitia yale majina, baadhi ya majina alionekana kuyatilia shaka na hivyo alikuwa akiyaandika pembeni kwenye notebook yake.
Alichukua muda mrefu akizichunguza zile namba kwenye ile simu, na wakati akiendelea na uchunguzi ule mara mlango wa kile chumba cha mahojiano ukagongwa na kumfanya ageuke kuutazama kule mlangoni.
Muda ule ule mlango ukafunguliwa na hapo akaingia Sajenti Mapambano akiwa ameongozana na Nassos Chatzopoulos. ASP Komba alimtazama Nassos kwa makini na kumuonesha sehemu ya kuketi. Kwa mkono
Nassos aliketi kimya akiwa na wasiwasi kidogo huku akimtazama ASP Komba kwa umakini zaidi. ASP Komba aliendelea kuzipitia zile namba za simu kwenye ile simu ya Yusuf na baadaye alifungua sehemu ya ujumbe mfupi na kuanza kusoma ujumbe uliokuwa umetumwa katika ile simu.
Alisoma ujumbe kwa umakini huku akizinakiri baadhi ya namba za simu zilizokuwa zimetumika kutuma ule ujumbe na kuandika taarifa fulani kwenye kitabu chake kidogo na alipomaliza kuandika aliinua uso wake kumtazama Nassos huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“You’re welcome,” (Karibu sana) ASP Komba alimkaribisha Nassos kana kwamba ndiyo alikuwa amemuona kwa mara ya kwanza.
“Thank you, officer,” (Ahsante, afande) Nassos alijibu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Do you know Swahili?” (Unajua Kiswahili?) ASP Komba alimuuliza huku akimtulizia macho.
“Yes, but a little, officer,” (Ndiyo, lakini kidogo, afande) Nassos alijibu kwa kujiamini.
“Are you the chief executive director of The Jacarandah Group, right?” (Wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa The Jacarandah Group, sawa?) ASP Komba alimuuliza Nassos huku akiwa amemtulizia macho yake usoni pasipo kupepesa.
“Yes, officer,” (Ndiyo, afande) Nassos alisema huku akilamba midomo yake iliyoanza kukauka.
Itaendelea...