Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,711
- Thread starter
- #81
HEKAHEKA! 17
Na Bishop Hiluka
Nilihisi akili yangu ikipoteza uwezo wake, nikaamua kuikabidhi roho yangu kwa Mungu huku nikifumba macho na kufanya maombi kimya kimya kumuomba Mungu aninusuru na mateso makali ambayo yangenisababishia kupoteza uhai, hasa nikiamini kuwa mateso ambayo ningepewa na wale makomandoo wa idara ya ujasusi jeshini yangekuwa makali sana.
“Brown…!” Sauti nzito ya yule kamanda aliyekuwa ameketi kwenye kiti ikayarudisha mawazo yangu mle ndani. Hata hivyo sikuitikia kwani niliamini hilo halikuwa jina langu.
“Wewe!” aliniita tena yule komandoo, safari hii kwa ukali kidogo.
“Naam!”
“Unajua kwanini tumekufungua pingu? Tunataka uwe huru na tuzungumze kiurafiki, ila usidhani kama unaweza kutoroka…” yule kamanda akasema huku tabasamu zaidi likichanuwa usoni kwake.
Endelea...
“Sasa tuambie taratibu na bila kificho chochote kuhusu misheni yenu, nani washirika wenzako na wapi mlipoficha silaha,” aliniambia akinikazia macho.
“Kwa kweli sifahamu kitu chochote kuhusu hizo silaha unazosema, ningekuwa najua kwanini niwasumbe?” nikaongea kwa utulivu.
“Naona umejitolea kufa peke yako huku wenzako wakiendelea kustarehe mafichoni, siyo? Au unadhani utasifiwa kwa upuuzi huu?” aliniuliza kwa sauti ya upole na tulivu lakini iliyokuwa imebeba kitu fulani kilichonionya kutoongopa.
“Kweli kabisa sielewi chochote, kwa miaka yote hii mimi naishi nchini Uholanzi na sijui chochote kilichokuwa kinaendelea hapa nchini zaidi ya yale niliyoyasoma kwenye mitandao,” nilisema nikiendelea kushikilia msimamo wangu.
Yule komandoo akanitazama kwa kitambo kirefu huku akiendelea kuruhusu tabasamu pana kuchanua usoni mwake. Sikujua kwanini alitabasamu na lile tabasamu lilikuwa likiashiria nini, hivyo hali ile ikanisumbua sana akili yangu.
“Kwa hiyo, hujui wenzako wako wapi wala silaha zimefichwa wapi?” yule komandoo akaniuliza tena kwa kujiamini kana kwamba alikuwa na hakika na anachokizungumza.
“Wenzangu akina nani?” niliuliza huku nikionekana kuanza kuchoshwa na maswali yasiyo na kichwa wala miguu niliyokuwa naulizwa tangu nilipokamatwa kule uwanja wa ndege.
“Brown, labda nikwambie kitu, wengi wanaoletwa katika chumba hiki na kushikilia misimamo yao huishia kuongea ukweli huku wakiwa na hali mbaya sana na wengine huwa tayari wamepata ulemavu wa kudumu. Sidhani kama utapenda tufike huko!” aliniambia yule komandoo huku akinitazama kwa makini.
“Wala sipendi tufike huko ingawa sijui kwanini hamtaki kuniamini,” nikamjibu yule komandoo huku nami nikimtazama kwa makini.
“Kama hupendi tufike huko basi tuambie ukweli kisha uombe msamaha ili tukusamehe… vinginevyo kitakachokupata ni dhambi hata kusimulia.”
“Nimekwisha waambia kuwa sifahamu chochote…” nilisema kwa hamaki.
Muda uleule nilijikuta nikitulizwa kwa kuzabwa kofi zito kutoka kwenye kiganja kilichokomaa kwa mazoezi cha yule komandoo aliyekuwa amesimama nyuma yangu na hivyo kunisababishia maumivu makali sana kichwani. Japo kile kilikuwa kipigo cha mara moja tu lakini maumivu yake yalikuwa hayasimuliki!
“Sasa mbona unanipiga?” nikamuuliza yule komandoo aliyekuwa amesimama nyuma yangu kwa hasira huku nikigeuka kumtazama.
“Hapa bado hujapigwa, nilichojaribu kufanya ni kukukumbusha kuwa unatakiwa kujibu maswali unayoulizwa, usitulazimishe kutumia nguvu kisha ukajuta,” akasema yule komandoo kwa namna ya kunionya.
“Nimesema sijui lolote lakini hamniamini, na hiki mlichokifanya ni utekaji nyara na uvunjaji wa haki za binadamu. Ninaweza kuwafungulia mashtaka kwa unyanyasaji kwani mnanitesa wakati sijafanya kosa lolote,” nilijaribu kujitetea, hata hivyo moyoni nilishaanza kuhisi juu ya hatari kubwa iliyokuwa ikininyemelea.
“Tunayo haki ya kumkamata mtu yeyote ambaye mienendo yake inaonekana kutishia usalama wa nchi yetu na kama hutozungumza ukweli idara haitalaumiwa kwa kifo chako, hivyo usijaribu kututisha,” yule kamanda aliyeketi akanionya huku akinitazama kwa macho makali yenye kuonya.
“Kwa hiyo mnadhani kuniua ndiyo mtakuwa mmetatua tatizo au kupata ufumbuzi wa haja yenu?”
“Huenda lisiwe suluhisho lakini angalau hutoweza kupanga tena mikakati ya ugaidi au kutishia usalama wa nchi yetu.”
“Kwani mipango gani ya ugaidi ambayo mimi nimeipanga?” nikauliza huku nikijaribu kununua muda.
“Acha maswali yasiyo na msingi wewe, unachotakiwa ni kujibu maswali unayoulizwa, basi!” yule komandoo aliyekuwa amesimama nyuma yangu akanionya huku akinisukasuka mgongoni.
“Sasa nitajibu nini wakati sifahamu chochote kuhusu ugaidi mnaousema! Au kosa langu ni kuja Tanzania kusalimia jamaa zangu?” niliuliza kwa hasira huku nikizidi kukerwa.
“Ooh… kwa hiyo unadhani kuwa umeletwa hapa ili tupige stori siyo? Kama unafikiri tunafanya utani basi subiri uone,” yule komandoo aliyekuwa nyuma yangu akaniambia huku akikisukasuka ovyo kichwa changu na kunipigapiga nyuma ya shingo yangu kwa dhihaka.
Kuona vile nikaamua kuinuka kutoka pale kwenye kiti nikiwa nimepandwa na hasira, na hapo ikaonekana kana kwamba nilikuwa nataka kupambana naye. Hilo lilikuwa kosa kubwa sana.
Kilichofuatia hapo nilitamani ardhi ipasuke ili niangukie ndani na kupotelea humo. Kwa kasi ya umeme yule komandoo aliruka juu, akajiviringisha hewani, hapo nikajua akitua chini ingekuwa balaa hivyo nilijiandaa kwa pigo lolote ambalo lingefuata.
Kwa kuwa nami sikuwa nyuma kwani nilikuwa nimepitia mafunzo ya kujihami ya karate na kufikia hatua ya mkanda mweusi, haraka nikajibetua na kuyakwepa mapigo ya haraka ya yule komandoo.
Kuona hivyo, yule komandoo alikusanya nguvu za kutosha kisha kufumba na kufumbua akajibetua na kuuzungusha chini mguu wake wa kulia akinichota ngwala maridadi yenye ufundi wa hali ya juu.
Niseme tu ukweli, sikutegemea kabisa hali ile, hivyo nilishikwa na taharuki ya aina yake wakati nilipokuwa nikitupwa hewani na kuweweseka kama niliyekuwa nimepagawa na mapepo.
Nilipotua chini nikashtukia napigwa ngumi tatu mfululizo za tumbo zilizonifanya nijipinde huku nikisikia maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi mgongoni.
Nikiwa bado nimejipinda yule komandoo alinichapa pigo baya la kareti mbavuni na maumivu yake yakanifanya niachie mguno mkali wa maumivu, nikayumba ovyo huku nikirudi nyuma lakini kabla sijaanguka aliruka na kunidaka kisha akaninyanyua juu juu kama kishada kwa nguvu zake zote na kunibwaga chini.
Hali ile ilinifanya nitue pale chini sakafuni kwa matako na hivyo kufanya maumivu makali yanisambae mwili mzima. Nikapiga yowe kali la maumivu huku nikijitahidi kuwahi kusimama lakini ilikuwa kazi bure.
Yule komandoo aliniwahi kabla sijasimama sawasawa akanikwida tena na kuninyanyua juu. Nilijitahidi kujitetea kwa kila namna lakini bado haikunisaidia kitu, yule komandoo alikuwa na nguvu nyingi zisizo za kawaida, hivyo alinibeba mzegamzega na kwenda kunibwaga juu ya ile meza ya chuma iliyopo katikati ya kile chumba kama furushi.
Muda wote yule komandoo mwingine aliyekuwa ameketi kwenye kiti alikuwa ametulia tuli bila kutingishika akiniangalia huku uso wake ukiwa bado umepambwa kwa tabasamu pana.
Baada ya kutua juu ya ile meza ya chuma kama furushi nilipiga tena yowe kali huku maumivu makali yakizidi kusambaa mwilini, nikajikuta nikianza kuingiwa na hofu kubwa.
Kisha yule komandoo alinijia kwa mapigo ya mateke ya haraka ambayo nilijitahidi kwa kila namna kuyapangua kwa mikono yangu bila mafanikio.
Nilitaka kuinuka lakini kizunguzungu kikanishika na kunifanya kutapika na hapo nikaanza kuishiwa nguvu na sikuona tena kama kungekuwa na namna nyingine ya kujiokoa kutoka kwenye mikono matata ya yule komandoo, hivyo niliamua kunyoosha mikono yangu juu kuashiria kwamba nilikuwa nimesalimu amri huku nikihema ovyo.
Yule komandoo alisimama akanitazama kwa makini na aliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, akaninyanyua na kunikalisha kwenye kile kiti cha chuma nilichokuwa nimeketi mwanzo, kisha akaniacha na kusogea kando huku akinitazama kwa makini.
Damu ilikuwa ikinitoka puani na mdomoni huku sehemu ya juu ya jicho langu la kushoto ikiwa imevimba na kuchanika na ilikuwa inavuja damu taratibu.
Moyo wangu ulikuwa unakwenda mbio na uliunguruma sana kama uliokuwa ukipambana na kazi isiyo ya kiasi chake. Mwili wangu nao ukawa mzito kama uliofungwa na tani kadhaa za mizigo huku jasho likinitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Itaendelea...