Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

HEKAHEKA! 24

Na Bishop Hiluka

“Chochote atakachowaleleza ni uongo, simjui huyu mtu na wala sijawahi kukutana naye,” nikasema kwa hasira kabla Trésor hajajibu lakini nikashtukia nikizabwa kofi la nguvu usoni lililonifanya kuona vimulimuli mbele ya macho yangu.

Shut up! Hujaulizwa wewe, unakimbilia kujibu!” Komandoo aliyenichapa kibao akafoka.

Nikasonya kwa hasira huku nikigeuza shingo yangu kumtazama yule komandoo, nikamtemea mate, kutahamaki nikazabwa kofi la pili lililonifanya kuyahisi maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi shingoni hadi mgongoni.

“Trésor, tueleze ni wapi mmeficha silaha!” Madame Pamela akamwambia Trésor kwa ukali kidogo.

Endelea...

“Ukweli japo mimi ni mshirika wa karibu wa Brown lakini naapa sijui mahali zilikofichwa kwani mkakati wote anaujua yeye na watu wengine wasiozidi watatu ambao mimi siwafahamu, mimi nilikuwa mtu wa kusubiri kupewa amri tu,” alisisitiza Trésor na kuniacha na mshangao usioelezeka.

“Na kuhusu washirika unaowafahamu?” aliuliza Madame Pamela.

“Wote ninaowafahamu ndio wale niliowataja, siwajui wengine labda muulizeni mwenyewe,” alisema Trésor huku akiyakwepa macho yangu na kuinamisha uso wake chini kwa hofu.

“Wapi mmezificha silaha, au unataka tukurudishe tena chumba cha mahojiano ndipo useme ukweli, siyo?” Madame Pamela alimuuliza Trésor kwa ukali.

“Nimewaambia Brown ndiye anayejua kila kitu, mimi ningekuwa najua zilipo ningewaambia, mbona haya mengine nimesema! Najua hata nikificha bado adhabu inayonikabili ni kifo tu,” alisema Trésor.

“Mimi naona mmeamua kupandikiza watu wenu ili mnikomoe, huu ni uongo mkubwa na ninaapa kuwa lazima niwashtaki kwenye mahakama ya haki za binadamu,” niling’aka kwa hasira.

“Kama unadhani kuwa Trésor ni muongo kwanini usijiulize tuliipata wapi ile picha mliyopiga wote mkiwa na Jasmine, au hujiulizi zile nyaraka zako zikiwemo zile pasipoti na kijitabu chenye mipango yako haramu tulivipataje kama siyo yeye aliyetusaidia kuvipata?” Madame Pamela akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi.

“Nimekwishawaambia mimi siitwi Brown. Sijui mmewatoa wapi hawa watu wanaotoa ushahidi wa uongo dhidi yangu, na mkakubali kudanganywa kiasi hiki! Muulizeni kila kitu yeye ndiye atakuwa anafahamu kuhusu hiyo mipango na ugaidi mnaonituhumu nao,” nilijitetea lakini haikuonekana kusaidia.

Madame Pamela alimpa ishara yule komandoo ya kumwondoa Trésor na kumrudisha alikomtoa. Wakati Trésor akiondolewa Madame Pamela alinigeukia akanitazama kwa uyakinifu huku akiachia tabasamu la ushindi.

“Sasa niambie, washirika wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza kwa sauti tulivu.

Sikumjibu bali niliendelea kubaki kimya huku nikimkodolea macho kwani nilionesha kuchoshwa na maswali yake.

Alishusha pumzi ndefu huku akiendelea kutabasamu na baadaye tabasamu lake liligeuka kuwa kicheko, kisha nikamuona yule komandoo aliyetoka na Trésor akirudi na muda huo huo Madame Pamela akawapa ishara fulani wale makomandoo ambayo sikufahamu maana yake.

Mara nikawaona wale makomandoo wakinisogelea kwa ukakamavu mkubwa, na kwa haraka sana wakanifungua zile pingu zilizokuwa zimefungwa kwenye mikono na miguu yangu pale kwenye kile kiti cha umeme kilichokuwa kikitumika kunisulubu.

Nikiwa bado nashangaa ghafla wale makomandoo wakanishika miguu yangu na kunivuta wakinishusha kwa nguvu kutoka pale kwenye kile kiti hali iliyonifanya nitue pale chini sakafuni kwa matako na kunifanya nisikie maumivu makali sana yaliyosambaa mwili mzima.

Nilijaribu kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani walianza kunishushia kipigo cha mateke mwilini mwangu na kujikuta nikiishiwa na nguvu na kulala sakafuni kama mfu.

Wale makomandoo waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaanza kuniburuza kibabe kuelekea kule kwenye lile tangi kubwa lililokuwa limejengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilikuwa limejazwa maji.

Walinibwaga pale chini jirani na lile tangi la maji. Nikiwa pale chini nikihema kwa nguvu kutokana na kile kipigo nilimuona Madame Pamela akinisogelea taratibu huku wale makomandoo wakinizunguka na hapo nikafungwa kamba mikononi.

“Tuambie wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza Madame Pamela kwa hasira.

“Wenzangu akina nani?” nilimuuliza kwa hasira.

“Unaoshirikiana nao kufanya ugaidi”

“Sifahamu chochote kuhusu ugaidi unaouzungumzia…”

Nilikatishwa na kipigo cha mateke ya mgongoni, kabla sijajua niseme nini mara nikabebwa mzobe mzobe na wale makomandoo kisha nikarushwa na kuangukia ndani ya lile tangi la maji. Matukio yote yale yalifanyika kwa haraka sana.

Nikajua sasa walikuwa wamedhamiria kunitesa kwa kunizamisha ndani ya lile tangi la maji kwa kufungulia umeme ulioungwa ndani ya lile tangi la maji ili kunipiga shoti mbaya na ikiwezekana kuniua kabisa.

Nikakumbuka kuwa niliwahi kusoma habari kuhusu matumizi ya mbinu za ukatili na utesaji kwa kuwaweka watuhumiwa kwenye maji, kuwakosesha usingizi, kuwapiga shoti ya umeme na kila aina ya utesaji ili kupata siri kutoka kwa magaidi.

Nilisimama na yale maji ndani ya lile tangi yaliishia usawa wa kifua changu. Nikiwa sijui kilichokuwa kinaendelea ghafla nikapigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima huku nikihisi ngozi yangu ikiunguzwa na moto wa umeme uliokuwa ukisambaa haraka sana mwilini mwangu.

Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nikaanza kutetemeka kama niliyekumbwa na ugonjwa mbaya wa degedege.

Nilifumbua mdomo wangu kupiga kelele za kumuomba Madame Pamela asitishe yale mateso lakini sauti yangu haikuweza kutoka, kila nilipopiga kelele niliisikia sauti yangu ikiishia ndani ya akili yangu.

Kwa mbali nikasikia mlango wa kile chumba ukigongwa kwa nguvu kisha ukafunguliwa na hapo nikasikia sauti ya vishindo vya watu waliokuwa wakija mbio kule kwenye lile tangi huku wakipiga kelele kumtaka Madame Pamela asitishe yale mateso.

Muda ule ule nikaanza kujiona nikipaa angani kwa kasi ya ajabu sana, na nilipofika juu zaidi nikajikuta nikianza kushuka chini kwa kasi ile ile na kisha nikatumbukia kwenye shimo refu sana lililokuwa na kiza kilichotisha.

Na mara giza zito likatanda kwenye mboni zangu za macho huku taratibu nguvu zikianza kuniishia na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda…

* * * * *

Nilizinduka nikajikuta nipo kwenye chumba kikubwa nikiwa nimelala kwenye kitanda kikubwa cha chuma cha futi nne na nusu kwa sita, nikiwa nimelalia foronya laini na mto wa kuegemeza kichwa.

Ndani ya chumba kile kulikuwa na hewa safi iliyokuwa ikisambazwa taratibu na kiyoyozi kilichokuwa juu ya dari ya kile chumba iliyokuwa imetengenezwa kwa gypsum nzuri ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kulining’inizwa taa nzuri.

Nilikuwa nimerudiwa na fahamu zangu na sikujua nilipoteza fahamu kwa muda gani, hisia zangu zilinitanabaisha kuwa nilikuwa nimerudiwa na fahamu huku nikikumbuka vizuri masaibu yote yaliyonitokea kule kwenye chumba cha mateso makali.

Sikuwa na uhakika kama nililetwa pale kwa gari, mkokoteni, machela au niliburuzwa kama ilivyotokea kule kwenye chumba cha mateso, kwa kuwa sikuwa na fahamu yoyote nilipokuwa nikiletwa pale.

Hata hivyo, jambo hilo halikuwa la muhimu sana kwangu. Jambo lililokuwa la muhimu ni kwamba nilikuwa bado nipo hai, na hivyo nikataka kujua nilikuwa wapi.

Mambo sasa yananoga, ni nini kitaendelea? Fuatilia kuujua mwisho wa Hekaheka...
 
HEKAHEKA! 25

Niliyatega masikio yangu kwa makini huku nikijaribu kutafakari kuwa pale nilikuwa wapi. Sikusikia sauti ya kitu chochote na utulivu ndani ya chumba kile ulikuwa ni wa hali ya juu kiasi kwamba nilianza tena kuingiwa na hofu.

Nilijaribu kujiinua kutoka pale kitandani nikahisi maumivu makali yakisambaa mwilini sambamba na kichwa kuuma huku nikihisi kizunguzungu na mwili wangu ulikuwa umedhoofika sana mithili ya mlevi aliyeamka na uchovu wa pombe.

Nilipojichunguza vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimefungwa bandeji na plasta maeneo mbalimbali ya mwili wangu. Kilichonishangaza zaidi ni kwamba nilikuwa nimevaa nguo zangu safi zilizokuwa kwenye begi langu tofauti na zile nilizokuwa nimevaa wakati nikiteswa, pia sikuwa nimefungwa pingu.

Kingine nilichogundua ni kuwa nilikuwa nimefunikwa kwa shuka safi la rangi ya samawati, nikashtuka. Niligeuza shingo yangu kuyatazama vizuri mandhari ya kile chumba na kugundua kuwa hakikuwa chumba nilichokizoea, na wala hakikuwa kile chumba cha mateso.

Hiki kilikuwa chumba maalumu kilichoonekana kama ni wadi maalumu ya VIP kikiwa na mitambo ya kisasa ya tiba ya hali ya juu yenye kumsaidia mgonjwa kupumua na mingine ya kusoma mapigo ya moyo jinsi yanavyoendelea.

Nikajikuta nikishikwa na mshangao huku nikiwaza pale nilikuwa wapi na nilifikaje!

Nilishangaa kuona kulikuwa na meza ndogo upande wangu wa kulia na juu ya ile meza kulikuwa na trei ndogo ya aluminium iliyokuwa na vifaa vyote muhimu vya tiba kama mikasi, bandeji, plasta, dawa ya kukaushia vidonda, mabomba ya sindano, glovu, chupa ya maji, bilauri na dawa za vidonge ambazo sikuzifahamu.

Baadhi ya vile vifaa vilikuwa vimefunguliwa na kuachwa wazi kitendo kilichoashiria kuwa tayari vilikuwa vimekwisha tumika.

Kando kidogo ya kile kitanda kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyokuwa imetundikiwa chupa mbili, moja ilikuwa chupa ya maji aina ya Dextrose 5% yaliyokuwa yamechanganywa na fulani dawa maalumu, na nyingine ilikuwa ni chupa ya damu.

Macho yangu yakapata uhai kidogo na nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa mirija ya zile chupa ilishuka hadi kwenye mkono wangu wa kulia na mwishoni kulikuwa na sindano mbili zilizokuwa zimechomekwa kwenye ule mkono na kupeleka maji na damu kwenye mishipa yangu ya damu.

Niliziangalia zile chupa zilizokuwa zimetundikwa kwenye chuma kwa makini na kushusha pumzi, kisha nikafumba macho yangu nikijaribu kutafakari.

Japo nilikuwa bado sijaelewa pale ni nilikuwa wapi lakini nilishangaa sana kujiona nikiwa ndani ya chumba kilichoonekana kuwa na mifumo ya kisasa kabisa ya uchunguzi kwa mgonjwa.

Nikaanza tena kujiuliza pale ni hospitali gani na nilifikaje lakini sikupata jibu, nikaanza kuyatembeza macho yangu taratibu huku na kule katika kutathmini vizuri mandhari yale. Nia yangu ilikuwa kuona kama kulikuwa na kielelezo chochote ambacho walau kingenifanya kuhisi pale nilikuwa katika hospitali gani.

Hata hivyo, nilipiga moyo konde na kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuniweka hai hadi wakati ule nikiamini kuwa Mungu alikuwa ametenda muujiza wake. Sikutaka kujiuliza maswali mengi kwa kuamini kuwa mambo mengine ningekuja kuyafahamu baadaye.

Nilitamani ile isiwe ndoto, niligeuza shingo yangu kuutazama mlango wa kile chumba kwa makini nikauona ukiwa umefungwa ingawa sikuweza kufahamu kama ulikuwa umefungwa kwa funguo au ulikuwa umerudishiwa tu.

Hata hivyo nilishindwa kuthibitisha kwani afya yangu ilikuwa dhaifu sana kiasi cha kushindwa hata kunyanyuka na kuketi pale kitandani.

Kutoka pale kitandani nilipolala nilibaki nikiwa mtulivu huku nikiutazama ule mlango wa kuingilia mle ndani, nikawa najiambia kuwa chochote ambacho kingetokea ingenipasa nisubiri tu kwani afya yangu ilikuwa dhaifu sana kuweza kuleta upinzani. Hivyo sikuwa na namna ila kuendelea kujipa subira.

Nikiwa bado nautazama ule mlango mawazo mengi yalikuwa yakipita kichwani mwangu na kunifanya nijihisi kama kiumbe kigeni katika sayari mpya.

Muda ule ule nikashtuka kuona kitasa cha ule mlango kikizungushwa taratibu kisha ule mlango ukasukumwa na kufunguka, nikajikuta nikiingiwa na hofu huku moyo wangu ukipoteza utulivu katika kiwango cha hali ya juu.

Niliyafumba haraka macho yangu nikatulia nikijifanya bado sijarudiwa na fahamu ili niweze kujua kwanini nilikuwa pale na nini kilikuwa kinaendelea pale.

Nilisikia kishindo cha mtu aliyekuwa akiingia na kisha akatembea kuja pale kitandani, kisha nikashtuka baada ya kuhisi mkono ukinigusa kwenye paji langu la uso.

Nilifumbua macho yangu taratibu kisha nikageuza shingo yangu kutazama upande ulikotokea ule mkono na kumuona mwanamume mnene na mrefu akiwa amesimama huku akinitazama kwa huruma.

Kwa haraka niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri uliokaribia miaka hamsini, maji ya kunde na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu vilimfanya aonekane kama bondia mkongwe. Alikuwa na uso mpana huku miwani yake mikubwa ikiwa imeyahifadhi macho yake makubwa.

Alikuwa amevaa suruali ya rangi nyeusi, shati la samawati na juu yake alivaa koti refu jeupe la kidaktari huku shingoni kwake akiwa amening’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ambacho kitaalamu kiliitwa stethoscope.

“Vipi Maximilian, unajisikiaje?” yule daktari aliniuliza baada ya kugundua kuwa nimeamka, hata hivyo sauti yake ilikuwa ya chini kana kwamba hakutaka watu wengine wasikie alichokuwa akiongea.

Kwanza nilisita baada ya kusikia nikiitwa kwa jina langu halisi, nikajiuliza niko wapi na nini kilikuwa kinaendelea. Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikimeza mate kuitowesha hofu ndani yangu.

“Nasikia maumivu ya mwili na kichwa, halafu ninahisi kizunguzungu na mwili umedhoofu sana,” hatimaye nikasema kwa sauti tulivu huku nikimtazama yule daktari kwa makini.

“Usijali, utapona… ulipoteza damu nyingi mwilini ila naamini utakapomaliza hii chupa ya tatu ya damu utapata afueni, kama hali yako haitabadilika,” alisema yule daktari aliyeonekana mchangamfu, mkarimu na rafiki kwa wagonjwa huku akinitazama kwa makini.

“Chukua hivi vidonge vya kutuliza maumivu, ukimeza utapata nafuu kabisa,” aliniambia huku akinipa vidonge viwili vya kutuliza maumivu na bilauri ya maji.

Wakati nikivichukua vile vidonge na kuvitupia mdomoni niliitupia jicho saa yake aliyokuwa ameivaa mkononi na kugundua kuwa ilikuwa inasomeka saa tatu na robo.

Muda ule miale ya jua la saa tatu asubuhi ilikuwa imepenya dirishani na kutuama chumbani na kuenea hadi pale kwenye kitanda nilipolala. Ni dhahiri kuwa joto la miale ile ya jua la saa tatu asubuhi lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwangu.

Naona sasa mambo yananoga, endelea kufuatilia Hekaheka...
 
Hakika mambo yananoga.. Pamela bila shaka Alipata taarifa ya kuonekana kwa Brown mahala.. Ndo pona pona ya Maximilian...
 
Hongera sana tena sana mtunzi hii hadithi inabidi uitolee kitabu maana inasisimua sana
HEKAHEKA! 24

Na Bishop Hiluka

“Chochote atakachowaleleza ni uongo, simjui huyu mtu na wala sijawahi kukutana naye,” nikasema kwa hasira kabla Trésor hajajibu lakini nikashtukia nikizabwa kofi la nguvu usoni lililonifanya kuona vimulimuli mbele ya macho yangu.

Shut up! Hujaulizwa wewe, unakimbilia kujibu!” Komandoo aliyenichapa kibao akafoka.

Nikasonya kwa hasira huku nikigeuza shingo yangu kumtazama yule komandoo, nikamtemea mate, kutahamaki nikazabwa kofi la pili lililonifanya kuyahisi maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi shingoni hadi mgongoni.

“Trésor, tueleze ni wapi mmeficha silaha!” Madame Pamela akamwambia Trésor kwa ukali kidogo.

Endelea...

“Ukweli japo mimi ni mshirika wa karibu wa Brown lakini naapa sijui mahali zilikofichwa kwani mkakati wote anaujua yeye na watu wengine wasiozidi watatu ambao mimi siwafahamu, mimi nilikuwa mtu wa kusubiri kupewa amri tu,” alisisitiza Trésor na kuniacha na mshangao usioelezeka.

“Na kuhusu washirika unaowafahamu?” aliuliza Madame Pamela.

“Wote ninaowafahamu ndio wale niliowataja, siwajui wengine labda muulizeni mwenyewe,” alisema Trésor huku akiyakwepa macho yangu na kuinamisha uso wake chini kwa hofu.

“Wapi mmezificha silaha, au unataka tukurudishe tena chumba cha mahojiano ndipo useme ukweli, siyo?” Madame Pamela alimuuliza Trésor kwa ukali.

“Nimewaambia Brown ndiye anayejua kila kitu, mimi ningekuwa najua zilipo ningewaambia, mbona haya mengine nimesema! Najua hata nikificha bado adhabu inayonikabili ni kifo tu,” alisema Trésor.

“Mimi naona mmeamua kupandikiza watu wenu ili mnikomoe, huu ni uongo mkubwa na ninaapa kuwa lazima niwashtaki kwenye mahakama ya haki za binadamu,” niling’aka kwa hasira.

“Kama unadhani kuwa Trésor ni muongo kwanini usijiulize tuliipata wapi ile picha mliyopiga wote mkiwa na Jasmine, au hujiulizi zile nyaraka zako zikiwemo zile pasipoti na kijitabu chenye mipango yako haramu tulivipataje kama siyo yeye aliyetusaidia kuvipata?” Madame Pamela akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi.

“Nimekwishawaambia mimi siitwi Brown. Sijui mmewatoa wapi hawa watu wanaotoa ushahidi wa uongo dhidi yangu, na mkakubali kudanganywa kiasi hiki! Muulizeni kila kitu yeye ndiye atakuwa anafahamu kuhusu hiyo mipango na ugaidi mnaonituhumu nao,” nilijitetea lakini haikuonekana kusaidia.

Madame Pamela alimpa ishara yule komandoo ya kumwondoa Trésor na kumrudisha alikomtoa. Wakati Trésor akiondolewa Madame Pamela alinigeukia akanitazama kwa uyakinifu huku akiachia tabasamu la ushindi.

“Sasa niambie, washirika wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza kwa sauti tulivu.

Sikumjibu bali niliendelea kubaki kimya huku nikimkodolea macho kwani nilionesha kuchoshwa na maswali yake.

Alishusha pumzi ndefu huku akiendelea kutabasamu na baadaye tabasamu lake liligeuka kuwa kicheko, kisha nikamuona yule komandoo aliyetoka na Trésor akirudi na muda huo huo Madame Pamela akawapa ishara fulani wale makomandoo ambayo sikufahamu maana yake.

Mara nikawaona wale makomandoo wakinisogelea kwa ukakamavu mkubwa, na kwa haraka sana wakanifungua zile pingu zilizokuwa zimefungwa kwenye mikono na miguu yangu pale kwenye kile kiti cha umeme kilichokuwa kikitumika kunisulubu.

Nikiwa bado nashangaa ghafla wale makomandoo wakanishika miguu yangu na kunivuta wakinishusha kwa nguvu kutoka pale kwenye kile kiti hali iliyonifanya nitue pale chini sakafuni kwa matako na kunifanya nisikie maumivu makali sana yaliyosambaa mwili mzima.

Nilijaribu kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani walianza kunishushia kipigo cha mateke mwilini mwangu na kujikuta nikiishiwa na nguvu na kulala sakafuni kama mfu.

Wale makomandoo waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaanza kuniburuza kibabe kuelekea kule kwenye lile tangi kubwa lililokuwa limejengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilikuwa limejazwa maji.

Walinibwaga pale chini jirani na lile tangi la maji. Nikiwa pale chini nikihema kwa nguvu kutokana na kile kipigo nilimuona Madame Pamela akinisogelea taratibu huku wale makomandoo wakinizunguka na hapo nikafungwa kamba mikononi.

“Tuambie wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza Madame Pamela kwa hasira.

“Wenzangu akina nani?” nilimuuliza kwa hasira.

“Unaoshirikiana nao kufanya ugaidi”

“Sifahamu chochote kuhusu ugaidi unaouzungumzia…”

Nilikatishwa na kipigo cha mateke ya mgongoni, kabla sijajua niseme nini mara nikabebwa mzobe mzobe na wale makomandoo kisha nikarushwa na kuangukia ndani ya lile tangi la maji. Matukio yote yale yalifanyika kwa haraka sana.

Nikajua sasa walikuwa wamedhamiria kunitesa kwa kunizamisha ndani ya lile tangi la maji kwa kufungulia umeme ulioungwa ndani ya lile tangi la maji ili kunipiga shoti mbaya na ikiwezekana kuniua kabisa.

Nikakumbuka kuwa niliwahi kusoma habari kuhusu matumizi ya mbinu za ukatili na utesaji kwa kuwaweka watuhumiwa kwenye maji, kuwakosesha usingizi, kuwapiga shoti ya umeme na kila aina ya utesaji ili kupata siri kutoka kwa magaidi.

Nilisimama na yale maji ndani ya lile tangi yaliishia usawa wa kifua changu. Nikiwa sijui kilichokuwa kinaendelea ghafla nikapigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima huku nikihisi ngozi yangu ikiunguzwa na moto wa umeme uliokuwa ukisambaa haraka sana mwilini mwangu.

Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nikaanza kutetemeka kama niliyekumbwa na ugonjwa mbaya wa degedege.

Nilifumbua mdomo wangu kupiga kelele za kumuomba Madame Pamela asitishe yale mateso lakini sauti yangu haikuweza kutoka, kila nilipopiga kelele niliisikia sauti yangu ikiishia ndani ya akili yangu.

Kwa mbali nikasikia mlango wa kile chumba ukigongwa kwa nguvu kisha ukafunguliwa na hapo nikasikia sauti ya vishindo vya watu waliokuwa wakija mbio kule kwenye lile tangi huku wakipiga kelele kumtaka Madame Pamela asitishe yale mateso.

Muda ule ule nikaanza kujiona nikipaa angani kwa kasi ya ajabu sana, na nilipofika juu zaidi nikajikuta nikianza kushuka chini kwa kasi ile ile na kisha nikatumbukia kwenye shimo refu sana lililokuwa na kiza kilichotisha.

Na mara giza zito likatanda kwenye mboni zangu za macho huku taratibu nguvu zikianza kuniishia na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda…

* * * * *

Nilizinduka nikajikuta nipo kwenye chumba kikubwa nikiwa nimelala kwenye kitanda kikubwa cha chuma cha futi nne na nusu kwa sita, nikiwa nimelalia foronya laini na mto wa kuegemeza kichwa.

Ndani ya chumba kile kulikuwa na hewa safi iliyokuwa ikisambazwa taratibu na kiyoyozi kilichokuwa juu ya dari ya kile chumba iliyokuwa imetengenezwa kwa gypsum nzuri ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kulining’inizwa taa nzuri.

Nilikuwa nimerudiwa na fahamu zangu na sikujua nilipoteza fahamu kwa muda gani, hisia zangu zilinitanabaisha kuwa nilikuwa nimerudiwa na fahamu huku nikikumbuka vizuri masaibu yote yaliyonitokea kule kwenye chumba cha mateso makali.

Sikuwa na uhakika kama nililetwa pale kwa gari, mkokoteni, machela au niliburuzwa kama ilivyotokea kule kwenye chumba cha mateso, kwa kuwa sikuwa na fahamu yoyote nilipokuwa nikiletwa pale.

Hata hivyo, jambo hilo halikuwa la muhimu sana kwangu. Jambo lililokuwa la muhimu ni kwamba nilikuwa bado nipo hai, na hivyo nikataka kujua nilikuwa wapi.

Mambo sasa yananoga, ni nini kitaendelea? Fuatilia kuujua mwisho wa Hekaheka...

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom