Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

HEKAHEKA! 28

Na Bishop Hiluka


“Kwa kifupi tu, taarifa hizo zilihusu kugunduliwa kwa eneo ambalo zilikuwa zimefichwa silaha ambazo ndizo zilizokuwa zimeibwa kule kwenye bohari ya silaha na zilikuwa zitumike kufanyia ugaidi, hivyo nikawaamuru wale makomandoo wakuwahishe hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya matibabu lakini wakihakikisha unawekewa ulinzi ili usiweze kutoroka hadi pale tutakapojiridhisha na zile taarifa kisha tukufungulie mashtaka ya ugaidi,” alipofika hapo aliweka kituo na kuangalia kando huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kuwaza mbali kidogo.

Kauli hiyo ikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, hofu ikiwa imeanza kuniingia moyoni nikamtazama Madame Pamela kwa wasiwasi huku nikianza kuhisi hali ya hatari iliyokuwa ikinikabili.

Endelea...

Nilimkodolea macho kwa wasiwasi kama vile nimeona guruneti lililokuwa limetelekezwa mle chumbani na magaidi wa kundi la al-Shabab na wakati wowote lilitaka kulipuka. Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu la kirafiki ili kunitoa hofu.

“Mchana wa siku ile kuna vijana wadogo walikuwa wanachunga mifugo yao katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani, eneo ambalo ni karibu na kijijini kwao! Wakati wakiwa ndani ya huo msitu wa Kazimzumbwi wakaokota bomba la PVC lililokuwa limefichwa, na baada ya kulifungua ndani walikuta lilikuwa na bastola na vitu vingine kadhaa vilivyowatia shaka.

“Wale vijana wakawataarifu wazazi wao ambao nao wakautaarifu uongozi wa serikali ya kijiji, ndipo ikashauriwa vitu vile vipelekwe polisi! Baada ya vitu hivyo kupelekwa polisi, vikachunguzwa na kukakutwa ramani ambayo polisi waliitilia shaka.

“Haraka sana polisi waliifuatilia ile ramani ndipo ikawapeleka moja kwa moja kwenye handaki dogo ndani ya ule msitu wa Kazimzumbwi. Kutokana na vitu vilivyokutwa ndani ya lile handaki polisi wakapata wasiwasi kuwa inawezekana walikuwa wanashughulika na jambo kubwa na nyeti zaidi kuliko uwezo wao, kwani kiliwachostaajabisha ni kuwa handaki lile lilichimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo na lilikuwa lina mpangilio wa hali ya juu wa kiwango cha kijeshi. Na hapo ndipo idara yetu ilipotaarifiwa kuhusu jambo hili,” alinyamaza Madame Pamela na kuinuka kisha akaanza kupiga hatua akizunguka zunguka mle ndani.

Nilibaki kimya nikimtazama Madame Pamela kwa wasiwasi, sikujua kwanini alikuwa akinieleza yale yote, na sikujua kama bado walikuwa wakidhani kuwa nilikuwa nahusika na uhalifu ule, hivyo alikuja ili nimpe taarifa nyingine zaidi! Muda huo huo nikahisi tena ubaridi wa woga wa aina yake ukinitambaa taratibu mwilini.

Niliendelea kumtazama Madame Pamela wakati akizunguka zunguka kwa muda mle chumbani kisha akageuka kunitazama huku akilamba midomo yake iliyoanza kukauka.

“Tulipopewa taarifa zile haraka sana niliwatuma watu wangu huko na walipowasili iliwachukua saa kadhaa tu kung’amua kuwa vitu walivyovikuta ndani ya lile handaki dogo vilikuwa vinahusiana moja kwa moja na mtu anayeitwa Brown Senga au Godwin Sengerema, vitu ambavyo imetuchukua muda mrefu tukihangaika kutafuta taarifa zake. Kisha watu wangu wakachunguza alama za vidole walizozikuta kwenye lile handaki na zilionekana kutofautiana sana na alama zako za vidole jambo lililozidi kutuchanganya, lakini alama zile zilifanana sana na alama za vidole kwenye nyaraka za Brown Senga.

“Ndipo tulipoanza kuhisi kuwa ninyi ni watu wawili tofauti ingawa mnafanana sana kwa karibu kila kitu. Mle ndani ya lile handaki pia tulikuta kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini, pia taarifa za uwepo wa mahandaki mengine mawili ya aina ile, moja likiwa katika pori la Hifadhi ya Moyowosi mkoani Kigoma na jingine likiwa wilayani Kongwa katika mkoa wa Dodoma, yote yalifanana kwa jinsi yalivyochimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo kama lile lililokutwa katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani…” alinyamaza na kumeza mate.

Nilibaki hoi kwa taarifa zile za kiintelijensia ambazo zilisababisha nywele zangu zisisimke kichwani.

Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu pana la kunifariji kisha akasogea pale kwenye kiti na kuketi tena.

“Nimekueleza yote haya ili ufahamu ni kwa namna gani hatulali kuhakikisha nchi hii inakuwa salama lakini wakati mwingine tunakuwa katika mazingira tata yenye mkanganyiko wa taarifa, hasa kwa mambo makubwa kama haya yanayohusu usalama wa nchi na wananchi wake,” alisema Madame Pamela na kuweka tena kituo.

“Kwa kutumia taarifa zilizokuwa ndani ya kile kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini tukaanza kumfuatilia Brown Senga mpaka tukafanikiwa kumpata na kumkamata akiwa kajichimbia mafichoni Dodoma kwenye maktaba yake ya siri iliyosheheni nyaraka mbalimbali za kijasusi, na ndani ya maktaba hiyo kulikuwa na kila kitu ambacho angekihitaji, silaha, nyaraka za kijasusi, kifurushi cha kujikimu, dawa za dharura za huduma ya kwanza, fedha nyingi za kigeni na za Tanzania nadhani ni zile zilizoporwa katika Benki ya Wananchi…

“Pia kulikuwa na majarida ya mazoezi ya kawaida na ya kijeshi na vitu vingine vingi ikiwemo mtambo maalumu wa udukuzi wa mawasiliano wa Satellite GPS and Traces wenye mvuto wa hatari uliotengezwa kwa madini ya Uranium ambao ulikuwa umefungwa kwenye kompyuta maalumu ukifanya kazi ya kufuatilia taarifa na mawasiliano yote ya simu, kompyuta na vifaa vyote vya kielektroniki viwezavyo kutumia Intaneti…

“Tulimkamata wakati akiandaa mkakati wa mwisho wa namna ya kutekeleza tukio kubwa la mauaji ambayo angeyafanya kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wiki ijayo katika siku ya Mei Mosi, kwani walitega mabomu mawili yenye nguvu kubwa karibu na jukwaa kuu na alikuwa na saa ambayo akiibonyeza tu yanaanza kujihesabu na ikifika kumi yangelipuka na kuifanya nchi hii iingie kwenye taharuki isiyoelezeka… kama hufahamu siku ya Mei Mosi ni siku kubwa sana ya wafanyakazi ambayo inakusanya wafanyakazi na viongozi mbalimbali wa serikali kwa ajili ya kusherehekea, na mwaka huu imepangwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye atakayekuwa mgeni rasmi siku hiyo.

“Mpango huo wa mauaji ulikuwa umepewa jina la ‘Operation Underground Elimination’ na ndani ya huo mpango kulikuwa na orodha ya washirika wote katika mtandao wa kigaidi aliouongoza, baadhi yao ni wanasiasa, maofisa wa jeshi, vigogo waliowahi kutumbuliwa serikalini kwa tuhuma mbalimbali, wafanyabiashara wakubwa na watu kutoka nje ya nchi waliopewa jina la ‘wafadhili’. Wengi wao hasa waliopo hapa nchini tayari tumekwisha wakamata na wengine bado tunawasaka kwa udi na uvumba popote walipo duniani, tutawakamata na kuwafikisha katika mahakama ya ugaidi.”

Kauli ile ya Madame Pamela ikawa imeamsha nguvu mpya kwenye mwili wangu na hapo hapo nikajihisi kupona.

“Kwa kuwa wewe umeingia kwenye matatizo haya makubwa yaliyokaribia kuyagharimu maisha yako kutokana na kufanana sana na Brown Senga, Rais amenituma nije kukuomba radhi na kukueleza kuwa serikali inaomba radhi na itakupa dola laki moja za Marekani kama fidia,” alisema Madame Pamela na kusimama.

Nilijikuta nikiyasahau machungu yote kutokana na furaha kubwa niliyokuwa nayo, kisha kitambo kifupi cha ukimya kikapita tena mle ndani huku wote tukizama kwenye tafakuri. Madame Pamela alinitazama jinsi nilivyokuwa nikionesha furaha isiyoelezeka.

Nilifungua mdomo nikataka kusema lakini sauti ikagoma, nilikosa kabisa neno la kusema na hivyo nikajikuta nikiwa nimeganda kama sanamu nikimkodolea macho yule bosi wa usalama wa taifa utadhani nilikuwa nimegeuka sanamu!

Mara kikohozi kidogo kikanitoka, na nyuma yake wimbi la machozi ya furaha lilikuja mbio, machozi ya furaha yakamwagika na kuanza kulowesha mto niliokuwa nimeegemeza kichwa changu utadhani milizamu iliyopasuka.

Nilijaribu kuyazuia machozi lakini nikashindwa, sikuwa na namna nyingine yoyote ya kuyazuia yasitoke, hivyo niliyaacha yamwagike huku nikiendelea kumtumbulia macho yule bosi wa usalama wa taifa bila kusema chochote.

Muda wote Madame Pamela alikuwa akinitazama kwa tabasamu kisha akatoa simu ya mkononi kutoka kwenye mkoba wake na kunipa. Nilipoitazama vizuri ile simu nikagundua kuwa ilikuwa ni simu yangu iliyochukuliwa pale uwanja wa ndege na watu wa usalama nilipokuwa nahojiwa.

“Kwa sasa unaweza kuwasiliana na yeyote utakaye, tumekwisha wasiliana na familia yako na kuwaeleza kuwa ulipofika Dar es Salaam ulipata matatizo ya kuvamiwa yaliyosababisha ulazwe hospitali, hatukutaka kuwaeleza jinsi tukio lilivyotokea kwani haya mengine yatabaki kuwa siri kati ya serikali na wewe,” alisema.

Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiachia tabasamu.

“Halafu huwezi kuamini, kumbe wewe ni kaka binamu, babu yako mzaa mama na babu yangu mzaa baba walizaliwa kwa baba mmoja na mama mmoja! Mungu akuponye haraka, mdogo wangu, na nimeambiwa kuwa huenda ukaruhusiwa kutoka hospitali baada ya siku tatu au nne kama hali haitabadilika. Nitarudi tena baada ya siku mbili kukuona,” alisema Madame Pamela na kunipapasa kwenye paji langu la uso katika namna ya upendo.

Kisha alipiga hatua zake taratibu kuufuata mlango na alipoufikia alishika kitasa cha ule mlango na kukinyonga taratibu, mlango ukafunguka, akachungulia nje na kugeuka kunitazama kwa tabasamu.

“Nilisahau kukwambia, Susan na Pamela wapo hapa kukuona,” alisema na kutoka nje akiuacha mlango wazi, na muda huohuo nikamuona mchumba wangu Susan na binti yetu Pamela wakiingia. Nilipata mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha isiyoelezeka.

“Asante Mungu,” nilijikuta nikisema kwa furaha huku nikiwatazama kwa makini na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. Machozi ya furaha yakaanza tena kunitoka na kuulowesha mto niliolalia.

MWISHO.

0685666964 au bjhiluka@yahoo.com
Inahuzunisha sana...

Ila safi sana...


Chapter Closed


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom