Haya mama, nimeitika maana neno lako kwangu ni sheria...
Kizungumkuti! - 41
Na Bishop Hiluka
ILIPOISHIA
“
Prove to me, who came here today from our company to take money?” (Nithibitishie, ni nani aliyekuja leo kutoka kwenye kampuni yetu kuchukua pesa?) Nassos alimuuliza Yusuf kwa ghadhabu huku akiwa amemkazia macho yaliyokuwa yakiwaka kwa ghadhabu.
Muda ule wote wafanyakazi wengine wa ile benki pamoja na wateja walibaki kimya wakiwatazama kwa mshangao Nassos na Yusuf waliokuwa wakilumbana, ni dhahiri walionekana kushindwa kuelewa kilichokuwa kinaendelea pale.
“
Three people came here, and two were wearing your company’s NeoVision Security uniform. And the checks they came with is here,” (Walikuja hapa watu watatu, tena wawili walikuwa wamevaa sare za kampuni yenu ya
NeoVision Security. Na hundi waliyokuja nayo ni hii hapa) Yusuf alisema kwa kujitetea huku akimwonesha Nassos ile hundi.
Sasa endelea...
Nassos alimwangalia Yusuf kwa ghadhabu kisha macho yake yalitua kwenye ile hundi aliyoishika, alitaka kusema neno lakini akasita na kunyoosha mkono wake ili apokee ile hundi.
Pamoja na uwepo wa viyoyozi vilivyokuwa vikitoa ubaridi mkali mle ndani ya benki lakini Yusuf alikuwa akihisi kupigwa na upepo wenye joto kali sana uliokuwa ukilijaza eneo lile alilosimama na kuifanya ngozi yake kuungua huku nywele zake zikimsimama. Ilikuwa ni hisia tofauti sana ambayo hakuwahi kuihisi hapo awali na ilikuwa na nguvu kubwa.
Ukimya ulidumu kwa kitambo kifupi huku Nassos akimkazia macho Yusuf na kuipokea ile hundi aliyoishika Yusuf iliyotoka kwa kina Kisu, Yusuf hakuwa na namna nyingine isipokuwa kuitoa ile hundi, japo kwa shingo upande.
Nassos alipoikamata mkononi mwake ile hundi aliitazama kwa makini na kwa nukta chaache tu tangu alipoitia machoni alionekana kushtuka sana, macho yake hayakuamini kabisa kile alichokuwa anakiona kwenye ile hundi. Ilikuwa ni hundi halali ya kampuni yake iliyokuwa na saini zile zile za watiaji saini wa kampuni. Alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku akishika kichwa chake, alionekana kupigwa na butwaa na kuishiwa nguvu.
“
This is robbery, and it’s too foolish!” (Huu ni wizi, tena wizi wa kipumbavu sana!) Nassos alisema kwa hasira huku akimtazama Yusuf kwa macho yenye ghadhabu. Alikunja ngumi na kugongagonga juu ya ile kaunta akiwa na hasira.
“
I'm sure some of you here in the bank are involved in this robbery. I would like to see the branch manager and talk to him,” (Nina hakika baadhi yenu hapa benki mnahusika kwenye huu wizi. Naomba kuonana na meneja wa tawi niongee naye) Nassos alisema kwa hasira huku akiwa ameshika kiuno.
Sasa Nassos alikuwa anahema kwa nguvu kama aliyekuwa akipigania hewa ya mwisho kabla ya kukata roho, alitaka kusema neno lakini akashindwa na kumnyooshea Yusuf kidole chake cha shahada huku akimtazama kwa ghadhabu. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya.
“
I said I need to see the branch manager right now,” (Nimesema nahitaji kuonana na meneja wa tawi sasa hivi) Nassos alisisitiza huku akianza kuzunguka zunguka katika eneo lile jirani na kaunta kwa hasira na kuwafanya watu wote wamwangalie kwa wasiwasi.
Askari wa ulinzi katika benki ile walikwisha fika haraka na kumsikiliza Nassos, wakati huo Yusuf alikuwa ameketi kwenye kiti akionekana kugwaya sana na moyo wake ulipiga kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikimtoka.
* * * * *
Kwenye sebule kubwa ya jumba kubwa la kifahari la ghorofa moja katika eneo la Mtoni Kijichi, Carlos akiwa na kampani nzima ya watu waliofanikisha operesheni maalumu ya kuzipata fedha kutoka Benki ya Biashara, walikuwa wameketi sebuleni kwenye masofa wakijipongeza kwa kunywa mvinyo na kuvuta sigara.
Lile jumba lilikuwa na vyumba vitano vya kulala vilivyosheheni samani zote muhimu lakini lilikuwa halikaliwi na mtu yeyote, ingawa ndani yake kulikuwa na kila aina ya samani, tena zilizonunuliwa kwa bei mbaya. Lilikuwa na sebule mbili kubwa chini na juu, ukumbi wa chakula, ofisi na maktaba maalumu ya siri, sehemu ya ghorofani ya kubarizi yenye viti vya sofa, maliwato, jiko kubwa la kisasa, stoo na kadhalika.
Kwenye sebule ya chini, ambako ndiko Carlos na kampani yake walikuwa wameketi, mandhari yake ilipambwa kwa seti mbili za makochi ya sofa yaliyopangwa kwa kuizunguka ile sebule. Katikati ya ile sebule kulikuwa na meza kubwa lakini fupi ya kioo iliyokuwa na umbo la yai. Na kulikuwa na madirisha makubwa yaliyofunikwa na mapazia marefu mepesi ya kuvutia.
Kupitia yale madirisha makubwa ya sebule mtu yeyote ambaye angeketi pale sebuleni angeweza kuona mandhari nzuri na tulivu ya miti ya kivuli, nyasi zilizokatiwa vizuri za kijani kibichi na bustani ya maua ya kupendeza katika sehemu ya kupumzikia iliyokuwa eneo la nyuma la lile jumba kando ya bwawa la kuogolea.
Pia ndani ya lile jumba kulikuwa na gereji iliyotumika kulaza magari ikiwa na uwezo wa kulaza magari matatu hadi manne kwa wakati mmoja, lakini siku zote kulikuwa kunalazwa gari moja tu aina ya
Toyota Alphard jeupe ambalo halijawahi kutumika tangu lilipoingizwa kinyemela nchini kutoka Afrika Kusini na halikuwa limesajiliwa.
Hii ndiyo nyumba ambayo baada ya Jacky kutoka kule Benki ya Biashara alimwambia yule dereva wa teksi-bubu kumleta Mtoni Kijichi, ingawa hakuletwa moja kwa moja hadi pale bali alizuga kushukia kituo cha daladala kisha akachukua bodaboda iliyomleta pale.
Alikuja katika ile nyumba kwani hapo ndipo alipokuwa ameliacha gari lake aina ya
Range Rover Sport L494 la rangi nyeupe na kisha kuchukua gari aina ya
Toyota Alphard jeupe kwa ajili ya kutumika kwenye operesheni ya kuchukua fedha za
The Jacarandah Group.
Lile jumba Carlos na Jacky walilitumia mara chache sana, hasa pale walipohitaji faragha zaidi au walipohitaji kushughulika na mambo nyeti zaidi, kwa kuwa lilikuwa halifahamiki kwa jamaa wengi.
Ki ukweli lilikuwa jumba kubwa na zuri lililokuwa limezungukwa na ukuta mrefu usiomwezesha mtu kuona ndani na uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake, na lilikuwa na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri. Mbele yake kulikuwa na geti kubwa jeusi huku likizungukwa na miti mizuri ya kivuli.
Carlos na kampani yake walikuwa kimya pale sebuleni wakinywa na kutafakari, na juu ya meza ndogo zilizokuwa mbele yao kulikuwa na mizinga mitatu mikubwa ya mvinyo na bilauri kadhaa. Hii ilikuwa ni kama sherehe ndogo baada kwa kufanikiwa kufikisha mzigo salama licha ya hekaheka za kupita huku na kule, barabara hizi na zile katika safari ya mzunguko ambao ingekuwa vigumu sana mtu yeyote kuelewa walielekea wapi endapo angejaribu kuwafuatilia.
Kwa kifupi ni kwamba, baada ya kutoka pale Benki ya Biashara tawi la barabara ya Lumumba gari lao aina ya
Ford Transit lenye nembo ya
NeoVision Security liliifuata barabara ya Bibi Titi Mohammed na kwenda moja kwa moja hadi makutano ya barabra ile na barabara ya mtaa wa Nkrumah.
Hapo Carlos aliongeza kasi ya mwendo wa gari huku akipiga king’ora kuyataka magari mengine yakae kando huku akikatisha katikati ya majengo ya ghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), yaliyokuwa katika pande zote mbili za barabara ile ya Nkrumah.
Itaendelea...
CC
Tater