Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

HEKAHEKA! 14

Na Bishop Hiluka

Wakati tukiendelea na safari nilitamani sana kujua tulikokuwa tukielekea lakini sikuweza. Nilianza kujilaumu sana kwa kutomsikiliza Susan, niliamini kuwa alikuwa na maono aliponitaka niahirishe safari yangu lakini nikakataa.

Nikajikuta nikiilaumu sana siku hiyo ambayo ilikuwa ya hekaheka sana kwangu, maana katika kipindi cha saa kumi na mbili tu tayari nilikuwa nimekwishapata jambajamba mara mbili kwenye viwanja vya ndege viwili tofauti!

Maana kabla ya mkasa huu wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, nilikuwa nimepatwa na mkasa uliofanana na huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Schiphol jijini Amsterdam, katika siku hiyo hiyo moja ya safari! Kwa kweli siku hiyo ilikuwa ni siku ya hekaheka!

Alfajiri ya siku ile nikiwa na Susan na binti yetu, Pamela aliyekuwa na miaka minne, tulitoka nyumbani kwetu Stadsdeel Nieuw-West jijini Amsterdam na kuelekea katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Schiphol.

Tulifika pale uwanja wa ndege asubuhi ya saa kumi na mbili kasoro dakika ishirini, ikiwa ni dakika hamsini kabla ndege niliyotarajia kusafiria nayo haijaruka.

Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Schiphol jijini Amsterdam, ambacho jina lake kamili kwa Kiholanzi kikiitwa Luchthaven Schiphol, kilikuwa kiwanja kikubwa sana cha kisasa kikiwa kati ya viwanja vya ndege vikubwa duniani chenye kupokea abiria zaidi ya milioni 46 kwa mwaka, idadi iliyokifanya kushika nafasi ya tatu barani Ulaya na nafasi ya 12 duniani.

Kiwanja hicho cha ndege kipo kilomita 9 kusini magharibi ya Amsterdam katika manispaa ya Haarlemmermeer kikiwa na kituo (terminal) kikubwa kimoja kilichokuwa kimegawanywa katika vituo vikubwa vitatu vya kuondokea (Departure Halls).

Tulifika pale uwanjani tukaingia moja kwa moja katika eneo la chini la Departure Hall 2 kwenye geti namba E-10 na haraka haraka nilikaanza mchakato wa kukamilisha taratibu zote za uhamiaji pale uwanja wa ndege kabla ya kuondoka.

Niliwaacha Susan na Pamela wakilinda mizigo yangu nikapanga foleni kwenye dirisha la ofisi ya uhamiaji pale uwanjani kisha nikapenyeza vibali vyangu vyote vya kusafiria kwenye dirisha dogo la kioo la chumba kilichomhifadhi msichana mmoja mlimbwende aliyekuwa na sura ya uchangamfu.

Msichana yule ofisa uhamiaji akavipokea vibali vyangu vya kusafiria huku akiliachia tabasamu lake maridhawa na kulifanya lizisumbue fikra zangu.

Japo mchumba wangu Susan alikuwa mrembo kwelikweli lakini nilikuwa mgonjwa kwa walimbwende kama huyu na sikuwa nikiridhika, nilimtamani kila msichana mrembo niliyemuona mbele yangu.

Mambo yote yalikuwa chapuchapu kwani yule ofisa uhamiaji alimaliza haraka kuingiza taarifa zangu kwenye kompyuta yake kisha akagonga mhuri kwenye hati yangu ya kusafiria na hivyo safari yangu kuelekea nchini Tanzania ikawa imeidhinishwa rasmi.

Bila kupoteza muda nikaipokea pasi yangu ya kusafiria na kuitia mfukoni huku tabasamu langu la kichokozi likichomoza na kuzisumbua vibaya hisia za yule ofisa uhamiaji.

Kisha nikanyoosha mkono wangu kumpa, wakati tukipeana mkono wa kuagana na yule ofisa uhamiaji nikapitisha kidole changu cha shahada katikati ya kiganja chake kumtekenya, kitendo kile kikamfanya yule ofisa uhamiaji ashtuke na kuruka huku akiutoa haraka mkono wake kutoka kwenye kiganja changu.

Sikuishia hapo, nikamkonyeza kidogo kumchombeza lakini nikihakikisha Susan haoni kitendo kile. Nikashukuru kuwa Susan alikuwa hajashtukia mchezo ule vinginevyo kwa jinsi nilivyokuwa namfahamu Susan, kwa vyovyote moto ungewaka palepale.

Wakati yule ofisa uhamiaji akiwa bado ana mshangao usoni kwake nikamnong’oneza kuwa siku nikirudi Amsterdam nitamtafuta, kisha nikanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu kuliacha eneo lile.

Yule ofisa wa uhamiaji hakujibu bali alibaki ameduwaa huku macho yake yakinisindikiza nyuma yangu hadi pale nilipopotea mbele ya macho yake.

Kwa kusaidiwa na mchumba wangu Susan tulichukua mizigo yangu na kwenda kupanga foleni kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo.

Wakati zamu yangu ikikaribia mara nikahisi mchafuko mbaya wa tumbo huku dalili za kuendesha zikiibuka. Katika hali ile nilijikuta nikihitaji sana kukimbilia maliwatoni hivyo nilikuwa natweta huku jasho likinitoka.

Kutokana na hali ile ya kubabaika, ofisa mmoja wa usalama wa eneo lile aliniona akanishtukia kisha alituchukua kando mimi na Susan kwa ajili ya upekuzi zaidi wa mizigo yetu.

Na baada ya kufanya upekuzi wa mizigo yangu katika kila eneo yule ofisa usalama aliomba usaidizi wa kupata ofisa mwingine ili kufanya upekuzi zaidi.

Wakati tukimsubiri ofisa usalama mwingine afike ndipo nikafanya kosa kubwa kwa kumwambia yule ofisa usalama kuwa nilihitaji sana kwenda maliwato kwa kuwa nilikabiliwa na mchafuko wa tumbo.

Yule ofisa usalama alinitazama kwa makini zaidi kisha akaniuliza ikiwa nilikuwa nimekula au kunywa chochote kibaya usiku wa kuamkia alfajiri ile nami nilimjibu kuwa sikuwa nimekula wala kunywa chochote kibaya.

Aliniuliza tena ikiwa nilimhitaji daktari wa kunichunguza tumbo langu ili kujua kilichokuwa kikinisumbua, nikasema nilikuwa sawa, bali nilichohitaji ilikuwa kwenda maliwatoni tu.

Yule ofisa usalama alinitazama katika mtizamo ambao baadaye niligundua kuwa hatukuwa tumeelewana kuhusu kilichokuwa kikinisumbua. Yule ofisa usalama alisisitiza kuwa mchafuko wa tumbo langu ulisababishwa na kumeza mihadarati niliyokuwa nikijaribu kuisafirisha.

Kwa kuwa hali ya mchafuko wa tumbo ilinifanya kutweta na jasho jingi kunitoka, yule ofisa usalama hakutaka kunipa nafasi ya kutoroka kutoka eneo lile wala kwenda maliwato.

Nilijaribu kumwelewesha lakini hakutaka kunielewa na mara nikawaona maofisa wengine wawili wa usalama wakifika eneo lile wakiwa na mbwa, na wakatuchukua mimi na familia yangu hadi kwenye kibanda maalumu cha walinzi wa uwanja ule na hapo tukasubiri ukaguzi zaidi wa mizigo yetu kwa kutumia mashine maalumu.

Baada ya ukaguzi nikachukuliwa tena hadi kwenye chumba maalumu cha mahojiano, ambako ofisa wa polisi alijaribu kuligusagusa tumbo langu wakati akiniuliza maswali kama nimeshawahi kusumbuliwa na tatizo la aina ile na kama kuna dawa zozote maalumu nilizozoea kutumia nilipotokewa na tatizo kama lile.

Nilimweleza kuwa “bila shaka huwa nakunywa Imodium, lakini sijanywa leo.”

Yule ofisa wa usalama aliniambia kuwa, nilipaswa kuwa na subira wakati tukimsubiri daktari ili anifanye uchunguzi wa tumbo langu.

Nilijaribu kumwelezea kuwa shida yangu haikuwa kumwona daktari bali nilihitaji huduma ya maliwato, lakini haikuwa rahisi kuniruhusu muda ule.

Tulisubiri pale kwa dakika kadhaa, mchumba wangu Susan na mwanetu Pamela walikuwa wanalia kilio cha kwikwi; wale maofisa wa polisi walionekana kucheka kwa dharau na kutusanifu. Hatimaye mtu mmoja alifika ili kunifanyia uchunguzi lakini niligundua kuwa hakuwa daktari bali ni ofisa usalama.

Niliamua kumuuliza yule ofisa usalama kuhusu uwezo wake wa kidaktari lakini niliambiwa kuwa sikuwa na uchaguzi mwingine bali kuwasikiliza. Niliondoka nikiongozana na yule ofisa usalama.

Tulifika kwenye mlango mmoja na kusimama, hapo yule ofisa usalama akanionesha kwa kidole huku akiniambia kuwa niingine maana kile kilikuwa chumba cha maliwato.

“Dah, hatimaye ninapata nafasi ya kujisaidia!” nikawaza kwa furaha.

Nilipoingia ndani ya kile chumba, yule ofisa usalama pia akaingia akinifuata. Nikiwa mle ndani nikagundua kuwa kile chumba kilikuwa ni choo maalumu cha kutolea dawa za kulevya kwa njia ya haja kubwa kama nilichokuja kukikuta katika uwanja wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Nilibaki nimeshangaa nikimtazama yule ofisa usalama lakini yeye aliniambia kuwa alikuwa anataka kushuhudia iwapo nilikuwa nasema ukweli au la! Na aliniambia kuwa iwapo nilitaka kujisaidia mbele yake hakuwa na shida.

Wakati nikitaka kumwomba anipishe kwa muda ili nijisaidie kwa uhuru zaidi nilijikuta nikishindwa kuhimili zaidi mchafuko wa lile tumbo, hivyo sikujali tena kama alikuwa akinishuhudia. Nilishusha haraka suruali yangu, nikaachia mzigo nikimwaga haja kama maji huku nikipiga mabomu ya kutosha.

Itaendelea...
 
HEKAHEKA! 15

Na Bishop Hiluka

Nilibaki nimeshangaa nikimtazama yule ofisa usalama lakini yeye aliniambia kuwa alikuwa anataka kushuhudia iwapo nilikuwa nasema ukweli au la! Na aliniambia kuwa iwapo nilitaka kujisaidia mbele yake hakuwa na shida.

Wakati nikitaka kumwomba anipishe kwa muda ili nijisaidie kwa uhuru zaidi nilijikuta nikishindwa kuhimili zaidi mchafuko wa lile tumbo, hivyo sikujali tena kama alikuwa akinishuhudia. Nilishusha haraka suruali yangu, nikaachia mzigo nikimwaga haja kama maji huku nikipiga mabomu ya kutosha.

Wakati nikiendeleaa kushusha mzigo nilianza kujisikia faraja kubwa na muda huo huo nikamtupia jicho yule ofisa usalama huku nikiachia tabasamu la faraja lililokuwa na swali: “vipi bado hujaamini?”

Yule ofisa usalama aliziba pua yake huku akijitahidi kuvumilia kilichokuwa kikiendelea mle maliwatoni. Baada ya takriban dakika moja na ushee, yule ofisa usalama alionekana kuridhika na kutoka huku akiendelea kuziba pua yake na kuniacha naendelea kuachia fataki za kutosha.

Nilimaliza na kujisafisha na niliporudi nilimkuta Susan akimalizia kufungasha vitu vyangu, hata hivyo yeye na mwanetu walikuwa bado wana wasiwasi maana hawakujua maofisa usalama walikuwa wamenipeleka wapi.

Ndege niliyopaswa kuondoka nayo iliondoka na kuniacha japo ilisubiri kwa dakika kadhaa, hivyo ilibidi nilipe tena malipo mengine ya asilimia ishirini ya kiwango halali nilichokuwa nimelipa awali ndipo nikapata nafasi ya kuendelea na safari yangu kuelekea Tanzania.

Sasa huku Tanzania nimekutana tena na hekaheka nyingine iliyofanana na hiyo ya Uholanzi. Lakini hekaheka ya Dar es Salaam ilionekana kuwa kubwa na sikujua ingeisha vipi…

______

“Wewe wacha kulala au unadhani upo gesti? Teremka haraka na usijaribu kufanya ujanja, utajuta!” sauti kali ya ofisa wa usalama aliyekuwa amenishika mkono wangu akinivuta niteremke kutoka katika lile gari ilinishtua na kunikatisha mawazo yangu.

“Nishuke kwani mnanipeleka wapi?” niliuliza huku hofu ikizidi kunizonga.

“Siyo kazi yako kujua unapelekwa wapi,” alijibu kwa ukali huku nikihisi mtu mwingine akiongezeka pale nilipokuwa.

Nilishtukia nikiwa nimedakwa mikono na miguu kisha nikashushwa kwa nguvu kutoka katika lile gari na hapo nikadakwa juu kwa juu ili nisianguke chini huku nikishangazwa na uharaka wa matukio yale.

Kwa uharaka sana na kwa wepesi wa hali ya juu nikashtukia nikibebwa juu juu kama jeneza kisha nikahisi kuwa walionibeba walikuwa wakitembea haraka na kwa hatua za ukakamavu.

Baada ya kitambo fulani cha mwendo wa kijeshi nilihisi walikuwa wanapanda ngazi za jengo na kisha wakaanza kuingia ndani ya jumba kubwa, sikuweza kuielewa vizuri jiografia ya eneo lile kwa sababu nilikuwa bado nimefunikwa kichwa na ule mfuko mweusi.

Kisha walinitupa chini nikaanguka nikifikia kiuno na mgongo, hapo nilihisi maumivu makali sana yakisambaa mwilini. Mikono yenye nguvu ilinishika na kuniinua pale sakafuni nilipokuwa nimeanguka, nikasimama huku nikiugulia kwa maumivu makali.

Niliposimama kwa miguu yangu mwenyewe nikagundua haraka kuwa tulikuwa kwenye jumba kubwa la kale ambalo kwa vyovyote lilikuwa lina ulinzi mkali kila mahali.

Sikujua tulikuwa tumetumia muda gani kutoka uwanja wa ndege hadi kufika katika eneo lile na ni wakati gani tulikuwa pale kabla sijazinduliwa katika lindi la mawazo.

Kisha nilikokotwa kwa nguvu nikiongozwa kuelekea ndani zaidi ya lile jengo, na wakati tukielekea ndani zaidi nilihisi kuwa tulikuwa tunapita katika korido ndefu hadi mbele na hapo nikasikia mlango mkubwa ukifunguliwa kisha tukaingia na kutokea kwenye ukumbi mmoja mkubwa.

Sikuweza kuona tulikuwa wapi hasa na wapi tulikuwa tukielekea, hata hivyo hisia zangu zilinitanabaisha kuwa tulikuwa kwenye ukumbi mkubwa kisha tukashika uelekeo wa upande wa kushoto.

Baada ya kwenda mwendo mfupi tukakata kona na kushika uelekeo wa upande wa kulia kisha kushoto tena na baada ya muda tukaanza kuifuata korido nyingine ndefu. Muda wote huo ukimya ulikuwa umetawala.

Tulikuwa tukikatisha kwenye eneo lililokuwa na mazingira yenye utulivu wa kupita kiasi, wale maofisa usalama waliokuwa wakiniongoza kunipeleka nisikokujua walikuwa kimya kabisa na hapakuwa na maongezi yoyote baina yao.

Baada ya safari ya kitambo fulani tukipita kwenye korido ile ndefu tukaingia upande wa kulia tukikatiza katikati ya ukumbi ambao kwa hisia tu nilijua kuwa ulikuwa mdogo, kisha tukaifuata korido nyingine iliyokuwa ikielekea upande wa kushoto kabla ya kuzikuta ngazi zilizokuwa zikielekea eneo la chini la lile jumba.

Hapo tukaanza kuzishuka zile ngazi na kwa sababu nilikuwa sioni nilijikuta nikikanyaga ngazi vibaya na kuanguka kisha nikaburuzika kwenye zile ngazi hadi katika eneo la chini kabisa huku nikichubuka sehemu mbalimbali za mwili wangu.

Nikiwa hapo sakafuni mikono yenye nguvu ikanishika kwa nguvu na kuniinua na hapo nikagundua kuwa tulikuwa kwenye ukumbi mwingine ambao kwa kutumia mlango wangu wa sita wa fahamu niliweza kuhisi kuwa ulikuwa ukumbi mpana huku eneo lile likitawaliwa na hewa nzito.

Wasiwasi mkubwa ukaniingia, moyo wangu ukaanza kupiga kite kwa nguvu huku mwenendo wa mapigo yake ukianza kwenda katika utaratibu usio wa kawaida, miguu yangu ikaanza kuishiwa nguvu kama iliyoishiwa na damu na hivyo ikikaribia ganzi.

Hapo nikaanza kuhisi kuwa sikuwa sehemu salama bali nililetwa sehemu hatari zaidi isiyokuwa na utu, ambapo ningeweza kufanyiwa unyama wa kutisha na hata kuuawa na huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu.

Kwa kweli nikaanza kujuta majuto ya firauni kwa kushindwa kumsikiliza Susan na kuahirisha safari yangu, pengine haya yote yasingenikuta.

Nikiwa bado nimesimama nilishtukia mkono wenye nguvu wa ofisa mmoja wa usalama ukinishika kwa nguvu kama kishada na kuanza kuniburuta huku nikiongozwa kupita katikati ya ule ukumbi.

Ili nisiumie nikajikakamua na kusimama sawasawa kisha nikaanza kupiga hatua nikitembea haraka, tukakatisha katikati ya ule ukumbi mpana na kuifikia korido nyingine iliyokuwa na kona mbili-tatu kwa kuwa tulikuwa tukikata kona kila baada ya hatua kadhaa, mara tupinde kushoto mara kulia.

Kisha tukanyooka mbele zaidi na baada ya kitambo kifupi tukawa tumefika kwenye kona ambayo nilidhani ndiyo ilikuwa kona ya mwisho iliyokuwa upande wetu wa kulia.

Hapo niligundua kuwa kulikuwa na mlango mkubwa madhubuti wa chuma, maana nilimsikia ofisa usalama mmoja akikukuruka kuufungua ule mlango na kisha akauvuta kwa nje. Mlango ukasalimu amri na kufunguka ukituruhusu kuingia ndani.

Niliongozwa kuingia ndani ya kile chumba ambacho sikujua kilikuwa cha ukubwa gani, lakini mazingira yalikuwa ya ukimya mno ulionitisha sana.

Hapo tulisimama kisha ofisa mmoja wa usalama akanifungua ule mfuko mweusi niliokuwa nimefunikwa kichwani. Nikajaribu kuyakodoa macho yangu ili nione kilichokuwemo mle ndani.

Nilijiona nikiwa kwenye chumba kikubwa kilichokuwa chini ya ardhi kikiwa na kuta imara lakini hakina dirisha na kikiwa na kioo kipana ukutani ambacho kilimfanya mtu aliyekuwemo mle ndani asiweze kumuona mtu aliyekuwa nje ya chumba lakini yule mtu wa nje aliweza kumuona vizuri mtu aliyekuwa mle ndani.

Nilipozidi kutupa macho huku na huko nikaweza kuyaona mandhari ya chumba kile kikubwa. Katikati ya chumba kile niliona viti vitatu na meza kubwa ya chuma iliyovitenganisha vile viti katikati, upande mmoja ukiwa na viti viwili na upande mwingine kulikuwa na kiti kimoja cha chuma.

Juu ya meza ile kulikuwa na balbu ya umeme ya mwanga usiokuwa mkali sana kutoka katika dari ya chumba kile ikiwa imening’inizwa kwa waya mwembamba na mrefu kutoka darini.

Itawendelea...
 
HEKAHEKA! 16

Na Bishop Hiluka

Nilipozidi kutupa macho huku na huko nikaweza kuyaona mandhari ya chumba kile kikubwa. Katikati ya chumba kile niliona viti vitatu na meza kubwa ya chuma iliyovitenganisha vile viti katikati, upande mmoja ukiwa na viti viwili na upande mwingine kulikuwa na kiti kimoja cha chuma.

Juu ya meza ile kulikuwa na balbu ya umeme ya mwanga usiokuwa mkali sana kutoka katika dari ya chumba kile ikiwa imening’inizwa kwa waya mwembamba na mrefu kutoka darini.

Na kwenye vile viti viwili vilivyokuwa upande mmoja wa ile meza kubwa ya chuma niliweza kuwaona wanaume wawili makamanda shupavu, warefu na wenye miili iliyojengeka imara waliokuwa wameketi wakinitazama kwa makini.

Kwa uelewa wangu kutokana na kupenda kutazama sinema za kijasusi niliweza kubaini kuwa kile kilikuwa chumba maalumu kwa ajili ya kumuhoji mtuhumiwa kwa mdomo bila kumsulubisha. Na hata kama wangetaka kufanya hivyo, basi wangetumia viungo vyao kama ngumi na mateke.

Wale wanaume wawili makamanda shupavu walikuwa wamevaa kombati za rangi ya hudhurungi, kofia nyekundu za bareti vichwani mwao na buti ngumu za ngozi miguuni.

Walikuwa wamekunja mikono ya magwanda yao na kuruhusu misuli yao imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu kwa mazoezi ya nguvu yasiyokuwa na kikomo ionekane vyema.

Nilipowatazama kwa makini nikagundua kuwa walikuwa ni makomandoo waliofuzu vizuri katika medani za masuala ya kijeshi, na hata nyuso zao hazikuonesha mazingira yoyote ya urafiki.

Nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa nyuma ya wale makamanda wa jeshi kulikuwa na mlango mwingine mkubwa wa chuma uliokuwa umefungwa.

Niliyahamisha macho yangu kutoka kwa wale makamanda na kuyapeleka juu ya ile meza ya chuma, hapo hofu ikaongezeka zaidi na moyo wangu ukashikwa na mfadhaiko huku ukienda mbio na kuunguruma sana kama uliopambana na kazi isiyo ya kiasi chake.

Niliiona nembo kubwa ya CMI – Central Military Intelligence, ambayo ni idara maalumu ya ujasusi ndani ya jeshi. Hapo jasho jembamba likaanza kunitoka huku nikiihisi hatari iliyokuwa mbele yangu, maana hii ilikuwa ni Idara iliyofanya kazi ya kukusanya taarifa hatarishi za kigaidi au za kijasusi dhidi ya nchi.

Sasa sikuwa na shaka yoyote kuwa nilikuwa nimefikishwa kwenye makao makuu ya idara maalumu ya ujasusi ndani ya jeshi ili kuhojiwa! Mara nyingi maeneo kama yale walifikishwa watu walioonekana kuwa hatari zaidi, kama magaidi waliokubuhu au majasusi waliobobea.

Nilikuwa na hakika kabisa kuwa katika macho ya serikali nilionekana ni jasusi hatari sana kwa usalama wa nchi niliyekuwa na taarifa muhimu zilizotakiwa na idara ya ujasusi ili kusaidia kumaliza uhalifu nchini.

Wale makamanda waliendelea kunitazama bila kusema chochote huku macho yao makubwa yenye kila dalili ya ukatili yakionekana kunionya kuwa nisijaribu kuleta aina yoyote ya ufedhuli.

Tangu nilipofikishwa kwenye kile chumba sikuwa nimeulizwa chochote hadi muda ule, kitambo kirefu cha ukimya kilipita nikiwa bado nimesimama pale huku chumba kikiwa kimezingirwa na maofisa usalama na makamanda walionileta ambao walikuwa wakisubiri kupokea amri kutoka kwa wale makamanda wawili.

“Wakuu wanahitaji mtu huyu atapishwe taarifa zote muhimu anazozifahamu kwa namna yoyote ile,” ofisa usalama mmoja miongoni mwa wale maofisa walionileta mle ndani alivunja ukimya.

“Vipi kama dozi itamzidi na akapoteza maisha?” mmoja wa wale makomandoo tuliowakuta mle ndani akauliza huku akinitupia jicho kali.

“Roho ni ya kwake, sisi tunachohitaji ni taarifa zote muhimu,” alijibu yule ofisa usalama na kunifanya kuogopa sana.

“Okay! Tuachieni kazi hiyo tutajua namna ya kufanya,” yule komandoo akasema huku akionekana kutafakari jambo. Kisha nikamuona akiwapa ishara fulani wale maofisa usalama walionileta kuwa waondoke.

Niliwashuhudia wakiondoka na hatimaye tukabakia watu watatu tu, mimi na wale makomandoo wawili, hapo nikahisi mapigo yangu ya moyo yamesimama, hasa nilipoyafikiria maneno ya yule komandoo kuwa: ‘Sasa itakuwaje kama dozi itamzidi na akapoteza maisha’.

Hata hivyo nilijipa moyo kidogo kwa tukio lile la kuondoka kwa wale maofisa usalama kwani niliamini kuwa wale makomandoo wa idara ya ujasusi jeshini wangeweza kunielewa kwa kuwa walikuwa wamepitia mafunzo ya hali ya juu mno ya intelijensia ili kuweza kumbaini mhalifu na asiye mhalifu.

Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia nikiwa bado nimesimama huku tukitazamana, kisha nikawaona wale makamanda wakiinuka na kuanza kuzitupa hatua zao kunifuata wakitembea kikakamavu huku buti zao ngumu miguuni zikiitetemesha sakafu ya kile chumba kwa kiasi kikubwa.

Nilitamani nikurupuke na kuanza kutimua mbio. Lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa muda haukuniruhusu kufanya vile na wale watu walikuwa ni kama tayari wameshanifikia pale niliposimama.

Wale makamanda walipofika pale niliposimama wakajigawa katika mtindo wa kunizunguka. Komandoo mmoja akaja na kusimama nyuma yangu na mwingine akasimama mbele yangu.

Yule kamandoo aliyesimama mbele yangu alinitazama kwa kitambo na kuonekana kama aliyekuwa akinionea huruma kwa yatakayonipata kisha akaniashiria kwa mkono niketi kwenye kile kiti cha chuma kilichokuwa upande wa pili wa ile meza kubwa ya chuma.

Sikutaka kuleta ubishi wowote, nilikifuata kile kiti kisha nikaketi huku nikiwatazama kwa wasiwasi wale makamanda waliokuwa bado wamesimama wakinitazama kwa makini.

Kwa mara ya kwanza nilianza kuhisi kuwa akili yangu ilikuwa ikishindwa kufanya kazi, hasa nilipofikiria kitu gani kingefuatia kama wale makomandoo wasingefanikiwa kupata taarifa walizozihitaji kutoka kwangu.

Hata hivyo, bado nilipiga moyo konde huku nikijiambia ni lazima niwaaminishe kuwa nimefananishwa na mtu mwingine kwani mimi ni Maximilian Banda na si Brown Senga ili kujiokoa na adhabu ambayo wangeweza kunipa, vinginevyo ule ndiyo ungekuwa mwisho wangu.

Yule komandoo aliyekuwa amesimama mbele yangu aliendelea kunitazama kwa kitambo kisha nikaliona tabasamu likijitokeza taratibu usoni mwake.

Nami nikatabasamu kidogo kujifariji na kujaribu kuuondoa wasiwasi uliokuwa umetanda moyoni mwangu na hapo nikamuona yule komandoo akirudi kule kwenye kiti na kuketi bila kusema neno lakini yule mwenzake alibaki akiwa amesimama nyuma yangu.

Nikiwa bado nimeshikwa na mshtuko, niliyatembeza macho yangu taratibu nikizikagua vizuri sura za wale makomandoo huku nikijitahidi kuumeza wasiwasi niliokuwa nao moyoni.

Mara nikamuona yule komandoo aliyerudi kuketi kwenye kiti akimpa ishara fulani yule mwenzake aliyekuwa amesimama nyuma yangu.

Sikujua maana ya ile ishara ila nilishangaa kumuona yule kamanda aliyekuwa nyuma yangu akinisogelea na kuanza kunifungua zile pingu mikononi kitendo kilichonifanya nistaajabishwe sana na upendo ule wa ghafla.

Yule kamanda alipomaliza kunifungua zile pingu akanivua ile saa niliyokuwa nimevaa mkononi kisha akarudi nyuma hatua kadhaa na kusimama kama mwanzo.

Nikiwa bado nimeketi kwenye kile kiti mawazo mengi yakawa yanapita kichwani mwangu. Nilianza kumlaani mtu aliyeitwa Brown Senga au Godwin Sengerema kwa kuniponza huku pia nikiilaani siku ile.

Niliukumbuka vyema ule wasifu wa Brown Senga uliotolewa na Babra na baadaye Madame Pamela, kisha nikajaribu kuyafikiria mateso yaliyokuwa mbele yangu nikidhaniwa kuwa mimi ndiye huyo Brown Senga na hivyo kutakiwa kutapika taarifa zote muhimu zilizotakiwa na serikali.

Nilihisi akili yangu ikipoteza uwezo wake, nikaamua kuikabidhi roho yangu kwa Mungu huku nikifumba macho na kufanya maombi kimya kimya kumuomba Mungu aninusuru na mateso makali ambayo yangenisababishia kupoteza uhai, hasa nikiamini kuwa mateso ambayo ningepewa na wale makomandoo wa idara ya ujasusi jeshini yangekuwa makali sana.

“Brown…!” Sauti nzito ya yule kamanda aliyekuwa ameketi kwenye kiti ikayarudisha mawazo yangu mle ndani. Hata hivyo sikuitikia kwani niliamini hilo halikuwa jina langu.

“Wewe!” aliniita tena yule komandoo, safari hii kwa ukali kidogo.

“Naam!”

“Unajua kwanini tumekufungua pingu? Tunataka uwe huru na tuzungumze kiurafiki, ila usidhani kama unaweza kutoroka…” yule kamanda akasema huku tabasamu zaidi likichanuwa usoni kwake.

Itaendelea...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom