HEKAHEKA! 9
Na Bishop Hiluka
Hata hivyo, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Kilikuwa ni choo cha aluminium na kilikuwa tofauti kabisa na vyoo vingine vya pale uwanjani, hiki kilikuwa cha aina yake, kisafi sana kiasi kwamba mtu ungeweza hata kutengewa chakula na ukala bila ya kuhisi kinyaa.
Nilitegemea kuwa baada ya kukosa dawa za kulevya katika mizigo yangu wangenirejeshea uhuru wangu na kuniachia niende zangu nyumbani. Lakini haikuwa hivyo.
Walinirudisha tena kwenye kile chumba cha mahojiano. Sasa wakaacha habari za dawa za kulevya, wakahamia katika masuala ya uhalifu na vikundi vya kigaidi. Hapo nikashangaa sana!
Je, nini kitaendelea?...
“Tueleze, washirikia wenzako wako wapi na silaha mlizopora ili kutekeleza mipango yenu haramu mmezificha wapi?” yule ofisa mkuu wa usalama aliniuliza mara tu nilipoketi kwenye kiti mbele yake.
“Sifahamu chochote kuhusu silaha wala mipango haramu kama unavyosema,” nikamjibu yule ofisa mkuu wa usalama nikionesha kuchoshwa na maswali yao.
Yule ofisa usalama alinitazama kwa makini zaidi kisha akaongea kwa msisitizo huku akiendelea kunitazama.
“Nimekwishakuonya kuwa huwa siwavumilii kabisa waongo, elewa mimi ni mtu mwema sana lakini siyo mpumbavu kama unavyodhani, tumeelewana?”
“Nimekuelewa lakini mimi sifahamu chochote kuhusu uhalifu wala silaha unazosema na sina washirika wowote katika uhalifu,” nikaongea kwa msisitizo.
“Tuambie wenzako wako wapi na silaha mlizopora mmezificha wapi?” akazidi kuniuliza kwa kusisitiza.
“Wenzangu akina nani?”
“Wenzako ulioshirikiana nao kuvamia bohari kuu ya silaha na kupora silaha ili kufanya matukio ya ugaidi hapa nchini, tunajua mna mtandao mpana na wewe ndiye kiongozi wa ugaidi huu!”
“Kwa kweli sifahamu chochote kuhusu huo mtandao wa uhalifu unaosema wala hizo silaha.”
“Mmezificha wapi?” sasa yule ofisa mkuu wa usalama aliongea kwa sauti kali huku akianza kushindwa kudhibiti hasira zake.
“Kwa jinsi ninavyopenda amani kama ningekuwa na taarifa zozote kuhusu uhalifu mnaonituhumu nadhani nisingeshindwa kuwapa taarifa hizo,” nikajitetea huku nikiwa nimechanganyikiwa.
Yule ofisa usalama alinipuuza, badala yake akaruhusu tabasamu la kifedhuli kuchanua usoni kwake, kisha nikamuona akimpa ishara fulani kwa kichwa ofisa mmoja wa usalama aliyekuwa amesimama kando, ishara ambayo sikufahamu maana yake.
Na hapo yule ofisa usalama aliyepewa ishara ile akaondoka haraka na kufungua mlango kisha akatoka ndani ya chumba kile akielekea nisikokujua.
Wakati huo huo nikamuona yule ofisa mkuu wa usalama akiinuka na kuanza kupiga hatua taratibu kunisogelea huku akiwa amekunja uso wake na kutengeneza matuta usoni.
Nilimtazama kwa wasiwasi wakati akizidi kunisogelea huku nikiwa sijui anataka kufanya nini. Nilitamani kuinuka na kutimua mbio lakini sikuweza, hivyo nilisubiri kuona mwisho wake.
“Ni vyema ukasema ukweli vinginevyo utapata mateso makali sana, maana tunachohitaji ni taarifa zote muhimu kabla ya hii nchi haijaangukia kwenye machafuko,” yule ofisa usalama akaninong’oneza sikioni maneno yaliyonishtua sana.
Kisha akasimama na kunitazama kwa kitambo huku akiuma mdomo wake wa chini. Nilibaki kimya nikiwa nimemtumbulia macho maana sikujua nimjibu nini.
“Hivi unadhani tumekuleta hapa ili kupiga stori au kupoteza muda wetu!” yule ofisa mkuu wa usalama akanionya na kisha muda uleule alianza kupiga hatua taratibu kurudi kule alikotoka na kuketi kwenye kiti chake huku akinitazama kwa hasira.
“Pengine bado hujaelewa vizuri uzito wa jambo hili lililosababisha vifo vya askari wetu na wananchi wasio na hatia, na kwanini wewe upo hapa…” alisema yule ofisa na kuongeza.
“Kwa akili yako ulidhani kusafiri nje ya nchi kila unapokuwa umeandaa matukio ya uhalifu ili yatokee wakati wewe uko nje ya nchi tusingeweza kubaini kama wewe ndiye uliye nyuma ya mipango hii?” yule ofisa mkuu wa usalama akaniuliza huku akiendelea kutabasamu.
Sikujibu kitu bali nilibaki nikimtazama kwa mshangao huku hasira ikiwa imenikaba kooni. Sikujua kwanini nilikuwa nikiulizwa maswali ambayo kwa kweli sikuwa na majibu yake!
Muda huo huo ule mlango ukafunguliwa kisha yule ofisa usalama akaingia akiwa ameongozana na mwanamke mmoja mrefu kiasi aliyevaa gauni fupi jepesi la rangi ya pinki na mtandio mwepesi huku ndani ya lile gauni akiwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu.
Yule mwanamke alifika na kusimama mbele yangu, na hapo nikainua uso wangu kumtazama usoni, haikunichukua muda mrefu kumtambua.
Alikuwa ni yule mwanamke chotara mwenye mtoto niliyesafiri naye kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam. Lakini safari hii hakuwa na mtoto wake wala mizigo.
Yule mwanamke alinitazama kwa makini huku chuki ya waziwazi dhidi yangu ikijionesha kwenye macho yake wakati akinitazama.
“Unamfahamu huyo mwanamke aliyeko mbele yako?” yule ofisa mkuu wa usalama akaniuliza kwa udadisi.
“Hapana, simfahamu kabisa,” nikajibu huku nikitingisha kichwa changu kukataa.
“Una uhakika kuwa humfahamu?” aliniuliza tena huku akiwa amenikazia macho.
“Kweli simfahamu na sina sababu ya kuongopa,” nikamjibu yule ofisa usalama kwa kujiamini.
“Mbona yeye anakufahamu?”
“Hilo mimi sijui, labda muulizeni ananifahamu kivipi, ila kitu pekee ninachojua ni kwamba tumesafiri wote kwenye ndege moja ya KLM ingawa yeye alipandia Nairobi, basi!” nikajibu kwa hakika, hata hivyo jibu langu lilionesha halikunisaidia.
“Babra…” yule ofisa usalama akamwita yule mwanamke chotara.
“Abee!” yule mwanamke chotara ambaye sasa nilimtambua kwa jina la Babra aliitika kwa unyenyekevu huku akiyaondoa macho yake kutoka kwangu na kuyahamishia kwa yule ofisa usalama aliyemwita.
“Unamfahamu huyu mtu aliyeketi mbele yako?”
“Ndiyo namfahamu,” alijibu Babra kwa kujiamini huku akiyarudisha macho yake kwangu.
“Unaweza kutuleza unamfahamu kivipi?” yule ofisa usalama akamwuliza Babra kwa sauti tulivu.
“Namfahamu kama shemeji yangu, anaitwa Brown Senga ingawa yeye anataka watu wamwite Godwin Sengerema, na alikuwa anaishi na mdogo wangu Jasmine ambaye walikutana miaka sita iliyopita,” alianza kuelezea Babra huku akinitazama kwa chuki.
“Enhe, endelea kutuelezea jinsi unavyomfahamu,” yule ofisa usalama akasema huku akibetua kichwa chake.
“Niseme tu kuwa mwanzoni nilimuona ni mtu mchesi, mstaarabu na mwema sana kwani alionesha kumpenda sana mdogo wangu Jasmine ingawa nilimuona kuwa alikuwa na wivu sana kwa Jasmine, hivyo kila wakati alimpapatikia na alikuwa tayari kumtimizia chochote alichokitaka…” alinyamaza na muda huo nilimuona akimeza funda la mate kutowesha koo lake.
“Lakini kilichonishangaza ni kuwa alikuwa akikwepa sana kuongelea mambo yaliyohusu familia yake na wala hakupenda kupiga picha huku akisisitiza kuwa uhusiano wake na Jasmine usiwe wa wazi na ujulikane na watu wachache sana akidai kuwa hakutaka kumwingiza Jasmine katika hatari. Nilishangaa na nilikuwa nikimuuliza sana kuhusu kazi aliyokuwa akiifanya, maana nilimfahamu kama mfanyabiashara wa madini, hivyo niliuliza biashara hiyo ilihusianaje na kumuingiza Jasmine katika hatari, lakini Brown hakupenda sana kuongelea mambo ya kazi yake, na ilionekana kuwa hata Jasmine alikuwa akikubaliana naye kwa kila kitu!
“Alikuwa mtu wa safari nyingi sana na za ghafla na siku zote alikuwa na marafiki tofauti ambao sikuwa nikiwaelewa. Nikamshawishi Jasmine kuwa makini na amchunguze taratibu kabla hajaamua kuishi naye ili kufahamu zaidi undani wake na awafahamu wazazi wake na jamaa zake, lakini Brown aligundua na kumtaka Jasmine asipende kunisikiliza mimi kwani nilikuwa nataka kumpotosha, ili mradi wao walikuwa wanampenda sana na alimtimizia kila kitu bila ya matatizo yoyote hakukuwa na haja ya kuchunguzana.
“Siku moja nilikwenda kuwatembelea walipokuwa wanakaa, Brown alikuwa ametoka, nikamkuta Jasmine akifanya usafi chumbani kwake huku akipekua kila sehemu na kuiona bunduki aina ya SMG iliyokuwa imefichwa mahala fulani ndani ya kabati la ukutani. Jasmine alinionesha na sote tulishikwa na wasiwasi sana kwani tulianza kuhisi kuwa Brown alikuwa akijishughulisha na vitendo vya uhalifu. Jioni aliporudi kutoka kazini Jasmine alimuuliza kuhusu ile bunduki na Brown alimuelezea kuwa yeye kama mfanyabiashara mkubwa wa madini alipaswa kuwa na silaha kama ile kujilinda, kwani huko migodini wanakumbana na watu wa kila aina na kumuonya Jasmine kuwa asiitoe siri ile kwa mtu yeyote.”
“Lakini pia alipoona mimi ninazidi kuwa na mashaka naye waliamua kuhama walipokuwa wakiishi na kuhamia sehemu nyingine ambayo sikuijua na wakaamua kubadilisha namba zao za simu, na ninahisi pia alimkataza Jasmine asiwasiliane na mimi, na kwa kuwa alimpenda sana Brown akamsikiliza. Sikutaka kujishughulisha nao na kwa muda huo mimi na mume wangu tukawa kwenye pilika pilika za kuhamia jijini Nairobi nchini Kenya.
Itaendelea...